03-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa: (c) Vigawanyo Vya Masharti
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الإِشْتِرَاطُ فِيْ عَقْدِ النِّكَاحِ
Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa
03: Vigawanyo Vya Masharti: (c) Sehemu Ya Tatu: Masharti ambayo Allaah Hakuyaamuru wala Hakuyakataza, na ambayo kama yatashurutishwa yatakuwa na maslaha kwa mmoja wa wanandoa.
Ni kama mke kumshurutishia mume kwamba asimtoe toka nyumbani kwao au nchini kwake, au asisafiri pamoja naye, au asioe mke mwingine zaidi yake, au amwache aendelee na masomo yake au kazi yake na mfano wa hayo.
Hukmu yake: ‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na kuswihi kwa masharti kama haya katika kufunga ‘aqdi katika kauli mbili:
Kauli ya kwanza: Masharti haya si halali, ni batili, lakini ‘aqdi ni sahihi. Ni madhehebu ya Jumhuwr ya ‘Ulamaa. Dalili zao ni:
1- Kwamba kiasili, mikataba na masharti ni marufuku isipokuwa ile tu ambayo sharia imehalalisha (kwa mwono wao).
2- Ni kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"مَا بَال ُرِجَالٍ يَشْتَرِطُوْنَ شُرُوْطًا لَيْسَتْ في كِتَابِ اللهِ؟ مَنِ اشْتَرَطَ شَرْطًا لَيْسَ فِي كِتَابِ اللَّهِ فَهْوَ بَاطِلٌ، شَرْطُ اللَّهِ أَحَقُّ وَأَوْثَقُ "
“Inakuwaje watu wanashurutisha masharti ambayo hayako katika Hukumu za Allaah?!. Mwenye kushurutisha sharti lolote ambalo haliko katika Sharia za Allaah basi ni batili. Sharti la Allaah ndilo lenye haki kuliko yote na ndilo madhubuti zaidi”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (2155) na Muslim (1504)]
Wamesema: “Katika Kitabu cha Allaah” ina maana ya Hukmu ya Allaah na Rasuli Wake, au katika yale yaliyoashiriwa na Qur-aan na Sunnah. Hivyo, hakuna sharti inayozingatiwa isipokuwa ile tu iliyopo ndani ya Viwili hivi.
3- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"الْمُسْلِمُونَ عَلَى شُرُوطِهِمْ إِلَّا شَرْطًا حَرَّمَ حَلَالًا أَوْ أَحَلَّ حَرَامًا"
“Waislamu ni lazima wachunge masharti waliyowekeana isipokuwa sharti lenye kuharamisha halali au lenye kuhalalisha haramu”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy na Muslim (59)]
Wamesema: Masharti haya yanakwenda kinyume na dhana ya mkataba wa ndoa. Kuyabadilisha ni sawa na kuyabadilisha Aliyoyawajibisha Allaah. Ni sawa na kuibadilisha ibada yoyote katika ibada za Kiislamu. Hivyo basi, kuoa kwake mke mwingine, kusafiri na mfano wa hayo -mambo ambayo ni halali- kunakuwa ni haramu kwa mujibu wa mkataba, na hii inakuwa ni kukiuka Mipaka ya Allaah na kuongeza jambo ambalo haliko kwenye dini.
Kauli ya pili: Masharti ni halali, si lazima kuyatekeleza, na mwanamke anaweza kuvunja ndoa mume asipoyatekeleza.
Ni madhehebu ya Al-Imaam Ahmad, Al-Awzaaiy, Is-Haaq, Abu Thawr, ni kauli iliyopokelewa toka kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab, Sa-‘ad bin Abiy Waqqaasw, Mu’aawiyah na ‘Amri bin Al’Aaswiy (Radhwiya Allaah ‘anhum). Pia ni chaguo la Shaykhul Islaam. Hoja yao ni haya yafuatayo:
1- Asili ya mikataba na masharti ni jambo linaloruhusiwa kwa sababu ni katika mambo ya kawaida.
2- Ujumuishi wa Aayah na Hadiyth zenye kuamuru kutekeleza ahadi, masharti na mikataba. Kati yake ni:
(a) Kauli Yake Ta’aalaa:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَوْفُوا بِالْعُقُودِ"
“Enyi walioamini! Timizeni mikataba”. [Al-Maaidah: 01]
(b) Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَأَوْفُوا بِالْعَهْدِ ۖ إِنَّ الْعَهْدَ كَانَ مَسْئُولًا"
“Na timizeni ahadi, hakika ahadi itakuwa ni yenye kuulizwa”. [Al-Israa: 34]
(c) Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ"
“Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga”. [Al-Muuminuwna: 08]
(d) Kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu alama tatu za mnafiki ambayo mojawapo ni kuwa akiahidi hatekelezi ahadi.
Hivyo basi, ikiwa kutekeleza na kuchunga ahadi ni jambo lililoamuriwa, itajulikana moja kwa moja kwamba asili ni kuswihi kwa mikataba na masharti husika. Kwa kuwa, hakuna maana ya kuhalalisha kitu bila kuwepo athari na makusudio yake, na makusudio ya mkataba, ni kuutekeleza.
3- Maana ya kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"كُلُّ شَرْطٍ لَيْسَ فِي كِتَابِ اللَّهِ فَهُوَ بَاطِلٌ وَإِنْ كَانَ مِائَةَ شَرْطٍ"
“Sharti lolote ambalo haliko ndani ya Kitabu cha Allaah, basi hilo ni batili hata kama ni masharti mia moja”… ni kwamba chochote kilichokanushwa, au kuharamishwa, au kubatilishwa ndani ya Kitabu cha Allaah, basi hicho ni batili, na kama hakuna kinachoashiria haya matatu, basi ni halali.
Au maana nyingine ya kuwepo ndani ya Kitabu cha Allaah, ni kile ambacho Allaah Ta’aalaa Amekihalalisha. Ikiwa kilichoshurutishwa ni kitendo au hukumu halali (kinafaa kufanywa au kuachwa), basi itajuzu kukishurutisha na ni wajibu pia kukitekeleza. Na kama Allaah Hakukihalalisha, basi haijuzu kukishurutisha.
4- Hadiyth ya ‘Uqbah bin ‘Aamir kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَحَقُّ الشُّرُوطِ أَنْ تُوفُوا بِهِ مَا اسْتَحْلَلْتُمْ بِهِ الْفُرُوْجَ"
“Masharti yenye haki zaidi ya nyinyi kuyatekeleza, ni yale ambayo mmehalalishia kwayo tupu (kustarehe na mke)”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (2721) na Muslim (1418)]
Hadiyth inaonyesha kwamba kutekeleza masharti katika nikaah ni muhimu zaidi kuliko kwenye mikataba mingineyo. [Fat-hul Baariy (9/218)]
5- Hadiyth ya Al-Miswar bin Makhramah ambaye amesema:
"إنَّ عَلِيًّا خَطَبَ بنْتَ أبِي جَهْلٍ، فَسَمِعَتْ بذلكَ فاطِمَةُ، فأتَتْ رَسولَ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وسلَّمَ، فقالَتْ: يَزْعُمُ قَوْمُكَ أنَّكَ لا تَغْضَبُ لِبَناتِكَ، وهذا عَلِيٌّ ناكِحٌ بنْتَ أبِي جَهْلٍ! فَقامَ رَسولُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عليه وسَلَّمَ، فَسَمِعْتُهُ حِينَ تَشَهَّدَ يقولُ: أمَّا بَعْدُ؛ أنْكَحْتُ أبا العاصِ بنَ الرَّبِيعِ، فَحدَّثَني وصَدَقَنِي، وإنَّ فاطِمَةَ بَضْعَةٌ مِنِّي، وإنِّي أكْرَهُ أنْ يَسُوءَها، واللَّهِ لا تَجْتَمِعُ بنْتُ رَسولِ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّمَ وبِنْتُ عَدُوِّ اللَّهِ عِنْدَ رَجُلٍ واحِدٍ، فَتَرَكَ عَلِيٌّ الخِطْبَةَ"
“ ‘Aliy alimchumbia binti ya Abu Jahl, na Faatwimah akasikia habari hiyo. (Faatwimah) akamwendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Watu wako wanazungumza wakidai kwamba wewe hukasiriki kwa adha inayowapata mabanati zako. Sasa huyo ‘Aliy anakwenda kumwoa bint ya Abu Jahl. Hapo hapo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasimama, nami (Al-Miswar) nikamsikia baada ya kutashahadia akisema: Amma ba-‘adu: Nilimwozesha Abul ‘Aaswiy bin Ar-Rabiy’ah (binti yangu Zaynab), naye amekuwa mkweli kwa kila aliloniambia, na Faatwimah ni kipande kitokacho kwangu, na mimi nachukia yeyote kumfanyia lolote la kumuudhi. Naapa kwa Allaah! Binti ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na binti ya adui wa Allaah mustahili wawe wake wa mume mmoja. Na hapo ‘Aliy akaivunja posa”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy (3729) na Muslim (2449)]
Al-Haafidh (7/86) amesema: “Huenda yeye (yaani Abul ‘Aaswiy), alikuwa amejiwekea mwenyewe sharti la kwamba hatomwolea Zaynab mke mwenza, na ‘Aliy kadhalika (kwa Faatwimah). Na kama si hivyo, basi uko uwezekano kwamba ima ‘Aliy alisahau sharti hilo akaenda kumposa (binti huyo wa Abu Jahl), au hakukuweko sharti lolote juu yake kwa kuwa hajaligusia au kulisema. Lakini pamoja na yote, ilikuwa anapaswa kuchunga hadhi, na kwa sababu hiyo, Rasuli akamlaumu”.
[Kadhalika, hakuna uharamu wa ‘Aliy kumwoa binti ya Abu Lahab. Rasuli anasema:
"وإنِّي لَسْتُ أُحرِّمُ حَلالًا، وِلَا أُحِلُّ حَرامًا"
“Na mimi kwa hakika siwezi kuharamisha la halali, au kuhalalisha la haramu”.
Tatizo hapa ni kuzuia kumuudhi Rasuli wa Allaah kutokana na adha itakayompata Faatwimah kama ndoa hiyo ingepita. Maudhi yanayompata Faatwimah, yanampata pia Rasuli wa Allaah hata kwa jambo la halali kama hilo la ndoa, ni sawa kwa wivu ambalo ni jambo la kimaumbile kwa wanawake, au hata hisia ya uadui wa Abu Lahab aliokuwa nao dhidi ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam]
6- Toka kwa ‘Abdulrahmaan bin Ghanam, amesema: “Nilikuwa nimekaa kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab goti langu likiwa linagusana na goti lake. Mtu mmoja akamwambia ‘Umar: Nimemwoa huyu, lakini ameshurutisha abakie kwao nyumbani, na mimi nimeamua kuhamia mji mwingine. Akamwambia: Ana haki atimiziwe sharti lake. Mtu yule akasema: Kwa hali hii, wanaume wameangamia. Mwanamke akitaka kuvunja ndoa wakati wowote, anaivunja! ‘Umar akamwambia:
"المُسْلِمُونَ عَلَى شَرْطِهِمْ عِنْدَ مَقَاطِعِ حُقُوْقِهِمْ"
“Waislamu ni lazima wawajibishwe sharti walilowekeana mbele ya sehemu ya kuchanganua haki zao (mimbari au ofisi ya kadhi kama watazozana)”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy amesema ni Mu’allaq (9/323), Sa’iyd bin Mansuwr amesema ni Mawsuwl (663), ‘Abdulrazzaaq (10608), Ibn Abiy Shaybah (4/199) na Al-Bayhaqiy (7/249]
7- Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"الْمُسْلِمُونَ عَلَى شُرُوطِهِمْ إِلَّا شَرْطًا حَرَّمَ حَلَالًا أَوْ أَحَلَّ حَرَامًا"
“Waislamu ni lazima wachunge masharti waliyowekeana isipokuwa sharti lenye kuharamisha halali au lenye kuhalalisha haramu”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Al-Bukhaariy na Muslim (59)]
Kiufupi, ikiwa mwanamke atamshurutishia mumewe kwamba asioe mke mwingine zaidi yake, kwa mujibu wa sharti hili, ikiwa mwanaume huyu ataoa mwingine, basi si haramu kwake. Na akioa kweli, basi mwanamke ana haki ya kuvunja ndoa.
Ninasema: “Kauli iliyo na nguvu zaidi ni kuwa kuweka sharti kwa jambo ambalo ni la halali kisharia (yaani ambalo inafaa kulifanya au kuliacha) na ambalo sharia haijalikataza, kunajuzu katika ndoa kwa mujibu wa dalili zilizotangulia, na pia watu wanaweza kuhitajia hilo katika baadhi ya nyakati. Na ikiwa mmoja wa wana ndoa atakiuka masharti, basi mwingine atakuwa na haki ya kuvunja ndoa. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.