13-Nuru Ya Qur-aan: Dhana Ya Kusimamisha Swalah

 

Nuru Ya Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

13:  Dhana Ya Kusimamisha Swalah:

 

Allaah Ta’aalaa Anasema:

 

"وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ"

 

“Na simamisheni Swalaah”.  [Al-Baqarah: 43]

 

Kusimamisha swalah maana yake ni kuitekeleza katika wakati wake maalumu pamoja na kuhifadhi nguzo zake, wajibu zake, masharti yake pamoja na unyenyekevu na khushuu ndani yake.  Khushuu pamoja na haya tuliyoyataja, ni sababu ya kumfanya Mwislamu afanikiwe katika maisha yake ya hapa duniani na huko akhera.  Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

 

"قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ • الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ"

 

Kwa yakini wamefaulu Waumini ●  Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea”.  [Al-Muuminuwna: 1-2]

 

Maulamaa wamejaribu kuelezea njia kadhaa za kufanikisha suala la khushuu katika swalah.  Njia hizo zimefikia takriban 33, nasi tutajaribu kuzitaja baadhi yake tu hapa ili Mwislamu aweze kuzizingatia na kupata mafanikio hayo yaliyoelezewa na Allaah Mtukufu katika aayah hii.  Njia hizi ni:

 

1-  Kujiandaa na swalah na kujiweka tayari nayo.  Huku kunaanzia tokea pale Mwislamu anapomjibisha mwadhini adhana na kisha kuomba du’aa ya baada ya adhana.  Kabla ya adhana inakuwa pia ni vizuri zaidi kuanza maandalizi ili kudhamini kuipata safu ya kwanza yenye fadhila nyingi sana.  Kisha baada ya hapo kuchukua wudhuu wake kama inavyotakikana kisheria.  Halafu kuvaa kivazi kizuri kabisa ili kuonyesha heshima kwa Allaah, kwani Mwislamu anakuwa kana kwamba anakwenda kumtembelea Allaah katika Nyumba Yake.  Halafu hatimaye kuelekea Masjid katika hali ya utulivu na utuvu, kwani katika hatua zote hizi, Mwislamu anazingatiwa kwamba ashaingia ndani ya wigo wa swalah.

 

2-  Mwenye kuswali kujua na kutambua kwamba Allaah Anamjibisha katika swalah wakati anaposoma Suwrat Al-Faatihah

 

Imepokelewa toka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaah ‘anhu) kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Al-Hadiyth Al-Qudsiy:

 

"إنَّ اللهَ تعالى يقولُ: قَسَّمْتُ الصَّلاةَ بَيْني وَبَيْنَ عَبْدِي نِصْفَيْنِ ، نِصْفُهَا لِيْ وَنِصْفُها لِعَبْدِيْ ولِعَبْدِيْ ما سألَ ، فَإذا قَالَ : الحَمْدُ للهِ ربِّ العَالمين، قالَ اللهُ : حمِدني عَبْدِي ، وإذا قالَ : الرَّحمنِ الرَّحيمِ ، قالَ اللهُ : أَثْنَى عَلَيَّ عَبْدِيْ ، وإذَا قَالَ : مَالِكِ يومِ الدِّينِ، قال اللهُ عَزَّ وَجَلَّ : مجَّدَنِي عَبْدِي، وإذا قالَ : إياكَ نعبدُ وإياكَ نستعينُ، قال : فَهذِهَ الآيةُ بَيْنِي وَبَيْن عبْدِي نِصْفَيْنِ وَلِعَبْدِي مَا سَألَ ، فإذا قالَ : اهدنا الصراطَ المستقيمَ صراطَ الذين أنعمتَ عليهم غيرِ المغضوبِ عليهم ولا الضالينَ،  قال : فهؤلاءِ لعبدي ولعبدي ما سألَ"

 

 

“Hakika Allaah Ta’aalaa Anasema:  Nimeigawanya Suwrat Al-Faatihah kati Yangu na Mja Wangu nusu  mbili, nusu moja ni Yangu na nusu ya pili ni ya Mja Wangu, na Mja Wangu Nitampa analoliomba.

(Mja) anaposema:  “Al-Hamdulil Laahi Rabbil 'aalamiyna”, Allaah Husema:  Mja Wangu Amenihimidi.    Anaposema:  “Ar Rahmaanir Rahiym”, Allaah Husema: Mja Wangu Amenisifu.  Anaposema:  “Maaliki yawmid Diyn”, Allaah ‘Azza wa Jalla Husema:  Mja Wangu Amenitukuza utukuzo mkubwa.  Anaposema:  “Iyyaaka na-'abudu wa iyyaaka nasta'iyn”, Allaah Husema:  Aayah hii ni nusu mbili kati Yangu na Mja Wangu, na Mja Wangu Nitamjibu atakaloliomba. Anaposema:  “Ihdinas swiraatwal mustaqiym, swiraatwal ladhiyna An'amta 'alayhim ghayril maghdhwuubi 'alayhim waladh dhwaalliyna”, Allaah Husema: Haya ni ya Mja Wangu (aliyoyaomba), na Mja Wangu atajibiwa aliyoyaomba”.  [Hadiyth Swahiyh.  Chanzo:  Majmuw’ul Fataawaa (7/14)]

 

Ni nafasi pekee anayoipata Muislamu ya kujibishwa na Mola wake kila siku mara 17 kwenye swalaah za faradhi na nyinginezo za sunnah.

 

Ni nafasi pekee ya kumsifu Allaah, kumtukuza na kumwomba mubashara Atuthibitishe katika Njia Yake iliyonyooka ya wale Aliyowaneemesha kati ya Manabii, Swalihina, Waliosadikisha Imani yao kikweli.   Tukijua hili, basi swalah itakuwa daima ndio kimbilio letu la kufarijika mbele ya Allaah.  Ndio maana Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihii wa sallam alikuwa akimwambia Bilaal:

 

"يا بلالُ، أَقِمِ الصَّلاةَ، أَرِحْنا بها"

 

“Ee Bilaal!  Kimu swalah, tupe faraja za nyoyo kwayo”. 

 

3- Utulivu wa viungo na moyo katika swalah.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipokuwa anaswali, alikuwa akitulia mpaka kila kiungo kinarejea mahala pake.  Baadhi ya wenye kuswali utawalahidhi kwamba hawatulii kabisa baada ya kuingia kwenye swalaah; mara kajikuna kichwa, mara kakamata ndevu, mara kanyoosha nguo yake huku macho yake yakizunguka hapa na pale.  Hii si tabia nzuri kabisa.

 

4-  Kukumbuka mauti wakati wa swalah kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

"اذْكُرِ المَوْتَ في صَلاتِكَ، فإنَّ الرَّجُلَ إذَا ذَكَرَ المَوْتَ في صَلاتِهِ لحَرَيٌّ أَنْ يُحْسِنَ صَلاتَه، وَصَلِّ صَلاةَ رَجُلٍ لا يَظُنُّ أَنْ يُصلِّيَ صلاةً غيرَها، وَإِيَّاك وكلُّ أمرٍ يُعتذرُ منه"

 

“Yakumbuke mauti katika swalah yako, kwani ikiwa mtu atayakumbuka mauti katika swalah yake, basi ni hakika kwamba ataiswali vyema swalah yake.  Swali swalah ya mtu ambaye hana uhakika ya kwamba ataswali swalah nyingine tena.  Na jiepushe na kila jambo utakalokuja kuomba usamehewe”.  [Imesimuliwa na Anas bin Maalik na iko kwenye As-Silsilat As-Swahiyhah (2839).  Isnaad yake ni Hasan.  Imechakatwa na Al-Bayhaqiy katika Az-Zuhdul Kabiyr (527) na Ad-Daylamiy katika Al-Firdaws (1755)].

 

5-  Kuzizingatia aya zinazosomwa na adhkari nyinginezo za swalah na kuchangamkiana nazo.  Mazingatio ya aya hayaji ila kwa kuelewa maana yake, na hili ni kwa wale wenye kufahamu lugha ya Kiarabu.  Ama kwa wale wasio fahamu lugha ya Kiarabu, hawa itawatosha kumsikiliza imamu kisomo chake kwa umakini, kwani usikilizaji huo utawafanya Qur-aan iwaathiri na kuwapa msisimko.

 

6-  Kusoma Qur-aan kwa tartiyl na kwa sauti nzuri.  Allaah Mtukufu Anatuambia:

 

"وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا"

 

“Na soma Qur-aan kwa tartiyl; kisomo cha utaratibu upasao, kuitamka vizuri na kutaamali”.   [Al-Muzzammil: 04]

 

Na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:

 

"زيِّنوا القرآنَ بِأصْواتِكم، فإنَّ الصَّوتَ الحَسَنَ يزيدُ القرآنَ حُسنًا"

 

 “Ipambeni Qur-aan kwa sauti zenu, kwani sauti nzuri huizidishia Qur-aan uzuri”.  [Imechakatwa na Al-Bukhaariy (7544), Abu Daawuwd (1468), An-Nasaaiy (1015), Ibn Maajah (1342), Ahmad (18517) na Al-Haakim (2125)]

 

7-  Kutuliza jicho mahala pa kusujudia bila kugeuka huku wala kule.  Hii husaidia kwa kiasi kikubwa katika kuleta khushuu katika swalah.

 

8-  Kusoma "Isti’aadhah" (أعوذ بالله من الشيطان الرجيم) kwa ajili ya kumweka mbali shetani na swalah.  Kama tujuavyo, shetani ndiye adui wetu mkubwa.  Shetani hujaribu kwa njia zote kumshawishi Mwislamu asiende kwenye swalah. Anaposhindwa hilo, basi humwandama ndani ya swalah yake kwa kumshawishi hadi kumtoa nje kabisa ya khushuu na khudhuu, Mwislamu akatoka kwenye swalah na maksi ndogo kabisa.

 

9-  Kujitahidi kuomba du’aa na hususan wakati wa kusujudu.  Wakati huu mja anakuwa karibu zaidi na Allaah kuliko kipindi kingine chochote.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia:

 

"أَقْرَبُ مَا يَكُونُ الْعَبْدُ مِنْ رَبِّهِ وَهُوَ سَاجِدٌ فَأَكثِرُوا الدُّعَاءَ"

 

 “Wakati ambao mja anakuwa karibu zaidi na Mola wake, ni pale anapokuwa amesujudu.  Basi kithirisheni dua”.  [Hadiyth Swahiyh.  Swahiyh Muslim (482)]

 

Haya ndiyo muhimu yanayosaidia kumfanya mtu aswali kwa khushuu. Mengineyo ya haraka haraka ni pamoja na kutoswali na nguo yenye madoido ya kuvutia, kutoswali wakati chakula kiko tayari mezani, kutoswali wakati mtu amebanwa na haja ndogo au kubwa, kutonyanyua macho juu, kutotema mate mbele bali pembeni, kutoswali nyuma ya mtu aliyelala au anayezungumza na kutogeukageuka katika swalah.

 

 

Share