15-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mahari: Vyombo Vya Biharusi Ni Jukumu La Nani?:

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

الصَّدَاقُ

 

Mahari

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

15:   Vyombo Vya Biharusi Ni Jukumu La Nani?:

 

 

Hivi ni vyombo ambavyo bi harusi hupelekwa navyo kwa mumewe kama fenicha, vyombo vya jikoni, matandiko na kadhalika.

 

Jumhuwr ya ‘Ulamaa wanasema kwamba si wajibu kwa mwanamke kutumia mahari yake au pesa nyingine kununulia vyombo, bali hilo ni jukumu la mume.  Mume ni lazima amtayarishie mkewe nyumba iliyokamilika kwa vyombo vyote vinavyohitajika kwa mujibu wa uwezo wake na mazingira yalivyo, ili nyumba iwe ni makazi ya kuwatuliza wote wawili.  Allaah Ta’alaa Amesema:

 

"أَسْكِنُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ سَكَنتُم مِّن وُجْدِكُمْ"

 

“Wawekeni wanawake kwenye majumba mnayokaa nyinyi kwa kadiri ya kipato chenu”.  [At-Twalaaq: 06]

 

Mahari iliyolipwa si kwa ajili ya kununulia vyombo, bali ni tunu kwa mwanamke kama Alivyosema Allaah Mtukufu:

 

"وَآتُوا النِّسَاءَ صَدُقَاتِهِنَّ نِحْلَةً"

 

“Na wapeni wanawake mahari zao kwa maridhawa.”  [An-Nisaa: 04]

 

Kadhalika, mahari ni kwa mkabala wa kuhalalikiwa mume kustarehe na mkewe kama ilivyotangulia, na kitu kimoja hakikabiliwi na badali mbili.  Na hii ni hata kama mume atalipa mahari mara mbili ya ile iliyobainishwa kwa matarajio ya mke kununulia vyombo vya thamani ya juu.  Kama anataka hivyo, basi mahari iwe kando na pesa za vyombo ziwe kando.  Akifanya hivyo, hapo itakuwa ni wajibu kwa mwanamke kununua vyombo kwa pesa hiyo.

 

Na ikiwa mwanamke atanunua vyombo vyake mwenyewe, au akanunuliwa na jamaa zake, basi vyombo vitabaki mali yake.

 

Faida:

 

Ikiwa mke au jamaa zake watanunua vyombo vyovyote kwa ridhaa yao bila kulazimishwa, basi hilo ni jambo jema.  Toka kwa ‘Aliy, amesema:

 

"جَهَّزَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَاطِمَةَ فِي خَمِيلٍ وَقِرْبَةٍ وَوِسَادَةِ أَدَمٍ حَشْوُهَا لِيفُ الْإِذْخِرِ‏"

 

“Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimtayarishia Faatwimah mavazi ya mahameli, kiriba cha maji, na mto uliojazwa nyuzi za idhkhir”.   [Hadiyth Hasan.  Imechakatwa na An-Nasaaiy (6/135) na Ibn Maajah (4152)]

 

“Idhkhir” ni aina ya mmea wenye harufu nzuri.  

 

 

 

Share