11-Nuru Ya Qur-aan: Maumbile Ya Mwanadamu
Nuru Ya Qur-aan
11: Maumbile Ya Mwanadamu:
Kutokana na kisa cha baba yetu Aadam kama kilivyoelezewa na Qur-aan Tukufu ni kuwa mwanadamu kiasili ameumbwa kutokana na udongo na mpulizo uliotokana na Roho ya Allaah. Hivyo basi, mwanadamu ni mzaliwa wa ardhi, mlelekaji katika ardhi, mkaazi wa ardhi na mwenye kuishi juu ya ardhi. Anafanya kazi na shughuli zake zote juu ya ardhi, anahangaika huku na kule, anazitumia rasilmali za ardhi kwa ajili ya maslaha yake ya kuiamirisha ardhi na amepewa uwezo wa kuvitawala viumbe vinginevyo.
Mwanadamu huyu sura yake ilifinyangwa kwa udongo na Malaika, kisha ukaja mpulizo toka kwa Allaah, na udongo huo ukawa ni mtu mwenye uwezo wa kufikiri, kuzungumza, kujifunza, kutafiti, kuutaamuli ulimwengu na kuujenga hatua kwa hatua.
Huyu ndiye mwanadamu mwenye kiwiliwili cha udongo, akili ya kiroho, mwenye utambuzi, mwenye nishati na nguvu za mwili, na mwenye khiyari ya kujichagulia mambo. Na kwa ajili hiyo, amekuwa ni “Mukallaf”, kwa maana amebebeshwa na Allaah maamrisho ya kuyafuata na makatazo ya kuyaepuka kupitia kwa Mitume Wake Aliowatuma kuwafikishai watu Ujumbe Wake.
Mwanadamu huyu amekirimiwa na Mola wake kwa kuumbwa kutokana na elementi zile zile za ardhi anayoishi, akawekewa sheria zinazoendana na maumbile yake, na akakatazwa yale yote yatakayomweka mbali na kheri na usalama. Na lau kama mwanadamu angeliumbwa kwa udongo wa kutoka sehemu nyingine, basi asingeliweza kuishi katika ardhi hii na kutulia au kunufaika na rasilmali zake zilizopo. Kuumbwa kwa udongo hakumaanishi kumtweza mwanadamu au kumshusha thamani, bali udongo huu ni tunu ya kipekee isiyo na mfano wake. Kutokana na udongo huu, vimeundika vito na madini za thamani kubwa kati ya lulu, marijani, dhahabu, silva na mengineyo. Na vyote alivyoviunda mtu na kuvitengeneza, vimetoka kwenye udongo. Hata mazao ya vyakula, maji anayokunywa, moto anaoutumia ukitokana na gesi au mkaa au mada nyingine yoyote, vyote hivyo vimetoka ardhini.
Mbali ya hayo, mwanadamu huyu amepewa uwezo wa kujiweka mwenyewe pale atakapo. Akitaka anaweza kuwa ni kito cha thamani kubwa, na kama atataka, atakuwa ni udongo wa tope uliovunda, au jiwe gumu. Allaah Subhaanahuu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"لَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ فِي أَحْسَنِ تَقْوِيمٍ ● ثُمَّ رَدَدْنَاهُ أَسْفَلَ سَافِلِينَ إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ فَلَهُمْ أَجْرٌ غَيْرُ مَمْنُونٍ"
“Kwa yakini Tumemuumba mwana-Aadam katika umbile bora kabisa ● Kisha Tukamrudisha chini kabisa ya walio chini ● Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema; hao watapata ujira usiokatika”. [At-Tiyn: 4-6]
Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"تَجِدُونَ النَّاسَ مَعَادِنَ، خِيَارُهُمْ فِي الْجَاهِلِيَّةِ خِيَارُهُمْ فِي الإِسْلاَمِ إِذَا فَقِهُوا"
“Mtawakuta watu wana asili tofauti (kama yalivyo madini). Waliokuwa wema wao enzi ya kabla ya Uislamu, wanakuwa ni wema wao baada ya kuingia kwenye Uislamu kama watafahamu vyema (Uislamu)”. [Imechakatwa na Al-Bukhaariy (3493) na Muslim (2526)]
Hadiyth hii ina maana kwamba watu wanatofautiana katika “silica” (ghariza) na maumbile yao kama yanavyotofautiana madini yaliyoko ardhini, na kwamba kujikita makhitalifiano ndani ya nafsi, ni kama kujikita mizizi ya madini ndani ya ardhi. Kama ilivyo kwa madini kuwa yapo ambayo sifa zake hazibadiliki, ni hivyo hivyo kwamba sifa ya utukufu wa mtu haibadiliki katika dhati yake. Anayekuwa mtukufu kwenye ujahili kisha akasilimu na kuingia kwenye Uislamu, basi utukufu na wema wake utaendelea katika Uislamu zaidi na zaidi.
Na tokea dakika za mwanzo, Allaah Subhaanahuu wa Ta’alaa kabla ya kumuumba Aadam (‘Alayhis Salaam), Aliwaambia Malaika ya kwamba Yeye Atamweka katika ardhi mwandamizi (Khalifa) kwa ajili ya kuja kuiamirisha ardhi hii, kuijenga na kuistawisha. Na kwa hilo, yakadhihiri majaliwa ya Allaah katika kumkirimu mwanadamu kwa kumpa ukhalifa huo, au kumwakilisha katika kufichua majaliwa ya Muumbaji katika kubuni vitu, kutengeneza, kuchanganua, kupandikiza, kuhamisha "modulation", kugeuza na kufichua yaliyomo juu na ndani ya ardhi kati ya nishati, hazina, malighafi, na mengineyo. bNa hii yote ni kwa ajili ya kuweza kutekeleza kazi kubwa aliyonayo mwanadamu juu ya uso huu wa ardhi.
Hakika nafasi au roli ya mwanadamu kama Alivyomkadiria Allaah Mtukufu, ndio roli ya kwanza. Yeye ndiye mwenye kugeuza na kubadili maumbo ya ardhi kwa shughuli zake za kilimo, majenzi, miundo mbinu na kadhalika. Mtizamo wa Qur-aan unamfanya mwanadamu huyu kwa ukhalifa wake ardhini, kuwa ni kitenda kazi muhimu katika mfumo wa ulimwengu huu. Ukhalifa wake unahusiana na mafungamano mbalimbali na mbingu, upepo, mvua, nyota na sayari mbalimbali. Na ili mwanadamu aweze kuendeshana na yote yenye kumzunguka kwa ajili ya kufanikisha lengo la kuweza kuishi kama inavyotakikana, Allaah Amempa uwezo wa kujifunza na kufahamu siri ya mambo mbalimbali yaliyopo juu ya ardhi, ndani ya ardhi, kwenye vina vya bahari na hata kwenye anga za juu. Baba yetu Aadam alijifundisha majina ya vitu vyote, na Allaah aliidhihirisha sifa hii ya kujifunza mbele ya Malaika ili wahakikishe Hikma ya Allaah katika mapendeleo Yake na Uwezo Wake, na ili hilo liwe pia ni jaribio la kiutendaji kwa wana wa Adamu walibebe baada yake katika maisha yao huku wakiwa wamejivika silaha ya elimu, ufahamu, udadisi, utafiti na upekuzi katika nyanja zote za maisha. Na hili bila shaka linaonekana wazi kabisa katika ardhi yetu hii. Hakuna kiumbe chochote kinachoishi katika ardhi hii kilichofanya hata asilimia moja tu ya aliyoyafanya mwanadamu.
Na kwa ajili ya kuweza kuishi maisha shwari na tulivu ya kumwezesha kuisimamia roli yake na nafasi yake kwa mujibu wa akili na nguvu alizopewa mwanadamu, Allaah Amemwekea mwanadamu huyu mipaka ambayo inabidi aishi ndani yake. Ikiwa mwanadamu huyu atajiona kwamba ana uwezo kuliko ule aliopewa na Allaah, au nguvu za juu zaidi kuliko zile alizoumbiwa nazo, basi bila shaka atagongana na kitu asichoweza kukikabili.
Mwanadamu huyu ameumbwa akiwa na uwezo wa kufikiri, kuangalia na kuchagua. Ni kiumbe aliyepewa uhuru wa kujichagulia yale anayoyaona yananasibiana naye kwa fikra zake na kwa akili yake. Ana uhuru wa kufanya ibada au kutofanya ibada lakini baada ya Allaah kumtumia Mitume wa kumwonyesha njia ya haki na njia isiyo ya haki kisha uhuru akaachiliwa yeye mwenyewe ajichagulie alitakalo. Anapondokea kulielekea la kheri kwa dhati yake, au hulitamani la shari kwa irada yake, na yote mawili yana tija yake. Aadam na mkewe walilipa thamani ya matashi yao yaliyowapelekea kuula mti, wakatolewa Peponi na kuteremshwa ardhini. Hivyo basi, maasia ya kwanza ya mwanadamu yalikuwa ni ya kitendo cha uhuru wa kujichagulia. Na kwa ajili hiyo, Allaah Mtukufu Aliikubali toba ya Aadam na Akamghufiria kama ilivyotueleza Qur-aan Tukufu.
Mbali ya yote hayo, mwanadamu ameumbwa akiwa na maadui kadhaa mbele yake ili apate changamoto ya kuweza kujiimarisha na kujiwekea kinga dhidi ya maadui hao. Kuwepo kwa changamoto katika maisha ya mwanadamu, kumemfanya afanikishe maendeleo yote tunayoyashuhudia kwa hivi sasa na kwa siku za usoni.
Adui yake wa mwanzo ni nafsi yake mwenyewe yenye kumwamrisha mabaya. Nafsi hii ndiyo iliyomwezesha Ibliys kumpoteza na kumpotoa Aadam na Hawwaa, wakaula mti kwa ajili ya kupata ufalme na umilele kama walivyolaghaiwa na Ibliys.
Adui yake wa pili ni marafiki na masahibu wabaya. Hawa hawampelekei isipokuwa kwenye madhara na machafu.
Adui wa tatu ni Ibliys na askari wake. Huyu ndiye adui hatari zaidi kwa kuwa anaishi pamoja na mawazo yanayompitikia mwanadamu katika nafsi yake, anapita ndani ya damu ya mwanadamu, anajiingiza kwenye mahangaiko ya ndani na ghariza za kimatamanio, na huyapa nguvu matumaini yake ambayo aghalabu huwa ni matumaini hewa.
Allaah kwa Rehma Zake, Amemjulisha mwanadamu kinga zote za kujihami na maadui hao kupitia Mitume na Vitabu walivyokuja navyo. Kinga hizi ni pamoja na kujiepusha na maadui hao, kuchagua marafiki wema, kuamiliana na ndugu wa kheri, kusuhubiana na watu wema wachaMungu na kuomba hifadhi kwa Allaah kutokana na shetani aliyewekwa mbali na rehma za Allaah.
