03-Nuru Ya Qur-aan: Suwrat Al-Faatihah

 

 

Nuru Ya Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

 

03:   Suwrat Al-Faatihah

 

Suwrat Al Faatihah, ni mama wa Qur-aan Tukufu, nayo ndiyo sura ya mwanzo kabisa kuandikwa kwenye Msahafu wa ‘Uthmaan.  Aya zake ni saba.

 

Sura hii ina majina mbalimbali.   Kati ya majina hayo ni:

1-  Faatihatul Kitaab  "فَاتِحَةُ الكِتَابِ"(Kifungua Kitabu(.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"‏لاَ صَلاَةَ لِمَنْ لَمْ يَقْرَأْ بِفَاتِحَةِ الْكِتَابِ" 

 

“Swalah haiswihi kwa asiyesoma Faatihatul Kitaab”.  [Swahiyh Muslim (394)]

 

2- Ummul Qur-aan na Ummul Kitaab "أُمُّ القُرْآنِ وَأُمُّ الكِتَابِ" (Mama wa Qur-aan na Mama wa Kitabu).

 

Ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam:

 

 "كُلُّ صَلاَةٍ لاَ يُقْرَأُ فِيهَا بِأُمِّ الْكِتَابِ فَهِيَ خِدَاجٌ ‏"

 

“Swalah yoyote ambayo haikusomwa ndani yake Ummul Kitaab, basi ni pungufu”.  [Sunan Ibn Maajah: 840]

 

3-  As Sab-‘u Al-Mathaaniy "السَّبْعُ المَثَانِيْ"

Hii ni kwa vile aya zake ni saba ambazo hukaririwa kwenye swalah moja.   Baadhi ya Mufassiruuna wanasema kwamba sababu ya kuitwa hivyo ni kwa vile ilishuka mara moja Makkah na ikashuka mara nyingine Madiynah.

 

4-  Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym "القُرْآنُ العَظِيْمُ"

 

Ni kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam:

 

"(الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ) هِيَ السَّبْعُ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنُ الْعَظِيمُ الَّذِي أُوتِيتهُ" 

 “Al-Hamdu Lillaahi Rabbi Al-‘Aalamiyna, ni As Sab-‘ul Mathaaniy, na Al-Qur-aan Al-Adhwiym niliyopewa”.  [Hadiyth Swahiyh.  Swahiyhul Bukhaariy (5006)]

 

Haya ndiyo majina yake mashuhuri zaidi.  Ina majina mengineyo kama:

 

الْحَمْدُ، الصَّلاةُ، الشِّفَاءُ، الرُّقْيَةُ، أَسَاسُ القُرْآنِ، الوَاقِيَةُ، الكَافِيَةُ، الوَافِيَةُ

 

Himdi, du’aa, ponyo, zinguo. msingi wa Qur-aan, kinga, toshelezi, yenye kukidhi.

 

Na majina yote haya bila shaka yanaonyesha nguvu ya sura hii na yale yaliyomo ndani yake.

 

Fadhila Yake:

 

Kuna Hadiyth nyingi zinazozungumzia kuhusiana na fadhila za sura hii. Kati ya hizo ni:

 

(a)  Imepokelewa toka kwa Abu Sa’iyd bin Al-Mu’allaa Radhwiya Allaahu ‘anhu, amesema:  

 

" كُنْتُ أُصَلِّي فِي الْمَسْجِدِ، فَدَعَانِي النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم فَلمْ أُجِبْهُ حَتَّى صَلَّيْتُ ثُمَّ أَتَيْتُهُ. فَقُلْتُ يَا رَسُولَ اللَّهِ: إِنِّي كنت أُصَلِّي، فَقَالَ: أَلَمْ يَقُلِ اللَّهُ: اسْتَجِيبُوا لِلَّهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دعَاكُمْ، ثمَّ قَالَ لي: أَلَا أُعَلِّمُكَ أَعْظَمَ سُورَةٍ فِي الْقُرْآنِ قَبْلَ أَنْ تَخْرُجَ مِنَ الْمَسْجِدِ. فَأَخَذَ بِيَدِي، فَلَمَّا أَرَادَ أَنْ يَخْرُجَ قُلْتُ لَهُ: أَلَمْ تَقُلْ لَأُعَلِّمَنَّكَ سُورَةً هِيَ أَعْظَمُ سُورَة مِنَ الْقُرْآنِ، قَالَ: الْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ، هِيَ السَّبْعُ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنُ الْعَظِيمُ الَّذِي أُوتِيتهُ "

 

“Nilikuwa nikiswali Msikitini, kisha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaniita, nami sikumwitikia.  Nikamaliza kuswali kisha nikamwendea na kumwambia:  Ee Rasuli wa Allaah!  Nilikuwa naswali”.  Akaniambia:  Je, Hakusema Allaah: Mwitikieni Allaah na Rasuli Anapokuiteni?!”  Kisha akaniambia:  Je, nikufundishe sura iliyo adhimu zaidi ndani ya Qur-aan Tukufu kabla hujatoka Msikitini?.   Kisha akaukamata mkono wangu.  Na wakati alipotaka kutoka nilimwambia:  Si umeniambia kwamba utanifundisha sura adhimu zaidi katika Qur-aan!  Akasema:  Al-Hamdu Lillaahi Rabbil ‘Aalamiyna, ndiyo As Sab-‘ul Mathaaniy na Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym niliyopewa”.  Hadiyth Swahiyh.  Swahiyhul Bukhaariy (5006)]

 

(b)  Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema:  

 

"بَيْنَمَا جِبْرِيلُ قَاعِدٌ عِنْدَ النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم سَمِعَ نَقِيضًا مِنْ فَوْقِهِ فَرَفَعَ رَأْسَهُ فَقَالَ: هَذَا بَابٌ مِنَ السَّمَاءِ فُتِحَ الْيَوْمَ لَمْ يُفْتَحْ قَطُّ إِلاَّ الْيَوْمَ، فَنَزَلَ مِنْهُ مَلَكٌ فَقَالَ: هَذَا مَلَكٌ نَزَلَ إِلَى الأَرْضِ لَمْ يَنْزِلْ قَطُّ إِلاَّ الْيَوْمَ فَسَلَّمَ وَقَالَ: أَبْشِرْ بِنُورَيْنِ أُوتِيتَهُمَا لَمْ يُؤْتَهُمَا نَبِيٌّ قَبْلَكَ: فَاتِحَةُ الْكِتَابِ وَخَوَاتِيمُ سُورَةِ الْبَقَرَةِ، لَنْ تَقْرَأَ بِحَرْفٍ مِنْهُمَا إِلاَّ أُعْطِيتَهُ"

 

“Wakati Jibriyl alipokuwa amekaa kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), mara alisikia sauti toka juu yake.  Akanyanyua kichwa chake akamwambia:  “Huu ni mlango wa mbinguni, umefunguliwa leo.  Haujawahi kamwe kufunguliwa isipokuwa leo.  Malaika akateremka kupitia mlango huo na Jibriyl akamwambia Rasuli:  Huyu Malaika ameteremka ardhini, kamwe hakuwahi kuteremka isipokuwa leo.  Malaika  akamtolea salaam (Nabiy) na kumwambia:  Furahia nuru hizi mbili ulizopewa, hakupewa Nabiy yeyote kabla yako:  Faatihatul Kitaab na aya (mbili) za mwishoni mwa Suwrat Al-Baqarah.  Hutasoma herufi yeyote toka humo isipokuwa utapewa (nuru zake na kujibiwa du’aa zilizomo humo)”.    [Hadiyth Swahiyh.  Swahiyh Muslim (806)]

 

Maana Ya Kiujumla Ya Suwrat Al Faatihah:

 

Katika sura hii, Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Anawaelezea Waja Wake kwamba Yeye Pekee Ndiye Anayestahiki himdi yote, na kwamba himdi hii ni lazima iendelee wakati wote, kwani Yeye Ndiye Mfalme Anayeuendesha ulimwengu huu wote ukiwa ndani ya rehma kamili, ya kudumu na jumuishi.  Kama ambavyo Yeye Subhaanahu wa Ta’alaa, Ndiye Mwenye mamlaka ya mwisho huko akhera ambapo Atawafanyia viumbe vyote hisabu kutokana na matendo yao waliyoyafanya hapa duniani, mema yatalipwa kwa mema na ziada, na mabaya yatalipwa mabaya mithili yake.  Siku hiyo hakuna kiumbe chochote kitakachoweza kufurukuta kama ilivyo hapa duniani ambapo viongozi wenye madaraka makubwa, ndio wanaojiona kwamba wao ndio wao.  Siku hiyo wote watanywea na Uadhama wa kweli wa Allaah utadhihiri mbele ya viumbe vyote kuanzia Malaika, majini, wanadamu na vinginevyo.

 

Kisha sura hii inabainisha njia ya kuokoka, nayo ni kumfanyia Allaah ibada Yeye tu na kumtakasia nia, na kumtaka msaada Yeye tu pasina mwingine.  Na hapo ndipo unapodhihiri utwana wa viumbe mbele ya Mwabudiwa Mtukufu Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Ambaye Hafai kushirikishwa na kiumbe chochote katika ibada. Na wakati mja anapoishi katika hali ya utumwa, hapo anahisi daima kumhitajia Mola wake, kumtaka msaada na kumwomba wakati wote.  Hapo ndipo inapobubujika Nuru ya Allaah  kwenye nafsi yake na akili yake, na anakuwa na furaha ya kufuata njia ya kweli iliyo sahihi ambayo Allaah Ta’aalaa Amemwamuru Rasuli kuifuata.  Njia hii ni ile waliyoifuata Manabii, wasadikishaji na mashahidi ambao Allaah Ta’aalaa Amewaneemesha.  Na wakati huo huo, mja huyu anajiepusha na njia ya upotovu na anajiepusha kwa akili yake na wasiwasi wa shetani na anaishi ndani ya Radhi za Allaah Mtukufu.

 

Hakika kilele cha kuomba msaada kwa Allaah Mtukufu kiko katika dua ambayo kwayo Mwislamu kwa nia safi kabisa na kwa ikhlasi ya mwisho, anaelekea kwa Mola wake akimwomba Amwepushe na njia ya wenye kutangatanga waliopotea ambao Allaah Amewaghadhibikia kwa kupotoka kwao na kwenda njia nyingine, huku ukweli wakiujua na kuukataa kwa kiburi, inda na hasadi.  Na hao wanaongozwa na Ahlul Kitaab.

 

Kuisoma Suwratul Faatihah katika Swalah.

 

Mafuqahaa wamekhitalifiana kuhusiana na suala la kusoma Al-Faatiha katika swalah katika rai mbili:

 

Rai Ya Kwanza:

 

Wenye rai hii wanasema kwamba kusoma Al-Faatihah katika swalah ni sharti ya kusihi kwa swalah na mwenye kuiacha pamoja na kuwa na uwezo wa kuisoma, basi swalah yake hubatilika.  Dalili yao ni Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"‏لاَ صَلاَةَ لِمَنْ لَمْ يَقْرَأْ بِفَاتِحَةِ الْكِتَابِ" 

 

“Swalah haiswihi kwa asiyesoma Faatihatul Kitaab”.  [Swahiyh Muslim (394)]

 

Rai Ya Pili:

 

Hawa wanasena kwamba Al-Faatihah si sharti ya kusihi swalah.  Mwenye kuaicha na akasoma sura nyingine, basi swalah yake ni sahihi.  Dalili yao ni Kauli Yake Ta’alaa:

 

"إِنَّ رَبَّكَ يَعْلَمُ أَنَّكَ تَقُومُ أَدْنَىٰ مِن ثُلُثَيِ اللَّيْلِ وَنِصْفَهُ وَثُلُثَهُ وَطَائِفَةٌ مِّنَ الَّذِينَ مَعَكَ ۚ وَاللَّـهُ يُقَدِّرُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ ۚ عَلِمَ أَن لَّن تُحْصُوهُ فَتَابَ عَلَيْكُمْ ۖ فَاقْرَءُوا مَا تَيَسَّرَ مِنَ الْقُرْآنِ"

 

“Hakika Rabb wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Anajua kwamba unasimama (kuswali) karibu na thuluthi mbili za usiku au nusu yake, au thuluthi yake, na pia kundi miongoni mwa wale walio pamoja nawe.  Na Allaah Anakadiria usiku na mchana.  Anajua kwamba hamuwezi kuukadiria wakati wake na kusimama kuswali, hivyo basi Amepokea tawbah yenu.  Basi someni kile kilicho chepesi katika Qur-aan”.   [Al-Muzzammil: 20]

.

Mufassiruna wote wanakubaliana kwamba aya hii iliteremka kuhusiana na swalah ya usiku isipokuwa wenye rai hii wanasema kwamba inahusiana na swalah za usiku na swalah nyinginezo kiujumla.

 

 

Share