037-Majina Ya Allaah Mazuri Na Sifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-WAHHAAB

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Sifa Zake

 

Alhidaaya.com

 

الْوَهَّاب

037-Al-Wahhaab

 

 

 

Al-Wahhaab: Mwingi Wa Kutunuku

 

 

Jina hili tukufu limetajwa mara tatu katika Qur-aan. Miongoni mwa Aayah ni Kauli Yake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

أَمْ عِندَهُمْ خَزَائِنُ رَحْمَةِ رَبِّكَ الْعَزِيزِ الْوَهَّابِ ﴿٩﴾

Au wanazo hazina za Rehma za Rabb wako Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa Kutunuku? [Swaad (38:9)]

 

 

Hibaa: Ni kumilikisha kitu bila ya kupata kwa mkabala, yaani, bila ya thamani wala kiasi cha kulipwa, ni utoaji usiotarajia kitu kwa anayepewa.   

 

 

Al-Wahhaab: Anatoa bila ya mbadala, Anatoa kwa mapenzi na Anawaneemesha Waja Wake kwa kuombwa au hata bila ya kuombwa.

 

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Al-Wahhaab: Mwenye kutoa kwa wingi kwa viumbe vyote, waliomo mbinguni na ardhini, utoaji Wake hauishi wala haukatiki, Anatoa kwa wote bila ya kutaka alipwe.

 

 

Na utoaji Wake mkubwa zaidi ni kwa Manabii Wake na Waja Wake wema ambao hupata furaha ya milele, duniani na Aakhirah. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

وَوَهَبْنَا لَهُم مِّن رَّحْمَتِنَا وَجَعَلْنَا لَهُمْ لِسَانَ صِدْقٍ عَلِيًّا ﴿٥٠﴾

Na Tukawatunukia katika Rehma Zetu, na Tukawajaalia wenye kutajwa kwa sifa nzuri za kutukuka. [Maryam (19:50)]

 

 

Basi Akawatunukia Manabii Wake kama vile Alivyomtunukia Nabiy Ayuuwb (‘alayhis-salaam), kumjaalia ahli, siha na mali baada ya mitihani ya maradhi na upotezaji mali aliyokumbwa nayo:

 

وَوَهَبْنَا لَهُ أَهْلَهُ وَمِثْلَهُم مَّعَهُمْ رَحْمَةً مِّنَّا وَذِكْرَىٰ لِأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿٤٣﴾

Na Tukamtunukia ahli zake na wengine mfano wao pamoja nao ikiwa ni Rehma kutoka Kwetu, na ni ukumbusho kwa wenye akili. [Swaad (38:43)]

 

 

Na Nabiy Ibraahiym (‘alayhis-salaam) aliomba al-hukmaa, naye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Akamtunukia:  

 

 

 

 

رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ ﴿٨٣﴾

Rabb wangu! Nitunukie hukmah,[1] na Unikutanishe na Swalihina.  [Ash-Shu’araa (26:83)] 

 

 

 

Na Waja wema waliokuwa na msingi madhubuti wa ilimu ya Dini Yake tukufu waliomba:

 

رَبَّنَا لَا تُزِغْ قُلُوبَنَا بَعْدَ إِذْ هَدَيْتَنَا وَهَبْ لَنَا مِن لَّدُنكَ رَحْمَةً ۚ إِنَّكَ أَنتَ الْوَهَّابُ ﴿٨﴾

 

 (Husema): Rabb wetu!  Usizipotoe nyoyo zetu baada ya kuwa Umetuhidi na Tutunukie kutoka Kwako Rehma. Hakika Wewe Ni Mwingi wa Kutunuku na Kuneemesha. [Aal-‘Imraan (3:8)]

 

 

 

Yaani: Wewe Ndiye Utoaye kwa waja Wako na Unayewapa tawfiyq na kuwathibitishia katika Dini Yako na kusadikisha kitabu Chako na Rusuli Wako.[2]

 

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah, Al-Wahhaab:

 

 

 

1-Mpende Al-Wahhaab kwa kukutunukia khayraat zote Aliokujaalia duniani, na pia mshukuru sana Al-Wahhaab, kwa sababu unapomshukuru basi Yeye Allaah (‘Azza wa Jalla) Anaahidi kumwongezea yule anayemshukuru kama Anavyosema:

 

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكُمْ لَئِن شَكَرْتُمْ لَأَزِيدَنَّكُمْ ۖ وَلَئِن كَفَرْتُمْ إِنَّ عَذَابِي لَشَدِيدٌ﴿٧﴾

Na pindi Alipotangaza Rabb wenu: Ikiwa mtashukuru, bila shaka Nitakuzidishieni (Neema Zangu), na mkikufuru, basi hakika Adhabu Yangu ni kali. [Ibraahiym (14:7)]

 

Na yule anayetunukiwa, anapaswa kumshukuru aliyemtunukia japo kama mtoaji huyo hakutaraji kushukuriwa, na pia amuombee duaa Al-Wahhaab Amzidishie kumtunukia khayraat.

 

 

2-Usitumie neema yoyote ile au Aliyokutunukia Al-Wahhaab katika maasi, au katika ubadhirifu, bali tumia katika utii Wake na katika mambo yenye kumridhisha Yeye Al-Wahhaab, yakiwemo katika kunusuru Dini Yake, na mambo yote mengineyo ambayo yatarudi kukupatia malipo mema duniani na Aakhirah.

 

 

3-Unapotoa swadaqah zako kwa mafuqara na masaakini, toa kwa mapenzi na bila ya kutaraji malipo au shukurani kutoka kwako kwa kumbuka kwamba Al-Wahhaab Ndiye Aliyekujaalia mali hiyo.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

وَيُطْعِمُونَ الطَّعَامَ عَلَىٰ حُبِّهِ مِسْكِينًا وَيَتِيمًا وَأَسِيرًا﴿٨﴾ إِنَّمَا نُطْعِمُكُمْ لِوَجْهِ اللَّـهِ لَا نُرِيدُ مِنكُمْ جَزَاءً وَلَا شُكُورًا﴿٩﴾

 

Na wanalisha chakula, juu ya kuwa wao wanakipenda, masikini na mayatima na mateka. Hakika sisi tunakulisheni kwa ajili ya Wajihi wa Allaah, hatukusudii kutoka kwenu jazaa wala shukurani. [Al-Insaan (76:8-9)]

 

 

 

4-Pendelea kutunukia watu kwa zawadi kwani inajenga mapenzi kama alivyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللهُ عَنْهُ عَنِ النَّبِيِّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ قَالَ: {تَهَادُوْا تَحَابُّوا} رَوَاهُ اَلْبُخَارِيُّ فِي " اَلْأَدَبِ اَلْمُفْرَدِ " وَأَبُو يَعْلَى بِإِسْنَادٍ حَسَن

Amesimulia Abuu Hurayrah  (Radhwiya-Allaahu ‘anhu). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Peaneni zawadi   mutapendana.” [Al-Bukhaariy katika Al-Adab Al-Mufrad na Abuu Ya’laa ameipokea kwa Isnaad Hasan]

 

 

 

5-Omba duaa ifuatayo katika Qur-aan ambayo ni miongoni mwa sifa za Waja wa Ar-Rahmaan:

 

وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا ﴿٧٤﴾

Na wale wanaosema: Rabb wetu! Tutunukie katika wake zetu na dhuria wetu viburudisho vya macho yetu, na Tujaalie kuwa waongozi kwa wenye taqwa. [Al-Furqaan (25:74)]

 

Na daima unapoomba ahli au kizazi basi fuata mfano wa Nabiy Zakariyyaa (‘alayhis-salaam) alipoomba kizazi chema:

 

 

 هُنَالِكَ دَعَا زَكَرِيَّا رَبَّهُ ۖ قَالَ رَبِّ هَبْ لِي مِن لَّدُنكَ ذُرِّيَّةً طَيِّبَةً ۖ إِنَّكَ سَمِيعُ الدُّعَاءِ ﴿٣٨﴾

Hapo hapo Zakariyyaa akamwomba Rabb wake, akasema: Rabb wangu! Nitunukie kutoka Kwako kizazi chema, hakika Wewe Ni Mwenye Kusikia duaa yangu. [Aal-‘Imraan (3:38)]

 

 

Na Al-Wahhaab Anapokutunukia kizazi ahli na kizazi chema, basi usiache kumshukuru. Tazama mfano mwema wa Nabiy Ibraahiym (‘alayhis-salaam) alipoomba:

 

 

الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي وَهَبَ لِي عَلَى الْكِبَرِ إِسْمَاعِيلَ وَإِسْحَاقَ ۚ إِنَّ رَبِّي لَسَمِيعُ الدُّعَاءِ ﴿٣٩﴾

AlhamduliLLaah (Himdi Anastahiki Allaah), Ambaye Amenitunukia juu ya umri mkubwa wangu Ismaa’iyl na Is-haaq. Hakika Rabb wangu bila shaka Ni Mwenye Kusikia duaa yangu. [Ibraahiym (14:39)]

 

 

Na kumbuka kwamba neema yoyote ile, au kizazi chema ulichotunukiwa, ni kutoka kwa Al-Wahhaab, basi chunga ulichajaaliwa kutunukiwa na Al-Wahhaab kwa kulea kizazi hicho kwa malezi ya Kiislamu na katika utiifu wa Allaah. Na kamwe usijigambe kwa kutunukiwa kizazi chema, bali omba duaa Athibitishe kizazi hicho katika imaan na taqwa, na nyenyekea kwa Al-Wahhaab.

 

 

6-Unapojaaliwa kutunukiwa kizazi cha kike pekee, basi shukuru na kubali Qadar ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), na sio kuudhika na mke au kumkasirikia, kama wanavyoudhika baadhi ya watu juu ya wake zao kuwa wanazaa watoto wa kike pekee ilhali si yeye mwenye uwezo wa kuchagua cha kuzaa, bali ni Al-Wahaab Ambaye Ndiye Mwenye kuruzuku jinsia ya kizazi Atakacho kama Anavyosema:

 

 

لِّلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ يَخْلُقُ مَا يَشَاءُ ۚ يَهَبُ لِمَن يَشَاءُ إِنَاثًا وَيَهَبُ لِمَن يَشَاءُ الذُّكُورَ﴿٤٩﴾

Ni wa Allaah Pekee ufalme wa mbingu na ardhi. Anaumba Atakacho. Humtunukia Amtakaye wana wa kike, na Humtunukia Amtakaye wana wa kiume. [Ash-Shuwraa (42:49)]

 

 

7-Tosheka, ridhia na kinaika na ulichutunikiwa na Al-Wahhaab. Na omba duaa ifuatayo aliyokuwa akiomba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 اللَّهُمَّ قَنِّعْنَي بِمَا رَزَقْتَنَي وَبَارِكْ لِي فِيهِ وَاخْلُفْ عَلَيَّ كُلَّ غَائِبَةٍ لِي بِخَيرٍ

Ee Allaah, nikinaishe kwa Ulivyoniruzuku, na nibarikie ndani yake, na nibadilishie kila kilichofichika (kiovu) kwa kheri.

 

[Al-Haakim na ameipa daraja ya Swahiyh na ameikubali Adh-Dhahabiy (1/510). Ibn Hajar Al-‘Asqalaaniy ameipa daraja ya Hasan katika Al-Futuhaat Ar-Rabbaaniyah (4/384)]

 

 

[1] Hukma:

 

Kumjua Allaah na Mipaka Yake, ilimu nyingi ya Dini yenye ufaqihi, ufahamu wa kina, busara, na utambuzi wa Sharia (hukumu) ya halali na haramu, na uwezo wa kuhukumu baina ya watu.

 

[2] Tafsiyr Atw-Twabariy (3/125).

 

 

 

Share