036-Majina Ya Allaah Mazuri Na Sifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-KABIYR
أسماء الله الحسنى وصفاته
Majina Ya Allaah Mazuri Na Sifa Zake
الْكَبِير
036-Al-KABIYR
Al-Kabiyr: Mkubwa Wa Dhati Vitendo Na Sifa
Jina hili limekariri katika Qur-aan mara sita na limetajwa pamoja na Al-‘Aliyyu au na Al-Muta’aal. Baadhi ya Kauli Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni zifuatazo:
وَلَا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ عِندَهُ إِلَّا لِمَنْ أَذِنَ لَهُ ۚ حَتَّىٰ إِذَا فُزِّعَ عَن قُلُوبِهِمْ قَالُوا مَاذَا قَالَ رَبُّكُمْ ۖ قَالُوا الْحَقَّ ۖ وَهُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ ﴿٢٣﴾
Na wala haitofaa shafaa’ah (uombezi) mbele Yake isipokuwa kwa yule Aliyempa idhini. Mpaka litakapoondolewa fazaiko nyoyoni mwao watasema: Amesema nini Rabb wenu? Watasema: Ya haki, Naye Ni Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mkubwa Kabisa. [Sabaa (34:23)]
عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْكَبِيرُ الْمُتَعَالِ ﴿٩﴾
Mjuzi wa ghaibu na dhahiri, Mkubwa kabisa Mwenye Uluwa. [Ar-Ra’d (13:9)]
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Tabaaraka ni Mkubwa Asiye ya ukomo:
i-Mkubwa kwa Dhati Yake hakuna zaidi yake kwa ukubwa. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٦٧﴾
Na hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria. Na hali ardhi yote Ataikamata Mkononi Mwake Siku ya Qiyaamah, na mbingu zitakunjwa kwa Mkono Wake wa kulia. Subhaanahu wa Ta’aalaa (Utakasifu ni wa Allaah na Ametukuka kwa ‘Uluwa) kutokana na yale yote wanayomshirikisha. [Az-Zumar (39:67)]
ii-Yeye ni Mkubwa kwa Sifa Zake, Utukufu, Hana mfano Wake katika hali yoyote ile. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾
Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ni Mwenye Kusikia yote, Mwenye Kuona yote. [Ash-Shuwraa (42:11)]
iii-Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Mkubwa kwa matendo Yake, ni Mkubwa kwa waja Wake, wanashuhudia utukufu wa matendo Yake. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ﴿٥٧﴾
Bila shaka uumbaji wa mbingu na ardhi ni mkubwa zaidi kuliko uumbaji wa watu, lakini watu wengi hawajui. [Ghaafir (40:57)]
iv-Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ana Ukubwa, Utukufu, Uadhimu, Ujalali mbinguni na ardhini, Anasema:
وَلَهُ الْكِبْرِيَاءُ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۖ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ﴿٣٧﴾
Na Ukubwa, Uadhama, Ujalali ni Wake Pekee mbinguni na ardhini. Naye Ndiye Mwenye Enzi ya Nguvu Asiyeshindika, Mwenye Hikmah wa yote. [Al-Jaathiyah (45:37)]
v-Aliye Mkuu kabisa na juu kwa kila chenye kuabudiwa asiyekuwa Yeye, Hakubali aabudiwe asiyekuwa Yeye. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَـٰهٌ وَفِي الْأَرْضِ إِلَـٰهٌ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ﴿٨٤﴾
Na Yeye Ndiye Muabudiwa wa haki mbinguni na ardhini pia (Ndiye Huyo Huyo) Ilaah. Naye Ndiye Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa yote. [Az-Zukhruf (43:84)]
Na Anasema pia:
ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ الْبَاطِلُ وَأَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْعَلِيُّ الْكَبِيرُ ﴿٦٢﴾
Hivyo ni kwa kuwa Allaah Ndiye wa Haki, na kwamba vile wanavyoomba badala Yake ndiyo batili, na kwamba Allaah Ndiye Mwenye ‘Uluwa Uliotukuka, Mkubwa Kabisa. [Al-Hajj (22:62)]
vi-Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ni Mkubwa, Mwenye kuwafanya waja Wake Akitakacho, katika maamrisho na makatazo, kwa ukamilifu na hekima na uadilifu, halihukumiwi jambo bila Yake, wala hukumu Yake hairejeshwi na yeyote ulimwenguni.
Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah Al-Kabiyr:
1-Kumbuka kwamba Kumtukuza Al-Kabiyr kumethibiti katika hali nyingi mno, ambazo haiwezekani kuzitaja katika makala fupi kama hizi! Basi hebu kumbuka chache zifautaz, tukianza na Adhana ya Swalaah ambayo inaanzwa kwa kumtukuza Al-Kabiyr. Basi ee ndugu Muislamu, itikia adhana kwa kutamka kama anavyotamka Mwadhini, kisha itikia wito huo wa Swalaah, ukumbuke kuwa Al-Kabiyr Ndiye Mkubwa kuliko shughuli yoyote ile uliyonayo hapo inapoadhiniwa. Basi mwelekee Al-Kabiyr katika wito Wake huo wa Swalaah.
2-Mtukuze Al-Kabiyr katika duaa ya kufungulia Swalaah, ni kama ilivyokuja katika Hadiyth ifuatayo:
عَنِ ابْنِ عُمَرَ، قَالَ بَيْنَمَا نَحْنُ نُصَلِّي مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم إِذْ قَالَ رَجُلٌ مِنَ الْقَوْمِ اللَّهُ أَكْبَرُ كَبِيرًا وَالْحَمْدُ لِلَّهِ كَثِيرًا وَسُبْحَانَ اللَّهِ بُكْرَةً وَأَصِيلاً . فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم " مَنِ الْقَائِلُ كَلِمَةَ كَذَا وَكَذَا " . قَالَ رَجُلٌ مِنَ الْقَوْمِ أَنَا يَا رَسُولَ اللَّهِ . قَالَ " عَجِبْتُ لَهَا فُتِحَتْ لَهَا أَبْوَابُ السَّمَاءِ . قَالَ ابْنُ عُمَرَ: فَمَا تَرَكْتُهُنَّ مُنْذُ سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم يَقُولُ ذَلِكَ
Amesimulia Ibn ‘Umar (Radhwiya-Allaahu ‘anhumaa): Tulipokuwa tunaswali pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), mtu mmoja alisema:
اللَّهُ أَكْبَرُ كَبِيرًا وَالْحَمْدُ لِلَّهِ كَثِيرًا وَسُبْحَانَ اللَّهِ بُكْرَةً وَأَصِيلاً
Allaah ni Mkubwa, na Himdi Anastahiki Allaah kwa wingi, na Ametakasika Allaah asubuhi na jioni.
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema (baada kumaliza Swalaah): “Nani aliyesema maneno hayo?” Mtu mmoja akasema kuwa ni yeye. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “(Maneno yake) yamenishangaza kwani mbingu zimefunguliwa kwayo.” Ibn ‘Umar akasema: Sikuacha kusema maneno haya tangu nilipomsikia Rasulis akisema hivyo. [Muslim]
3-Ndani ya Swalaah kuna kumtukuza Al-KAbiyr katika kila kitendo cha Swalaah, unapotaka kurukuu, kusujudu, kuinuka na kadhalika, basi kumbuka Utukufu na Ukubwa wa Al-Kabiyr na kwamba hakuna mwenye Ukubwa zaidi Yake.
4-Hali kadhalika kumtukuza Al-Kabiyr hakika kumethibiti katika hali nyingi mno, kama vile katika kupanda kilima cha Swafaa na Marwa, au katika kupanda bonde lolote lile, au katika kuanza safari na kipando cha safari, katika kurudi safari, na katika hali mbalimbali, na imeamrishwa kumtukuza Al-Kabiyr katika masiku ya mwanzo ya mwezi wa Dhul-Hijjah. Kwa hiyo usiache kumtukuza kwa wingi katika masiku hayo matukufu.
5-Mtukuze Al-Kabiyr katika hali nyenginezo nyingi, kama katika Adhkaar za asubuhi na jioni.
6-Mtukuze pia Al-Kabiyr kama Anavyoamrisha katika Kauli Zake:
وَرَبَّكَ فَكَبِّرْ﴿٣﴾
Na Rabb wako mtukuze. [Al-Muzzammil (74:3)]
Mtukuze pia Al-Kabiyr kwa kumtakasa na shirki na maovu yote:
وَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي لَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَلَمْ يَكُن لَّهُ وَلِيٌّ مِّنَ الذُّلِّ ۖ وَكَبِّرْهُ تَكْبِيرًا ﴿١١١﴾
Na sema: AlhamduliLLaah (Himidi Anastahiki Allaah) Ambaye Hakujifanyia mwana na wala Hakuwa na mshirika katika ufalme, na wala Hakuwa dhalili hata Awe (Anahitaji) mlinzi (na msaidizi), na mtukuze matukuzo makubwa kabisa. [Al-Israa (17:111)]
7-Ikiwa umejaaliwa cheo au mamlaka fulani, basi usitakabari na kuwadharau wengine, wala usiwe na kibri, wala usiwakhofishe watu au kuwadhulumu! Kumbuka kuwa Al-Kabiyr Ndiye Mkubwa kwa Sifa na Matendo! Na yeyote yule anayedhululmiwa au anayekhofu kudhulumiwa na mwenye cheo au mamlaka fulani, basi asijali, bali na aombe duaa ifuatayo iliyothibiti katika hali hiyo:
الله أكْبَر، الله أعَزُّ مِنْ خَلْقِهِ جَمِيْعاً، الله أعَزُّ مِمَّا أخَافُ وَأحْذَر، أعُوذُ بِاللهِ الَّذِي لاَ إِلَهَ إِلاَّ هُوَ، الْمُمْسِكِ السَّمَوَا تِ السَّبْعِ أَنْ يَقَعْنَ عَلَى الأَرْضِ ِإلاَّ بِإِذْنِهِ، مِنْ شَرِّ عَبْدِكَ (فلان) وَجُنُوْدِهِ وَأَتْبَاعِهِ وَأَشْيَاعِهِ، مِنَ اْلجِنِّ والإِنْسِ، اَلَّلهُمَّ كُنْ لِيْ جَاراً مِنْ شَرِّهِمْ، جَلَّ ثَنَاؤُكَ وَعَزَّ جَارُكَ، وَتَبَارَكَ اسْمُكَ، وَلاَ إلَهَ غَيْرُكَ
Allaah ni Mkubwa, Allaah, ni Mwenye nguvu na Mshindi kuliko viumbe Vyake vyote. Allaah ni Mwenye nguvu na Mshindi kuliko kila nikiogopacho na kujihadhari. Najikinga kwa Allaah Ambaye hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye tu Ambaye Ameshikilia mbingu saba ili zisiangukie ardhi ila kwa idhini Yake, kutokana na shari ya mja (fulani - mtaje mtu unayemhofu) na majeshi yake, na wanaomfuata, na wafuasi wake miongoni mwa majini na watu. Ee Allaah, kuwa Mlinzi wangu kutokana na shari yao. Zimetukuka sifa Zako na Umehishimika ulinzi Wako na Limebarikika Jina Lako, na hapana mwabudiwa wa haki ghairi Yako [Al-Bukhaariy fiy Adabil-Mufrid (708) na ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Adab Al-Mufrad (546)].
8-Usiwe na kibri kwa kukataa kutekeleza maamrisho ya Al-Kabiyr. Tazama dhambi ya Ibilisi; alikataa kumsujudia Aadam kwa sababu ya kibri. Basi tazama juu na ufikirie kuwa Al-Kabiyr Anakutazama na Anajua kibri chako, basi je, unaweza kuthubutu kutenda maasi ilhali Al-Kabiyr Anakuona?
