09-Nuru Ya Qur-aan: Kuanza Mapambano Kati Ya Aadam (‘Alayhis Salaam) Na Ibliys
Nuru Ya Qur-aan
09: Kuanza Mapambano Kati Ya Aadam (‘Alayhis Salaam) Na Ibliys:
Allaah Ta’alaa Anatuambia:
"وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ وَاسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ"
“Na pale Tulipowaambia Malaika: Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys, alikataa na akatakabari, na akawa miongoni mwa makafiri. [Al-Baqarah: 34]
Baada ya Aadam (‘alayhis Salaam) kuweza kuyataja majina ya vitu ambavyo Allaah Ta’aalaa Alimfundisha na Malaika kushindwa kuvijua, Allaah Ta’aalaa Aliwaamrisha wamsujudie Aadam. Makusudio ya sijdah hapa ni kumpa heshima na taadhima na wala si kumsujudia sijdah ya ibada, kwa kuwa kusujudiwa kwa ibada hakuwi isipokuwa kwa Allaah Peke Yake.
Kumsujudia Allaah kumegawanyika mafungu mawili. Fungu la kwanza ni sijdah inayofanywa na wanadamu na majini waliokalifishwa. Hii inahusiana na sijdah za aina zote tunazozifanya katika swalah zetu za faradhi na za sunnah, au hata sijdah za kumshukuru Allaah kwa neema Alizotuneemesha.
Fungu la pili ni sijdah inayofanywa na viumbe vyote kwa Allaah Mtukufu. Allaah Anatuambia:
"وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَظِلَالُهُم بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ" ۩
“Na waliomo mbinguni na ardhini humsujudia Allaah Pekee wakipenda wasipende na vivuli vyao pia (vinamsujudia) asubuhi na jioni”. [Ar-Ra’ad: 15]
Na Anasema tena:
"وَالنَّجْمُ وَالشَّجَرُ يَسْجُدَانِ"
“Na nyota na miti vinasujudu”. [Ar-Rahmaan: 06]
Maulamaa wanasema kwamba Ibliys aliyetajwa hapa hayuko katika kundi la Malaika, bali ni katika majini. Wametolea dalili kwa haya yafuatayo:
(a) Ni kutokana na Neno Lake Ta’alaa:
"وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ كَانَ مِنَ الْجِنِّ"
“Na pindi Tulipowaambia Malaika: Msujudieni Aadam. Wakasujudu isipokuwa Ibliys, alikuwa miongoni mwa majini”. [Al-Kahf: 50]
(b) Ibliys aliasi amri ya Allaah, na Malaika hawaasi kabisa Amri ya Allaah. Allaah Anatuambia:
"لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ"
“Hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa”. [At-Tahriym: 06]
(c) Ibliys alitakabari, na Malaika hawatakaburi.
(d) Malaika wameumbwa kutokana na nuru wakati Ibliys ameumbwa kutokana na moto. Na hili linabainishwa na Kauli Yake Ta’alaa:
"قَالَ مَا مَنَعَكَ أَلَّا تَسْجُدَ إِذْ أَمَرْتُكَ ۖ قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِّنْهُ خَلَقْتَنِي مِن نَّارٍ وَخَلَقْتَهُ مِن طِينٍ"
“(Allaah) Akasema: Nini kilichokuzuia usisujudu Nilipokuamrisha? Akasema (Ibliys): Mimi ni mbora kuliko yeye. Umeniumba kwa moto, na yeye Umemuumba kwa udongo”. [Al-A’araaf: 12]
Lakini Maulamaa wengine wanaona kwamba Ibliys ni katika Malaika kwa kuwa Allaah Alipowaamuru kumsujudia Aadam, Alielekeza amri kwa wote Akiwaambia: Msujudieni Aadam. Wanasema kwamba hakuna dalili ya nguvu ya kutofautisha kati ya Malaika na majini. Linaloonekana ni kwamba majini ni katika jamii ya Malaika, na mashetani ni katika jamii ya majini. Allaah Mtukufu Amelitumia jina la "الْجِنَّةُ"(majini) kwa maana ya Malaika katika Kauli Yake Aliposema:
"وَجَعَلُوا بَيْنَهُ وَبَيْنَ الْجِنَّةِ نَسَبًا ۚ وَلَقَدْ عَلِمَتِ الْجِنَّةُ إِنَّهُمْ لَمُحْضَرُونَ"
“Na wakafanya baina Yake (Allaah) na baina ya Malaika unasaba. Na hali Malaika wamekwishajua kwamba wao (washirikina) bila shaka watahudhurishwa (kuadhibiwa)”. [As-Swaaffaat: 158]
Aidha, Amelitumia jina "الْجِنَّةُ"(majini) Akikusudia mashetani katika Suwrat An Naas Aliposema:
"مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ"
“Miongoni mwa (mashetani) majini na watu”. [An-Naas: 06]
Kiujumla, tunasema kwamba hayo yote ni majina. Majina haya yako katika ulimwengu wa ghaibu ambao sisi hatuujui ukweli wake wowote. Ni vizuri tutosheke na yaliyoelezewa bila kupekua kitu ambacho hatuwezi kukifikia undani wake.
Kiufupi, tunasema kwamba kwa kukataa amri hii ya Allaah, na Ibliys kujiona kwamba yeye ni bora kuliko Aadam kwa kuwa ameumbwa kwa moto na Aadam kaumbwa na udongo, Allaah Alimlaani na Akamweka mbali na Rehma Zake na akawa ni katika makafiri. Na hapo ndipo uadui ukaanza kutokota ndani ya nafsi yake, lakini Alimwomba Allaah Mtukufu Ampe umri wa kuweza kuishi mpaka Siku ya Qiyaamah ili aweze kuwapoteza wana wa Aadam, na Allaah Akamkubalia. Na hapa mtu anaweza kusema kwa nini Allaah Alimkubalia aje atupoteze na kutushawishi kufanya maasia?
Jibu ni kwamba kila jambo lina hikma yake. Na hikma ya hilo ni kwamba hakuna mafanikio yanayopatikana bila ya taabu. Wanadamu tumeumbiwa matamanio ya mambo mbalimbali. Kila mwanadamu inabidi ayadhibiti matamanio yake ili aweze kufanikisha malengo yake. Mfungaji kwa mfano, ili aweze kuikamilisha saumu yake, inabidi awe na subira ya mwisho kabisa ya kuacha matamanio yake yote kwa ajili ya kuitii amri ya Allaah Mtukufu.
Hivyo basi, ikiwa Mwislamu ataweza kupambana na ushawishi wa shetani, akakabiliana na uchochezi wake wa kumpambia maasi, basi bila shaka huyo atakuwa amefaulu mafanikio makubwa. Pepo kama tunavyojua ina mambo ambayo hakuna jicho lililoyaona, wala sikio lililoyasikia wala hata pia kumpitikia mwanadamu katika akili yake. Hayo yaliyomo humo hayawezi kupatikana kwa usahali, bali ni lazima yakabiliwe na kila aina ya ugumu. Na ugumu huo uko katika mikono ya shetani na Ibliys.
Dunia yetu kama tunavyoiona, inazidi kusonga mbele kutokana na matatizo yanayotukabili tukayatafutia ufumbuzi na kutokana na changamoto tunazopambana nazo tukazishinda. Bila kuwepo matatizo, hakutakuweko maendeleo, na bila kuwepo changamoto, ladha ya maisha itakosekana.
Hivyo basi, kuwepo kwa Ibliys wa kutushawishi, na sisi kuweza kukabiliana naye, kutatuwezesha kuwa na mafanikio makubwa kabisa huko akhera.
Mapambano kati ya mwanadamu na shetani yalianzia Peponi wakati alipokataa shetani kuitii amri ya Mola wake ya kumsujudia Aadam. Allaah Akamfukuza toka peponi na Akamlaani. Na hapo Akaapa mbele ya Allaah kwamba atampoteza Aadam pamoja na wanawe kwa nguvu na mbinu zake zote. Allaah Mtukufu Anatuambia:
"قَالَ فَبِعِزَّتِكَ لَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ"
“(Ibliys) akasema: Naapa kwa Utukufu Wako, bila shaka nitawapotosha wote ● Isipokuwa waja Wako miongoni mwao waliokhitariwa kwa ikhlasi zao”. [Swaad: 82-83]
Raundi ya kwanza ya upotezaji huo ilikuwa ni kwa wazazi wetu wawili. Shetani alifanikiwa kuwapoteza na hivyo kusababisha kutolewa Peponi na kuteremshwa hapa ardhini ili Aadam pamoja na wanawe waendelee kukabiliana na njama za shetani za kuwapotosha. Shetani huyu ana silaha mbalimbali za kufanikisha vita vyake na mwanadamu. Kati ya silaha hizo ni pamoja na:
1- Uwezo wa kumpambia mwanadamu maasia mpaka akajisahau na kujikuta ameshatumbukia kwenye shimo la maasia. Allaah Anasema:
"قَالَ رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِي الْأَرْضِ وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ"
“(Ibliys) akasema: Rabb wangu! Kwa vile Umenihukumia kupotoka, basi bila shaka nitawapambia (maasi) katika ardhi na nitawapotoa wote”. [Al-Hijri: 39]
Anasema tena:
"تَاللَّـهِ لَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَىٰ أُمَمٍ مِّن قَبْلِكَ فَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَهُوَ وَلِيُّهُمُ الْيَوْمَ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ"
“Ta-Allaahi, kwa yakini Tulipeleka (Rusuli) kwa nyumati za kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), na shaytwaan akawapambia vitendo vyao. Na yeye leo ni rafiki mwandani wao, nao watapata adhabu iumizayo”. [An-Nahl: 63]
2- Uwongo na hadaa. Uwongo huu ulionekana pale alipoweza kuwashawishi Aadam na Hawaa kula mti waliokatazwa. Aliwahadaa na kuwaambia kwamba ikiwa wataula mti huo, basi watakuwa ni malaika wawili au watakuwa ni katika watu watakaoishi milele. Mbali ya hivyo, aliwaapia ya kwamba anayoyasema ni kweli tupu. Allaah Anatuambia:
"فَوَسْوَسَ لَهُمَا الشَّيْطَانُ لِيُبْدِيَ لَهُمَا مَا وُورِيَ عَنْهُمَا مِن سَوْآتِهِمَا وَقَالَ مَا نَهَاكُمَا رَبُّكُمَا عَنْ هَـٰذِهِ الشَّجَرَةِ إِلَّا أَن تَكُونَا مَلَكَيْنِ أَوْ تَكُونَا مِنَ الْخَالِدِينَ ● وَقَاسَمَهُمَا إِنِّي لَكُمَا لَمِنَ النَّاصِحِينَ"
“Basi shaytwaan (naye ni Ibliys) akawatia wasiwasi ili awafichulie sehemu zao za siri zilizositiriwa. Na akasema: Rabb wenu Hakukukatazeni huu mti isipokuwa msije kuwa Malaika wawili au kuwa miongoni mwa wenye kudumu milele ● Naye akawaapia: Hakika mimi ni katika wenye kukunasihini kidhati. [Al-A’araaf: 20-21]
Na Anasema tena Allaah Mtukufu:
" الشَّيْطَانُ يَعِدُكُمُ الْفَقْرَ وَيَأْمُرُكُم بِالْفَحْشَاءِ"
“Shaytwaan anakutishieni ufukara na anakuamrisheni machafu.” [Al-Baqarah: 268]
3- Yeye anatuona wakati sisi hatumwoni, naye tunaye miilini mwetu ndani ya damu zetu. Allaah Anatuambia:
"إِنَّهُ يَرَاكُمْ هُوَ وَقَبِيلُهُ مِنْ حَيْثُ لَا تَرَوْنَهُمْ"
“Hakika yeye (Ibliys) anakuoneni, yeye na kabila lake (la mashaytwaan) na hali ya kuwa nyinyi hamuwaoni”. [Al-A’araaf: 27]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"إِنَّ الشَّيْطَانَ يَجْرِي مِنِ ابْنِ آدَمَ مَجْرَى الدَّمِ ".
“Hakika shetani anatembea ndani ya (mwili) wa mwanadamu kama inavyotembea damu yake”. [Hadiyth Swahiyh. Al-Bukhaariy (2038) na Muslim (2175)]
Kwa maana anaweza kucheza na akili ya binadamu, moyo wake na hisia zake kumpeleka kwenye mabaya kwa wepesi mno mtu akijiachaia ovyo.
Na lengo kuu la mwisho la shetani kwa mwanadamu, ni kuwafikisha wote kwenye moto wa Jahannamu. Allaah Anatuambia:
"وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلَالًا بَعِيدًا"
“Na shaytwaan anataka awapoteze upotofu wa mbali”. [An-Nisaa: 60]
Na Anatuambia tena:
"إِنَّ الشَّيْطَانَ لَكُمْ عَدُوٌّ فَاتَّخِذُوهُ عَدُوًّا ۚ إِنَّمَا يَدْعُو حِزْبَهُ لِيَكُونُوا مِنْ أَصْحَابِ السَّعِيرِ"
“ Hakika shaytwaan kwenu ni adui, basi mfanyeni kuwa ni adui. Hakika anaitia kikosi chake ili wawe miongoni mwa watu wa moto uliowashwa vikali mno”. [Faatwir: 06]
Na ikiwa shetani hakufanikiwa katika lengo lake la kuwapoteza watu au kuwakufurisha, basi hakati tamaa, bali huendelea hivyo hivyo tu hata kama anaona hakuna matunda ya kazi yake.
Katika maisha yote ya mwanadamu, shetani humganda mwanadamu katika hali zake zote huku akiwa na mbinu mbalimbali za kumpotosha. Humjilia katika kila kitu chake kinachomuhusu. Humjia katika swalah yake ili amshawishi asiweze kufanya khushuu. Wakati mwingine mtu hujikuta amemaliza swalah yake na wala hajui ni rakaa ngapi kaswali au ni sura zipi kazisoma. Shetani pia hula pamoja naye kama hakusema Bismillaah, na hata wakati wa tendo la ndoa huwepo, na anaweza kushiriki ikiwa Mwislamu hakumdhukuru Allaah kabla ya kuanza. Na kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametutaka tuwalinde watoto wetu wanaotarajiwa kutokana na tendo la ndoa kwa kusoma baadhi ya nyiradi ili watoto wetu waweze kusalimika na vitimbi vya shetani huyu. Na hata kabla ya kulala, imesuniwa kusoma nyiradi maalumu alizotufundisha Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya kujilinda na shari kiumbe huyu na balaa zingine.
Mgando wa shetani kwa mwanadamu huendelea hata katika dakika za mwisho za mwanadamu za kuondoka hapa duniani. Na kwa ajili hiyo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha dua ya kujikinga naye katika dakika hizo ngumu za kutoka roho. Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anaomba kinga kwa Allaah akisema:
"وَأَعُوذُ بِكَ أَنْ يَتَخَبَّطَنِي الشَّيْطَانُ عِنْدَ الْمَوْتِ"
“Na najilinda Kwako shetani asije kunizuga zuga wakati wa kufa”. [An-Nasaaiy 5531) na Abu Daawuwd (1552)]
