04-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa: Nini Hukmu Ya Ndoa Ya Misyaar المِسْيَارُ?

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

الإِشْتِرَاطُ فِيْ عَقْدِ النِّكَاحِ

 

Kuwekeana Masharti Katika ‘Aqdi Ya Ndoa

 

Alhidaaya.com

 

 

04:  Nini Hukmu Ya Ndoa Ya Misyaar المِسْيَارُ?

 

“Ndoa ya “Misyaar” ni katika aina za ndoa zilizojitokeza katika miaka ya hivi mwishoni katika baadhi ya nchi.  Ndoa hii inakuwa kwa mwanaume kufunga ndoa halali ya kisharia na mwanamke ikitimiza masharti yote na nguzo zote, isipokuwa tu mwanamke anaachilia kwa ridhaa yake mwenyewe baadhi ya haki zake stahiki za ndoa kama makazi ya kuishi, pesa za matumizi, mume kulala kwake, zamu ya kulala kama mwanaume ana wake wengine na mfano wa hayo.

 

Miongoni mwa sababu kubwa zilizopelekea kujitokeza kwa aina hii ya ndoa na kuenea kwenye baadhi ya nchi, kwa upande wa wanawake, ni kuwepo idadi kubwa ya wanawake waliofikia umri wa kuolewa na umri wao ukasonga mbele bila ya kuolewa, au kuwa waliolewa kisha wakafarikiana na waume zao kwa sababu ya kifo au talaka, kutafuta shibisho halali la hamu ya tendo la ndoa, na mwanamke kuhitajia tu kuwa na mwanaume pembeni yake.

 

Ama kwa upande wa wanaume, baadhi yao wanaweza kusukumwa kwenye ndoa hii kutokana na matamanio makali ya kujimai, kutotosheka na mke mmoja, kutokuwa na uwezo wa kubeba gharama za kuoa mke mwingine kuanzia mahari, matumizi, nyumba na kadhalika, kuwa na tamaa ya kutwaa mali za mwanamke hususan akiwa tajiri na sababu nyinginezo.  

 

Hukmu Ya Ndoa Hii:

 

Inabainika kutokana na taarifu kwamba, ndoa ya “Misyaar” ni ndoa yenye sharti la kudondosha baadhi ya haki za mke zinazomlazimu mume.  Kwa picha hii, Fuqahaa wa enzi yetu ya leo wamekhitilafiana kuhusiana na kuswihi kwa ndoa hii katika kauli tatu:  

 

Kauli ya kwanza: 

 

Ni halali pamoja na ukaraha.  Ni halali kwa sababu imetosheleza nguzo na masharti ya kisharia, na pia haikufanywa kuwa njia ya kwenda kwenye haramu kama ndoa ya mhalalishaji au ya muda maalum (mut’a).  Mhimili mkuu hapa ni kuwa wote wawili wamekubaliana kwa ridhaa yao kwamba mke hana haki ya mume kulala kwake, au kupata zamu sawa na wake wengine, au kupewa pesa za matumizi na kadhalika. 

 

Imethibiti kwamba Mama wa Waumini Sawdah binti Zum-‘atah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) alipozeeka, aliitoa siku yake ya Rasuli kulala kwake kwa mke mwenza wake ‘Aaishah.  Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa anagawa siku mbili kwa ‘Aaishah; siku yake na siku ya Sawdah. [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5212) na Muslim (1463)]

 

Tunafahamu kutokana na Hadiyth hii kwamba mwanamke ana haki ya kudondosha baadhi ya haki zake alizodhaminiwa na sharia kama pesa za matumizi au mume kulala kwake na kadhalika.

 

Halafu, ndoa ni shibisho la hisia za kimaumbile za mwanamke za jimai, lakini pia ndoa inamzuia asifanye machafu, isitoshe, anaweza kwa ndoa hiyo kupata mtoto. 

 

Ama siri ya ndoa hii kuwa na ukaraha, ni kuwa -pamoja na uhalali wake- lakini inakosa ufanikishaji wa dhana ya kisharia ya ndoa kama nyumba ya utulivu, mume kuwa karibu na mkewe na watoto, uangalizi wa karibu wa familia, malezi bora na kadhalika.

 

Kauli ya pili:

 

Ni haramu.  Kwa sababu:

 

(a)  Inakwenda kinyume na makusudio ya ndoa kwa upande wa kijamii, kisaikolojia na kisharia kati ya mapenzi, huruma, makazi tulivu, na kusimamia haki na mawajibiko yanayozalikana kutokana na ‘aqdi ya ndoa ya kisharia.  Mazingatio katika mikataba ni dhana na maana, na si matamshi.

 

(b)  Inakwenda kinyume na mfumo wa ndoa ulioletwa na sharia, na Waislamu hawakuwa wakijua aina hii ya ndoa huko nyuma.

 

(c)  Ndanimwe kuna baadhi ya masharti yanayokiuka makusudio na dhana ya ‘aqdi.

 

(d)  Ni njia ya kuleta uharibifu.  Ndoa haitoi uzito wa kukadiria mahari, mume habebi jukumu la familia, na inaweza pia kuwa ni siri au bila ya walii.

 

Kauli ya tatu:

 

Kunyamazia na kuivutia subra hukmu yake.   Ni maneno yaliyonukuliwa toka kwa Al’Allaamah Ibn ‘Uthaymiyn (Rahimahul Laah).

 

Ninasema:  “Kipambanuzi cha mvutano ni uoanishaji wa sharti la kudondosha matumizi na kulala na upeo wa athari yake kwa upande wa kuswihi kwa ‘aqdi ya ndoa.  Nasi tumeshasema nyuma kwamba masharti yanayohusiana na ‘aqdi ya ndoa ni ya aina tatu: Kwanza:  Masharti yanayoendana na dhana ya ‘aqdi na dhana ya kisharia.  Pili:  Masharti yasiyoendana na dhana ya ‘aqdi, au yenye kwenda kinyume na Hukmu ya Allaah na Sharia Yake (masharti mabovu).  Tatu:  Masharti ambayo Allaah Hakuyaamuru wala Hakuyakataza, na ambayo kama yatashurutishwa yatakuwa na maslaha kwa mmoja wa wanandoa.

 

Ninaloliona mimi kuwa lina nguvu ni kwamba kushurutisha kudondosha matumizi, kulala na mfano wa hayo katika mambo ambayo ni ya wajibu kisharia kwa mume, ni katika masharti mabovu.  Hivyo basi nasema kiufupi kwamba ‘aqdi ni sahihi, na ndoa ni sahihi, lakini masharti ndio mabovu.  Na ndoa hii itabeba athari zote za kisharia ikiwa ni pamoja na uhalali wa kimwingilia mke, kuthibiti nasaba kwa watoto watakaozaliwa, wajibu wa kutoa matumizi na zamu ya kulala kwake.  Kadhalika, ni haki ya mwanamke kuzidai haki hizo.  Lakini, ikiwa mwenyewe ataridhia kuziachia, basi hakuna ubaya, kwa kuwa ni haki yake.

 

Juu ya yote haya, ni lazima tukumbuke kwamba aina hii ya ndoa haisalimiki na kuwemo ndani yake ukaraha.  Kadhalika, wigo wake usiachiwe ukatanuka kiholela.  Na huenda picha hii imewafanya baadhi ya ‘Ulamaa kunyamazia kuhusu hukmu yake.  Allaah Ndiye Ajuaye zaidi usahihi wake”. 

 

 

 

Share