02-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Kutangaza Ndoa: Kutangaza Ndoa: Miongoni Mwa Munkarati Za Ndoa
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
اعْلَانُ النِّكَاحِ
Kuitangazia Ndoa
02: Miongoni Mwa Munkarati Za Ndoa:
1- Bi harusi kwenda saluni kupambwa usiku wa kupelekwa kwa mumewe:
Hili ni moja kati ya munkarati mbaya zaidi ambazo zimekuwa ni jambo la kawaida kabisa hadi kufikia yule asiyelifanya kustaajabiwa. Mtihani mkubwa zaidi ni bibi harusi kufanyiwa shughuli ya kupambwa na mwanaume wa saluni ambaye atauchezea mwili wake kama atakavyo. Vipi msichana wa Kiislamu anauachia mwili wake kuchezewa kwa picha hii? Yuko wapi mume mwenye wivu na mkewe ambaye bado ni bi harusi na yeye mwenyewe bado hajamgusa vizuri? Je, ni dayyuth?! Hakika ni balaa kubwa mno zinazofanyika kwenye masaluni.
2- Wanawake kuangalia sehemu nyeti za bi harusi kwa hoja ya kumtayarisha kupelekwa kwa mumewe.
Hili ni haramu. Mwanamke haruhusiwi kuangalia uchi wa mwanamke mwenzake kwa neno la Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:
"لَا يَنْظُرُ الرَّجُلُ إِلَى عَوْرَةِ الرَّجُلِ وَلَا الْمَرْأَةُ إِلَى عَوْرَةِ الْمَرْأَةِ"
“Mwanaume haruhusiwi kuangalia sehemu nyeti za mwanaume mwenzake, na mwanamke pia haruhusiwi kuangalia sehemu nyeti za mwanamke mwenzake”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyh At-Tirmidhiy (2793)]
Uchi wa mwanamke kwa mwanamke mwenzake ni kama uchi wa mwanaume kwa mwanaume mwenzake ambao ni toka kitovuni hadi magotini.
Mwanamke haruhusiwi kuonyesha sehemu hizo hata kwa mama yake, au dada yake au binti yake. Hawa ni watu wake wa karibu na hairuhusiwi, basi vipi kwa watu wa mbali! Ni lazima mwanamke ajue kwamba anapofikisha miaka saba, basi haruhusiwi mama yake, au dada yake, au binti yake kuangalia uchi wake.
3- Kushikilia sherehe ya ndoa ifanyike kwenye kumbi au mahoteli bila kuchunga maadili ya dini.
Mara nyingi sherehe humo huambatana na israfu, ubadhirifu na kufanyika madhambi yanayotokana na kuagiza waimbaji wanawake na wanaume kutumbuiza kwa mahadhi yanayochemsha hisia na kuacha athari mbaya kwenye nyoyo. Kadhalika, wanaume na wanawake huchanganyika na hata kucheza pamoja huku wakiwa wamejipodoa na kuvaa kinyume na maadili ya Kiislamu. Haya hawezi kuyafanya Muislamu anayemkhofu Allaah, na sherehe kama hizi ni haramu bila shaka yoyote.
Jua dada yangu Muislamu kwamba wanawake kwenye mnasaba huu wameruhusiwa kupiga dufu, kuimba mashairi, kuitangaza ndoa na kuonyesha furaha madhali hayo yatakuwa mbali na mambo machafu, utumiaji wa ala za muziki na kuchanganyika na wanaume.
4- Bi harusi kujishaua usiku wa kupelekwa kwa mumewe:
Hili ni haramu ikiwa watakaomuona si wanawake wenzake au maharimu zake. Bi harusi anaruhusiwa kujipamba na kujishaua atakavyo kwa sharti tu asionwe na wasio maharimu zake au wanawake wenzake.
5- Bwana na bibi harusi kukaa kwenye kochi mbele ya wanawake na wanaume:
Hili ni kosa kubwa na ni haramu. Kwanza, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewakataza wanaume kuingia sehemu waliko wanawake aliposema:
" إِيَّاكُمْ وَالدُّخُولَ عَلَى النِّسَاءِ"
“Epukeni kuingia sehemu walipo wanawake”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyh At-Tirmidhiy (1171)]
Pili, inakuwa ni mlango wazi wa kuangaliana kati ya wanawake na wanaume, na wote wakiwa wamevalia na kujipamba vilivyo.
Kamati ya ‘Ulamaa Wakubwa wa Saudia ilitoa fatwaa ya uharamu wa jambo hili kwa nambari (8854/1405).
6- Wanawake kucheza na kunengua:
Ikiwa kunengua na kucheza kutakuwa mbele ya wanaume na watu wa kando, basi itakuwa ni munkari mbaya zaidi. Ama ikiwa ni sehemu iliyotengwa maalum kwa wanawake tu, basi itakuwa pia bora kuacha, kwa kuwa kucheza kawaida huenda sambamba na mahadhi ya muziki ambao ni haramu.
Isitoshe, sanjari na udhaifu wa iymaan na kuharibika nafusi, mwanamke anaweza kwenda kumsimulia mumewe namna fulani alivyokuwa akicheza na kukatisha mauno, na hapo balaa likaanza, mume akapagawa.
7- Kupiga picha mjongeo au za kawaida matukio ya mnasaba:
Ni uovu mkubwa na shari yenye kuenea. Inakuwa ni balaa kubwa kuwapiga wanawake picha wakiwa wamejipamba na kujiremba halafu baadaye picha hizo kusambazwa mitandaoni na kwingineko. Hii ni fitna kubwa kabisa ya kukashifu sehemu zao za mwili zisizopasa kuonekana, ni upandaji wa mbegu za shari, na kuanika wazi maasiya. Kupiga picha kwa mujibu wa rai ya baadhi ya ‘Ulamaa ni haramu kabisa. Kwa ajili hiyo, ni lazima wahusika wa minasaba hii na hususan akina mama, waachane na tabia hii mbaya na badala yake wajitahidi kufanya yale Aliyoyahalalisha Allaah Mtukufu.
8- Israfu katika walima wa harusi:
Kwa himizo na shinikizo lisilokabilika la baadhi ya akina mama wasiojitambua, watu wamekuwa wakishindana kutumia fedha nyingi mno kwa ajili ya kuandaa mlo wa walima ambao kiasi chake mara nyingi huzidi idadi ya waalikwa. Matokeo yake ni kumwagwa kinachobaki huku kukiweko masikini wengi wanaolala njaa. Allaah Ta’aalaa Ameikemea vibaya tabia ya israfu kwenye jumla ya aayah 22 katika Kitabu Chake Kitukufu. Miongoni mwa aayaat hizo ni:
"وَكُلُوا وَاشْرَبُوا وَلَا تُسْرِفُوا ۚ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْرِفِينَ"
“Na kuleni na kunyweni na wala msifanye israfu. Hakika Yeye (Allaah) Hapendi wanaofanya israfu”. [Al-A’araaf: 31]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"كُلُوا، واشْرَبُوا، وتَصَدَّقُوا، والْبَسُوْا فيْ غَيْرِ إسْرافٍ ولا مَخِيْلَةٍ"
“Kuleni, kunyweni, toeni swadaqah na vaeni bila kufanya israfu au kiburi”. [Imechakatwa na An-Nasaaiy (5/79) na Al-Haakim katika Al-Mustadrak (4/135) kwa Sanad Hasan]
9- Bi harusi kuacha kuswali usiku wa harusi:
Wengi katika mabibi harusi huanza maandalizi ya usiku wa ndoa toka baada ya swalah ya adhuhuri kuanzia kuoga, kujipamba, kujipodoa, kuvaa veli na mengineyo. Haya yote yanaweza kumsahaulisha baadhi ya swalah. Ni lazima kuchunga sana wasije kusahau swalah katika siku hii ya furaha na kumkasirisha Allaah.
10- Kuwapongeza maharusi kwa maneno yaliyo kinyume na mafundisho ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye kiigizo chetu. Imepokelewa:
"أنَّ النَّبيَّ صلَّى اللَّهُ علَيهِ وسلَّمَ كانَ إذا رفَّأَ الإنسانَ إذا تزوَّجَ قالَ: بارَكَ اللَّهُ لَكَ، وبارَكَ علَيكَ، وجمعَ بَينَكُما في خيرٍ"
“Kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anapompongeza mtu na kumwombea baada ya kuoa humwambia: Allaah Akubarikie, Akuteremshie barakah Zake, na Awatangamanishe kati yenu ndani ya kheri zote”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyh Abu Daawuwd (2130)]
Pia alikuwa akiwaombea maharusi kwa kusema:
"اللهُمَّ بَارِكْ لَهُمْ وَبَارِكْ عَلَيْهِمْ"
“Ee Allaah! Wabarikie na Wateremshie barakah Zako”. [Imechakatwa na An-Nasaaiy (3371) na Ibn Maajah (1906)]
