15-Nuru Ya Qur-aan: Dhana Ya Hijja: (a) Mwitiko Wa Nguvu Wa Waumini Na Shauku Kubwa Ya Kufanikisha ‘Amali Hii

 

Nuru Ya Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

 

15:  Dhana Ya Hijja:  (a)  Mwitiko Wa Nguvu Wa Waumini Na Shauku Kubwa Ya Kufanikisha ‘Amali Hii:

 

Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Ameifanya Nyumba Takatifu ya Makkah kuwa ni mahala pa kujikurubisha Kwake.  Ameifanya Nyumba hii kuwa ni mahala pa kumwabudu Yeye na mtu kujipa nafasi na wasaa wa kumwabudu Yeye tu.  Na kwa ajili hiyo, imekuwa ni katika hikma ya amali ya hijja kwamba Allaah Mtukufu Amewaamuru Waumini waiendee Nyumba hiyo wakiacha nyuma yao nyumba zao, wake zao, watoto wao, mali zao, kazi zao, starehe zao, burudani zao na kila kile kinachowashughulisha katika dunia yao, ili dunia hii isiwe ni kikwazo kati ya mja na Mola wake.

 

Allaah Mtukufu Amewaamuru watu wamwendee Yeye na wajiweke mbali na dunia yao.  Na wanapofika kwenye Ardhi Takatifu na kuanza amali za hiJja, hapo Anawaharamishia baadhi ya mambo ambayo kwa kawaida ni halali kwao kama kuvaa nguo iliyoshonwa kwa wanaume.  Shuka mbili wanazovaa wanaume, huwasahaulisha mavazi yao mazuri ya mitindo tofauti wanayovaa, viatu vyao vya aina tofauti na mapambo mengineyo huku mkusanyiko wao wa pamoja toka pande zote za dunia, ukiwakumbusha saa ya kufufuliwa na saa ya kukusanywa viumbe vyote vya kuanzia mwanzo hadi mwisho.

 

Katika amali hii ya hijja, Allaah Amewaamuru Waislamu wafunge safari toka makwao hadi Makka na waache kila kitu chao.  Na hapa bila shaka Anataka kuwakumbusha kwamba kuna kitu kiitwacho kuiacha dunia kupitia mauti.  Hijja hii inakuwa ni kama ukumbusho wa siku ya mwisho inayomsubiri kila mwanadamu ambapo ataondoka hapa duniani na kuelekea akhera kwa Mola wake Mtukufu.  Na hili halina shaka kwa yeyote.

 

Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Ameifanya Nyumba Hii kuwa ni mahala patakatifu na Akaiita "Haram" kwa kuwa ni haramu kufanya katika Nyumba hii jambo lolote lenye kumuudhi kiumbe.  Kuna Miezi Mitakatifu ambapo inakuwa ni kosa kubwa sana kutenda madhambi katika miezi hiyo, kama ambavyo imekatazwa kupigana ndani ya Msikiti Mtakatifu wa Makka, kulipiza kisasi, kufanya uadui au kuua kiwindwa jambo ambalo sehemu nyingine ni halali.  Yeyote mwenye kuingia kwenye Nyumba hii basi huyo yuko salama hata kama inabidi auawe.  Na hii yote inaonyesha utukufu wa sehemu hiyo.  Hapo ni mahala pa ibada tu, mahala pa kutaabudia, mahala pa kuitakasa nafsi, mahala pa kujiweka mbali na dunia, migogoro yake, matatizo yake na mivutano yake.  Ni mahala pa kuwakumbusha watu Siku ya Mwisho, na kuwakumbusha kwamba watahamia na kugura kwa Mola wao.  Na kwa ajili hiyo, inabidi kila mwenye kuweko kwenye Nyumba hiyo, autumie wakati wake wote kwa ajili ya kulifanya kila lile litakalomkurubisha kwa Allaah Mtukufu.

 

Na Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa kutokana na hekima Zake, Ameijaalia Al-Ka’aba kuwa katika bonde lisilo na mmea wowote, wala mvua wala hali nzuri ya hewa.  Amefanya hivi ili asiikusudie sehemu hiyo isipokuwa mwenye nia ya kuhiji tu.  Na lau kama ingelikuwa kwenye bonde lenye mimea, hali nzuri ya hewa, maziwa, milima ya kijani, mito inayobubujika na kadhalika, basi wangeliiendea Mahujaji na watalii.  Lakini kwa mujibu wa hali yake hiyo, haiendewi isipokuwa na mwenye kuhiji pekee ingawa joto la Makka ni kali pamoja na msongamano mkubwa wa Mahujaji toka pande zote za dunia.  Na la kushangaza, pamoja na joto kali au msongamano mkubwa au tabu nyinginezo wanazokabiliana nazo mahujaji, utawasikia baadhi yao wakisema:  "Sikuonja katika maisha yangu neema na furaha kama ya hijja hii".  Kana kwamba kuna mmetuko wa utwaharifu kwa Mahujaji hawa toka kwa Allaah Mtukufu, kwani Mahujaji hawa ni Wageni Wake.  Mwislamu anapoingia kwenye msikiti wowote kwa ajili ya ibada katika nchi yake, hawezi kupata hisia na furaha kama hii ingawa Allaah Humkirimu mwisho wa kumkirimu anapokuwa ndani ya msikiti.

 

Ikiwa mambo yenyewe yako hivi ikiwa utaingia kwenye msikiti wowote nchini kwako kwa ajili ya kufanya ibada, basi hali itakuwaje ikiwa utatafuta pesa za halali, kisha ukafunga safari hadi Makkah ukiacha mambo yako yote nyuma kwa ajili ya kuitikia wito wa Mola wako wa kutekeleza faradhi ya hijja?!!  Kwa ajili hiyo, Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema katika Hadiyth yake tukufu:

 

"لَا تُشَدُّ اَلرِّحَالُ إِلَّا إِلَى ثَلَاثَةِ مَسَاجِدَ: اَلْمَسْجِدِ اَلْحَرَامِ، وَمَسْجِدِي هَذَا، وَالْمَسْجِدِ اَلْأَقْصَى "

 

“Mtu asifunge safari isipokuwa kuiendea Misikiti Mitatu:  Al-Masjidul Haraam (Makkah), Masjid yangu hii (Madiynah), na Al-Masjidul Al-Aqswaa (Palestina) ”.  [Hadiyth Swahiyh.  Al-Bukhaariy (1197) na Muslim (2/975)]

 

Misikiti hii Mitatu ina hadhi yake maalumu mbele ya Allaah Mtukufu.

 

Bila shaka haiingii akilini Allaah kukuita wewe toka nchini mwako ufunge safari yako yote toka popote pale ulipo hapa duniani ukaacha mambo yako yote, kisha ukaenda halafu Allaah Asikukikirmu inavyopasa kukirimiwa.  Hili bila shaka ni katika mambo yasiyowezekanika.  Na kwa ajili hiyo, Allaah Anatuambia:

 

"لِيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ""

 

“Ili washuhudie manufaa yao”.

 

Maulamaa katika kuifasiri aya hii wanasema kwamba kuna manufaa ya kiroho na kuna manufaa ya kidunia.  Hijja pamoja na kuwa kwake ibada tukufu, vile vile huwafanya Waislamu kukutana toka pande zote za dunia wakiwa na lugha tofauti, rangi tofauti, desturi tofauti, uraia tofauti na kadhalika, lakini wote wanajikuta kwamba wao ni umma mmoja wakiunganishwa na Uislamu pamoja na tofauti zao hizo.  Hilo bila shaka huwazidishia imani zaidi, mahaba zaidi, mshikamano zaidi na mapenzi zaidi kati yao.  Na hapa ndipo linapothibitika neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"تَرَى المُؤْمِنِينَ في تَراحُمِهِمْ وتَوادِّهِمْ وتَعاطُفِهِمْ، كَمَثَلِ الجَسَدِ، إذا اشْتَكَى عُضْوًا تَداعَى له سائِرُ جَسَدِهِ بالسَّهَرِ والحُمَّى"

 

 

“Utawaona Waumini katika kuoneana kwao huruma, kupendana kwao, na kufanyiana kwao upole, ni kama kiwiliwili kimoja.  Ikiwa kiungo chochote kitashtakia (adha), basi mwili mzima utaitana kwa ajili ya homa na kukesha”.  [Hadiyth Swahiyh.  Muslim (2586) na Al-Bayhaqiy (91)]

 

Mwislamu kwa ibada hii, huondoka na hisia na kumbukumbu ambayo itakuwa ni vigumu mno kufutika katika akili yake mpaka siku yake ya mwisho ya kuondoka hapa duniani.  Mbali na manufaa hayo, wafanyabiashara pia hutumia nafasi hii kukaguakagua bei za vitu na aina ya biashara ambayo wanaweza kuchukua na faida nyinginezo kemkem zinazopatikana kwa amali hii ya hijja.

 

Mwislamu aliyehiji hija ya kisawasawa, utamwona anatamani ahiji kila mwaka kutokana na athari njema iliyomganda katika nafsi yake.  Anatamani lau kama masiku ya umri wake wote yangelikuwa ni hija.  Huyu ndiye yule aliyeutumia wakati wake wote vyema wakati akiwa katika pilikapilika za hijja kama Anavyosema Allaah:

 

"لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ"

 

“Ili wahudhurie kupata manufaa yao, na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu”.  [Al-Hajji 28]

 

Mwenye kuhiji katika masiku haya machache ya kufanya amali za hija hujaribu kwa nguvu zake zote kumdhukuru Allaah Mtukufu wakati wote anapokuwa katika pilikapilika za amali za hijja.  Anapolala na kuamka, hujikuta akimdhukuru Allaah, akikutana na wenzake hujikuta akimdhukuru Allaah. 

 

Hijja yote kwake inakuwa ni dhikri, hijja yote kwake ni dua, hija yote kwake ni swalah na maombi, na hijja yote ni mawasiliano ya moja kwa moja kati ya Allaah na Waja Wake.

 

 

 

Share