01-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Walima Wa Harusi: Maana Na Hukmu Yake

 

Swahiyh Fiqh As-Sunnah

 

كِتَابُ الزَّوَاجِ

 

Kitabu Cha Ndoa

 

 

 

وَلِيْمَةُ العُرْسِ

 

Walima Wa Harusi

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

01:  Maana Na Hukmu Yake:

 

Walima "الوَلْيْمَةُ" ni jina la chakula maalum cha harusi, nacho ni sunnah inayopendeza iliyokokotezwa.   Hutayarishwa na mume kwa mujibu wa hali yake inavyoruhusu.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwafanyia walima wakeze na akawahimiza Maswahaba wake kufanya hivyo.

 

Toka kwa Anas:

 

"أَصْبَحَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِهَا عَرُوسًا، فَدَعَا الْقَوْمَ فَأَصَابُوا مِنَ الطَّعَامِ، ثُمَّ خَرَجُوا وَبَقِيَ رَهْطٌ مِنْهُمْ عِنْدَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَأَطَالُوا الْمُكْثَ"

 

“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipambaukiwa akiwa ameshamwoa (Zaynab bint Jahsh).  Akawaalika watu wakala chakula, kisha wakatoka na wakabakia kundi dogo kati yao kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wakakaa sana”.  [Al-Bukhaariy (1428), Muslim (5166), At-Tirmidhiy (3218) na An-Nasaaiy (6/136)]

 

‘Abdulrahmaan bin ‘Awf alipooa, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia:

 

" أَوْلِمْ وَلَوْ بِشَاةٍ ‏"

 

“Fanya walima japo kwa kondoo mmoja”.  [Hadiyth iko kwa Al-Bukhaariy (5169).  Angalia Fat-hul Baariy (9/237)]

 

Katika walima, si sharti kondoo au mnyama mwingine, bali chochote kwa mujibu wa uwezo wa mume.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitayarisha “Hays” alipomwoa Swafiyyah”.  [Al-Bukhaariy (2048) na Muslim (1427)]

 

“Hays” ni tende zilizotolewa kokwa, zikachanganywa na samli au unga, na kuwa mlo.

 

Wakati Wake:

 Je, ni wakati wa kufungwa ndoa, au baada yake, au wakati wa mume kukutana na mkewe, au baada yake?

 

Wakati mwafaka wa walima ni wakati wa mume kukutana na mkewe au baada yake, na si wakati wa kufungwa ndoa.  Ni kutokana na Hadiyth iliyopita punde kuhusu ndoa ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwoa Zaynab bint Jahsh ambapo alifanya walima asubuhi baada ya kukutana na mkewe usiku.

 

Baadhi ya ‘Ulamaa wamesema kwamba wakati wake umeachiwa wazi kuanzia kufungwa ndoa hadi kumalizika kwa mujibu wa hali na mazingira.

 

 

 

Share