05-Nuru Ya Qur-aan: Kuthibitisha Ujumbe Wa Rasuli Na Malipo Kwa Wenye Kuamini Na Makafiri

 

 

Nuru Ya Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

05:  Kuthibitisha Ujumbe Wa Rasuli Na Malipo Kwa Wenye Kuamini Na Makafiri:

 

Allaah Ta’alaa Anatuambia:

 

" وَإِن كُنتُمْ فِي رَيْبٍ مِّمَّا نَزَّلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا فَأْتُوا بِسُورَةٍ مِّن مِّثْلِهِ وَادْعُوا شُهَدَاءَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ   فَإِن لَّمْ تَفْعَلُوا وَلَن تَفْعَلُوا فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ۖ أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ"

 

“Na ikiwa mko katika shaka kutokana na Tuliyoyateremsha juu ya Mja Wetu (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi leteni Suwrah mfano wake, na waiteni mashahidi wenu pasipo na Allaah mkiwa ni wakweli  ●  Msipofanya, na wala hamtoweza kufanya, basi ogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, umeandaliwa kwa makafiri”.  [Al-Baqarah: 23-24]

 

Qur-aan Tukufu ni Maneno ya Allaah Aliyoyateremsha kwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kidogo kidogo kwa ajili ya kuwalingania watu, kuwafundisha Uislamu na kuwaongoza katika Njia iliyonyooka.  Na kwa vile makafiri wameukanusha ukweli wa risala ya Uislamu aliyokuja nayo Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na wakadai kwamba Qur-aan hii imetungwa na mwanadamu, na kwamba Muhammad amenukulu kutoka kwa watu tena wasio Waarabu, kutokana na madai haya, Allaah Amewachalenji Akiwataka watunge wao mfano wa sura fupi zaidi iliyopo kwenye Qur-aan Tukufu.  Wametakiwa hivyo, kwa kuwa herufi za Qur-aan ni herufi zao, nao ni watu mafasaha wa lugha yao kwa balagha na kwa bayaan, na wao ni mashuhuri kwa utunzi wa mashairi na uandishi wa nathari.  Lakini pamoja na yote hayo, walishindwa kutunga angalau kijisura kimoja kilicho mfano wa Qur-aan Tukufu. Kushindwa huko, pamoja na uweledi wao na ubingwa wao wa kuichezea lugha yao wenyewe, kumethibitisha wazi kabisa kwamba Qur-aan si maneno ya binadamu, bali ni Maneno ya Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Aliyoyateremsha kwa Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuyafanya ni muujiza wenye kuthibitisha na kushuhudia ukweli wake.  Na chalenji hiyo haikukomea kwao tu, bali imeelekezwa kwa wakanushaji wote, wasaidizi wao, wanaowaunga mkono na walio mithili yao mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Na Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Ametueleza kwamba hawatoweza kamwe kuleta mfano wa Qur-aan Tukufu, na kwa ajili hiyo, Amewataka wauogope moto na waiamini risala ya Uislamu, kwa vile moto umeandaliwa kwa kila mpingaji wa ukweli na mkanushaji wa jambo lisilokanushika.  Na hao ndio makafiri katika zama zote.

 

فَاتَّقُوا النَّارَ الَّتِي وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ ۖ أُعِدَّتْ لِلْكَافِرِينَ"

 

“Basi ogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, umeandaliwa kwa makafiri.”

 

Na hii ndio sifa ya moto ambao Allaah Anawaonya kwao makafiri hao.  Moto huu unawaunguza watu na mawe, na watu ndio mafuta yake.  Hali hii inabainisha ukali wa moto huo na makali ya uchungu wa adhabu yake.  Ni moto wenye kuhisika machungu yake mpaka ndani ya nyoyo, wenye harufu mbaya mno ya kuchukiza, wenye moshi mzito, wenye joto kali la ajabu, na wenye kuambata miili ya waliomo humo.

 

Na ikiwa itaulizwa:  “Watu watachomwa kwa ajili ya kulipwa matendo yao ya kuukanusha wahyi na kumpinga Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi nini hikma ya kuchomwa mawe?”.

 

Jawabu linasema kwamba muradi wa mawe ni masanamu yao waliyokuwa wakiyachonga na kisha kuyaabudu.  Na hili linathibitishwa na Kauli Yake Ta’alaa:

 

"إِنَّكُمْ وَمَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ حَصَبُ جَهَنَّمَ أَنتُمْ لَهَا وَارِدُونَ"

 

Hakika nyinyi na yale mnayoyaabudu badala ya Allaah ni vichochezi vya moto wa Jahannam, nyinyi mtauingia”.  [Al-Anbiyaa: 98]

 

Moto huu uko tayari na umeshaumbwa ukiwasubiri watu wake.

 

Kisha baada ya Allaah Mtukufu kutuelezea kuhusu hatima ya watu hao wanaopinga risala, moja kwa moja Ameingia kutoa bishara na hatima njema kwa WachajiMungu.  Anatuambia:

 

"وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ كُلَّمَا رُزِقُوا مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقًا ۙ قَالُوا هَـٰذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَأُتُوا بِهِ مُتَشَابِهًا ۖ وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ ۖ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ"

 

Na wabashirie wale walioamini na wakatenda mema kwamba watapata Jannaat (bustani) zipitazo chini yake mito, kila watakaporuzukiwa humo katika matunda kuwa ni riziki husema:  Haya ndiyo yale tuliyoruzukiwa kabla.  Na wataletewa hali ya kuwa yanashabihiana, na watapata humo wake waliotakaswa, nao humo ni wenye kudumu”.  [Al-Baqarah: 25]

 

Bishara maana yake ni kutoa habari ya furaha.  Na katika aya hii tukufu, Allaah Subhaanahu wa Ta’alaa Anamwamuru Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awabashirie Waumini Jannah yenye sifa kemkem zilizotajwa.  Kati ya sifa hizo ni kuwa Jannah hii inapita chini yake mito isiyokauka.  Mito hii kama ilivyoelezewa kwenye aya nyingine ni ya maji safi tamu, asali safi iliyosafishwa, maziwa tamu yasiyochachuka na pombe yenye ladha tamu kabisa.  Ladha ya vinywaji hivyo haina mfano, na huko vitakuwa vimetakaswa kabisa na aina yoyote ya madhara. Aidha, kuna matunda ya aina tofauti na ya kila aina yasiyokatika kwa msimu maalumu au kwa sababu maalumu, bali yako daima dom.  

 

Mbali ya hayo, wataozeshwa mahurl ‘ayn waliotakasika na kasoro zozote walizonazo wanawake wa hapa duniani.  Utwaharifu wao hapa haujaainishwa, bali unahusiana na kila utwaharifu unaohitajika kuwepo kwao. Wametwaharika kimwenendo, wametwaharika kisura, wametwaharika kimatamshi, na wametwaharika kiuoni na kimwono.  Isitoshe, ni wanawake waliohirimu moja na waume zao, wenye kupendeza kwa waume zao kwa akhlaki bora kabisa, matendo bora kabisa ya kuridhiwa, ukomo wa mwisho wa hishma na adabu katika mazungumzo yao, na utwaharifu wa kutokana na hedhi, nifasi, manii, kwenda haja ndogo na kubwa, kutokwa makamasi, kutokwa mate, au kuwa na harufu mbaya.  Wanawake hao hawana kasoro yoyote, bali ni wake wema wazuri kabisa wenye kuinamisha macho yao kwa waume zao tu.  Wake hao si kwa ajili ya kuzaa nao, bali ni kustarehe nao milele na milele.

 

Haiwezekani kwa akili zetu za kibinadamu kuyajengea taswira yaliyomo humo isipokuwa kwa yale ambayo tunayo hapa duniani na Allaah Akatueleza kwamba yako mfano wake huko kama asali, matunda, mahurul ‘ayn na kadhalika.  Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatueleza katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy:

 

"أَعْدَدْتُ لِعِبَادِيَ الصَّالِحِينَ مَا لَا عَيْنٌ رَأَتْ وَلَا أُذُنٌ سَمِعَتْ وَلَا خَطَرَ عَلَى قَلْبِ بشر. واقرؤوا إِنْ شِئْتُمْ: (فَلَا تَعْلَمُ نَفْسٌ مَا أُخْفِيَ لَهُمْ مِنْ قُرَّة أَعين"

 

 “Nimewaandalia Waja Wangu wema mambo ambayo hakuna jicho lolote lililopata kuyaona, wala jicho lolote kupata kuyasikia, wala hata kupitikiwa kwenye moyo (akili) wa mwanadamu yeyote.  Na someni mkitaka:  Basi nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika yanayoburudisha macho.  Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (4779) na Muslim (2824)]

 

Ni mambo ambayo pamoja na sisi kujiona kwamba tumefikia kwenye kilele cha teknolojia cha kutuwezesha kuwa na vyombo vya aina tofauti, lakini hivyo na vinginevyo vitakavyogunduliwa baadaye, haviko huko Peponi, bali kuna mengine ambayo hatuwezi kuyaelewa wala kuyafahamu.  

 

Haya yote yanawasubiri Waumini wachaMungu, na hayo pia yanawasubiri wake zao wachaMungu. Watakutanishwa wote huko Peponi na kuwa pamoja wastarehe humo milele.

 

Bishara hii aliyoamriwa Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuitoa, inamhusu kila yule aliyetekeleza ipasavyo yale yote aliyokalifishwa nayo hapa duniani.  Na hii ni ili watu wajue kwamba matendo yao husajiliwa, na kwamba ni wajibu kwao wamwamini Allaah kikweli kweli, na wakusanye kati ya kuyasadikisha aliyokuja nayo Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na matendo mema anayotakiwa mja kuyafanya.  Imani ni lazima iambatane na matendo bora. Ikiwa viwili hivi vitapatikana, basi mja atastahiki kuipata Jannah hiyo yenye sifa hizi kidogo zilizogusiwa na aya hii tukufu.

 

 

Share