10-Nuru Ya Qur-aan: Kukubaliwa Toba Ya Aadam (‘Alayhis Salaam):

 

 

Nuru Ya Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

10: Kukubaliwa Toba Ya Aadam (‘Alayhis Salaam):

 

Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

 

" فَتَلَقَّىٰ آدَمُ مِن رَّبِّهِ كَلِمَاتٍ فَتَابَ عَلَيْهِ ۚ إِنَّهُ هُوَ التَّوَّابُ الرَّحِيمُ "

 

Kisha Aadam akapokea maneno kutoka kwa Rabb wake; na (Rabb wake) Akapokea tawbah yake.  Hakika Yeye Ndiye Mwingi wa Kupokea tawbah, Mwenye Kurehemu.    [Al-Baqarah: 37]

 

Aadam (‘Alayhis Salaam) baada ya kughilibiwa na shetani na kumwasi Mola wake na kisha kuamuriwa wote wateremke ardhini, Aadam (‘Alayhis Salaam) alipokea maneno toka kwa Mola wake, na hapo hapo moja kwa moja akaomba toba na msamaha kwa Mola wake, Naye moja kwa moja Akaikubali.  Na kwa vile kufanya makosa ni jambo lisiloepukika kutokana na shetani kumwandama mwanadamu katika hali zake zote, Allaah Ametuwekea wazi milango ya toba ili tuweze kutubia wakati wowote tutakapoteleza na kufanya madhambi.  Na fursa hii ndiyo aliyoitumia Aadam (‘Alayhis Salaam) mara moja bila kuchelewa, na hili ni somo muhimu sana kwetu kwamba tunapoteleza na kufanya madhambi, basi tutubie hapo hapo bila kuchelewa.

 

Mufassiruuna wamekhitalifiana kuhusiana na maneno hayo ambayo Aadam (‘Alayhis Salaam) aliyapokea toka kwa Mola wake.  Baadhi wanasema ni yale ambayo Allaah Alimfunulia kwa njia ya wahyi na Akamfundisha kwayo njia ya kutubia na kurejea Kwake.  Na maneno haya kwa mujibu wa ilivyo mashuhuri kwa yaliyopokelewa toka kwa Ibn ‘Abbaas ni Kauli Yake Ta’alaa:

 

"قَالَا رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ "

 

“Wakasema:  Rabb wetu!  Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu,  bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika”.  [Al-A’araaf: 23]

 

Ama Mujaahid, yeye anasema kwamba maneno hayo ni:

 

"سُـبْحانَكَ اللّهُـمَّ، لا إِلهَ إِلَّا أَنْتَ، إِنّيْ ظَلَـمْتُ نَفْسِيْ فَاغْـفِرْ لِي، فَإِنَّهُ لا يَغْفِـرُ الذُّنوبَ إِلاّ أَنْـتَ"

 

“Nakutakasa (na kila sifa ya upungufu) Ewe Allaah!  Hakuna apasae kuabudiwa kwa haki isipokuwa Wewe tu.  Hakika mimi nimeidhulumu nafsi yangu, basi Nighufirie, kwani hakika hakuna aghufiriaye madhambi isipokuwa Wewe tu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Abu Daawuwd (2602) na tamshi ni lake, At-Tiemidhiy (3446) na Ahmad (753)]

 

Wengine wanasema kwamba makusudio ya maneno ni kulia na kutokwa machozi, kuhisi haya, kujuta, kuomba du’aa, kuomba maghfira, kuhuzunika na kadhalika, kwani haya yote yanakusanya maneno.

 

Baadhi ya Masalaf waliulizwa linalotakiwa kwa mtendaji dhambi aseme wakajibu kwamba atasema yale waliyoyasema wazazi wetu wawili (Aadam na Hawwaa):

 

(a)

 

"رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ "

 

“Rabb wetu!  Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu,  bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika”.  [Al-A’araaf: 23]

 

 

(b)  Yale aliyoyasema Nabiy Muwsaa (‘Alayhis Salaam):

 

"قَالَ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي"

 

Akasema:  Rabb wangu!  Hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu”.  [Al-Qaswas: 16]

 

(c)  Yale aliyoyasema Nabiy Yuwnus (‘Alayhis Salaam):

 

"لا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ"

 

“Hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Subhaanak!  Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu”.  [Al-Anbiyaa: 87]

 

(d)  Ni kusema:

 

"سُبحانَك اللَّهُمَّ وبحَمْدِك أشهَدُ أنْ لا إلهَ إلَّا أنت، أستَغفِرُك وأتوبُ إليك، عَمِلتُ سُوءًا وظلَمْتُ نفسي، فاغفِرْ لي؛ إنَّه لا يَغفِرُ الذُّنوبَ إلَّا أنت"

 

“Ninakutakasa (na kila upungufu) Ewe Allaah pamoja na kukuhimidi.  Hapana wa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Wewe tu.  Ninakuomba maghfirah na ninatubia Kwako.  Nimefanya mabaya na nimeidhulumu nafsi yangu, basi Nighufurie, kwani hakika hakuna yeyote mwenye kusamehe madhambi isipokuwa Wewe tu”.   [Imechakatwa na An-Nasaaiy (10188), Al-Haakim (1972) na At-Twabaraaniy (4/278)]

 

Na kama tujuavyo, toba ni kwanza kulijua dhambi alilolitenda mtu na madhara yake, kisha kujuta kwa kulifanya, halafu kuweka nia ya kweli ya kutolirudia, na mwisho kujiweka mbali na visababisho vyake.  Na kama kuna haki ya mtu inabidi irejeshwe.

 

Na bila shaka tutalahidhi kwamba katika aya tukufu, Allaah Anamalizia kwa kusema kwamba Yeye Ni Mwingi wa Kupokea toba na Mwingi wa rehma.  Hapa bila shaka kunakusudiwa maana nyingi:

 

1-  Kutilia nguvu matumaini na matarajio ya wafanyao dhambi, na kuiunga mioyo ya wakosefu kwa kuwathibitishia kwamba Allaah Yuko tayari kuwapokea kama watarejea Kwake wakati wowote ule.

 

2- Kwamba hata kama makosa yatakariri na kuwa mengi, Allaah Yu tayari kuikubali toba hata kama mja atakariri kosa mara kwa mara.  Muhimu ni mtu aweke nia ya kweli ya kutorejea kosa.

 

3-  Kwamba Allaah Huzikubali toba za watubiaji vyovyote iwavyo idadi yao.

 

4-  Kwamba fadhila za Allaah wigo wake ni mpana mno kwa kuzikubali toba za waja na kuwa Mrehemevu kwao.

 

Kwa haya yote, tunasema kwamba aya hii tukufu inaashiria juu ya kima muhimu ambacho Waislamu wote wanakihitajia, nacho ni toba na kurejea kwa Allaah Mtukufu.  Binadamu kama tujuavyo ni dhaifu na wakati mwingi hulemewa na matamanio na hawaa ya nafsi mbali na kushawishiwa na shetani.  Na kwa ajili hiyo, Allaah Amemwekea njia ya kurejea Kwake ambayo ni toba.

 

Kwa kuwepo toba, matumaini hujadidika na mwanadamu huwa na uwezo wa kujitakasa na makosa yoyote aliyoyafanya.  Toba huudhaminia umma mkondo sahihi wa kupita, kwa kuwa toba huliweka bayana kosa na humrejesha mkosaji kwenye mwelekeo sahihi, mbali na kudhamini haki za watu.  Na hii yote huwafanya watu kuishi kwa furaha chini ya kivuli cha Uislamu.

 

Na cha muhimu zaidi kwa Waislamu ni kuusiana kufanya mema na kuomba toba mara tu baada ya kufanya kosa bila kuchelewa chelewa, na kujiweka mbali na kukata tamaa na kupoteza matumaini.  Ni lazima tujue kwamba Allaah Hufurahia toba zenu na Hutupenda kwa kutubia na kurejea Kwake.  Anatuambia:

 

"إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ"

 

“Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha.” [Al-Baqarah: 222]

 

 

 

Share