14-Nuru Ya Qur-aan: Dhana Ya Zaka

 

Nuru Ya Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

14:  Dhana Ya Zaka:

 

Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

 

"وَآتُوا الزَّكَاةَ ۚ"

 

“Na toeni zaka”.  [Al-Baqarah: 110]

 

Zaka kama tujuavyo ndiyo anwani ya kijamii kwa imani ya mtu, ni madh-hari ya kumshukuru Allaah kwa neema Zake, na ni kiunganishi muhimu kati ya watu.

 

Agizo la kutoa zaka limekuja likikutanishwa na agizo la kusimamisha swalah kwa ajili ya kuzisafisha nafusi, kuzitakasa mali na kumtwaharisha mwanadamu, kwa kuwa kila kimoja kinakikamilisha kingine, na kukiacha kimoja, hukidhoofisha kingine.

 

Yeyote mwenye kuisimamisha swalah kama inavyotakikana, hapo ataikuta nafsi yake inasafika, anajikuta akiukumbuka wajibu wa kutoa zaka na kusaidia katika njia za kheri na kutoa msaada wowote unaohitajika kwa wahitajio.

 

Hivyo basi, ikiwa Waislamu wote watasimamisha swalah tano kama inavyotakikana, na wakatoa zaka kwa mpangilio mzuri, basi bila shaka wataishi maisha bora kabisa, wakijawa na utukuko wa kumwabudu Allaah, wakiwa wanyoofu katika matendo yao yote, wakijenga maadili bora kabisa ya Kiislamu, wakiunyanyua umma na kuwa ni wenye furaha hapa duniani na huko akhera.

 

Hakika Mwislamu mwenye kuishi katika hali ya kumwabudu Allaah wakati wote, anajijua kwamba yeye hakuumbwa kwa ajili ya nafsi yake pekee, bali ameumbwa ili awe ni kiungo hai nufaishi katika jamii itakayowageuza watu kuwa ni umma wenye kuishi ndani ya msafara mmoja wa haki, na wenye kumtii Allaah Ta’aalaa wakati wote.

 

Zaka bila shaka ni utakaso wa kinafsi na kisaikolojia.  Tajiri hali yake ya kisaikolojia inakuwa katika hali nzuri mno anapohisi kwamba yeye ni sababu ya furaha ya maelfu ya familia.  Ni wakati ule anapoiona mali yake imekuwa ni furaha kwenye nyuso za watu,  anapoona mali yake imevisha watu na kusitiri miili yao, anapoona mali yake imeyashibisha matumbo yenye njaa, anapoona mali yake imekuwa ni nyumba za kuwahifadhi wanafunzi wanaosoma Qur-aan Tukufu, anapoona mali yake imesomesha vijana wahitimu wa fani mbalimbali za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo na kusukuma mbele Uislamu na dunia kiujumla na kadhalika.  Hii ndio amali bora zaidi ya kuingiza furaha kwenye moyo wa mwanadamu.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"أحَبُّ النَّاسِ إلى اللهِ أنْفَعُهُمْ لِلنَّاسِ، وَأَحَبُّ الأعْمَالِ إلى اللهِ عزَّ وجلَّ سُرُورٌ يدْخِلُهُ عَلَى مُسْلِمٍ"

 

“Mtu anayependeka zaidi kwa Allaah ni yule mwenye kuwanufaisha zaidi watu, na amali inayopendwa zaidi kwa Allaah ‘Azza wa Jalla ni furaha anayoiingiza mtu kwa Muislamu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na At-Twabaraaniy (6026).  Iko katika Silsilat As-Swahiyhah (906)]

Hivyo basi, Mwislamu anatakiwa asije kufanya ubakhili wa mali yake akashindwa kuja kutoa zakatul maali au kutoa sadaka.  Allaah Ametoa onyo kali kwa wale wote wenye kufanya ubakhili hata kufikia kushindwa kutoa zaka. Anatuambia:

 

"وَلَا تَحْسَبَنَّ اللَّـهَ غَافِلًا عَمَّا يَعْمَلُ الظَّالِمُونَ ۚ إِنَّمَا يُؤَخِّرُهُمْ لِيَوْمٍ تَشْخَصُ فِيهِ الْأَبْصَارُ"

 

“Na wala usidhanie kabisa kwamba Allaah Ameghafilika na yale wanayoyatenda madhalimu.  Hakika Anawaakhirisha kwa ajili ya Siku ambayo macho yatakodoka (kwa kiwewe)”.   [Ibraahiym: 42]

 

Maana ya aya hii tukufu ni kwamba Allaah ‘Azza wa Jalla Ndiye Ampaye Amtakaye, na Ndiye Amnyimae Amtakaye, na hii yote ni kwa Hikma Yake ya juu kabisa.  Basi yule ambaye Allaah Atampa mali hapa duniani ambayo mali hiyo ni katika Fadhila Zake Allaah, basi asifanye ubakhili na choyo akaizuia na kuwanyima wengineo.  Ubakhili uliokusudiwa katika aya hii tukufu ni kutoitoa zaka stahiki kwa wenye kustahiki kwa mujibu wa walivyotajwa kwenye Qur-aan Tukufu.  Ubakhili huu wa kuzuia zaka, si kheri kwa mzuiaji kama anavyodhani mwenyewe, bali ni shari kwake, kwa kuwa Allaah Ta’aalaa Amekufanya kuyatoa mali kwa ajili Yake kuwa ndiyo sababu ya kuzidi mali na kuongezeka kinyume na ubakhili ambao hatima yake ni kuteketea mali na kuangamia hapa duniani, na huko akhera kuna adhabu chungu inayomsubiri.  Adhabu hiyo kama ilivyoelezewa na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ni mali yake kugeuka na kuwa joka kubwa lenye upara na ndimi mbili kali litakalomwadhibu Siku ya Qiyaamah. Aidha, mali za wasio toa zaka, zitageuka na kuwa moto utakaozichoma nyuso zao, mbavu zao na migongo yao.  Hayo yote ni kutokana na ubakhili wa kutoa zaka ya mali ambayo mtu hakuichuma kwa akili yake wala kwa jasho lake, bali kwa tawfiyq kutoka kwa Allaah Mtukufu.

 

 Toka kwa Abu Hurayrah kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"مَنْ آتَاهُ اللَّهُ مَالاً فَلَمْ يُؤَدِّ زَكَاتَهُ، مُثِّلَ لَهُ يوم القيامة شُجَاعًا أَقْرَعَ، لَهُ زَبِيبَتَانِ يُطَوَّقُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ، ثم يَأْخُذُ بِلِهْزِمَتَيْهِ ـ يَعْنِي شِدْقَيْهِ ـ ثم يَقُولُ أَنَا كنزك أنا مَالُكَ ‏.‏ ثُمَّ تَلاَ هَذِهِ الآيَةَ ‏: وَلاَ يَحْسِبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّهُ مِنْ فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖ ... بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ"

 

“Mtu ambaye Allaah Amempa mali naye asiitolee Zakaah yake, basi ataundiwa kwa mali hiyo Siku ya Qiyaamah mfano wa joka lenye kichwa cheupe (upara), lina mabaka meusi juu ya macho yake, litamviringa Siku ya Qiyaamah.   Kisha litambana kwa taya zake mbili liseme:  Mimi ni hazina ya mali yako, mimi mali yako.  Kisha akasoma Aayah hii:

 

"وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُم ۖ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ ۖ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُوا بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ وَلِلَّـهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ"

 

“Wala wasidhani kabisa wale wanaofanya ubakhili kwa yale Aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kwamba hayo ni khayr kwao, bali ni shari kwao.  Watafungwa kongwa yale waliyoyafanyia ubakhili Siku ya Qiyaamah.  Na ni Wake Allaah Pekee urithi wa mbingu na ardhi.  Na Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika”.   [Al-Bukhaariy (1403)]

 

“Toka kwa Abu Hurayrah amesema:  “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  Hakuna yeyote mwenye hazina ya mali ambayo haitolei Zakaah, isipokuwa atapashiwa moto kwenye moto wa Jahannam, kisha ifanywe vipande vipana [vya metali], achomwe navyo mbavu zake na kipaji chake mpaka pale Allaah Atakapohukumu kati ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini.  Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni.  Na hakuna yeyote mwenye kumiliki ngamia na asiwatolee Zakaah yake, isipokuwa atatandazwa kifudifudi mbele yao kwenye ardhi pana tambarare, wakiwa wakubwa kama walivyokuwa, watamkanyaga, kila wanapomaliza kumkanyaga wa mwisho wao, wa mwanzo wao watarejeshwa kumkanyaga tena mpaka Allaah Atakapohukumu baina ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini.  Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni.  Na hakuna yeyote mwenye kumiliki mbuzi na kondoo na asiwatolee Zakaah yake, isipokuwa atatandazwa kifudifudi mbele yao kwenye ardhi pana tambarare, wakiwa wakubwa kama walivyokuwa, watamkanyaga kwa kwato zao, na watampiga kwa pembe zao, hakuna kati yao mwenye pembe zilizopinda wala asiye na pembe, kila wanapomaliza kumkanyaga wa mwisho wao, wa mwanzo wao watarejeshwa kumkanyaga tena mpaka Allaah Atakapohukumu kati ya Waja Wake katika siku ambayo urefu wake ni miaka elfu khamsini katika mnayohesabu.  Halafu ataonyeshwa njia yake, ima ya kwenda Peponi, au ya kwenda motoni…”. [Muslim (987) na Abu Daawuwd (1642)]

 

 

Share