06-Swahiyh Fiqh As-Sunnah: Kitabu Cha Ndoa: Walima Wa Harusi: Adabu Za Usiku Wa Kukutana Mke Na Mume Baada Ya Kufunga Ndoa
Swahiyh Fiqh As-Sunnah
كِتَابُ الزَّوَاجِ
Kitabu Cha Ndoa
وَلِيْمَةُ العُرْسِ
Walima Wa Harusi
06: Adabu Za Usiku Wa Kukutana Mke Na Mume Baada Ya Kufunga Ndoa:
Hizi ni baadhi ya adabu ambazo inatakikana kwa maharusi kujipamba nazo usiku wa kwanza wa kukutana. Wakiingia nyumbani kwao inapendeza wafanye yafuatayo:
1- Mume amsalimie bi harusi wake. Kitendo hiki humwondoshea bi harusi hofu aliyonayo moyoni. Toka kwa Ummu Salamah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomwoa, alimtolea salamu alipotaka kumuingilia.
2- Mume amtulize bi harusi kwa kumpa kinywaji au chochote kitamu cha kula. Toka kwa Asmaa bint Yaziyd (Radhwiya Allaah ‘anhaa), amesema:
:"إِنِّيْ قَيَّنْتُ عَائِشَةَ لرَسُولِ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، ثُمَّ جِئْتُهُ فَدَعَوْتُهُ لِجَلْوَتِهَا، فَجَاءَ فَجَلَسَ إلى جَنْبِهَا، فَأَتَى بُعَسَّ فيْهِ لَبَنٌ، فَشَرِبَ ثُمَّ نَاوَلَهَا فَخَفَضَتْ رَأْسَهَا واسْتَحْيَتْ، قَالَت أَسْمَاءُ: فَانْتَهَرْتُهَا وَقُلْتُ لَهَا: خُذِيْ مِنْ يَدِ رَسُوْلِ الله صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، فَأَخَذَتْ فَشَرِبَتْ شَيْئًا"
“Mimi nilimpamba ‘Aaishah kwa ajili ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kisha nikamwendea Rasuli nikamtaka aje amwangalie alivyopendeza. Akaja na kukaa pembeni yake, kisha akachukua gilasi ya maziwa, akanywa kisha akampa ‘Aaishah, na ‘Aaishah akainamisha kichwa chake kwa haya. Nikamtolea macho na kumwambia: Chukua gilasi hiyo, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anakupa. Akapokea, akanywa kidogo..” [Ahmad (6/453) na Sanad yake inaelekea kuhasinishwa]
3- Mume amwekee mkono kichwani bi harusi wake na amwombee:
Ni kwa neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
" إذا تزوَّجَ أحدُكمُ امرأةً أوِ اشْتَرَى خَادِمًا فَلِيَأْخُذْ بِنَاصِيَتِها، وَلِيُسَمِّ اللهَ عَزَّ وجَلَّ، وَلِيَدْعُ بِالبَرَكَةِ ولِيَقُلْ: اللَّهُمَّ إنِّي أَسْأَلُكَ مِنْ خَيْرِهَا َوَخَيْرِ مَا جَبَلْتَهَا عَلَيْهِ، وأَعُوْذُ بِكَ مِنْ شَرِّهَا وَشَرِّ مَا فِيْهَا وَشَرِّ مَا جَبَلْتَهَا عَلَيْهِ"
“Akioa mmoja wenu mwanamke au akanunua mtumwa (au kijakazi), basi akamate ncha ya utosi wake, alitaje Jina la Allaah ‘Azza wa Jalla, na kisha aombe barakah kwa kusema: Ee Allaah! Ninakuomba kheri zake, na kheri Ulizomuumba nazo, na najilinda Kwako na shari zake, na shari alizonazo, na shari Ulizomuumba nazo”. [Abu Daawuwd (2160), An-Nasaaiy (241-264) na Ibn Maajah (1918) kwa Sanad Hasan]
4- Apige mswaki kusafisha mdomo kabla ya kumuingilia:
Hili bila shaka liko wazi katika kunogesha tendo la jimai na mazungumzo yao kiujumla. Na hili pia kwa bi harusi bila shaka linatakiwa.
Imepokelewa toka kwa Shurayh bin Haani, amesema:
"سَأَلْتُ عائِشَةَ، قُلتُ: بأَيِّ شيءٍ كانَ يَبْدَأُ النبيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إذا دَخَلَ بَيْتَهُ؟ قالَتْ: بالسِّواك".
“Nilimuuliza ‘Aaishah: Ni jambo gani ambalo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaanza nalo anapoingia nyumbani kwake? Akasema: Ni mswaki”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyh Muslim (253)]
5- Kupiga “Basmalah” na kuomba du’aa wakati wa jimai:
Toka kwa Ibn ‘Abbaas, amesema: “Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"أَمَا لو أنَّ أحَدَهُمْ يَقولُ حِينَ يَأْتي أهْلَهُ: باسْمِ اللَّهِ، اللَّهُمَّ جَنِّبْنِي الشَّيْطانَ، وجَنِّبِ الشَّيْطانَ ما رَزَقْتَنا، ثُمَّ قُدِّرَ بيْنَهُما في ذلكَ، أوْ قُضِيَ ولَدٌ، لَمْ يَضُرَّهُ شَيطانٌ أبَدًا"
“Naam. Lau mmoja wao atasema wakati anapoanza kumuingilia mkewe: “Bismil Laah. Ee Allaah! Niepushie shaytwaan, na mwepushie shaytwaan utakayeturuzuku”, kisha wakaandikiwa kupata mtoto kutokana na tendo hilo, basi shaytwaan hatomdhuru (mtoto) maisha yake yote”. [Al-Bukhaariy (5165) na Muslim (1434)]
6- Aswali pamoja naye rakaa mbili (hili limenukuliwa toka kwa Salaf).
