08-Nuru Ya Qur-aan: Neema Za Allaah Kwa Watu: (c) Neema Ya Tatu:Allaah Amempa Mwanadamu Uwezo Wa Kujifunza

 

 

Nuru Ya Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

08: Neema Za Allaah Kwa Watu: (c) Neema Ya Tatu:Allaah Amempa Mwanadamu Uwezo Wa Kujifunza:

 

Allaah Anatuambia:

 

"وَعَلَّمَ آدَمَ الْأَسْمَاءَ كُلَّهَا ثُمَّ عَرَضَهُمْ عَلَى الْمَلَائِكَةِ فَقَالَ أَنبِئُونِي بِأَسْمَاءِ هَـٰؤُلَاءِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ   قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا ۖ إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ"

 

“Na Akamfunza Aadam majina yote (ya kila kitu), kisha Akavionesha mbele ya Malaika Akisema:  Niambieni majina ya hivi mkiwa ni wakweli  ●  Wakasema: Utakasifu ni Wako, hatuna elimu isipokuwa Uliyotufunza, hakika Wewe Ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote”.  [Al-Baqarah: 31-32]

 

Maudhui ya aya hizi inazungukia kuhusu uwezo alionao mwanadamu katika kujifunza, kufahamu na kudiriki mambo.  Zinabainisha sifa za mwanadamu katika nyanja ya elimu ambazo Malaika hawanazo.

 

Tunakuta kwamba viumbe viko vya aina mbalimbali na aina nyingi, lakini vyenye akili za kuweza kuamrishwa kutenda na kutotenda ni viumbe vitatu:  Malaika, majini na wanadamu.  Mwanadamu ndiye aliyekirimiwa zaidi kwa kupewa uwezo mkubwa zaidi wa kufahamu, kujifunza, kutafiti, kubuni, kutengeneza, kuboresha na kadhalika.  Mwanadamu umbo lake ni dogo kulinganisha na baadhi ya viumbe wengineo ambao ni wakubwa na wenye nguvu zaidi kuliko yeye. Lakini pamoja na udhaifu wake huo, Allaah Amemkirimu na kumfadhilisha kwa elimu juu ya viumbe wengineo.  

 

Uwezo mkubwa wa mwanadamu umeonekana katika ulimwengu wetu huu. Tunashuhudia maajabu ya ujuzi na utaalamu wake katika kuyatoa madini mbalimbali toka ardhini na kuyatumia katika matumizi mbalimbali yaliyoleta mapinduzi makubwa ya kiteknolojia.  Kwa utaalamu wake na ujuzi wake, ameweza hata kwenda anga za juu na kugundua yaliyokuwa hayajulikani, amezamia kwenye vina virefu vya bahari na kugundua siri za baharini na mengi mengineyo yasiyoweza kufanywa na viumbe wengineo.  Na hapa mwanadamu anatakikana asisahau kwamba uwezo huu alionao, ni takrima tu toka kwa Allaah Mtukufu.  Ni lazima awajibike na ile mipaka Aliyowekewa na Allaah Ta’aalaa na aendelee kujiweka chini ya utumwa wa Allaah Mtukufu Aliyemfanya yeye kuwa ni khalifa wa kuiamirisha na kuijenga ardhi hii.  Na hili ndilo lililofanikishwa na mwanadamu.  Ameweza kufanya mapinduzi katika nyanja zote kuanzia majenzi, kilimo, tiba, uhandisi, uchumi na kadhalika, mbali na mawasiliano ambayo kwa leo yameshuhudia mapinduzi yanayofanana na muujiza.

 

Malaika pamoja na utukufu wao na utwaharifu wao wa kutomwasi kwao Allaah, walivyoambiwa wamweleze Allaah majina aliyofundishwa Aadam ambayo wao walikuwa hawayajui, walijibu moja kwa moja kwamba hawajui kwa kutanguliza neno la kumtakasa Allaah wakisema: “Subhaanak”.  Na hii ni kwa ajili ya kubainisha kwamba wao wana yakini ya kuwa Vitendo vya Allaah vimesimamia juu ya hikma ya juu kabisa, na kwamba wao wanakiri kwamba hawawezi kutaja majina ya vitu hivyo kwa kuwa wao hawajui isipokuwa yale tu Aliyowafundisha Allaah Mtukufu.  Hapo walijua kwamba maumbile ya mwanadamu yako tayari kupokea elimu ya majina hayo na elimu nyinginezo wakati ambapo maumbile yao yako mbali kabisa na hayo.  Na kwa ajili hiyo, walihitimisha kauli yao kwa kusema:

 

"إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ"

 

Kwa maana kwamba Wewe Pekee Ndiye Mjuzi kwa yaliyotuka, yenye kutuka na yatakayotuka mpaka Siku ya Qiyaamah, na Mwenye hekima kwa kila jambo.

 

Na hizi zilizotajwa ni baadhi ya Neema chache tu za Allaah kwetu.  Neema Zake hazihesabiki wala kukokotoleka.

 

 

Share