07-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Walima Wa Harusi: Adabu Na Ahkaam Za Jimai
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
وَلِيْمَةُ العُرْسِ
Walima Wa Harusi
07: Adabu Na Ahkaam Za Jimai:
Ili kukamilisha faida kwenye suala hili, ingelikuwa ni vizuri kuelezea baadhi ya adabu za ahkaam za jimai ambayo ni mhimili mkuu katika maisha ya ndoa. Kati ya adabu na ahkaam zake ni:
1- Inapendeza sana mume aanze kumchezea chezea mkewe kabla ya jimai.
Ni kwa Hadiyth ya ‘Amri bin Diynaar, amesema: Nilimsikia Jaabir bin ‘Abdillaah akisema:
"قَالَ لِي رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: "هَلاَّ جَارِيَةً تُلاَعِبُهَا وَتُلاَعِبُكَ"
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniambia (baada ya kujua nimeoa mwanamke mkubwa): Kwa nini usioe msichana mdogo (bikra) ukamchezea chezea naye akakuchezea chezea”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (5247) na Muslim (715)]
2- Mume anaruhusiwa kumuingilia kwa namna yoyote aipendayo kwa sharti iwe kwenye tupu ya mbele tu
Toka kwa Jaabir, amesema:
"كانتِ يَهودُ تقولُ مَنْ أَتَى امْرَأتَهُ في قُبُلِهَا مِنْ دُبُرِهَا كَانَ الْوَلدُ أَحْوَلَ، فَأَنْزَلَ اللَّهُ سبحانَهُ: نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أنَّى شِئْتُمْ"
“Mayahudi walikuwa (wanawaambia Waislamu) kwamba atakayemjimai mkewe kwa mtindo wa nyuma, basi mtoto (atakayezaliwa) atakuwa makengeza. Na hapo Allaah Ta’aalaa Akateremsha:
"نِسَاؤُكُمْ حَرْثٌ لَّكُمْ فَأْتُوا حَرْثَكُمْ أَنَّىٰ شِئْتُمْ"
“Wake zenu ni konde kwenu. Basi ziendeeni konde zenu (panapotoka kizazi) vyovyote mpendavyo ”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (4528), Muslim (1435), At-Tirmidhiy (2978), An-Nasaaiy (8976) na Ibn Maajah (1925)]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مُقْبِلَةً وَمُدْبِرَةً، ما كَانَ في الفَرْجِ"
“Ni sawa kuelekeana uso kwa uso, au kwa mgongo, lakini kwa sharti iwe kwenye tupu ya mbele”. [Asili yake ni kwenye Swahiyh mbili. Hili ni tamko la At-Twahaawiy katika Sharhul Ma’aaniy (3/41) kwa Sanad Swahiyh]
3- Mume anaruhusiwa kutembea kwenye mwili wote wa mkewe wakati wa jimai isipokuwa utupu wa nyuma.
Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) amesema:
"لا يَنْظرُ اللهُ عزَّ وجلَّ إلى رجُلٍ أتى رجُلًا أو امرأةً في دُبُرِهَا"
“Allaah ‘Azza wa Jalla Hatomwangalia Siku ya Qiyaamah mtu aliyemuingilia mwanaume au mwanamke nyuma”. [At-Tirmidhiy (1165), An-Nasaaiy (9001) na Ibn Abiy Shaybah (17070)]
Imepokelewa kwamba mtu mmoja alimuuliza Ibn Mas-‘uwd akisema:
"يَا أَبَا عَبْدِ الرَّحْمَنِ، آتِي امْرَأَتِي أَنَّى شِئْتُ؟، وحَيْثُ شِئْتُ؟، وَكَيْفَ شِئْتُ؟ قَالَ: نَعَمْ، فَنَظَرَ لهُ رَجُلٌ فَقَالَ لَهُ: إِنَّهُ يُرِيدُ الدُّبُرَ، قَالَ عَبْدُ الله: لَا، مَحَاشُّ النِّسَاءِ عَلَيْكُمْ حَرَامٌ "
“Ee Abu ‘Abdulrahmaan: Je, naweza kumuingilia mke namna yoyote nitakayo, popote nitakapo, na mtindo wowote nitakao? Akamwambia: Na’am. Mtu mwingine akamtazama na kumwambia: Anakusudia tupu ya nyuma huyu!!. Ibn Mas-‘uwd akamwambia: Tundu ya nyuma ya mwanamke ni haramu kwenu”. [Ibn Abiy Shaybah (3/530), Ad-Daarimiy (1/259) na At-Twahaawiy (3/46). Sanad yake ni Swahiyh]
Angalizo: Lililo haramu ni kujimai kwenye tupu ya nyuma (mapitio au njia ya haja kubwa). Ama kustarehe na kupapasia kwenye makalio mawili bila kuingiza dhakari nyuma, hili halina ubaya. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
4- Hairuhusiwi kumuingilia mke wakati wa hedhi:
Mwanamke anapokuwa hedhini, mwanaume anaruhusiwa kufanya naye mambo yote isipokuwa jimai tu.
5- Mwanamume akihisi hamu akataka kurudia raundi nyingine, basi atawadhe:
Ni kwa Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"إِذَا أَتَى أَحَدُكُمْ أَهْلَهُ ثُمَّ أَرَادَ أَنْ يَعُودَ فَلْيَتَوَضَّأْ"
“Akimuingilia mmoja wenu mke wake, kisha akataka tena, basi atawadhe”. [Swahiyh Muslim (308)]
6- Hakuna ukakasi wowote kama mke na mume watavua nguo zote wakati wa tendo la jimai:
Hakuna mpaka wa uchi kati ya mke na mume. Wanaweza kuangaliana sehemu zote za mwili. Hili limeelezwa kwenye mlango wa hukumu za kuangalia.
7- Haijuzu mwanamke kugomea tendo la ndoa mume wake akiwa na hamu nalo:
Ni kwa Hadiyth ya Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِذَا دَعَا اَلرَّجُلُ امْرَأَتَهُ إِلَى فِرَاشِهِ فَأَبَتْ أَنْ تَجِيءَ، لَعَنَتْهَا اَلْمَلَائِكَةُ حَتَّى تُصْبِحَ "
“Mume akimwita mkewe kitandani na mke akagoma kwenda, basi Malaika watamlaani mpaka asubuhi”. [Al-Bukhaariy (5193) na Muslim (1436)]
8- Kama jicho la mwanaume litapiga kwa mwanamke mwingine akamsisimua, basi aende akamuingilie mkewe:
Imepokelewa toka kwa Jaabir bin ‘Abdullaah (Radhwiya Allaah ‘anhu):
"أنَّ رَسُولَ اللهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ رَأَى امْرَأَةً، فأتَى امْرَأَتَهُ زَيْنَبَ وَهي تَمْعَسُ مَنِيئَةً لَهَا، فَقَضَى حَاجَتَهُ، ثُمَّ خَرَجَ إلى أَصْحَابِهِ، فَقالَ: إنَّ المَرْأَةَ تُقْبِلُ في صُورَةِ شيطَانٍ، وَتُدْبِرُ في صُورَةِ شيطَانٍ، فَإِذَا أَبْصَرَ أَحَدُكُمُ امْرَأَةً فَلْيَأْتِ أَهْلَهُ؛ فإنَّ ذلكَ يَرُدُّ ما في نَفْسِهِ"
“Kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwona mwanamke, na hapo hapo akamwendea mkewe Zaynab ambaye alikuwa akiichakata ngozi, akamuingilia. Kisha akatoka kwa Maswahaba wake na kuwaambia: “Hakika mwanamke huwaelekea wanaume kwa picha ya shaytwaan na huwapita kwa picha ya shaytwaan. Basi yeyote akimwona mwanamke (akamsisimsha), amwendee mkewe, kwani hilo litamwondoshea moyo wake hisia aliyoipata”. [Muslim (1403), Abu Daawuwd (2151), na At-Tirmidhiy (1158), na riwaayah ni yake].
9- Yeyote katika wanandoa asieleze au kufichua siri za jimai baina yao:
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إِنَّ مِنْ أَشَرِّ النَّاسِ عِنْدَ اللَّهِ مَنْزِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ الرَّجُلَ يُفْضِي إِلَى امْرَأَتِهِ وَتُفْضِي إِلَيْهِ ثُمَّ يَنْشُرُ سِرَّهَا ".
“Hakika mtu ambaye atakuwa na hadhi mbaya zaidi miongoni mwa watu mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah, ni yule anayemvaa mkewe kimwili na mkewe akamvaa, kisha akaja kuelezea siri zake kwa watu”. [Muslim (1437) na Abu Daawuwd (4870)]
Lakini hili linajuzu kwa ajili ya maslaha ya kisharia kama walivyokuwa wake za Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakielezea ili kubainisha kwa watu namna Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akifanya ili tupate kumfuata. Kama yatakuwepo maslaha ya kisharia, basi hakuna ubaya. Allaah Ndiye Ajuaye zaidi.
10-Mume anaporudi toka safari, asimshtukize mkewe, bali amjulishe siku na wakati wa kuwasili:
Ili mke apate kujitayarisha kwa ajili yake kwa usafi, kujitia manukato na kujipamba. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إذا قَدِمَ أَحَدُكُمْ لَيْلًا، فلا يأتيَنَّ أَهْلهُ طُرُوقًا، حتى تَسْتَحِدَّ المُغِيبَه، وتَمْتَشِطَ الشَّعِثَه
“Anaporudi mmoja wenu safari usiku, basi asimjie mkewe usiku huo huo, ili mkewe ambaye yeye amekuwa mbali naye, aweze kunyoa kinena, na kuzichana vizuri nywele alizokuwa hazishughulikii”. [Muslim (715)]
11- Mume anaweza kumjimai mkewe anayenyonyesha:
Toka kwa ‘Aaishah, toka kwa Judaamah bint Wahab Al-Asadiyyah kwamba alimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema:
"لَقَدْ هَمَمْتُ أَنْ أَنْهَى عَنِ الْغَيْلَةِ حَتَّى ذُكِّرْتُ أَنَّ الرُّومَ وَفَارِسَ يَفْعَلُونَ ذَلِكَ فَلاَ يَضُرُّ أَوْلاَدَهُمْ "
“Hakika nilidhamiria kukataza mume kumuingilia mkewe wakati ananyonyesha, kisha nikaona Warumi na Wafursi wanafanya hivyo, na watoto wao hawapati madhara yoyote”. [Muslim (1442)]
Maana ya "الغِيْلَةُ" ni mume kumuingilia mkewe wakati ananyonyesha, au kumuingilia wakati akiwa mja mzito.
12- Ni karaha mwanaume kumwaga manii nje ya tupu:
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa kuhusu suala hili akasema:
" ذلِكَ الوَأْدُ الخَفِيُّ"
“Huo ni uzikaji siri wa kiumbe hai”. [Muslim (1442), Abu Daawuwd (3882), At-Tirmidhiy (2077), An-Nasaaiy (6/106) na Ibn Maajah (2011)]
Na hii ni sambamba na Kauli Yake Ta’aalaa:
"وَإِذَا الْمَوْءُودَةُ سُئِلَتْ"
“Na mtoto wa kike aliyezikwa hali akiwa yuhai atakapoulizwa”. [At-Takwiyr: 08]
Jaabir (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:
"سَأَلَ رَجُلٌ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ: إِنَّ عِنْدِي جَارِيَةً لِي وَأَنَا أَعْزِلُ عَنْهَا. فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: "إِنَّ ذَلِكَ لَنْ يَمْنَعَ شَيْئًا أَرَادَهُ اللَّهُ"
“Mtu mmoja alimuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimwambia: Mimi nina kijakazi changu, lakini nikimuingilia, namwagia manii nje (nini hukmu yake)? Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: Hilo halitozuia chochote Akitakacho Allaah.” [Muslim (1439)]
Toka kwa Jaabir (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:
"كُنَّا نَعْزِلُ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَالْقُرْآنُ يَنْزِلُ "
“Tulikuwa enzi za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tunamwagia manii nje huku Qur-aan inateremka”. [Al-Bukhaariy (5208) na Muslim (1440)]
Matini zote hizi zinaonyesha kwamba mwanaume kumwagia nje manii wakati wa tendo la jimai na mkewe ni jambo lililokirihishwa. Na ijulikane kwamba hakuna nafsi yoyote ambayo Allaah Ameandika kwamba Ataiumba isipokuwa Atatimiza hilo, ni sawa mtu akimwagia nje au ndani. Kama Allaah Ameandika mimba ikamate, basi itakamata tu, ni sawa mtu amwagie maji ya uzazi nje, au avae kinga, au hata mwanamke atumie madawa, sindano, coil na kadhalika, itashika tu.
