14-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Mahari: Kinachotolewa Zaidi Ya Mahari "الحِبَاءُ"
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
الصَّدَاقُ
Mahari
14: Kinachotolewa Zaidi Ya Mahari "الحِبَاءُ"
"الحِبَاءُ", ni mtu kuchukua mahari ya binti yake kwa faida yake binafsi, ni sawa kwa kupewa, au kwa kumshurutisha mume kiasi fulani cha pesa nje ya mahari.
‘Ulamaa wamekhitilafiana kuhusiana na hukmu ya hili katika kauli tatu:
Ya kwanza:
Inafaa kwa baba tu. Ni madhehebu ya Mahanafiy, Mahanbali na baadhi ya Mashaafi’iy. Hoja yao ni:
1- Kauli Yake Ta’aalaa:
"قَالَ إِنِّي أُرِيدُ أَنْ أُنكِحَكَ إِحْدَى ابْنَتَيَّ هَاتَيْنِ عَلَىٰ أَن تَأْجُرَنِي ثَمَانِيَ حِجَجٍ ۖ فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ ۖ وَمَا أُرِيدُ أَنْ أَشُقَّ عَلَيْكَ ۚ سَتَجِدُنِي إِن شَاءَ اللَّـهُ مِنَ الصَّالِحِينَ"
“Akasema: Mimi nataka nikuozeshe mmojawapo wa binti zangu hawa wawili kwa sharti kuwa unitumikie miaka minane, na ukitimiza kumi, basi ni uamuzi wako. Na wala sitaki kukutia mashakani, utanikuta In Shaa Allaah miongoni mwa Swalihina”. [Al-Qaswas: 27]
Wamesema: Mzee huyo aliyafanya mahari kuwa ni kumtumikisha Muwsaa amchungie wanyama wake.
2- Kauli ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"أَنْتَ وَمَالُكَ لأَبِيكَ "
“Wewe na unavyomiliki, vyote ni mali ya baba yako”. [Sunan Ibn Maajah 2291]
Kauli ya pili:
Ikiwa hilo litashurutishwa wakati wa kufunga ndoa, basi ni haki ya mwanamke, na ikiwa ni baada, basi ni haki ya baba. Ni madhehebu ya Maalik, na ni kauli ya ‘Umar bin ‘Abdul Aziyz, Ath-Thawriy na Abu ‘Ubayd. Kwa sababu kushurutisha wakati huo inakuwa ni kama tuhuma ya kwamba mahari ni pungufu, lakini baada ya ‘aqdi tuhuma inakuwa mbali kabisa.
Wametoa dalili kwa Hadiyth ya ‘Amri bin Shu’ayb, toka kwa baba yake, toka kwa babu yake kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَيُّمَا اِمْرَأَةٍ نَكَحَتْ عَلَى صَدَاقٍ، أَوْ حِبَاءٍ، أَوْ عِدَةٍ قَبْلَ عِصْمَةِ اَلنِّكَاحِ فَهُوَ لَهَا، وَمَا كَانَ بَعْدَ عِصْمَةِ اَلنِّكَاحِ فَهُوَ لِمَنْ أُعْطِيَهُ، وَأَحَقُّ مَا أُكْرِمَ اَلرَّجُلُ عَلَيْهِ اِبْنَتُهُ أَوْ أُخْتُهُ "
“Mwanamke yeyote atakayeolewa kwa mahari, au zawadi, au kuahidiwa kitu kabla ya fungamano la ndoa, basi ni haki yake, na kinachokuja baada ya fungamano la ndoa, basi ni cha mwenye kupewa. Na cha haki zaidi anachokirimiwa kwacho mwanaume, ni binti yake au dada yake”. [Hadiyth Hasan. Imechakatwa na Abu Daawuwd (2129), An-Nasaaiy (6/120), Ibn Maajah (1955) na Ahmad (2/182)]
Kauli ya tatu:
Haijuzu kabisa, inaharibu mahari, na mwanamke atapewa mahari mithili. Ni madhehebu ya Ash-Shaafi’iy.
Ninasema: “Kauli yenye nguvu ni kwamba mwanamke atastahiki kile kilichotajwa kabla ya kufungwa ‘aqdi, ni sawa ikiwa ni mahari au zawadi, hata kama zawadi hiyo itakuwa imeainishiwa mtu mwingine kama baba yake na kadhalika. Ama kinachotajwa baada ya ‘aqdi, basi hicho ni kwa yule aliyeainishiwa, ni sawa akiwa walii wake au mtu mwingine, na hii ni kutokana na Hadiyth iliyotangulia. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi”.