14-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kufunga Ndoa: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti La Tatu: Mahari, Ni Sawa Yakatajwa Au Yasitajwe
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
عَقْدُ الزَّوَاجِ
Kufunga Ndoa
14: Masharti Ya Kuswihi ‘Aqdi Ya Ndoa: Sharti La Tatu: Mahari, Ni Sawa Yakatajwa Au Yasitajwe:
Ikiwa mke na mume watakubaliana kuoana bila mahari, basi ndoa hiyo inakuwa imeharibika, kwani mahari ni lazima, ni sawa yawe yametajwa au hayakutajwa.
Kushurutisha mahari katika ndoa ni madhehebu ya Maalik, moja ya riwaayah mbili toka kwa Ahmad, na ni chaguo la Sheikh wa Uislamu. Dalili ya wayasemayo ni:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَآتُوا النِّسَاءَ صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً"
“Na wapeni wanawake mahari zao kwa maridhawa”. [An-Nisaa: 04]
Wamesema kwamba maana ya نِحْلَةً ni kwa “Wajibu na lazima”, nayo ndio kauli ya Mufassiruna wengi. [Angalia Al-Qurtubiy na Ibn Kathiyr Suwrat An-Nisaa 04]
2- Kauli Yake Ta’aalaa:
"فَمَا اسْتَمْتَعْتُم بِهِ مِنْهُنَّ فَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ فَرِيضَةً"
“Basi mliostarehe nao, wapeni mahari yao kuwa ni waajib.” [An-Nisaa: 24]
3- Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَلَا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ أَن تَنكِحُوهُنَّ إِذَا آتَيْتُمُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ"
“Na wala si dhambi kwenu kufunga nao nikaah mkiwapa mahari yao”. [Al-Mumtahinah: 10]
4- Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَامْرَأَةً مُّؤْمِنَةً إِن وَهَبَتْ نَفْسَهَا لِلنَّبِيِّ إِنْ أَرَادَ النَّبِيُّ أَن يَسْتَنكِحَهَا "
“Na mwanamke Muumini akijitunuku mwenyewe kwa Nabiy, ikiwa Nabiy anataka kumuoa”. [Al-Ahzaab: 50]
Hapa kuoa bila mahari ni mahsusi kwa Nabiy tu na si kwa mwingine yeyote.
5- Hadiyth ya Ibn ‘Abbaas:
" لَمَّا تَزَوَّجَ عَلِيٌّ فَاطِمَةَ عَلَيْهِمَا اَلسَّلَامُ قَالَ لَهُ رَسُولُ اَللَّهِ َصلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: أَعْطِهَا شَيْئًا، قَالَ: مَا عِنْدِي شَيْءٌ . قَالَ: فَأَيْنَ دِرْعُكَ الحُطَمِيَّةُ "
“ ‘Aliy alipomwoa Faatwimah (‘Alayhimas Salaam), Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: Mpe chochote. Akasema: Sina kitu. Akamwambia: Liko wapi deraya lako la Kihutwami?” [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Abu Daawuwd (3125) na An-Nasaaiy (6/129)]
6- Hadiyth ya Sahl bin Sa’ad -kuhusiana na mwanamke aliyejipeleka mwenyewe kwa Rasuli kumwambia kuwa yuko tayari kuolewa naye bila mahari, na Rasuli hakuonyesha yuko tayari kwa hilo- ambapo sehemu ya Hadiyth inasema:
"فَقَامَ رَجُلٌ فَقَالَ: يا رَسُولَ الله، زَوِّجْنِيهَا إِنْ لَمْ يكُنْ لَكَ بِهَا حَاجَةٌ. فَقَالَ رَسُولُ الله صلى الله عليه وسلم: "هَلْ عِنْدَكَ مِنْ شيء تُصَدِقُهَا إِيَّاهُ؟ ". قَالَ مَا عِنْدِي.... فَقَالَ صلى الله عليه وسلم: "الْتَمِسْ وَلَوْ خَاتَمًا مِنْ حَدِيدِ "....[ثُمَّ قَالَ فِي آخِرِهِ] : زَوَّجْتُكَهَا بِمَا مَعَكَ مِنَ الْقُرْآنِ ".
“Mtu mmoja akasimama na kusema: Ee Rasuli wa Allaah! Niozeshe mimi ikiwa wewe humtaki. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: Je, una chochote ukampa kwacho mahari yake? Akasema: Sina. Rasuli akamwambia: Basi angalia hata pete ya chuma. [Kisha mwishowe akamwambia: Basi nimekuozesha kwa kiasi ulichohifadhi katika Qur-aan”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5149) na Muslim (1425)]
7- Yaliyosimuliwa toka kwa ‘Aaishah, amesema:
"أَمَرَنِي رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ أَنْ لا أُدْخِلَ امْرَأَةً على زَوْجِهَا قَبْلَ أَنْ يُعْطِيَهَا شَيْئًا"
“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameniamuru nisimwingize mwanamke yeyote kwa mumewe kabla hajampa chochote”. [Hadiyth hii ni dhaifu. Imechakatwa na Abu Daawuwd kwa njia ya Khaythamah bin ‘Abdulrahmaan toka kwa ‘Aaishah]
Mwonekano wa Hadiyth na aayaat zote hizi, unaonyesha kwamba kutajwa mahari na kukabidhiwa ni sharti ya kuswihi kwa ndoa. Lakini, Allaah Aliposema:
"لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً"
“Hakuna dhambi kwenu mkiwataliki wanawake ambao hamkuwagusa au kuwabainishia mahari yao”, aayah hii inaonyesha kwamba ndoa inaswihi bila ya kutaja mahari na kabla ya kuyakabidhi, na hii ndiyo itifaki ya ‘Ulamaa.
Lakini lenye uimara zaidi ni kauli ya kwanza. Sheikh wa Uislamu amesema (29/344): “Mwenye kusema kwamba mahari siyo yenye kukusudiwa, basi hiyo ni kauli isiyo na mashiko. Mahari ni nguzo ya nikaah, na kama itashurutishwa, inakuwa na uhakika zaidi kutokana na kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"إِنَّ أَحَقَّ الشُّرُوطِ أَنْ تُوفُوا بِهِ مَا اسْتَحْلَلْتُمْ بِهِ الْفُرُوجَ "
“Hakika sharti lenye haki zaidi ya nyinyi kulitekeleza, ni lile la kuhalalisha tupu”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5151) na Muslim (1418)]
Mali huhalalishwa kwa mbadala wake, na tupu hazihalalishwi ila kwa mahari. Na hakika si jinginelo, ndoa inafungika bila kutaja mahari au kuyakadiria, lakini hayakanushwi, lazima yawepo mahari tajwa au yaliyonyamaziwa”.