01-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kutangaza Ndoa: Maana Na Hukmu Yake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

اعْلَانُ النِّكَاحِ

 

Kuitangazia Ndoa

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

01:  Maana Na Hukmu Yake:

 

Kuitangazia ndoa ni kuitolea taarifa na kueneza habari yake kwa watu wote wanaohusika.  Hukumu yake imeelezwa nyuma katika sharti la nne la masharti ya kuswihi kwa ‘aqdi ya ndoa.

 

Kuitangazia kunakuwa kwa wanawake kupiga dufu na kuimba nyimbo zinazoruhusika kisharia ili kueneza furaha na kuziburudisha nyoyo.  Nyimbo hizi zinaruhusika -kwenye minasaba - kwa masharti kwamba zisiwe na uchafu bayana au wa kificho, zisichochee madhambi au kutaja yaliyoharamishwa, na zisiambatane na ala za muziki (isipokuwa dufu tu).

 

Miongoni mwa dalili kuhusu hili ni:

 

(a)  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"فَصْلُ مَا بَيْنَ الْحَلاَلِ وَالْحَرَامِ الدُّفُّ وَالصَّوْتُ فِي النِّكَاحِ"

 

“Kinachotenganisha kati ya ndoa halali na haramu ni (kupigwa) dufu na kuimba”.  [Imechakatwa na At-Tirmidhiy (1088), An-Nasaaiy (6/127) na Ibn Maajah (1896) kwa Sanad Hasan]

 

(b)  ‘Aaishah alimtayarisha bi harusi na kumpeleka kwa mumewe Muanswaar na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia:  

 

"يَا عَائِشَةُ مَا كَانَ مَعَكُمْ لَهْوٌ؟ فَإِنَّ الأَنْصَارَ يُعْجِبُهُمُ اللَّهْوُ ‏"‏‏

 

“Ee ‘Aaishah!  Hivi hamkuwa na chochote cha kutumbuiza?  Maanswaar wanapenda vitumbuizo (kupiga dufu na nyimbo halali).”  [Al-Bukhaariy (5163)]  

 

(c)  Ar-Rubayyi’u bint Mu’awwidh bin ‘Afraa amesema:

 

"جَاءَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَدَخَلَ حِينَ بُنِيَ عَلَيَّ فَجَلَسَ عَلَى فِرَاشِي، فَجَعَلَتْ جُوَيْرِيَاتٌ لَنَا يَضْرِبْنَ بِالدُّفِّ وَيَنْدُبْنَ مَنْ قُتِلَ مِنْ آبَائِي يَوْمَ بَدْرٍ إِذْ قَالَتْ إِحْدَاهُنَّ: وَفِينَا نَبِيٌّ يَعْلَمُ مَا فِي غَدٍ فَقَالَ: دَعِي هَذِهِ وَقُولِي بِالَّذِي كُنْتِ تَقُولِينَ"

 

“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja wakati nilipoingia nyumbani kwa mume wangu (baada ya nikah).  Akakaa kwenye tandiko langu, na mabinti zetu wadogo wakaanza kupiga dufu na kuimba wakiwaenzi kwa sifa njema mababu zangu waliouliwa kwenye Vita vya Badr.  Na mara mmoja wao akasema:  Na hali ya kuwa tunaye Nabiy anayejua yatakayotokea kesho”.  Rasuli akamwambia:  Wacha maneno haya na sema yale uliyokuwa unasema”.   [Imechakatwa na Al-Bukhaariy (5147), Abu Daawuwd (4922), At-Tirmidhiy (1090) na Ibn Maajah (1897)

 

Ama tumbuizo kwa kutumia ala za muziki, maneno  yakawa yanasifia wanawake, au nyimbo zikawa chafu zinazobomoa maadili mema kwa vijana, basi tumbuizo kama hilo bila shaka yoyote litakuwa ni haramu kwa itifaki ya Maswahaba, Taabi’iyna na Maimamu Wanne.

 

Al-‘Izzu bin ‘Abdus Salaam amesema:  “Ama udi, na ala nyinginezo maarufu zenye nyuzi kama rababa, gitaa na kadhalika, hizi, kwa ilivyo mashuhuri, ni haramu kupiga au kusikiliza”.

 

 

 

Share