02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa: (b) Vigawanyo Vya Masharti

 

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

الإِشْتِرَاطُ فِيْ عَقْدِ النِّكَاحِ

 

Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

02:  Vigawanyo Vya Masharti: (b) Sehemu Ya Pili:  Masharti yasiyoendana na dhana ya ‘aqdi, au yenye kukiuka Maagizo ya Allaah na Sharia Zake (masharti mabovu).

 

Ni kama mke mtarajiwa kushurutisha asimtii mumewe, au atoke bila idhini yake, au asiwape zamu wakewenza wake wala matumizi, au asimpe tendo la ndoa.  Au ashurutishe asipewe mahari na mfano wa hayo.  Haya yote ni masharti yanayokwenda kinyume na sharia.

 

Hukmu Ya Masharti Haya: 

 

Kwa mujibu wa itifaki ya ‘Ulamaa, masharti kama haya hayafai, kwa kuwa ndanimwe kuna kuamuru Aliyoyakataza Allaah, au kukataza Aliyoyaamuru, au kuharamisha Aliyohalalisha, au kuharamisha Aliyohalalisha.  Na hii ndio maana ya kauli yake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"مَنِ اشْتَرَطَ شَرْطًا لَيْسَ فِي كِتَابِ اللَّهِ فَهُوَ بَاطِلٌ، وَإِنِ اشْتَرَطَ مِائَةَ شَرْطٍ، شَرْطُ اللَّهِ أَحَقُّ وَأَوْثَقُ"

 

“Mwenye kushurutisha sharti lolote ambalo haliko katika Sharia za Allaah basi ni batili, hata akishurutisha masharti mia moja.  Sharti la Allaah ndilo lenye haki kuliko yote na ndilo madhubuti zaidi”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (2155) na Muslim (1504)]

 

Lakini, Nini Hukmu Ya ‘Aqdi Yenye Masharti Batili Kama Haya?

 

Baada ya kujua kwamba masharti haya mabovu hayatakikani yawepo na yasitekelezwe, tunakuta kwa upande mwingine ‘Ulamaa wakikhitilafiana kuhusiana na hukmu ya ‘aqdi iliyowekewa masharti kama haya katika kauli tatu:

 

Kauli ya kwanza:  ‘Aqdi haibatiliki kwa masharti mabovu, isipokuwa sharti la ndoa ya muda maalum (ndoa ya mut’a), sharti hili linabatilisha ‘aqdi.

 

Haya ni madhehebu ya Mahanafiy.  Wanasema kwamba ndoa zilizokatazwa kama ndoa ya shighaar au ndoa ya kumhalalishia mke mtu aliyeacha talaka tatu, hizi zinaswihi ikiwa hazitokuwa na masharti mabovu isipokuwa ndoa ya mut’a, hii haiswihi, kwa kuwa sharti la muda maalum lipo ndani yake.

 

Kauli ya pili:  Kuna ‘aqdi ambazo zinabatilika kwa kuwepo sharti bovu na kuna zingine ambazo hazibatiliki.

 

Haya ni madhehebu ya Mashaafi’iy na Mahanbali.  Kidhibiti cha sharti ambalo linabatilisha ‘aqdi kwa mujibu wa mwono wao, ni sharti kuwa linafisidi dhana ya ndoa, kama vile mume kushurutisha amtaliki mke, au asimjimai, au ndoa iwe ya muda maalum.

 

Ama kidhibiti cha sharti ambalo halifisidi ndoa kwa mujibu wa mwono wao, ni kuwa sharti lisiwe linafisidi dhana ya ndoa.  Ni kama mke kushurutisha awe na uhuru wa kutoka nyumbani wakati wowote atakao, au mume amtaliki mkemwenza wake na mfano wa hayo.

 

Kauli ya tatu:   ‘Aqdi ambayo ndanimwe kuna sharti bovu ni batili.

 

Haya ni madhehebu ya kundi la ‘Ulamaa.  Pia ni chaguo la Ibn Taymiyah.  Hoja zao ni:

 

1-  Katazo lililopo ndani ya masharti haya linatosha kubatilisha ‘aqdi mbali na kuwepo uharibifu ndani yake.  Ni kama ndoa ya shighaar, ndoa ya mhalalishaji, au ndoa ya mut’a.

 

2-  Maswahaba walitengua ndoa za aina hii kwa kumwachisha mke na mume katika ndoa ya shighaar, wakaifanya ndoa ya mhalalishaji kwa aliyemwacha mkewe talaka tatu kuwa ni zinaa, na wakatoa onyo kali kwa mhalalishaji kuwa atapigwa mawe hadi kufa.

 

3-  Kuzifanya ndoa kama hizi kuwa ni sahihi sambamba na ubatilifu wa masharti mabovu, kunapelekea kulazimisha ndoa bila ya ridhaa za wanandoa wawili au mmoja wao.  Kwa sababu, kusema kwamba ‘aqdi ni sahihi, ni ima iambatane na sharti haramu lisilofaa au iambatane na kulibatilisha sharti.  Ikiwa hivi: (a) Tukisema ‘aqdi ni sahihi pamoja na uwepo wa sharti haramu ndani yake, hii itakuwa ni kinyume na Qur-aan na itifaki ya ‘Ulamaa.  (b)  Tukisema ‘aqdi ni sahihi pamoja na kuibatilisha sharti, hiyo itakuwa ni kumlazimisha mhusika kuingia kwenye ‘aqdi ambayo yeye hajaridhika nayo wala Allaah Hakumlazimisha.  Na mikataba au makubaliano hayawi wajibishi ila ile tu ambayo Allaah Ameamuru iwe lazima mtu kuwajibika nayo.  Hivyo basi, hiyo inakuwa ni kumlazimisha jambo ambalo Allaah na Rasuli Wake Hawajalilazimisha.  Na hii haijuzu. 

 

Ninasema:  “Madhehebu haya ya mwisho ndiyo yenye nguvu zaidi isipokuwa yanatiwa dosari (kwa mujibu wa mwono wangu) na Hadiyth ya ‘Aaishah ambayo ndiyo mhimili katika mlango huu.  Bi ‘Aaishah alipotaka kumnunua kijakazi (aitwaye Bariyrah) ili amkomboe na utumwa, watu wake walikataa kumuuza isipokuwa kwa sharti kwamba “Walaa” wa Bariyrah ubakie kwao wao.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:

 

 

"‏اشْتَرِيهَا وَأَعْتِقِيهَا، فَإِنَّمَا الْوَلاَءُ لِمَنْ أَعْتَقَ، ثُمَّ قَامَ فَخَطَبَ:  مَا بَال ُرِجَالٍ يَشْتَرِطُوْنَ شُرُوْطًا لَيْسَتْ في كِتَابِ اللهِ"

 

“Mnunue kisha mwache huru, kwani, hakika si jinginelo, “Walaa” ni kwa mwenye kuacha huru”.  Kisha Rasuli akasimama na kukhutubu akisema:  Inakuwaje watu wanashurutisha masharti ambayo hayako katika Hukumu za Allaah?!  [Hadiyth Swahiyh.  Imetajwa nyuma]

 

 "الوَلَاءُ"](Walaa) ni fungamano linalobakia kati ya mwenye kumkomboa mtumwa na mtumwa mwenyewe, yaani, ikiwa mtumwa huyu atakufa, na hana watu wake wa kumrithi, basi aliyemkomboa ndiye anamrithi kwa “Walaa”.  “Walaa” ni kama nasaba].  

 

Dalili hapa ni kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimruhusu aingie mkataba pamoja na uwepo ndanimwe sharti lisilofaa.

 

 

Share