06-Nuru Ya Qur-aan: Neema Za Allaah Kwa Watu: (a) Neema Ya Kwanza: Allaah Amewaleta Ulimwenguni Baada Ya Kuwa Hawapo
Nuru Ya Qur-aan
06: Neema Za Allaah Kwa Watu: (a) Neema Ya Kwanza: Allaah Amewaleta Ulimwenguni Baada Ya Kuwa Hawapo:
Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"كَيْفَ تَكْفُرُونَ بِاللَّـهِ وَكُنتُمْ أَمْوَاتًا فَأَحْيَاكُمْ ۖ ثُمَّ يُمِيتُكُمْ ثُمَّ يُحْيِيكُمْ ثُمَّ إِلَيْهِ تُرْجَعُونَ
“Vipi mnamkufuru Allaah na hali mlikuwa wafu Akakuhuisheni, kisha Atakufisheni, kisha Atakuhuisheni, kisha Kwake mtarejeshwa? [Al-Baqarah: 28]
Katika aya hii tukufu, Allaah Anauliza swali la kimshangao kuhusiana na msimamo wa makafiri kwa upande wa Tawhiyd. Swali hili linaistaajabia hali ya makafiri hawa wanaouona mbele yao ukweli na kisha kuukataa. Je, kuna yeyote aliyewahi kudai kwamba yeye kayafanya haya Aliyoyaelezea Allaah Mtukufu katika aya hii? Je, kuna yeyote mwenye uwezo wa kufanya angalau chembe tu ya haya yaliyoelezewa katika aya hii? Si haya tu, bali makafiri hawa wanaompinga Allaah, wanaishi katika neema zote ambazo Allaah Anawapa na kuwaruzuku kuanzia vyakula wanavyokula, vinywaji na mengineyo mengi ambayo wao wamekuja hapa duniani na kuyakuta yako tayari kwa ajili yao na kwa ajili ya wengineo. Je, hawafikirii haya!?
Makafiri hawa wanaomkanusha na kumkataa Allaah, walikuwa hawako katika maisha wanayoishi hivi sasa. Kisha Allaah Akawatoa hai toka matumboni mwa mama zao. Je, kwanza hawaangalii tu muujiza wa mchakato wa mlolongo wa kuumbiwa tumboni kuanzia tone la manii hadi kuwa binadamu kamili?! Ni nani awezaye kufanya haya kama si Allaah Mweza wa kila jambo?! Kisha baada ya kutoka matumboni, wakakuta maziwa ya mama yako tayari kabisa, nayo hayapatikani kama mama hana mtoto? Nani Aliyeyaweka maziwa haya tayari yakiwa na elementi zote muhimu za kumfaa mtoto mchanga? Kisha wakakua na kupata akili ya kuweza kupambanua mambo kwa akili waliyopewa na Allaah, na hatimaye wanaona kila siku watu wakifa bila ya yeyote kuweza kuyaepa mauti hayo na kuishi milele. Je, ni nani Anayeyaendesha haya yote?!
Na hakuna shaka yoyote kwamba Huyu Allaah Aliyeyafanya yote haya, Ana uwezo wa kuwarejesha tena kwenye uhai mpya Siku ya Qiyaamah ambapo wanadamu wote watasimamishwa mbele Yake kwa ajili ya kuhesabiwa matendo yao yote waliyoyafanya katika kipindi chote cha maisha yao ya hapa duniani ambapo watalipwa mema kwa mema, na mabaya kwa adhabu.
