035-Majina Ya Allaah Mazuri Na Sifa Zake أسماء الله الحسنى وصفاته: AL-QAAHIR, AL-QAHHAAR

 

 

 

أسماء الله الحسنى وصفاته

Majina Ya Allaah Mazuri Na Sifa Zake

 

 

Alhidaaya.com

 

 

الْقَاهِر- الْقَهَّار

034-Al-Qaahir, Al-Qahhaar

 

 

 

 

Al-Qaahir, Al-Qahhaar: Mwenye Kuteza, Nguvu, Mshindi, Mwenye Kudhibiti, Asiyepingika

 

 

Qahar ni neno lenye maana ya kushinda kitu, kuwa juu kabisa.

 

 

Tofauti kati ya Al-Qaahir na Al-Qahhaar:   

 

Al-Qaahir: Ni Mwenye shani ya kuwa juu kabisa, Mwenye Nguvu na Uwezo juu ya waja Wake wote kwa tofauti zao.

 

Al-Qahhaar: Ni Aliyezidisha kufanya haya.

 

Miongoni mwa Aayah zilizotajwa Majina haya:

 

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۚ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْخَبِيرُ ﴿١٨﴾

Naye Ndiye Aliyedhibiti vyote chini ya Mamlaka Yake Aliye juu ya Waja Wake. Naye Ndiye Mwenye Hikmah wa yote, Mjuzi wa Khabari za dhahiri na siri. [Al-An’aam (6:18)]

 

قُلْ إِنَّمَا أَنَا مُنذِرٌ ۖ وَمَا مِنْ إِلَـٰهٍ إِلَّا اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿٦٥﴾

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Hakika mimi ni mwonyaji tu. Na hakuna Muabudiwa wa haki yeyote isipokuwa Allaah Mmoja Pekee, Asiyepingika. [Swaad (38:65)]

 

 

Al-Qahhaar Yeye ni zaidi, Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ndiye Aliyewashinda majabari wasio na hesabu. Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Humshinda kila atakayeshindana Naye. Aliwaangamiza kaumu ya Nuwh, Aliwashinda kina ‘Aad, Thamuwd na Akawashinda na kuwabwaga baharini Firawni na Haaman, Nimruwdh (mfalme dhalimu aliyetakabari) Abu Jahl (kafiri mkuu wa ki-Quraysh) na wengineo kama yeye, na watu wengineo waliotakabari, wasio na idadi.

 

Allaah (Tabaaraka wa Ta'aalaa) ni Al-Qaahir, Al-Qahhaar kwa waliomo ardhini na mbinguni:

 

 

i-Mwenye kutenza na kudhalilisha viumbe vyote vikawa chini ya uweza Wake na matakwa Yake.  Hakitokei chochote ila kwa idhini Yake, wala hakitulii kitu ila kwa idhini Yake vile vile.

 

 

ii-Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hutenza nguvu watu wa mbinguni na ardhini.  

 

 

iii-Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Yuko juu ya waja Wake kwa dhati Yake, na juu kwa utawala Wake na juu kwa kushinda na kwa sehemu na uwezo:

 

وَهُوَ الْقَاهِرُ فَوْقَ عِبَادِهِ ۖ وَيُرْسِلُ عَلَيْكُمْ حَفَظَةً حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَكُمُ الْمَوْتُ تَوَفَّتْهُ رُسُلُنَا وَهُمْ لَا يُفَرِّطُونَ ﴿٦١﴾

Naye Ndiye Aliyedhibiti vyote chini ya Mamlaka Yake, Aliye juu ya Waja Wake.  Na Anakutumieni Malaika wachungaji wadhibiti, hata yanapomfikia mmoja wenu mauti, Wajumbe Wetu humfisha, nao hawafanyi taksiri. [Al-An’aam (6:61)]

 

 

iv-Yeye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewashinda wenye inadi kwa Alichowasimamishia Aayah na dalili nyingi, kuhusu Tawhiyd Yake na kuwa ni Yeye Pekee tu Ndiye Anayestahiki kuabudiwa ilivyokuja katika Qur-aan:

 

يَا صَاحِبَيِ السِّجْنِ أَأَرْبَابٌ مُّتَفَرِّقُونَ خَيْرٌ أَمِ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ﴿٣٩﴾

Enyi masahibu wangu wawili wa jela! Je, miola wengi wanaofarakana ni bora au Allaah Mmoja Pekee, Asiyepingika? [Yuwsuf (12:39)]

 

 

v-Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Huwashinda waja Wake kwa kuwafufua waja Wake na kuwahesabu na kuwasimamishia haki na mizani ya uadilifu, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَوْمَ تُبَدَّلُ الْأَرْضُ غَيْرَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتُ ۖ وَبَرَزُوا لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ﴿٤٨﴾

Siku ardhi itakapobadilishwa kuwa ardhi nyingine na mbingu pia, na (viumbe wote) watahudhuria kwa Allaah Mmoja Pekee, Asiyepingika. [Ibraahiym (14:48)]

 

 

 

Faida, Mafunzo Tuyapatayo Na Jinsi Ya Kufanyia Kazi Jina Hili La Allaah Al-Qaahir, Al-Qahhaar:

 

 

1-Zingatia Uwezo na Nguvu za Al-Qaahir, Al-Qahhaar jinsi Anavyoendesha mambo na Anavyosakhirisha (kutiisha vikubali kufanya Atakavyo) Alivyoviumba ardhini na mbinguni, mambo ambayo hakuna Awezaye kuyafanya kama Anavyosema:

 

 

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ سَخَّرَ لَكُم مَّا فِي الْأَرْضِ وَالْفُلْكَ تَجْرِي فِي الْبَحْرِ بِأَمْرِهِ وَيُمْسِكُ السَّمَاءَ أَن تَقَعَ عَلَى الْأَرْضِ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِالنَّاسِ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٦٥﴾

Je, huoni kwamba Allaah Amevitiisha kwa ajili yenu vile vilivyomo katika ardhi na merikebu zipitazo baharini kwa Amri Yake. Na Anazuia mbingu zisianguke juu ya ardhi isipokuwa kwa Idhini Yake. Hakika Allaah kwa watu ni Mwenye huruma mno, Mwenye Kurehemu. [Al-Hajj (22:65)]

 

Na pia:

 

اللَّـهُ الَّذِي رَفَعَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۖ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ يُفَصِّلُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُم بِلِقَاءِ رَبِّكُمْ تُوقِنُونَ ﴿٢﴾

Allaah Ambaye Ameinua mbingu bila ya nguzo mnaziona, kisha Akawa juu ya ‘Arsh. Na Akavitiisha jua na mwezi, vyote vinakwenda mzunguko hadi muda maalumu uliokadiriwa. Anadabiri mambo, Anazifasili waziwazi Aayaat (Ishara, Dalili) ili mpate kuwa na yakini ya kukutana na Rabb wenu. [Ar-Ra’d (13:2)]

 

 

 

2--Zingatia pia Nguvu na Uwezo Wake jinsi Anavyozuia madhara kuwafika waja Wake kama Alipojaalia moto usimuunguze Nabiy Ibraahiym (‘alayhis-salaam), nyangumi asimmeze Nabiy Yuwnus (‘alayhis-salaam), kisu kimsichinje Nabiy Ismaa’iyl (‘alayhis-salaam), makafiri Quraysh wasimpate Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  alipojificha ndani ya pango pamoja na swahibu wake Abu Bakr (Radhwiya-Allaahu ‘anhu), na mengi mengineyo.

 

 

3-Usitumie nguvu na uwezo wako kuwakandamiza walio dhaifu kama yatima, Anakataza hayo Al-Qaahir, Al-Qahhaar katika Kauli Zake:

 

فَأَمَّا الْيَتِيمَ فَلَا تَقْهَرْ ﴿٩﴾ وَأَمَّا السَّائِلَ فَلَا تَنْهَرْ ﴿١٠﴾

 

Kwa hivyo basi yatima usimuonee. Na ama mwombaji, basi usimkaripie. [Adhw-Dhwuhaa (93:9-10)]

 

 

4-Madhalimu watahadhari Siku ya Qiyaamah, Siku ambayo madhalimu watahesabiwa na Al-Qahhaar kwa dhulma zao, na kwa kutakabari kwao kwa kuwa walikuwa duniani wana nguvu na uwezo wakawakandamiza na kuwadhulumu waliodhaifu. Siku hiyo adhimu hakutakuwa na mwenye nguvu wala uwezo wala hapatakuwa na ufalme wowote ule, bali Al-Qahhaar Atawaondosha viumbe wote wakiwemo waliojifanya majabari duniani. Basi hakuna atakayebakia isipokuwa Yeye Al-Qahhaar Pekee Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

 

 

يَوْمَ هُم بَارِزُونَ ۖ لَا يَخْفَىٰ عَلَى اللَّـهِ مِنْهُمْ شَيْءٌ ۚ لِّمَنِ الْمُلْكُ الْيَوْمَ ۖ لِلَّـهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ﴿١٦﴾ الْيَوْمَ تُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ ۚ لَا ظُلْمَ الْيَوْمَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَرِيعُ الْحِسَابِ﴿١٧﴾

Siku watakayotokeza wao, hakitofichika kitu chochote chao kwa Allaah. Ufalme ni wa nani leo (Allaah Mwenyewe Atajijibu): Ni wa Allaah Pekee Mmoja, Asiyepingika.  Leo kila nafsi italipwa kwa yale iliyoyachuma, hakuna dhulma leo!  Hakika Allaah Ni Mwepesi wa Kuhesabu. [Ghaafir (40:16-17)]

 

 

Na katika Hadiyth:

 

وَحَدَّثَنَا أَبُو بَكْرِ بْنُ أَبِي شَيْبَةَ، حَدَّثَنَا أَبُو أُسَامَةَ، عَنْ عُمَرَ بْنِ حَمْزَةَ، عَنْ سَالِمِ، بْنِ عَبْدِ اللَّهِ أَخْبَرَنِي عَبْدُ اللَّهِ بْنُ عُمَرَ، قَالَ قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم ‏ "‏ يَطْوِي اللَّهُ عَزَّ وَجَلَّ السَّمَوَاتِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ثُمَّ يَأْخُذُهُنَّ بِيَدِهِ الْيُمْنَى ثُمَّ يَقُولُ أَنَا الْمَلِكُ أَيْنَ الْجَبَّارُونَ أَيْنَ الْمُتَكَبِّرُونَ ثُمَّ يَطْوِي الأَرَضِينَ بِشِمَالِهِ ثُمَّ يَقُولُ أَنَا الْمَلِكُ أَيْنَ الْجَبَّارُونَ أَيْنَ الْمُتَكَبِّرُونَ ‏"‏ ‏.‏

 

Amesimulia ‘Abdullaah Bin ‘Umar (Radhwiya-Allaahu ‘anhumaa): Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: Allaah ('Azza wa Jalla)  Atakunja mbingu zote Siku ya Qiyaamah kisha Atazikamata Mkononi Mwake wa kuume kisha Atasema: Mimi Ndiye Mfalme. Wako wapi waliojifanya majabari? Wako wapi waliotakabari? Kisha Atazikunja ardhi kwa Mkono Wake wa kushoto na Atasema: Mimi Ndiye Mfalme. Wako wapi waliojifanya majabari? Wako wapi waliotakabari?” [Muslim]

 

 

5-Unapokosa usingizi usiku ukawa unageukageuka, soma duaa ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo, yenye kutaja Al-Qahhaar kwani Yeye Ndiye Mweza kukuwezesha kupata usingizi:

 

 

عن عائشة أم المؤمنين رضي الله عنها ان رسولُ اللهِ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم إذا تضوَّر مِن اللَّيلِ قال: ((لا إلهَ إلَّا اللهُ الواحدُ القهَّارُ ربُّ السَّمواتِ والأرضِ وما بينَهما العزيزُ الغفَّارُ))

 

Amesimulia Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya-Allaahu ‘anhaa): Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alipokuwa akihangaika kupata usingizi usiku akisema:

 

لا إِلـهَ إِلاّ اللهُ الـواحِدُ القَهّـار، رَبُّ السَّـمواتِ وَالأرْضِ وَما بَيْـنَهـما، العَزيـزُ الغَـفّار

Laa ilaaha illa-Allaahul-Waahidul-Qahhaar. Rabbus-samawaati wal ardhwi wamaa baynahumaal-’Aziyzul-Ghaffaar.

 

Hapana mwabudiwa wa haki ila Allaah  Al-Waahid (Mmoja Pekee) Al-Qahhaar (Mshindi Mwenye kudhibiti na kudhalilisha). Rabb wa mbingu na ardhi na vilivyo kati yake, Al-’Aziyz (Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika daima) Al-Ghaffaar (Mwingi wa kughufuria)) [An-Nasaaiy katika As-Sunan Al-Kubraa (10700), Swahiyh Ibn Maajah (5530), Swahiyh Al-Jaami’ (4693), Al-Haakim na ameisahihisha Adh-Dhahabiy (1/540), An-Nasaaiy katika ‘Amal Al-Yawm wal-Laylah (864) na Ibn As-Sunniy katika ‘Amal Al-Yawm wal-Laylah (757)]

 

 

 

 

Share