17-Nuru Ya Qur-aan: Dhana Ya Hijja: (c) Matunda Mema Ya Baada Ya Kuhiji

 

Nuru Ya Qur-aan

 

Alhidaaya.com

 

17:  Dhana Ya Hijja: (c) Matunda Mema Ya Baada Ya Kuhiji

 

Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

 

"قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ   لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ"

 

 

“Sema:  Hakika Swalaah yangu, na ‘ibaadah yangu ya kuchinja, na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu.   Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza (katika ummah huu)”.  [Al-An’aam: 162-163]

 

Hivi ndivyo Waislamu wote duniani tunavyowashuhudia wenzetu waliopewa khatua ya kutekeleza nguzo ya tano ya Uislamu Hijja wakirejea makwao baada ya kuimaliza safari ya kiimani iliyojaa Baraka na kuwajumuisha Waislamu toka pembe zote za dunia.  Hawa wote pamoja na tofauti zao za kilugha, kiutaifa, kitamaduni na mengineyo, walijumuishwa pamoja na wito wa Allaah Ta’aalaa  wa kuitekeleza nguzo hiyo kupitia kwa Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis Salaam) tokea miaka maelfu iliyopita.  Mjumuiko wao huu ukawathibitishia kwamba wao ni umma mmoja na Mola wao ni Mmoja na hakuna ubora kati ya Mwarabu juu ya asiye Mwarabu, wala mweupe juu ya mweusi isipokuwa kwa uchaMungu.  Hao wote tuna matarajio makubwa kabisa kwamba wanarejea makwao hali ya kuwa wamesamehewa madhambi yao yote kutokana na neno lake Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) asemaye:

 

"مَنْ حَجَّ لِلَّهِ فَلَمْ يَرْفُثْ وَلَمْ يَفْسُقْ، رَجَعَ كَيَوْمِ وَلَدَتْهُ أُمُّهُ"

 

“Atakayehiji, kisha asifanye jimai na vitangulizi vyake (au maneno ya ovyo), au lolote la kumtoa nje ya mstari wa utiifu kwa Allaah, basi hurudi na kuwa kama siku aliyozaliwa na mama yake”.  [Hadiyth Swahiyh.  Bukhaariy (1521) na Muslim (1350)]

 

Miongoni mwa siri kubwa za hijja ni kuwa hijja inatuunganisha na kiongozi wetu mkuu Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyetuambia:

 

"خُذُوا عَنِّيْ مَنَاسِكَكُمْ"

 

“Jifunzeni kutoa kwangu amali zenu za Hijja”.  [Abu Daawuwd (2877), Ahmad (15041) na Ibn Khuzaymah]

 

Hivyo basi, aliyefanya amali zake zote za hijja kwa mujibu wa maelekezo ya Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi huyo bila shaka, atakuwa akijitahidi kuishi maisha yake yote juu ya uongofu wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kazi zake, shughuli zake, ibada zake na kila hatua zake zote za kimaisha mpaka siku yake ya mwisho ya kuondoka hapa duniani.  Wakati wote anakuwa akilikumbuka Neno Lake Ta’aalaa kama tulivyoanza mwanzoni:

 

"قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ"

 

 

“Sema:  Hakika Swalaah yangu, na ‘ibaadah yangu ya kuchinja, na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah Pekee Rabb wa walimwengu. ●  Hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza (katika ummah huu)”.  [Al-An’aam: 162-163]

 

Maisha yote ya mwanadamu bali hata umauti wake, ni lazima uwe kwa mujibu wa njia na uongofu wa Allaah Ta’aalaa na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam).  Akiswali aswali kwa mujibu wa alivyoelekeza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akifunga ni lazima afunge kama alivyoelekeza Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akifanya lolote lile ni lazima liwe juu ya msingi wa methodolojia ya Allaah na Rasuli Wake, na kinyume na hivyo, mtu ataangamia.

 

Na kati ya siri nyingine ya hajji na manufaa yake, ni kuzilea nafsi juu ya utwaharifu na adabu ya hali ya juu kabisa.  Allaah Ta’aalaa Anatuambia:

 

"الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ ۚ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلَا رَفَثَ وَلَا فُسُوقَ وَلَا جِدَالَ فِي الْحَجِّ ۗ وَمَا تَفْعَلُوا مِنْ خَيْرٍ يَعْلَمْهُ اللَّـهُ ۗ وَتَزَوَّدُوا فَإِنَّ خَيْرَ الزَّادِ التَّقْوَىٰ ۚ وَاتَّقُونِ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ"

 

“Hajj ni miezi maalumu.  Na atakayekusudia kuhiji ndani ya miezi hiyo (akahirimia), basi asifanye tendo la ndoa wala ufasiki wala mabishano katika Hajj. Na lolote la khayr mlifanyalo basi Allaah Analijua.  Na chukueni masurufu, kwani hakika bora ya masurufu ni taqwa.  Na nicheni Mimi enyi wenye akili!  [Al-Baqarah: 197]

 

 

Tukirudi kiuchambuzi kwenye aya hizi tukufu, tunasema:  Kwanza kabisa, sababu ya kushushwa kwake kwa mujibu wa wanavyosema Mufassiruna ni kuwa washirikina walikuwa wakiyaabudu masanamu na wakichinja wanyama kwa ajili yake.  Na hapo Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Akamwamuru Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Waumini  waende kinyume na hayo wanayoyafanya washirikina hao kwa kuyaelekeza makusudio yao, hima zao na yote wanayoyafanya kwa ajili Yake Allaah Ta’aalaa Peke Yake.

Pili, tukijaribu kuchanganua neno moja baada ya jingine tunasema, Allaah Ta’aalaa Anaposema "صَلَاتتِيْ" , Mufassiruna wanasema makusudio yanaweza kuwa kwa maana ya swalah kijumuishi yaani dua yangu, unyenyekevu wangu na ibada yangu.  Au inaweza kuwa kwa maana ya swalah za faradhi na za sunnah ambazo mimi ninaziswali kwa ajili ya Allaah Ta’aalaa Peke Yake bila ya kumshirikisha na chochote.  Na hapo ikiwa kwa maana ya swalah za faradhi ambazo ni tano, tutakuta kwamba hiyo ni nguzo kuu ya pili kati ya nguzo za Kiislamu ambayo haipomoki kwa Mwislamu vyovyote hali yake itakavyokuwa.  Ni lazima kila Mwislamu atekeleze swalah tano kwa hali yoyote ya uzima na ugonjwa na hata katika wakati wa vita.  Shahada moja inamtosha Mwislamu kuthibitisha Uislamu wake, swaumu inaweza kupomoka kwa Mwislamu kama hawezi kufunga, hajji kama mtu hana uwezo wa kimali na kiafya hawajibikiwi, lakini swalah ni wajibu katika hali zote.  Kama mtu hawezi kusimama ataswali kwa kukaa, kama hawezi kwa kukaa, ataswali kwa kulala kwa ubavu, au chali na kadhalika isipokuwa tu kama amepoteza fahamu.  Lakini fahamu zinapomrejea ni lazima ailipe swalah iliyompita.

 

Hivyo basi, Allaah Ta’aalaa Anapomwambia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aseme hapa "Hakika swalah yangu", Anataka kutukumbusha sisi kwamba swalah ndiyo nguzo kuu ya Uislamu ambayo inabidi tuishikilie kwa magego yetu na kwa nguvu na hali zetu zote..
 

·        Hadhi Ya Swalaah Katika Uislamu:

 

1-  Swalah ndiyo faradhi iliyosisitiziwa na iliyo bora zaidi baada ya shahada mbili na ni moja kati ya nguzo za Kiislamu.

 

Imepokelewa na Ibn 'Umar (Radhwiya Allaah ‘anhumaa) kwamba Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:



"بُنِيَ الإسْلَامُ علَى خَمْسٍ: شَهَادَةِ أنْ لا إلَهَ إلَّا اللَّهُ وأنَّ مُحَمَّدًا رَسولُ اللَّهِ، وإقَامِ الصَّلَاةِ، وإيتَاءِ الزَّكَاةِ، والحَجِّ، وصَوْمِ رَمَضَانَ"

 

“Uislamu umejengewa juu ya (nguzo) tano:   Kushuhudia kwamba hapana mungu mwingine isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Rasuli wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zaka, kuhiji na kufunga Ramadhani”.   [Hadiyth Swahiyh.  Imechakatwa na Al-Bukhaariy (08) na Muslim (16)]

 

 2-  Allaah Ta’aalaa Ametoa onyo kali kwa mwenye kuacha swalah kufikia mpaka Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumnasibisha mtu huyo na ukafiri na ushirikina, akasema: 

 

"إنَّ بيْنَ الرَّجُلِ وبيْنَ الشِّرْكِ والْكُفْرِ تَرْكَ الصَّلاةِ"

 

“Hakika baina ya mtu na (kuingia kwenye) shirki na ukafiri ni kuacha swalah”.  [Hadiyth Swahiyh.  Muslim (82)]

 

‘Abdullah bin Shuqayq ambaye ni Taabi’iy amesema:  “Maswahaba wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikuwa hawaoni amali ambayo kuiacha kwake ni ukafiri isipokuwa swalah”.

 

3-  Swalah ndio nguzo ya dini, na dini haisimami ila kwa nguzo hii.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

"رأسُ الأمرِ الإسلام، وعمودُه الصَّلاةُ، وذِروةُ سَنامِهِ الجِهادُ"

 

“Kichwa cha mambo yote ni Uislamu, nguzo yake kuu ni swalah, na kilele chake cha juu kabisa ni kufanya Jihadi”.   [Hadiyth Hasan.  Imechakatwa na At-Tirmidhiy (2616), An Nasaaiy katika Al-Kubraa (11330) na Ibn Maajah (3973)]

 

4-  Ni jambo la kwanza atakalohisabiwa mja Siku ya Qiyaamah.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"إِنَّ أَوَّلَ مَا يُحَاسَبُ بِهِ الْعَبْدُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مِنْ عَمَلِهِ صَلَاتُهُ. فَإِنْ صَلُحَتْ فَقَدْ أَفْلَحَ وَأَنْجَحَ، وَإِنْ فَسَدَتْ فَقَدْ خَابَ وَخَسِرَ"

 

“Hakika jambo la kwanza atakalohisabiwa kwalo mja siku ya Qiyaamah katika matendo yake ni swalah zake.  Zikikutwa ziko sahihi, basi atakuwa amefaulu na kufuzu.  Na kama zitakuwa mbovu, basi atakuwa amepita utupu na amekula hasara”.  [Hadiyth Hasan Ghariyb.  Sunan At-Tirmidhiy (413)]

5-  Swalah ilikuwa ndio kitulizo cha jicho kwa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika maisha yake.  Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"حُبِّبَ إِلَىَّ النِّسَاءُ وَالطِّيبُ وَجُعِلَتْ قُرَّةُ عَيْنِي فِي الصَّلاَةِ ‏"

 

“Nimefanywa kuwapenda wanawake na mafuta mazuri, na kitulizo cha jicho langu kimewekwa ndani ya swalah”.  [An-Nasaaiy (3939) na Ahmad (13079)]

 

6-  Swalah ilikuwa ndio wasiya wa mwisho wa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa umati wake wakati wa kufariki kwake.  Amesema:

 

"الصَّلاةَ وما ملَكَت أيمانُكم، الصَّلاةَ وما مَلَكت أيمانُكم"

“Chungeni swalah, na walio na vilivyo chini ya mamlaka yenu.  Chungeni swalah, na walio na vilivyo chini ya mamlaka yenu”.  [Hadiyth Swahiyh.  Al-Jaami’u As-Swaghiyr (5154)]

 

7-  Ni ibada pekee isiyombanduka aliyebaleghe.  Humganda maisha yake yote na wala hasameheki nayo vyovyote hali iwavyo.

 

8-  Swalah ina sifa za kipekee kulinganisha na ibada nyinginezo.  Kati ya sifa hizo:

 

(a)  Allaah Mtukufu Aliifaradhisha Yeye Mwenyewe kwa kuzungumza moja kwa moja na Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) usiku wa Miiraji.

 

(b)  Ni faradhi iliyotajwa zaidi katika Qur-aan Tukufu.

 

(c)  Ni ibada ya kwanza Aliyoifaradhisha Allaah Mtukufu kwa Waja Wake.

 

(d) Imefaradhishwa mara tano mchana na usiku kinyume na ibada na nguzo nyinginezo.

 

Ama Neno Lake Ta’aalaa  "وَنُسُكِيْ",  Mufassiruna wanasema  "النُّسُكُ" maana yake ni ibada.  Nusuk vile vile ni wingi wa  "نَسِيْكَة", nayo  ina maana ya mnyama wa kuchinjwa.  Pia neno hili humaanisha matendo maalumu yanayofanyika katika amali ya hijja kama kutufu, kusai, kusimama Arafah, kutupia viguzo  na kadhalika.  Matendo yote haya huitwa "نُسُك"
 

Ibn Kathiyr anasema kwamba An Nusuk maana yake ni wanyama wanaochinjwa kwa ajili ya hijja au umra.  Na hii ni kwa vile Waarabu walikuwa wakifanya vitendo vya ushirikina huku wakidai kwamba wao wako katika Dini ya Ibraahiym.  Na hapo ndipo Allaah Ta’aalaa Alipomwamuru Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awabainishie ya kwamba Ibraahiym alikuwa ni mnyoofu, anayemwabudu Allaah Ta’aalaa Peke Yake bila ya kumshirikisha na yeyote au chochote.

 

Hivyo basi, inatakikana Mwislamu anapomchinja mnyama wakati wa sikukuu ya eid au kwenye amali za hijja, amchinje kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allaah Ta’aalaa Pekee na si kwa ajili ya malengo ya kidunia ya kusifiwa na kadhalika.
 

Ama Neno Lake Ta’aalaa "مَحْيَاي وَمَمَاتِيْ", Mufassiruna wanasema kwamba "المَحْيَا" na "المَمَات" zina maana ya amali za wakati wa uhai na amali za wakati wa kufa.  Amali zote za uhai huungana na kipindi cha wakati mtu anapokufa.  Ikiwa matendo ya katika uhai wa mtu yalikuwa ni mazuri, basi mtu huyu bila shaka atafia katika hali njema na mwisho mwema.  Na ikiwa matendo yake ni mabaya, basi mauti yake yatamkuta akiwa katika ubaya na mwisho wake utakuwa ni mbaya.

 

 

 

 
 

Share