01-Nuru Ya Qur-aan: Al-Isti’aadhah
Nuru Ya Qur-aan
01: "الإِسْتِعَاذَةُ" Al-Isti’aadhah (A’uwdhu Bil Laahi Minash-Shaytwaan Ar Rajiym)
"الإِسْتِعَاذَةُ" (Al-Isti’aadhah), ni kuomba kinga kutokana na Neno Lake Taalaa: "أَعُوْذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيْمِ".
Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Ametuwekea neno hili ili liwe ni njia kwa mwanadamu kuweza kujilinda na shetani na kumweka mbali naye ili asiweze kusababisha aina yoyote ya madhara kwake.
Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Anatuambia:
"وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ● وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ"
“Na sema: Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na udokezi wa mashaytwaan • Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie”. [Al-Muuminuwna: 97-98]
Na Anatuambia tena:
"فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ"
“Unaposoma Qur-aan basi (kwanza) omba kinga kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa”. [An Naml: 98].
Kuna aya nyingi zinazozungumzia suala hili na zote zinaonyesha juu ya umuhimu wa kujilinda na shari za kiumbe huyu ambaye ni adui mkubwa wa watu wote.
Hivyo basi, maana ya (Isti’aadhah) ni kujilinda au kukimbilia kwa mwenye kutoa hifadhi kutokana na jambo lenye kuogopewa. Mfano wa maana hiyo ni Kauli Yake Ta’alaa:
"وَقَالَ مُوسَىٰ إِنِّي عُذْتُ بِرَبِّي وَرَبِّكُم مِّن كُلِّ مُتَكَبِّرٍ لَّا يُؤْمِنُ بِيَوْمِ الْحِسَابِ"
“Na Muwsaa akasema: Hakika mimi najikinga kwa Rabb wangu na Rabb wenu, kutokana na kila mwenye kutakabari asiyeamini Siku ya Hesabu”. [Ghaafir: 27]
Miundo Ya Isti’aadhah:
Tamshi hili la isti’aadhah lina miundo kadhaa, nayo ni kama ifuatavyo:
1- أعُوْذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيْمِ
“Najilinda kwa Allaah kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa”.
Ni kutokana na Kauli Yake Ta’alaa:
"فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ"
“Unaposoma Qur-aan, basi (kwanza) omba kinga kwa Allaah dhidi ya shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa”. [An-Nahl: 97].
2- أَعُوْذُ بِاللهِ السَّمِيْعِ العَلِيْمِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيْمِ
“Najilinda kwa Allaah Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa”.
Ni kutokana na Kauli Yake Ta’alaa:
"وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۚ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ"
“Na pindi utakapokuchochea uchochezi kutokana na shaytwaan, basi omba kinga kwa Allaah. Hakika Yeye Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote”. [Al-A’araaf: 200]
3- أَعُوْذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيْمِ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيْعُ العَلِيْمُ"
“Najlinda kwa Allaah kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa, hakika Yeye (Allaah) Ni Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote”.
Tamko hili limechanganya aya mbili zilizotangulia.
4- أَعُوْذُ بِاللهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيْمِ مِنْ نَفْخِهِ، وَنَفْثِهِ، وَهَمْزِهِ
“Najilinda kwa Allaah na shetani aliyewekwa mbali na rehma za Allaah kutokana na kiburi chake, mashairi yake, na wasiwasi wake”.
Kwa maana, najilinda kwa Allaah shetani asinipulizie sifa ya kuwa na kibri, wala kunikoroga nikatunga mashairi potoshi, wala kunishawishi akanitia kwenye upotovu.
Matamshi haya yote yanafaa kisheria kutokana na kuthibiti kwake kwenye Qur-aan na Sunnah.
Isti’aadhah inatubainishia uhakika wa mwanadamu kwamba ni kiumbe mhitaji, kiumbe dhaifu, na kiumbe mwenye uwezo mdogo kabisa. Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Anaujua udhaifu huu wa mwanadamu na Anajua kwamba shetani ndiye adui wake mkubwa anayemwandama kwa ushawishi, na kumuingiza kwenye maasia, machafu na madhara mengineyo katika kipindi cha masaa 24. Na mwanadamu kutokana na udhaifu wake huu, ni vigumu mno kukabiliana na ushawishi huu wa shetani usiokoma. Na hapa ndipo unapokuja umuhimu wa isti’aadha kwa Mwislamu ambapo anakimbilia kwa Allaah Mtukufu ili Amlinde kutokana na uadui huu, na ili aweze kushikamana ipasavyo na Njia ya Allaah Mtukufu iliyonyooka. Yeye Pekee Ndiye Mweza wa kumshinda shetani na kumwepushia Mwislamu shari zake na adha zake.
Bila shaka kumshinda shetani kunakuwa kwa kumtii Allaah, kumdhukuru na kunyooka sawasawa. Mwislamu anawajibika kupambana na shetani kwa njia zote ambazo Allaah Ameziweka, kwa kuwa shetani ni adui mbaya zaidi kuliko adui wa kibinadamu anayeonekana. Adui anayeonekana ni rahisi kukabiliana naye hata kama ana nguvu. Ama asiyeonekana, bila shaka inakuwa ni vigumu mno kukabiliana naye. Adui wa kibinadamu anawezekana kufanya naye mazungumzo ya suluhu, anaweza kukabiliwa kwa mujibu wa nguvu zake kwa mikakati tofauti na pia uadui wake unaweza kumalizwa kwa njia ya kidiplomasia. Allaah Anatuambia:
"وَلَا تَسْتَوِي الْحَسَنَةُ وَلَا السَّيِّئَةُ ۚ ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ فَإِذَا الَّذِي بَيْنَكَ وَبَيْنَهُ عَدَاوَةٌ كَأَنَّهُ وَلِيٌّ حَمِيمٌ"
“Na wala haulingani sawa wema na uovu. Zuia (uovu) kwa ambalo ni zuri zaidi. Hapo utamkuta yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui, kama ni rafiki mwandani”. [Fusswilat: 34]
Hivyo basi, ni wajibu kwa Mwislamu ajilinde daima kwa Allaah kutokana na shari za kiumbe huyu akichukua kwa hilo kigezo chema toka kwa Manabii wa Allaah pamoja na watu wema ambao kutokana na kujilinda kwao huku, Allaah Aliwaepushia shari za shetani na kuwafanikishia mambo yao mema waliyokuwa wakiyatarajia. Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Akituelezea kuhusu Nabii Nuhu ‘Alayhis Salaam Anatuambia:
"قَالَ رَبِّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ أَنْ أَسْأَلَكَ مَا لَيْسَ لِي بِهِ عِلْمٌ ۖ وَإِلَّا تَغْفِرْ لِي وَتَرْحَمْنِي أَكُن مِّنَ الْخَاسِرِينَ"
“Akasema: Ee Rabb wangu! Hakika mimi najikinga Kwako kukuomba yale nisiyo na elimu nayo. Na Usiponighufuria na Ukanirehemu, nitakuwa miongoni mwa waliokhasirika”. [Hud: 47]
Na hapo Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Alimpa mambo mawili ambayo ni amani na Baraka kama linavyoelezea Neno Lake Ta’alaa:
"قِيلَ يَا نُوحُ اهْبِطْ بِسَلَامٍ مِّنَّا وَبَرَكَاتٍ عَلَيْكَ وَعَلَىٰ أُمَمٍ مِّمَّن مَّعَكَ ۚ وَأُمَمٌ سَنُمَتِّعُهُمْ ثُمَّ يَمَسُّهُم مِّنَّا عَذَابٌ أَلِيمٌ"
“Pakasemwa: Ee Nuwh! Teremka (jahazini) kwa salama kutoka Kwetu na baraka nyingi juu yako, na juu za umati zilizo pamoja na wewe. Na umati Tutakazozistarehesha, kisha zitawagusa kutoka Kwetu adhabu iumizayo”. [Hud: 48]
Naye mama wa Maryam aliposema kama inavyotuelezea Quraan Tukufu:
"وَإِنِّي أُعِيذُهَا بِكَ وَذُرِّيَّتَهَا مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ"
“Nami namkinga Kwako na dhuria wake kutokana na shaytwaan aliyetokomezwa mbali na kulaaniwa”. [Aaal ‘Imraan: 36]
Allaah Mtukufu Akamkirimu kama Anavyotuambia:
"فَتَقَبَّلَهَا رَبُّهَا بِقَبُولٍ حَسَنٍ وَأَنبَتَهَا نَبَاتًا حَسَنًا وَكَفَّلَهَا زَكَرِيَّا"
“Basi Rabb wake Akampokea kwa kabuli njema, na Akamkuza mkuzo mwema, na Akamfanya Zakariyyaa kuwa mlezi wake”. [Aaal ‘Imraan: 37]
Kadhalika, Bi Maryam ‘Alayhas Salaam wakati alipomwona Jibriyl katika sura ya mwanamume akimjia naye yuko peke yake mbali kabisa na watu alisema kama inavyotuhadithia Quraan:
"قَالَتْ إِنِّي أَعُوذُ بِالرَّحْمَـٰنِ مِنكَ إِن كُنتَ تَقِيًّا"
“(Maryam) akasema: Najikinga kwa Ar-Rahmaan usinidhuru, ukiwa ni mwenye taqwa”. [Maryam: 18]
Na hapo bi huyo akapata neema mbili; mtoto bila ya baba na utakaso toka kwa Allaah kupitia ulimi wa kitoto chake kichanga baada ya kutuhumiwa kwamba amezini.
Ama tukija kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), tunakuta kwamba Allaah Subhaanahu wa Taalaa Amemwelekeza faida ya neno hili mbali na kumwamuru kushikamana nalo katika mwenendo mzima wa maisha yake. Allaah Anamwambia:
"وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ● وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ"
“Na sema: Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na udokezi wa mashaytwaan ● Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie”. [Al-Muuminuwna: 97-98]
Na Anamwambia tena:
"وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ"
“Na utakapokuchochea uchochezi kutoka kwa shaytwaan, basi omba kinga kwa Allaah. Hakika Yeye Ndiye Mwenye Kusikia yote, Mjuzi wa yote”. [Fusswilat: 36]
Na imepokelewa toka kwa Khawlah binti Hakiym kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"مَنْ نَزَلَ مَنْزِلًا فَقَالَ: أَعُوْذُ بِكَلِمَاتِ اللهِ التَّامَّاتِ مِنْ شَرِّ مَا خَلَقَ، لَمْ يَضُرَّهُ شَيءٌ حَتَى يَرْتَحِلَ مِنْ مَنْزِلِه"
“Mwenye kufikia kwenye nyumba yoyote kisha akasema: Najilinda kwa Maneno ya Allaah yaliyotimia kutokana na shari ya Alivyoviumba, basi hakitomdhuru chochote mpaka aondoke kwenye nyumba hiyo”. [Hadiyth hii iko kwenye Fat-hul Baariy kwa Sharh ya Swahiyh Al Bukhaariy].
Kadhalika, imepokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu Anhumaa) akisema:
" انَ رسولُ اللَّهِ صلى اللَّهُ عليهِ وسلَّمَ كَانَ يعوِّذُ الحسنَ والحسينَ ، يقولُ : أعيذُكُما بِكلماتِ اللَّهِ التَّامَّةِ ، مِن كلِّ شيطانٍ وَهامَّةٍ ومن كلِّ عينٍ لامَّةٍ"
“Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwaombea kinga Al-Hasan na Al-Husayn akisema: Nawalindeni kwa usaidizi wa Maneno ya Allaah yaliyotimia kutokana na mashetani wa aina zote na wanyama wenye sumu, na kutokana na kila jicho lenye kudhuru”. [Hadiyth Swahiyh. Swahiyhul Bukhaariy (3371)]
