04-Nuru Ya Qur-aan: Ulinganio Wa Tawhiyd

 

Nuru Ya Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

04:  Ulinganio Wa Tawhiyd:

 

Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

 

"يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ فِرَاشًا وَالسَّمَاءَ بِنَاءً وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجَ بِهِ مِنَ الثَّمَرَاتِ رِزْقًا لَّكُمْ ۖ فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ"

 

“Enyi watu!  Mwabuduni Rabb wenu Ambaye Amekuumbeni na wale wa kabla yenu mpate kuwa na taqwa.   Ambaye Amewafanyieni ardhi kuwa ni tandiko na mbingu kuwa ni paa, na Akateremsha kutoka mbinguni maji, Akawatolea kwayo matunda kuwa ni riziki zenu.  Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua”.  [Al-Baqarah: 21-22]

 

Aya hizi mbili tukufu zinaelekezwa kwa watu wote juu ya kutofautiana akida zao na mapote yao, na juu ya kupita na kutanuka zama mpaka Siku ya Qiyaamah.  Aya hizi zinawazindua juu ya ulazima wa kumpwekesha Allaah Mtukufu na kumtakasia ibada Yeye Peke Yake, kwani Yeye Ndiye Anayestahiki kwa hilo. Imekuwa ni katika Neema Zake Allaah Mtukufu kuwajulisha watu mambo ambayo yanaonyesha juu ya Upweke wa Allaah Aliyeuumba ulimwengu wote huu na kuweka ndani yake yale yote wanayoyahitajia viumbe Vyake katika maisha yao.  Amewakumbusha hapa kwamba Yeye Ndiye Aliyewapatisha baada ya kuwa hawapo, Akawaumba, Akawaweka sawa, Akawapa akili na nguvu na Akawafadhilisha wanadamu kuliko viumbe vinginevyo Alivyoviumba.

 

Yeye Ndiye Aliyewaumba wanadamu waliopita, waliopo hivi sasa na watakaokuja baadaye.  Na hii si kwa wanadamu tu, bali hata kwa viumbe vinginevyo hai na visivyo hai.  Viko vilivyoanza vikaondoka, na viko vinavyokuja na kufuatiliwa na vinginevyo mpaka mwisho wa ulimwengu wetu huu.  Na huu ndio Ukamilifu wa Qudra na Uwezo wa Allaah Mtukufu.  Ukweli huu unawathibitishia wanadamu na viumbe vinginevyo vyote ya kuwa wakati wao wa kuondoka hapa duniani unapofika, basi wataondoka na kurejea kwa Rabi wao.  Na wanadamu kwa kuwa ndio waliobeba jukumu la amana ya taklifu kwa vitendo vyao, Allaah Atawafanyia hisabu kwa matendo yao waliyoyachuma hapa duniani, mema kwa mema na mabaya kwa mabaya.  Shani yao katika hilo ni shani ya wale waliowatangulia, hakuna yeyote atakayesazwa au kusahauliwa.  Watu wote watasimamishwa mbele ya Mola wao Siku ya hisabu ili kila mmoja apate jaza yake. Na hili ndilo linalomwogopesha Mwislamu daima na kujikuta akijitahidi kufanya mambo mema na kujiepusha na mambo machafu ili aweze kuipata  Jannah.  Allaah Anatuambia:

 

"فَأَمَّا مَن طَغَىٰ وَآثَرَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا فَإِنَّ الْجَحِيمَ هِيَ الْمَأْوَىٰ وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَىٰ فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ"

 

 

“Basi yule aliyepindukia mipaka kuasi •  Na akahiari uhai wa dunia  ●  Basi hakika moto uwakao vikali mno ndio makaazi yake  ●  Ama yule aliyekhofu kisimamo mbele ya Rabb wake, na akaikataza nafsi yake na hawaa  ●  Basi hakika Jannah ndio makaazi yake”.   [An-Nazi’aat: 38-41]

 

 

Na kati ya dalili za Uwezo Wake Allaah Mtukufu na ujumuishi wa Fadhila Zake kwa Viumbe Vyake, ni kuwakunjulia ardhi na kuifanya kama tandiko la kupumzikia na kuweza kuendesha maisha yao bila ya matatizo yoyote.  Ardhi yetu ingawa ni ya mviringo au umbo la yai, lakini hata hivyo popote anapokuwa mtu, basi hujikuta yuko kwenye ardhi iliyonyooka kabisa mbele yake inayomwezesha kugura huku na kule kwa usahali na wepesi kabisa bila ya kikwazo chochote.  Ardhi hii pia imewekewa nguvu ya mvutano ili kuvikita imara vilivyoko juu yake.  

 

Mbali ya ardhi hii, Allaah Ameikita milima na majabali ardhini ili yawe kama ni vigingi vya kuizuia ardhi isipate kuyumbayumba na kuyafanya maisha yasiwezekane, mbali na manufaa mengi yanayopatikana kutokana na milima na majabali.  

 

Aidha, kuna bahari kubwa (oceans) na ndogo (sea) zenye manufaa makubwa kabisa kwetu kuanzia harakati za usafiri, samaki freshi, chumvi, vito vya thamani, kuwa chanzo cha mvua na mengineyo mengi tunayoyapata kutokana na bahari. Zaidi ya asilimia 75 ya uso wa ardhi imefunikwa na maji chumvi ya bahari wakati ambapo maji tamu yanayopatikana kwenye maziwa, mito, chemchemu na kadhalika, kiwango chake hakizidi zaidi ya asilimia 2.2.

 

Mbali ya hayo, Allaah Ameiteremsha mvua toka kwenye mawingu yaliyo juu kwa ajili ya kuotesha mimea yenye kuzalisha mazao ya aina mbalimbali kuanzia nafaka, matunda na mbogamboga, mbali na maji hayo kuwa ndio chanzo kikuu cha uhai kwa viumbe hai.  Neema hii ya chakula ni moja kati ya neema kubwa kabisa ambayo inabidi tuizingatie na tuitaamuli.  Yote haya yanaonyesha uwezo wa Allaah katika mchakato mzima wa kupatikana chakula hicho ambacho mtu hukitenga mezani na kukila bila kurudi nyuma na kutaamuli namna kilivyoanzia mpaka kumfikia mezani au jamvini.  Allaah Anatuambia:

 

"فَلْيَنظُرِ الْإِنسَانُ إِلَىٰ طَعَامِهِ أَنَّا صَبَبْنَا الْمَاءَ صَبًّا    ثُمَّ شَقَقْنَا الْأَرْضَ شَقًّا   فَأَنبَتْنَا فِيهَا حَبًّا    وَعِنَبًا وَقَضْبًا  وَزَيْتُونًا وَنَخْلًا    وَحَدَائِقَ غُلْبًا    وَفَاكِهَةً وَأَبًّا  مَّتَاعًا لَّكُمْ وَلِأَنْعَامِكُمْ"

 

Basi atazame mwana Aadam chakula chake  ●  Kwamba Sisi Tumemimina maji kwa uneemefu  ●   Kisha Tukaipasua ardhi ikafunguka (kwa mimea)  ●  Tukaotesha humo nafaka  ●  Na mizabibu na mimea ya mboga (ikatwayo ikamea tena)  ●  Na mizaituni na mitende  ●  Na mabustani yaliyositawi na kusongamana ●  Kwa ajili ya manufaa kwenu na kwa wanyama wenu wa mifugo.”.  [‘Abasa: 25-32]

 

 

Haya yote ili Tawhiyd izame na ijikite zaidi ndani ya nyoyo zetu.  Tumtakasie Yeye tu katika ibada zetu zote na tujiweke mbali kabisa na aina yoyote ya shirki ya dhahiri au ya iliyofichikana.  Na kwa ajili hiyo, Allaah Anatuambia:

 

"فَلَا تَجْعَلُوا لِلَّـهِ أَندَادًا وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ"

 

“Basi msimfanyie Allaah waliolingana naye na hali ya kuwa nyinyi mnajua”.  [Al-Baqara: 22]

 

Kwa maana kwamba tusimfanyie Allaah mfano Wake nailhali sisi tunajua kwamba hakuna kinachofanana Naye ambacho kinastahiki kuabudiwa kama Anavyoabudiwa Yeye.

 

Ni lazima tujue kwamba Tawhid ndiyo msingi wa Uislamu uliyolinganiwa na Mitume wote.  Wote hao wametumwa kwa ajili ya kuitangaza na kuilingania Tawhiyd.  Allaah Mtukufu Anatuambia:

 

"وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ"

 

“Na Hatukutuma kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Rasuli yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba:  Hakika hapana mwabudiwa wa haki ila Mimi; basi Niabuduni”.  [Al-Anbiyaa: 25]

 

Tawhiyd na ibada kwa ajili ya Allaah Peke Yake ni nyuso mbili za sarafu moja.  Na kutokana na umuhimu wa Tawhiyd, tunamwona Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiilingania huko MakkaH kwa muda wa miaka 13 na wala hakuingia kwa kina kwenye masuala mengineyo isipokuwa baada ya kupata uhakika kwamba Tawhiyd ishajikita katika nyoyo za waliomwamini.

 

Tawhiyd ya kweli, ni ile iliyowaunganisha Waislamu wote kuwa ni wamoja kutokea Nabiy wa mwanzo hadi Nabiy wa mwisho Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Al-Imaam Ash-Shaaf’iy aliulizwa na watu:  “Nini dalili ya kuwepo Muumbaji?”

 

Akajibu:  “Ni majani ya mforosadi.  Je, ladha yake, rangi yake, na harufu yake ni moja?”  Wakajibu: “Ndio”.  Akasema:  “Majani yake huliwa na nondo akatoa hariri, huliwa na nyuki akatoa asali, huliwa na mbuzi akatoa kinyesi chake, na huliwa na digidigi akatoa miski.  Je, ni nani aliyeyafanya mambo yote haya pamoja na kwamba mti ni huo huo mmoja?!”   Waulizaji wakageuka mabubu na wakasilimu.  Walikuwa ni watu 27.

 

Naye bedui mmoja aliulizwa kuhusu dalili ya kuwepo kwa Allaah Mtukufu akasema:  “Kinyesi cha ngamia huonyesha kwamba kuna ngamia, kinyesi cha punda huonyesha kwamba kuna punda, na athari ya unyayo huonyesha mwendo. Basi mbingu zenye minara, ardhi zenye njia na bahari zenye mawimbi, je hayo yote hayaonyeshi kwamba kuna Muumbaji, Aliye Mjuzi, Mwenye uwezo?!”

 

 

Share