16-Nuru Ya Qur-aan: Dhana Ya Hijja: (b) Manufaa Makuu Ya Hijja
Nuru Ya Qur-aan
16: Dhana Ya Hijja: (b) Manufaa Makuu Ya Hijja:
Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"لِّيَشْهَدُوا مَنَافِعَ لَهُمْ وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ ۖ فَكُلُوا مِنْهَا وَأَطْعِمُوا الْبَائِسَ الْفَقِيرَ"
“Ili wahudhurie kupata manufaa yao, na walitaje Jina la Allaah katika siku maalumu kupitia yale Aliyowaruzuku kati ya wanyama wenye miguu minne wa mifugo. Basi kuleni sehemu yake, na lisheni mwenye shida fakiri”. [Al-Hajj: 28]
Hapa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anawaasa Waislamu wamdhukuru kwa wingi sana Yeye katika masiku maalumu kutokana na neema kubwa Aliyowapa kutoka kwa wanyama wa kufugwa; ngamia, ng’ombe, mbuzi na kondoo. Wanyama hawa kwetu ni neema kubwa sana ambayo Allaah Ametupa. Allaah Ametuwezesha kupata manufaa kutoka kwa wanyama hawa kama nyama, maziwa, ngozi na kadhalika, kutokana na kuwapa hulka na tabia ya sisi kuweza kuwadhibiti bila ya matatizo yoyote. Ngamia pamoja na ukubwa wake na nguvu zake, utamkuta akiongozwa na mtoto mdogo kabisa bila ya matatizo yoyote, lakini nyoka hata awe ni mdogo vipi, utakuta watu wote wanamwogopa na hakuna yeyote awezaye kumdhibiti. Hivyo basi, lau kama Allaah Angelipandikiza kwa wanyama hawa tunaowafuga hulka ya wanyama wakali kama fisi, simba, chui na kadhalika, basi bila shaka tusingeliweza kufaidika nao kabisa.
Hivyo basi, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anawaambia mahujaji kwamba wale sehemu ya nyama ya wanyama hawa waliowachinja na wawalishe nyama hiyo wenye shida waliyo mafakiri. Na kwa ajili hiyo, wanachuoni wamejuzisha mwenye kuhiji ale sehemu ya nyama. Na kama tunavyojua, mwenye kuhiji anaweza kufanya “Ifraad”, anaweza kufanya “Tamattui”, na anaweza kufanya “Qiraan”. Mwenye kufanya “Ifraad”, huyu halazimiki kuchinja. Ama mwenye kufanya “Tamattui” au “Qiraan”, huyu ni lazima kuchinja. Kuchinja kwa mwenye kufanya “Tamattui”, kunakuwa ni kwa kuunga (jabr), na mwenye kufanya “Qiraan” inakuwa ni kama zawadi ya shukrani, kwa kuwa Allaah Amemsaidia na kumwezesha kufanya ‘umrah pamoja na hijja. Na kwa ajili hiyo, ni juu yake kuchinja mnyama wa shukrani. Ama mwenye kufanya “Tamattui”, huyu atachinja mnyama wa kuunga, kwa kuwa yeye amefanya ‘umrah, kisha akafanya tahalluli, halafu akaja tena kuhirimia toka Makkah muda mdogo kabla ya kuanza hijja. Huyu inakuwa juu yake kuchinja mnyama wa kuunga.
Maulamaa wamejuzisha mwenye kuhiji ale sehemu ya nyama aliyochinja ima kwa njia ya sunna, au kwa njia ya wajibu, au kwa njia ya mubaha. Atakula sehemu ndogo tu, kisha sehemu iliyobaki atawalisha masikini asiyeomba na masikini aombaye. Mnyama aliyechinjwa kama kafara ya kosa alilolifanya mwenye kuhiji, au kwa ajili ya kutekeleza nadhiri, basi hapo mwenye kuhiji anatakikana asile chochote katika nyama ya mnyama aliyemchinja.
Kisha Allaah Anaendelea kutuambia:
"ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ "
“Kisha wajisafishe taka zao, na watimize nadhiri zao, na watufu kwenye Nyumba ya Kale (Al-Ka’bah)”. [Al-Hajji: 29]
Mwanadamu wakati anapokata kucha zake anakuwa anaondosha uchafu wa mwili wake. Anaponyoa nywele za kichwa na hata za kinenani, anaondosha uchafu. Anapooga na kuondosha jasho la mwili, anakuwa akiondosha uchafu wa mwili wake. Mwenye kuhiji baada ya kuhirimia tarehe nane mfungo tatu (Siku ya At-Tarwiyah), au kwa mwenye kufanya “Tamattui” ambapo huhirimia umra na kuendelea na hijja, hao wote huendelea kuwepo ndani ya ihramu yao kwa siku kadhaa bila kuoga, bila kugusa manukato, bila kunyoa na bila ya kuvaa nguo ya kushonwa huku wakikabiliana na mikikimikiki ya amali za hijja ya kupanda na kushuka, wakitokwa jasho, wakiparazana na mahujaji wenzao na hasa katika kipindi cha joto kali, na hata wakati mwingine wakikabiliana na vumbi ikiwa ni siku ya upepo. Yote haya huifanya miili yao kuwa katika hali ya uchafu. Baada ya yote haya, unapokuja wakati wa kufanya tahalluli, Allaah Anawaambia:
“Kisha wajisafishe taka zao, na watimize nadhiri zao, na watufu kwenye Nyumba ya Kale (Al-Ka’bah)”.
Mahujaji baada ya kutupia Jamaratul Aqabah, na baada ya kuchinja, kunyoa na kuoga, wanakuwa wamefanya tahalluli ya kwanza. Hapa wanaweza kufanya kila lile lililokuwa haramu kulifanya isipokuwa tendo la ndoa. Na wanapotufu Twawafur Rukni, yaani Twawaaful Ifaadhwah, hapo kila kitu kilichokuwa marufuku kitakuwa ni halali kwao ikiwemo kuwaingilia wake zao.
Na Allaah Anapotuambia:
وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ "
“Na watufu kwenye Nyumba ya Kale (Al-Ka’bah)”. [Al-Hajji: 29]
Maulamaa wa lugha wanatueleza kwamba kitenzi "طَوَّفَ" (Twawwafa) hapa kiko katika uzani wa "فَعَّلَ" (shadda juu ya ‘ayn), na uzani huu wa "فَعَّلَ" unakuja mara zote kwa ajili ya kuonyesha wingi au ukaririfu wa kitenzi au kitendo. Wanasema kwa mfano kitenzi "كَسَّرَ"(Kassara) si sawa na "كَسَرَ" (Kasara). "كَسَّرَ" inakuwa na maana amevunjavunja vipande vipande wakati "كَسَرَ" ina maana amevunja ima kidogo tu au vipande viwili.
Hivyo basi, Allaah Ta’aalaa Anaposema hapa وَلْيَطَّوَّفُواkwa kutumia kitenzi "طَوَّفَ" katika uzani wa "فَعَّلَ" , basi hapa kwa mujibu wa Maulamaa hawa mabingwa wa Lugha, ina maana kwamba watu wakithirishe kuitufu Al-Ka’aba. Na hili ndilo alilolifahamu Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Uchache wa mizunguko (ashwatw) katika Al-Ka’aba ni minne tu, na huu ndio wajibu, lakini sunnah ni mizunguko saba. Yeyote mwenye kuzunguka mizunguko minne kisha akapoteza fahamu au akashindwa kukamilisha kwa sababu yoyote ile, basi huyo anakuwa ashatekeleza faradhi yake.
Na Al-Ka’aba hii wanayoizunguka mahujaji, imeitwa kongwe kwa kuwa ndiyo nyumba kongwe zaidi katika uso wa dunia, au kwa kuwa kwake iko huru haijaguswa na mikono yoyote ya wavamizi au watawala madikteta. Neno "العَتِيْقُ" lina maana ya kongwe au iliyo huru. Vita vyote vilivyoshuhudiwa na ulimwengu wa Kiislamu, hakuna vita vyovyote vilivyofanikiwa kuingia kwenye Al-Ka’aba Tukufu na Al-Ka’aba kuwa chini ya utawala wa kiongozi dikteta.
Maana nyingine ni kuwa kila mwenye kuingia ndani ya Nyumba hii huku akiwa ni mwenye kumtakasia Allaah ibada, basi Allaah Humwacha huru na moto. Na hii pia inawahusu mahujaji ambao Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia katika Hadiyth yake:
"مَنْ حَجَّ فَلَمْ يَرْفُثْ وَلَمْ يَفْسُقْ رَجَعَ كَيَوْمِ وَلَدَتْهُ أمُّهُ"
“Mwenye kuhji, halafu asiingilie au kufanya tendo lolote baya, basi hurejea kama siku aliyozaliwa na mama yake”. [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na kwa ajili hiyo, Maulamaa wanatuambia kwamba mwenye kumiminika toka ‘Arafaat na wala dhana yake haikulemea ya kwamba Allaah Amemsamehe makosa yake, basi huyo hana hijja. Ni kwa nini? Ni kwa kuwa mtu huyo ametoka mbali maelfu ya kilometa kwa mujibu wa eneo lake kijiografia, akalipa gharama zote za safari, akaacha shughuli zake zote na kuwaacha watu wake wote, kisha akaja Makkah kwa ajili ya hijja. Kwa nini amekuja? Je, si kwa ajili ya kutafuta na kutaka maghfira ya Mola wake? Basi ni kwa nini baada ya yote hayo asihisi kwamba ameghufiriwa madhambi yake? Huyu inabidi ajitafiti vizuri kuanzia chumo lake na matendo yake yote mengineyo. Huenda chumo lake ni la haramu, huenda ana haki za watu ambazo hataki kuzirejesha na kadhalika. Na Allaah Hatokubali kwa hali yoyote amali kama hii iliyofanywa kutokana na chumo la haramu. Na hata du’aa ya mtu mwenye kula vya haramu, Allaah Haikubali kamwe sembuse ibada zinginezo zote.
Allaah Ta’aalaa Anaendelea kutuambia:
"ذَٰلِكَ وَمَن يُعَظِّمْ شَعَائِرَ اللَّـهِ فَإِنَّهَا مِن تَقْوَى الْقُلُوبِ"
“Hayo ndio hivyo. Na yeyote anayeadhimisha Ishara za Allaah, basi hayo ni katika taqwa ya nyoyo”. [Al-Hajj: 32]
"شَعَائِرُ" ni wingi wa "شَعِيْرَةُ" , na maana yake ni alama au ishara yenye kutaarifu amali ya hijja au ibada yoyote ile. Al-Ka’aba ni katika Alama za Allaah, Al-Baytul Haraam ni katika Alama za Allaah, Al-Haram ya Makka pamoja na mipaka yake yote ni katika Alama za Allaah, Msahafu ni katika Alama za Allaah, Msikiti wowote ni katika Alama za Allaah, Muumini ni katika Alama za Allaah, mwenye kutafuta ‘ilmu ya dini anakuwa ni katika Alama za Allaah na kadhalika. Alama zote hizi ni lazima ziheshimiwe na kutukuzwa. Na hata ngamia na wanyama wengineo wanaopelekwa Makkah kwa ajili ya kuchinjwa wanakuwa ni katika Alama za Allaah. Allaah Anatuambia:
"وَالْبُدْنَ جَعَلْنَاهَا لَكُم مِّن شَعَائِرِ اللَّـهِ لَكُمْ فِيهَا خَيْرٌ ۖ فَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ عَلَيْهَا صَوَافَّ"
“Na ngamia na ng’ombe Tumekufanyieni kuwa ni miongoni mwa Ishara za Allaah; kwa hao mnapata khayr nyingi. Basi tajeni Jina la Allaah juu yao wanapopangwa safu (kuchinjwa)”. [Al-Hajji: 36]
