01-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa: (a) Vigawanyo Vya Masharti
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الإِشْتِرَاطُ فِيْ عَقْدِ النِّكَاحِ
Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa
01: Vigawanyo Vya Masharti: (a) Sehemu Ya Kwanza: Masharti yanayoendana na dhana ya ‘aqdi na makusudio ya kisharia.
Linalokusudiwa kiujumla ni mmoja kati ya wanandoa watarajiwa kumwekea mwenzake masharti yanayofungamanishwa na ‘aqdi ya ndoa au kabla ya kufungwa ‘aqdi.
Masharti haya yanagawanyika katika sehemu tatu:
Sehemu ya kwanza: Masharti yanayoendana na dhana ya ‘aqdi na makusudio ya kisharia.
Ni kama mke mtarajiwa kushurutisha mumewe mtarajiwa atangamane naye kwa wema, ampe matumizi, amnunulie mavazi na ampatie nyumba ya kuishi, na kama ana wake wengine, basi awatendee wote kwa usawa.
Au mume mtarajiwa ashurutishe mke asitoke nyumbani ila kwa idhini yake, au asimkatalie tendo la ndoa wakati akihitajia, au asitumie mali yake ila kwa ridhaa yake na mfano wa hayo.
Hukmu Ya Masharti Haya:
Kwa mujibu wa itifaki ya ‘Ulamaa, masharti haya yanakubalika kisharia, yako sahihi, na ni lazima yatekelezwe.