02-Nuru Ya Qur-aan: Basmalah
Nuru Ya Qur-aan
02: Basmalah:
"البَسْمَلَةُ" (Basmalah), ni kifupisho cha neno "بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ" (Bismil Laah Ar Rahmaan Ar Rahiym. Kwa ‘ijmaa ya Maulamaa, “Basmalah” ni sehemu ya aya ya Qur-aan kwenye Suwrat An Naml Anaposema Allaah Mtukufu:
"إِنَّهُ مِن سُلَيْمَانَ وَإِنَّهُ بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ"
“Hakika inatoka kwa Sulaymaan, na hakika (imeanza) Kwa Jina la Allaah, Ar-Rahmaan, Mwenye Kurehemu”. [An Naml: 30
Na mtu anaposema neno hili wakati wa kuanza jambo lake lolote, ni kana kwamba anasema: “Naanza kumtaja Allaah Mtukufu, na ninataka msaada na tawfiyq kwa Jina Lake Tukufu katika jambo langu hili, kwani Yeye Ndiye Mweza wa kila kitu, Mwenye Fadhila duniani na akhera, na Mwenye Kuwaneemesha viumbe wote”. Na Mwislamu anatakiwa wakati wote aianze kazi yake kwa kulitamka neno hili kwa ulimi wake na kulihudhurisha ndani ya moyo wake. Ikiwa atalitamka kwa nia safi na ya kweli, basi shetani atajiweka mbali naye, baraka ya kazi yake itaongezeka, na tawfiyq na utekelezaji mwema wa kazi utakuwa pamoja naye.
Uhakika wa neno hili unamaanisha kwamba Muislamu amejisalimisha na kuingia ndani ya kumbatio la Kimola, anafanya kazi yake kwa ajili ya Allaah Peke Yake, anatarajia msaada Wake Yeye Peke Yake, ametawakali Kwake Yeye Pekee na anatarajia kuzipata Rehma Zake za kudumu. Anakuwa kana kwamba anasema: “Hakika mimi ninafanya kazi yangu hii nikijivua kwamba inafanyika kwa jina langu mimi, bali kwa Jina la Allaah Mtukufu, kwa kuwa mimi ninapata nguvu na usaidizi kutoka Kwake Yeye tu. Nazitaraji ihsani Zake na Msaada Wake, kwani bila Yeye, mimi siwezi lolote wala chochote”.
Inatosha kwa Muislamu kuwa “Basmalah” inampa liwaziko kwamba yu pamoja na Allaah, na kwamba yeye anajipamba kwa lile Analolipenda Allaah, na kwamba madhali usaidizi wa Allaah u pamoja naye, basi amali yake na kazi yake haitokwenda arijojo.
Maulamaa wote wanakubaliana kwamba “Basmalah” ni muhimu mno katika kila kitendo na kila neno. Aidha, wamekubaliana kwamba Maswahaba walioandika Msahafu katika enzi ya ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu Anhum), waliandika “Basmalah” mwanzoni mwa kila sura, kwa kuwa “Basmalah”, ni aya ya Qur-aani Tukufu inayonasibiana na ufunguzi wa kila sura.
Lakini pamoja na hivyo, Maulamaa hawa wamekhitalifiana katika suala la kuizingatia “Basmalah” kwamba ni aya ya Quraan kwenye Sura nyinginezo ikiwemo Surat Al-Faatihah. Rai zao ziko kwenye mielekeo mitatu:
Mwelekeo wa kwanza:
“Basmalah” mwanzoni mwa sura si aya ya Qur-aan Tukufu, si katika Surat Al-Faatiha wala sura nyingineyo yoyote, bali imeandikwa mwanzoni mwa kila sura kwa ajili ya kutenganisha kati ya sura na nyingineyo. Wenye rai hii wametoa dalili za nukuu na dalili za kiakili.
Dalili Za Nukuu:
Dalili ya kwanza:
Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyopokelewa na Abu Hurayrah kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"قسَّمْتُ الصَّلاةَ بَيْنِي وَبَيْنَ عَبْدِيْ نِصْفَيْنِ، فَنِصْفُهَا لي وَنِصْفُهَا لِعَبْدِيْ، وَلِعَبْدِيْ مَا سَألَ ، فَإِذَا قَالَ : الحمدُ للهِ ربِّ العالمين، فَأَقُوْلُ: حمَدَنِي عَبْدِيْ...."
“Allaah Anasema: Nimeigawanya Al-Faatihah nusu mbili, kati Yangu na Mja Wangu. Nusu yake ni Yangu, na nusu nyingine ni ya Mja Wangu. Na Mja Wangu Nitampa analoliomba. Mja Wangu akisema: “Al-Hamdu Lillaahi Rabbil ‘Aalamiyna”, basi na Mimi Nasema: Mja Wangu Kanihimidi…..”. [Hadiyth Swahiyh. Imepokelewa na Abu Hurayrah]
Wanasema kwamba makusudio ya swalah hapa قَسَّمْتُ الصَّلَاة, ni kusoma Al-Faatihah katika swalah, kwani kila mwenye kuswali anaposoma aya ya sura hii, Allaah Humjibu mpaka mwisho wa sura kama ilivyobainisha Al Hadiyth Al-Qudsiy hii ambayo hatukuimalizia. Na katika Hadiyth hii, Rasuli Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuitaja “Basmalah”, na wala hakuizingatia kwamba ni sehemu ya Al-Faatihah.
Dalili ya pili:
Ubayya bin Ka’ab amesema: Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliniuliza:
"ما تقرأُ في الصَّلاةِ؟ فقرأتُ عليه أمَّ القرآنِ، فقال: والَّذي نفسي بيدِه ما أُنزِل في التَّوراةِ ولا في الإنجيلِ ولا في الزَّبورِ ولا في الفرقانِ مثلُها، إنَّها السَّبعُ المثاني، والقرآنُ العظيمُ الَّذي أُعطيتُه"
“Vipi unasoma unapoifungua swalah yako?” Nikamsomea Ummul Qur-aan. Akaniambia: Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake, haikuteremshwa si katika Tauraat, wala katika Injiyl, wala katika Zaburi, wala katika Furqaan mfano wake. Hakika hiyo ni As-Sab-’u Al-Mathaaniy (Aya saba zenye kukaririwa mara kwa mara), na Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym ambayo nimepewa”. [Imechakatwa na At-Tirmidhiy (2875), An-Nasaaiy katika As-Sunan Al-Kubraa (11205) na Ahmad (9345)]
Hii ni dalili kwamba Basmalah si katika Al-Faatihah, kwa kuwa Ubayya hakuisoma pamoja na aya nyingine za Surat Al-Faatihah. Na Rasuli akamkubalia hilo, na wala hakumweleza kwamba ni lazima asome Basmalah.
Dalili Za Kiakili:
Dalili ya kwanza:
Lau kama Basmalah ingelikuwa ni sehemu ya Qur-aan, basi ingelithibitishwa kwa njia ya masimulizi jumuiya ya kizazi hadi kingine “Tawaatur”, na hili halikutokea. Na lau kama lingetokea, basi lingejulikana kwa lazima.
Dalili ya pili:
Inatutosha sisi kujua kwamba Basmalah imekhitalifiwa kati ya Maulamaa, na Qur-aan haikhitilafiwi.
Dalili ya tatu:
Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameibainisha Qur-aan Tukufu ubainisho mmoja ulio sawa. Hakudhihirisha baadhi ya mambo na kuyaficha mengine, bali yote kayadhihirisha kwa usawa mmoja.
Mwelekeo Wa Pili:
Hawa wanasema kwamba Basmalah ni aya kamili ya Qur-aan Tukufu iliyoteremka kwa ajili ya kutenganisha kati ya sura. Dalili zao ni:
Dalili ya kwanza:
Kuandikwa Basmalah kwenye Msahafu, ni dalili kwamba ni Qur-aan, lakini haionyeshi kwamba ni aya katika Surat Al-Faatihah au kwenye sura nyingineyo yoyote ile.
Mwelekeo Wa Tatu:
Wanasema kwamba Basmalah ni aya katika Surat Al-Faatihah na katika kila sura ya Qur-aan Tukufu. Dalili zao ni hizi zifuatazo:
Dalili ya kwanza:
Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"إذَا قَرَأْتُم الحَمْدُ فَاقْرَؤُوْا بِسْمِ اللهِ الرّحْمَنِ الرّحِيمِ، إِنَّهَا أُمُّ القُرْآنِ وَأُمُّ الكِتَابِ والسَّبْعُ المَثَانِي وبِسْمِ اللهِ الرّحْمَنِ الرّحِيمِ إحدى آياتها"
“Mnaposoma Alhamdu, basi someni: Bismillaahi Ar Rahmaan Ar Rahiym, kwani hakika Al-Hamdu ni mama wa Qur-aan, mama wa Kitabu, na aya saba zenye kurudiwa mara kwa mara, na Bismil Laahir Rahmaanir Rahiym ni moja ya aya zake ”. [Imechakatwa na Ad-Daaraqutwniy (1/312) na Al-Bayhaqiy (2486)]
Dalili ya pili:
"سُئِلَ أنَسٌ: كيفَ كَانَتْ قِرَاءَةُ النَّبيِّ صلَّى اللهُ عليه وسلَّم؟ فَقالَ: كَانَتْ مَدًّا، ثُمَّ قَرَأَ: بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ [الفاتحة: 1]؛ يَمُدُّ بـ{بِسْمِ اللَّهِ}، ويَمُدُّ بـ{الرَّحْمَنِ}، ويَمُدُّ بـ{الرَّحِيمِ}"
“Anas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliulizwa namna Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa anaisoma Qur-aan akasema: “Alikuwa anavuta “madd” (herufi za kuvutwa kwa mujibu wa taaluma ya tajwiyd). Kisha akasoma: "بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ" hadi kuimaliza suwratil Faatihah yote. Akasema: Anavuta "بِسْمِ اللَّـهِ" , anavuta "الرَّحْمَـٰنِ", na anavuta "الرَّحِيمِ".” [Hadiyth Swahiyh. Swahiyhul Bukhaariy (5046)]
Hapa Anas ameanza kwa "بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ"
Dalili ya nne:
Hadiyth ya Anas Radhwiya Allaahu ‘Anhu:
"بَيْنَا رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم ذَاتَ يَوْمٍ بَيْنَ أَظْهُرِنَا، إِذْ أَغْفَىٰ إِغْفَاءَةً. ثُمَّ رَفَعَ رَأْسَهُ مُتَبَسِّماً. فَقُلْنَا: مَا أَضْحَكَكَ يَا رَسُولَ اللّهِ؟ قَالَ: أُنْزِلَتْ عَلَيَّ آنِفاً سُورَةٌ. فَقَرَأَ: بِسْمِ الله الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ ● إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ ● فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ● إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الأَبْتَرُ ، ثُمَّ قَالَ: أَتَدْرُونَ مَا الْكَوْثَرُ؟ فَقُلْنَا: الله وَرَسُولُهُ أَعْلَمُ. قَالَ: فَإِنَّهُ نَهْرٌ وَعَدَنِيهِ رَبِّي عَزَّ وَجَلَّ، ...."
“ Siku moja Rasuli wa Allaah (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokuwa nasi, alisinzia kidogo, kisha akanyanyua kichwa chake akitabasamu. Tukamuuliza: “Nini kimekuchekesha ewe Rasuli wa Allaah?!” Akasema: “Imenishukia sasa hivi Surah”. Kisha akasoma:
بِسْمِ الله الرَّحْمٰنِ الرَّحِيمِ ● إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ ● فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ ● إِنَّ شَانِئَكَ هُوَ الأَبْتَرُ
Kisha akauliza: “Mnajua ni nini Al-Kawthar?” Tukajibu: “Hapana”. Akasema: “Ni mto ambao Allaah Ameniahidi Peponi….”. [Hadiyth Swahiyh. Imechakatwa na Muslim (400)]
Wenye rai hii wanasema kwamba Hadiyth hii inaonyesha kwamba Basmalah ni aya ya katika kila Surah ya Qur-aan Tukufu kwa dalili kwamba Rasuli kaisoma mwanzoni mwa Surat Al-Kawthar.
Dalili ya tano:
Hii ni dalili ya kiakili wakisema kwamba Msahafu wa Al Imaam uliandikwa ndani yake Basmalah mwanzoni mwa Surat Al-Faatihah, na kila mwanzoni mwa Sura zote za Quraan tukufu isipokuwa Surah moja tu ambayo ni Baraa’. Na hili limekuwa kwa njia ya “tawaatur” kati ya Waislamu huku tukijua kwamba wao hawakuwa wakiandika kwenye Qur-aan kile ambacho si katika Qur-aan Tukufu.
Kutokana na dalili zote hizi zilizotiliwa nguvu kwa dalili hizi za kunukuliwa na dalili za kiakili toka kwa Maulamaa wetu hao wenye hima na shime kubwa ya kukilinda Kitabu chetu hiki, tunasema kwamba Basmalah ni aya ya Qur-aan ambayo imekariri mwanzoni mwa kila Sura kwa ajili ya kutabaruku.
Mwahala Ambapo Basmalah Imekokotezwa Kuitamka:
1- Wakati wa kuanza kusoma Qur-aan Tukufu.
2- Wakati wa kuanza khutba ya swalah ya ijumaa, khutba ya eid mbili na kadhalika.
3- Wakati wa kuingia chooni.
4- Wakati mtu anapoanza kutawadha.
.
5- Wakati wa kuanza kula.
.
6- Wakati wa kuchinja mnyama na katika kila shughuli yoyote ya kheri anayoifanya Muislamu.
