07-Nuru Ya Qur-aan: Neema Za Allaah Kwa Watu: (b) Neema Ya Pili: Allaah Amewasakharishia Vyote Vilivyoko Ardhini Ili Viwanufaishe Katika Maisha Yao
Nuru Ya Qur-aan
07: Neema Za Allaah Kwa Watu: (b) Neema Ya Pili: Allaah Amewasakharishia Vyote Vilivyoko Ardhini Ili Viwanufaishe Katika Maisha Yao:
Allaah Anatuambia:
"هُوَ الَّذِي خَلَقَ لَكُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا"
“Yeye Ndiye Ambaye Amekuumbieni vyote vilivyomo ardhini.” [Al-Baqarah: 29]
Aya hii inatueleza ikisema enyi watu, jueni kwamba Allaah Amekukirimuni nyinyi zaidi kuliko viumbe vingine vyote, kwani Yeye Amewasakharishieni vyote vilivyoko ardhini ikiwa ni pamoja na maji, mimea, wanyama, ndege na kila kitu. Haya yote ni kwa ajili ya kutuwezesha kuishi maisha bora ya kuweza kuiamirisha ardhi na kumwabudu Allaah kwa usahali, na hatimaye kuweza kufuzu na kuipata Jannah.
Allaah Anatuambia:
"يَا أَيُّهَا النَّاسُ اذْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ ۚ هَلْ مِنْ خَالِقٍ غَيْرُ اللَّـهِ يَرْزُقُكُم مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ ۚ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ فَأَنَّىٰ تُؤْفَكُونَ"
“Enyi watu! Kumbukeni Neema za Allaah kwenu. Je, kuna muumbaji yeyote badala ya Allaah Anayekuruzukuni kutoka mbinguni na ardhini? Hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye. Basi wapi mnapogeuzwa?” [Faatwir: 03]
Mwanadamu akijiangalia kulinganisha na viumbe vingine, atajikuta kuwa yeye ndiye mwenye neema zaidi zisizo na hisabu. Akianzia upande wa lishe, atajikuta kwamba Allaah Amemruzuku aina tofauti tofauti za vyakula vinavyopikwa kwa miundo tofauti na visivyopikwa. Halafu vinywaji navyo, havina idadi, kati ya moto na baridi. Kisha mavazi ya malighafi tofauti, ya kazi tofauti, minasaba tofauti na kadhalika. Hali kadhalika kwa makazi yake, vipando na vyote vinavyohusiana na maisha yake. Lakini viumbe wengine kama wanyama, zaidi hula aina moja tu ya chakula kama majani au nyama na hawana kingine zaidi ya hayo.
Haya yote ni neema kubwa kwa mwanadamu zisizo na hisabu. Na kila mtu anatakikana azitumie neema hizi kwa namna inayomridhisha Allaah, kwani kila mtu bila shaka, atakuja kuulizwa kuhusiana na neema hizi Siku ya Qiyaamah. Allaah Anatuambia:
"ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ"
“Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema”. [At-Takaathur: 08]
