12-Nuru Ya Qur-aan: Mwanadamu Alipitikiwa Na Kitambo Bila Kuwa Anajulikana

 

 

Nuru Ya Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

12:  Mwanadamu Alipitikiwa Na Kitambo Bila Kuwa Anajulikana:

 

Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

 

"هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا    إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا"

 

 

“Kwa hakika kilimpitia mwana-Aadam kipindi fulani katika dahari, hakuwa kitu kinachotajwa    Hakika Sisi Tumemuumba mwana-Aadam kutokana na tone la manii iliyochanganyika ili Tumjaribu, Tukamfanya mwenye kusikia na mwenye kuona”.  [Al-Insaan: 1-2]

 

 

 

Hebu rudi nyuma kupitia tarehe yako au siku yako au mwaka wako wa kuzaliwa, halafu jiulize: Je ulikuwepo?  Je, ulikuwa unatajika?  Je, kulikuweko yeyote anayekujua?  Je, kulikuweko yeyote anayekufikiria?  Bila shaka jibu litakuwa hapana, kwa maana kwamba wewe ni kiumbe mpya; hukuwepo kabla, uwepo wako haukuwepo, utajo wako haukuwepo, jina lako halikuwepo, hukuwa ukifikiriwa na yeyote, hakuna akujuaye, wala yeyote akutajaye na wala hakukuwepo na yeyote ajuaye kuja kwako isipokuwa Allaah Mtukufu.  Halafu jiulize, Huyu Aliyekupatisha ukapatikana baada ya kuwa hujulikani, Hawezi kukurejesha tena kwenye uhai baada ya kufa na kutowekea mchangani?

 

Na hapa inabidi kila mtu akumbuke kwamba kuna maagano aliyoyakiri mbele ya Allaah hapo kabla akiwa katika ulimwengu wa kiroho. 

 

Katika Hadiyth iliyopokelewa na Ibn ‘Abbaas na kufanyiwa ikhraaj na Ahmad, An-Nasaaiy, Ibn Jariyj na Al-Haakim, Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"إنَّ اللَّهَ تعالى أخذَ الميثاقَ من ظَهرِ آدمَ عليهِ السَّلامُ بنعمانَ يومَ عرفةَ فأخرجَ من صلبِه كلَّ ذرِّيَّةٍ ذرأَها فنثرَها بينَ يديه ثمَّ كلَّمَهم قُبُلًا قال تعالى: أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ؟ قَالُوا بَلَى شَهِدْنَا أَنْ تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَذَا غَافِلِينَ أَوْ تَقُولُوا إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِنْ قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً، أَفَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ الْمُبْطِلُونَ

 

“Hakika Allaah Alichukua maagano katika mgongo wa Aadam huko Nu’umaan Siku ya Arafah.  Akatoa toka mgongoni mwake watoto wote Aliowaumba, kisha Akawatawanya mbele Yake.  Halafu Akazungumza nao moja kwa moja mbele yao Akiwauliza:  Je, Mimi Si Rabbi wenu?  Wakasema: Kwani!  Tumeshuhudia.  Msije mkasema Siku ya Kiyama sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo.  Au mkasema:  Hakika baba zetu ndio walio shirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao.  Basi Utatuangamiza kwa sababu ya waliyo yafanya wapotovu?!” [Imechakatwa na Ahmad (2455), An-Nasaaiy (11191) na Al-Haakim (75)]

 

Hadiyth hii inatiliwa nguvu na Kauli Yake Ta'alaa:

 

"وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰ ۛ شَهِدْنَا ۛ أَن تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَـٰذَا غَافِلِينَ  •  أَوْ تَقُولُوا إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِن قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً مِّن بَعْدِهِمْ ۖ أَفَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ الْمُبْطِلُونَ"

“Na pindi Rabb wako Alipowaleta wana wa Aadam kutoka migongoni mwao kizazi chao, Akawashuhudisha juu ya nafsi zao (Akiwauliza):  Je, Mimi Siye Rabb wenu?  Wakasema:  Ndio bila shaka, tumeshuhudia!  (Allaah Akawaambia):  Msije kusema Siku ya Qiyaamah:  Hakika sisi tulikuwa tumeghafilika nayo haya  •  Au mkasema:  Hakika baba zetu ndio walioshirikisha kabla, nasi tulikuwa kizazi baada yao.  Basi Utatuangamiza kwa yale waliyoyafanya wabatilifu?   [Al-A’araaf: 172-173]

 

Pia inatiliwa nguvu na Hadiyth hii nyingine iliyopokelewa na Anas bin Maalik ambapo Nabiy (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"يقالُ للرجلِ من أهلِ النارِ يومَ القيامَةِ: أرأَيْتَ لو كان لكَ ما على الأرضِ من شيءٍ أكنتَ مفتديًا بِه؟ فيقولُ: نعم؟ فيقولُ اللهُ: كذبْتَ قدْ أردْتُّ منكَ أهونَ من ذلِكَ، قد أخذتُ عليكَ في ظهرِ آدمَ أن لَّا تُشرِكَ بي شيئًا فأبيتَ إلَّا أنْ تُشْرِكَ"

 

“Mtu katika watu wa motoni ataambiwa Siku ya Qiyaamah:  Unasemaje kama ungelikuwa na chochote katika vilivyoko juu ya ardhi,  je ungeliweza kukitolea fidia?  Atasema:  Ndio.  Na Allaah Azza wa Jalla Atamwambia: Umesema uongo.  Mimi Nilikutaka jambo dogo kuliko hilo. Nilichukua ahadi kwako katika mgongo wa Aadam kwamba usinishirikishe Mimi na chochote, nawe ukakataa, ukashikilia ushirikina”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (3334) na Muslim (2805)]

 

Hadiyth hii tukufu inaonyesha kwamba watoto wote wa Aadam, (yaani sisi wanadamu), wote walikuwa katika mgongo wake wakati ule wa kuumbwa yeye kati ya mabilioni ya wanadamu walioishi na wakafa, na sisi tulio hai kwa sasa tunaojaza pembe zote za dunia kwa zaidi ya watu bilioni saba, na kwa wale ambao bado hawajazaliwa na ambao wanazaliwa kila sekunde mpaka siku ya Qiyaamah.  Wote hawa, (mimi na wewe), tulikuwa kwenye mgongo wa baba yetu Aadam wakati ule alipoumbwa.  Kisha Allaah Mtukufu Alitutoa toka kwenye mgongo wa Aadam, halafu Akatushuhudilisha kwamba Yeye Ndiye Allaah, Muumbaji wa kila kitu, Mmoja Aliye Mpweke, Mwenye kulisimamia kila jambo, Asiye na mshirika katika Ufalme Wake, wala mpinzani katika Madaraka Yake, Asiye na mshabaha na chochote katika viumbe Vyake, na Asiye hitajia mke au mtoto, kwa kuwa hayo ni katika sifa za viumbe Vyake.

 

Na baada ya wanadamu wote kukiri hayo yote wakiwa katika ulimwengu wa roho, Malaika walisema:  "Sisi Tumeshuhudia hayo, msije mkasema Siku ya Qiyaamah sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo.  Au mkasema:  Hakika baba zetu ndio walio shirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao, basi Utatuangamiza kwa sababu ya waliyo yafanya wapotovu!?"

 

Anayejua ukweli na uhakika wa Uungu, bila shaka anajua kwamba Allaah Mtukufu ni Mweza wa kila kitu na Anapolitaka jambo lolote, basi Huliambia kuwa, nalo huwa hapo hapo.

 

Hivyo basi, haya yote yalitimu huko nyuma katika ulimwengu wa kiroho, kisha wanadamu wakaanza kuzaliwa kwa mujibu wa utaratibu Alioupanga Allaah wa kudhihiri kila mmoja katika ulimwengu wetu huu.  Tuko sisi tunaoishi katika enzi hii ya teknolojia, wako walioishi kabla yetu na kuna wengineo mabilioni kwa mabilioni ambao wako njiani kuja kuishi baada yetu sisi.  Sisi Tulikuwa hatujulikani na sasa tumejulikana na hata watoto tunaowatarajia kuwazaa mpaka sasa pia bado hawajulikani, na sisi hatuwajui.  Mababu zetu hawakujua lolote kuhusiana nasi, nasi hatujui lolote kuhusiana na vizazi vijavyo.  Ndio hapa Allaah Anapotuambia katika aya ya mada yetu ya leo:

 

"هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورً

 

Kwa hakika kilimpitia mwana-Aadam kipindi fulani katika dahari, hakuwa kitu kinachotajwa”.  [Al-Insaan: 01]

 

Kila mmoja kati yetu ana tarehe yake ya kuzaliwa, na baadhi yetu husherehekea kila mwaka sikukuu ya kuzaliwa.  Lakini kabla ya tarehe hii, hakuwa mtu ni mwenye kutajika, hakuna amjuaye, hakuna amdhukuruye, hana uwepo wowote, hana utajo, hana jina, hana utambulisho na hana chochote kijulikanacho kuhusu yeye.  Kisha baada ya hapo, mtu huzaliwa akatoka ndani ya tumbo la mama yake, akaanza kunyonyeshwa maziwa ya mama, akiogeshwa na kuvalishwa nepi, huku akiwa hajui chochote katika ulimwengu unaomzunguka.  Kisha kidogo kidogo anaanza kuvaana na mazingira yanayomzunguka akili yake ikiendelea kukua pamoja na mwili wake hadi anapokuwa kijana anayeweza kujitegemea kwa mambo yake yote.

 

Kisha baada ya hapo, anakuwa ni mtu mwenye shani kubwa katika jamii. Anaweza kuwa na shahada ya uzamivu au ya uzamili.  Anaweza kuwa na cheo kikubwa kabisa katika jamii akawa Mfalme, rais, waziri, daktari, mhandisi na kadhalika.  Haya yote anayafikia huku akisahau kwamba yeye alipitikiwa na kitambo cha zama nailhali hakuwa ni mtu mwenye kujulikana au kutajika kabisa.

 

Watu wakubwa duniani, walikuwa ni watoto wadogo, na wakati walipokuwa wadogo, hakukuwepo yeyote anayewajali au kuwatia akilini. Walikuwa wakinyonya maziwa ya mama zao, wakibebwa, wakilishwa, wakilalishwa, wakichungwa wasije kudhurika na vitu wasivyovijua hatari yake, wakijiendea haja wenyewe, wakisafishwa na kuvalishwa.

 

Lakini hawa wote, baada ya kufikia hapo walipo; wakiwa na madaraka makubwa, wakiwa na utajiri mkubwa, na wakiwa na ushawishi mkubwa, wameisahau kabisa safari yao yote ya utotoni na kuwakalia juu Waja wanyonge wa Allaah.  Watu hawa utakuta wakiwanyanyasa watu, wakiwanyonya nguvu zao, wakiwabeza, wakiwadhulumu na mengi mengineyo mabaya.  Baadhi yao hujenga ngome za utukufu wao kwa jasho la wengine, wengine hujenga utajiri wao kwa kuwadhulumu watu, na wengine hujichumia utajiri kwa kuwaua watu.  Na haya bila shaka yako wazi kabisa kwetu sote.  Na hii si tu kuwa iko kwa wakubwa, bali hata kwa wadogo pindi wanapopata nafasi ya kuwaumiza wengine kwa ajili ya maslaha yao.

 

Huyu ndiye mwanadamu ambaye hakuwa hapo kabla ni mwenye kujulikana.  Amemsahau Allaah Aliyemuumba, amemsahau Allaah Aliyemtia sura Aliyeitaka Yeye akiwa tumboni mwa mama yake, amemsahau Allaah Aliyemtoa kwa usahali kabisa toka ndani ya tumbo hilo wakati wa kuzaliwa.

 

"ثُمَّ السَّبِيلَ يَسَّرَهُ"

 

Kisha Akamuwepesishia njia”.  [‘Abasa: 20]

 

Halafu anamsahau Allaah Aliyempa ilhamu ya kunyonya maziwa ya mama hata bila ya kuyaona akiwa kitoto kichanga ambacho hata macho hakijaweza kufungua.   Hata baada ya kufungua macho, hata katika kiza kinene, mtoto hulijua titi la mama yake.  Mtoto huyu hakufundishwa na yeyote namna ya kunyonya, na wala hakusoma kitabu chochote cha kumpa maelekezo.  Utamwona akiweka midomo yake miwili kwenye titi la mama, halafu huikaza vizuri midomo yake, kisha huvuta hewa na kupata maziwa freshi.  Hii ni neema kubwa ya Allaah Aliyetupumzisha na kazi ya kuwafunza watoto namna ya kunyonya maziwa ya mama.

 

 

 

Share