15-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti La Nne: Uwepo Wa Mashahidi (Kuishuhudishia) Au Kuitangazia Ndoa

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

عَقْدُ الزَّوَاجِ

 

Kufunga Ndoa

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

15:  Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti La Nne: Uwepo Wa Mashahidi (Kuishuhudishia) Au Kuitangazia Ndoa:

 

 

Kwa sharti hili, ndoa inajipambanua na uchafu wa zinaa.  ‘Ulamaa wamekhitilafiana katika chenye kushurutishwa hapa, je, ni uwepo wa mashahidi au kuitangazia?  Je, ni yote mawili, au kimojawapo?  Au hakuna chochote katika hayo mawili?  Wamekhitilafiana katika kauli tano:

 

Ya kwanza:

 

Uwepo wa mashahidi ni sharti, lakini kuitangaza ni jambo linalopendeza.  Haya ni madhehebu ya Jumhuwr, ni kauli pia ya An-Nakh’iy, Ath-Thawriy na Al-Awzaaiy, na pia imepasishwa na waliokuja hivi mwishoni.  Hoja zao ni:

 

1-  Ziada ya “mashahidi wawili” iliyopo kwenye Hadiyth: 

 

 

"لَا نِكَاحَ إِلَّا بِوَلِيٍّ [وَشَاهِدَيْ عَدْلِ]"

 

“Hakuna ndoa bila walii [na mashahidi wawili]”.  Lakini ziada hii ina udhaifu kwa njia zote ingawa baadhi ya ‘Ulamaa wameipa usahihi.

 

Ash-Shaafi’iy amesema:  “Na hii ijapokuwa imekatika (mpokezi mmoja amedondoka), lakini hata hivyo ‘Ulamaa wengi wanaizingatia, na wanasema:  Tofauti kati ya ndoa na zinaa ni mashahidi”.

 

Naye At-Tirmidhiy amesema kuandamizia Hadiyth hii:  “Hili (la uwepo wa mashahidi) ndilo lililofanywa na ‘Ulamaa katika Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na waliokuja baada yao kati ya Taabi’iyna na wengineo.  Wote wamesema:  “Hakuna ndoa ila kwa mashahidi”.  Hakuna yeyote aliyekwenda kinyume na hilo katika wao, isipokuwa ‘Ulamaa waliokuja hivi mwishoni”.   

 

2-  Yaliyosimuliwa moja kwa moja toka kwa ‘Aaishah:

 

"كُلُّ نِكَاحٍ لَمْ يَحْضُرْهُ أَرْبَعَةٌ فَهُوَ سَفَاحُ: خَاطِبٌ، وَوَلِيُ، وَشَاهِدَانِ"

 

“Ndoa yoyote ambayo haijahudhuriwa na wanne, basi ni zinaa:  Mposaji, walii na mashahidi wawili”.   Hadiyth hii ni munkar, haizingatiwi.

 

3-   Yaliyosimuliwa moja kwa moja toka kwa Ibn ‘Abbaas:

 

"الْبَغَايَا اللَّاتِي يُنْكِحْنَ أَنْفُسَهُنَّ بِغَيْرِ بَيِّنَةٍ"

 

“Wanawake wazinifu ni wale wanaojiozesha wenyewe bila ushahidi”. [Imechakatwa na Ad-Daaraqutwniy (3/224).  Kuna mpokezi asiyejulikana katika mlolongo wa wapokezi wake]

 

4-  Kauli ya Ibn ‘Abbaas:

 

"لا نِكَاحَ إِلاَّ بِشَاهِدَيْ عَدْلٍ وَوَلِيٍّ مُرْشِدٍ"

 

“Hakuna ndoa isipokuwa kwa mashahidi wawili waadilifu na walii mwenye busara”.  [Angalia Al-Irwaa (6/235, 251)]

 

Ya pili: 

 

Kuitangazia ni sharti lakini kuishuhudishia ni jambo linalopendeza.  Na hili ndilo lililo sahihi.  Wenye kauli hii ni Maalik, Ahmad na baadhi ya ‘Ulamaa wa Kihanafiy.  Vile vile, ni chaguo la Sheikh wa Uislamu bin Taymiyah .

 

Wamesema:  “Lau walii atamwozesha mwanamke bila kuwepo mashuhuda, kisha akaja kuitangaza ndoa na habari ikatangaa kati ya watu, basi ndoa ni sahihi na makusudio yanakuwa yamepatikana”. 

 

Hoja zao ni:

 

1-  Lililoamuriwa ni kutangazwa ndoa kama alivyosema Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"أَعْلِنُوا هذَا النِّكَاحَ واضْرِبُوا عَليْهِ بالغِرْبَالِ"

 

“Itangazieni nikaah hii, na ipigieni dufu”.  [Swahiyh Ibn Maajah.  Imechakatwa na Ibn Maajah (1895) na Al-Bayhaqiy (15094)]

 

Linalolengwa katika nikaah ni kudhihirishwa na kutangazwa ili ijipambanue na siri ambayo ni zinaa.  Kutangazwa huku kunatangaa zaidi kuliko kushuhudiliwa na mashahidi, na kutangazwa kukitimia, basi hata uwepo wa mashuhuda unakuwa hahuhitajiki.  Na kama ikishindikana kutangazwa, basi uwepo wa mashuhuda unakuwa ni waajib, kwa kuwa inakuwa ni sehemu ya tangazo.

 

2-  Wakati wa enzi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), watu walikuwa wakiwaozesha wanawake, na Rasuli hakuwa akiwaamuru washuhudishie ndoa.  Kadhalika, hakuna Hadiyth iliyothibiti yenye kushurutisha uwepo wa mashahidi katika nikaah.

 

3-  Ni jambo lisilowezekanika kuwa jambo hili ambalo Waislamu wamekuwa wakilifanya siku zote liwe na masharti ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuyabainisha.  Ikiwa hivi, basi litakuwa ni tatizo kubwa mno.  Na lau kama uwepo wa mashahidi ungekuwa ni sharti, basi Rasuli kutaja sharti hilis ingelikuwa muhimu zaidi kuliko kutaja mahari na mengineyo.

 

4-  Mashuhuda wanaweza kufa, au hali zao zikabadilika.

 

5-  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwacha huru Swafiyyah kisha akamwoa bila mashuhuda.  Toka kwa Anas:

 

"اشْتَرَى رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ جَارِيَةً بِسَبْعَةِ أَرْؤُسٍ، فَقَاَل النَّاسمَا نَدْرِيْ أَتَزَوَّجَهَا رَسُوْلُ اللهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَمْ جَعَلَهَا أُمَّ وَلَدٍ؟ فَلَمَّا أَنْ أَرَادَ أَنْ يَرْكَبَ حَجَبَهَا، فَعَلِمُوْا أَنَّهُ تَزَوَّجَهَا"

 

“ Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimnunua kijakazi  (Swafiyyah) kwa (malipo ya) watumwa saba.  Watu wakasema:  Hatujui kama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amemwoa au amemfanya kijakazi wake wa kumzalia.  Na alipotaka kupanda naye ngamia, alimfunika, na hapo wakajua kwamba amemwoa”.

 

Wa kundi la awali wameijibu hoja hii wakisema kwamba kuoa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) bila mashuhuda ni jambo mahsusi kwake.  Allaah Amemruhusu kumwoa mwanamke anayejitunukisha kwake bila mahari, na kwa hivyo kuoa bila mashahidi kunakubalika zaidi.

 

6-  Mauziano ambayo Allaah Ta’aalaa Ameamuru uwepo ushuhuda ndani yake, zipo dalili zinazothibitisha kwamba ushuhuda huo si katika mambo ya lazima katika mauziano.  Hivyo basi, ndoa ambayo Allaah Ta’alaa Hakutaja ndani yake ushuhuda, inastahiki zaidi ushuhuda usiwe katika shuruti zake.

 

Kauli ya tatu:

 

Ni sharti kutangazwa na uwepo wa mashahidi.  Hii ni riwaayah ya tatu toka kwa Ahmad. 

 

Kauli ya tano:

 

Si sharti kutangazwa wala kuwepo mashahidi.  Ni kauli iliyokwenda kinyume na ‘Ulamaa wote (shaadh), nayo imenukuliwa toka kwa Ibn Abiy Laylaa na wengineo.

 

Ninasema:  “Kwa yaliyotangulia, tunasema kwa muhtasari:

 

1-  ‘Ulamaa wamekubaliana kwamba ndoa inayofungwa bila mashahidi wala kutangazwa ni batili.  

 

2-  Wamekubaliana kwamba ndoa inayoshuhudiwa na wanaume wawili au zaidi ya hapo na ikatangazwa, inakuwa ni sahihi.

 

3-  Wamekhitilafiana kuhusiana na kuswihi ndoa ambayo imeshuhudiwa na mashahidi lakini haikutangazwa kwa watu, na ile iliyotangazwa lakini mashahidi hawakuwepo kama ilivyoelezwa hapo nyuma.  Lililo karibu zaidi na usahihi hapa ni kwamba sharti ni kutangazwa ndoa kama mashahidi hawakuhudhuria, lakini uwepo wa mashahidi una akiba zaidi ya kuchunga na kuhifadhi haki za mke na watoto ambao baba yao anaweza kuwakana na nasaba kupotea”.

 

Faida Mbili:

Ya kwanza:  Ikiwa mke na mume, walii na mashahidi wawili watakubaliana ndoa wasiitangaze, je, ndoa itaswihi?

 

Suala hili tunaweza kusema kwamba ni matunda ya mvutano wa suala lililopita.  Anayeona kwamba mashahidi ni sharti, basi atasema ndoa ni sahihi, kwa kuwa mashahidi wawili wapo.  Ama anayeona kutangazwa ni sharti, atasema ndoa ni batili kwa kuwa sharti la kutangazwa halipo.

 

Ya pili:  Ni yapi masharti kwa mashahidi (kwa wanaosema ni sharti wawepo)?

 

1, 2-  Akili na kubaleghe.  Hili limekubaliwa na wote  Ndoa haifungiki kwa asiyekuwa na viwili hivi.

 

3-  Uislamu.  Hili halina mvutano wowote ikiwa wanaofunga ndoa ni Waislamu.  Ama ikiwa mke ni “dhimmiyyah” (si Muislamu na anaishi chini ya himaya ya Dola ya Kiislamu), kwa huyu, Abu Haniyfah na Abu Yuwsuf wamejuzisha mwanaume “dhimmiy” kuwa shahidi, lakini wengine wamekataa.

 

4-  Wawe wanaume.  ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy na Kihanbali wameshurutisha mashahidi wawili wawe ni wanaume, na wamekataa ushahidi wa wanawake.  Ama ‘Ulamaa wa Kihanafiy, wao wamejuzisha ushahidi wa mwanaume mmoja na wanawake wawili.     Ibn Hazm amesema hivyo hivyo na ameongezea juu ya hilo kwamba wanawake wanne wanatosha kuwa mashahidi.

 

5-  Wawe waadilifu:  Hili ni sharti kwa ‘Ulamaa wa Kishaafi’iy na Kihanbali.  Wanachokusudia kwa uadilifu kama inavyoonekana ni kuwa mashahidi hao wawe wamesitirika, yaani hawana dalili yoyote ya utendaji maovu.  Ama ‘Ulamaa wa Kihanafiy, wao wamesema ndoa ni sahihi hata kama mashahidi ni watenda maovu.

 

6-  Wawe ni wenye kusikia matamshi ya Iyjaab na Qabuwl na kufahamu pia makusudio yake.

 

 

 

Share