18-Nuru Ya Qur-aan: (a) Baadhi Ya Neema Za Allaah Kwa Bani Israaiyl
Nuru Ya Qur-aan
18: (a) Baadhi Ya Neema Za Allaah Kwa Bani Israaiyl :
Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ اذْكُرُوا نِعْمَتِيَ الَّتِي أَنْعَمْتُ عَلَيْكُمْ وَأَنِّي فَضَّلْتُكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ ● وَاتَّقُوا يَوْمًا لَّا تَجْزِي نَفْسٌ عَن نَّفْسٍ شَيْئًا وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا شَفَاعَةٌ وَلَا يُؤْخَذُ مِنْهَا عَدْلٌ وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ"
“Enyi wana wa Israaiyl! Kumbukeni Neema Zangu Nilizokuneemesheni, na hakika Mimi Nimekufadhilisheni juu ya walimwengu wote. ● Na iogopeni Siku ambayo nafsi haitoifaa nafsi nyingine kwa kitu chochote kile, na wala hautokubaliwa kutoka kwake uombezi wowote, na wala hakitochukuliwa kutoka kwake kikomboleo, na wala hawatonusuriwa”. [Al-Baqarah: 47-48]
Aya hizi zinawakumbusha Bani Israaiyl juu ya neema ambazo Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Aliwafadhili kwazo juu ya walimwengu au watu waliokuwa wakiishi katika zama zao, na Akawaamuru wawajibike na kufanya matendo mema ili wapate malipo mema katika siku ya mwisho ambapo kila mmoja atalipwa mema yake na mabaya yake hata kama yatakuwa na uzito wa atom.
Mara nyingi tunaona katika aya mbalimbali, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Akiwaita Bani Israaiyl kwa jina la baba yao Israaiyl ambaye ni Ya’aquuwb (Alayhis Salaam) ambaye wao kwao ni asili ya fahari yao na kujitukuza kwao. Kuwaita hivi ni dalili juu ya kubobea kwao katika maasi na uasi na kutojibisha kwao Wito wa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa. Na kwa ajili hiyo, Anawakumbusha baba yao na kwa picha ya ukaririfu ili wapate kurejea Kwake mbali na neema na fadhila nyingi Alizowapa.
Makusudio ya walimwengu hapa ni watu wale waliokuwa wakiishi katika enzi yao tu na si watu wote, kwa kuwa umati wa Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni bora kuliko wao kutokana na Neno Lake Ta’aalaa:
"كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ ۗ وَلَوْ آمَنَ أَهْلُ الْكِتَابِ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُم ۚ مِّنْهُمُ الْمُؤْمِنُونَ وَأَكْثَرُهُمُ الْفَاسِقُونَ"
“Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu; mnaamrisha mema na mnakataza munkari na mnamwamini Allaah. Na lau wangeliamini Ahlul-Kitaabi basi ingelikuwa ni bora kwao. Wako miongoni mwao wanaoamini lakini wengi wao ni mafasiki”. [Aal ‘Imraan: 110]
Hivyo kutokana na neema zote walizoneemeshwa, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anawakumbusha kwamba ni lazima waiogope siku ya mwisho ambayo ni tofauti kabisa na masiku ya hapa duniani. Siku hiyo ni kwa ajili ya malipo tu, na kwa hivyo basi, ni lazima wajitayarishe nayo kwa kufanya matendo mema. Siku hiyo ina sifa tatu za kipekee:
Kwanza:
Mtu hatoweza kumfaa mwingine kwa lolote. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"وَاتَّقُوا يَوْمًا لَّا تَجْزِي نَفْسٌ عَن نَّفْسٍ شَيْئًا"
“Na iogopeni Siku ambayo nafsi haitoifaa nafsi nyingine kwa kitu chochote kile”. [Al-Baqarah: 48]
Kama tujuavyo, nafsi za wanadamu ziko aina mbili. Kuna nafsi ya Muumini iliyo huru, na kuna nafsi ya kafiri iliyojifunga. Mtu yeyote mwenye kwenda kinyume na Maamrisho ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa na kutoka nje ya Njia Yake, basi huyo anajitendea ubaya mwenyewe, na anajifunga mwenyewe. Ndio pale Allaah Ta’aalaa Anapotuambia:
"كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ رَهِينَةٌ ● إِلَّا أَصْحَابَ الْيَمِينِ"
“Kila nafsi iko katika rehani kwa yale iliyoyachuma ● . Isipokuwa watu wa kuliani”. [Al-Muddath-Thir: 38-39]
Binadamu hapa duniani ikiwa anaishi kwenye jamii iliyojipangia sheria zake na mawajibiko yake, inabidi mtu huyo azitii na kuzifuata sheria hizo na kuwajibika na yote ambayo inampasa awajibike nayo. Ikiwa atakwenda kinyume, basi bila shaka atakamatwa, atawekwa mahabusu, atasomewa mashtaka na anaweza kufungwa. Na hapa bila shaka anakuwa amelipa thamani ya uhalifu na makosa yake. Huko jela atakuwa chini ya ulinzi, atakuwa hana uhuru wa kufanya mambo yake na kadhalika. Na hii ni hali yetu sisi wanadamu. Je, hali itakuwa vipi mbele ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa?
Hivyo, ubaya au maasia yoyote aliyoyafanya mtu, atafungika nayo na hatoweza kusonga mbele kupata Rehma za Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa isipokuwa kama Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Atapenda. Na hata kama atalipata hilo, lakini hata hivyo, atakuwa amepitia misukosuko mikubwa ya Siku ya Qiyaamah.
Na kwa ajili hiyo, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia tena:
"يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَلْتَنظُرْ نَفْسٌ مَّا قَدَّمَتْ لِغَدٍ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ"
“Enyi walioamini! Mcheni Allaah, na nafsi itazame imetanguliza nini kwa ajili ya kesho, na mcheni Allaah. Hakika Allaah Ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo”. [Al-Hashr: 18]
Ichungue kwa makini amali yako. Iangalie kwa makini kazi yako. Je, chumo lake unalolipata ni la halali safi isiyo na pumba yoyote ya ghushi, utegeaji, uzembe na kadhalika. Jiangalie, je unajenga utukufu wako juu ya migongo ya wengine? Je, wewe unashiba na wenzako wanalala njaa? Je, wewe unapata uhai na wengine wanakufa?
‘Umar bin Al-Khattwaab (Radhwiya Allaah ‘anhu) amesema:
"حاسِبوا أنفسَكم قبل أن تُحاسَبوا، وزِنوا أنفسَكم قبل أن تُوزنوا"
“Jitathminini wenyewe kabla hamjasailiwa, jipimeni wenyewe kabla amali zenu hazijakuja kupimwa”.
Kwa hiyo yeyote mwenye kujitathmini mwenyewe hapa duniani kama inavyotakikana, akajirekebisha kwa kasoro anazoziona na akalingamana sawasawa katika kufuata maamrisho na kuacha makatazo, basi huyo hisabu yake mbele ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa itakuwa ni nyepesi mno.
Pili:
Mtu hatokubaliwa uombezi wake. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"وَلَا يُقْبَلُ مِنْهَا شَفَاعَةٌ"
“Na wala hautokubaliwa kutoka kwake uombezi wowote”. [Al-Baqarah: 48]
"شَفَاعَةٌ"maana yake kilugha ni ombi. Ama kiistilahi kama alivyoeleza Al-Imaam As Saalimiy, ni ombi la kuharakiziwa kuingizwa Peponi, au kuongezewa daraja humo toka kwa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa kwa ajili ya Waja Wake Waumini.
Kutokana na taarifu hii, inatubainikia kwamba Shafa’ah maana yake imejizinga katika ombi la kuharakishiwa kuingizwa Peponi na kunyanyuliwa daraja ya Waumini huko.
Maulamaa wanatuambia kwamba kuna watu maalumu ambao Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Atawapa nafasi ya kufanya uombezi kwa wengineo. Na hawa ni Waumini wenye kumpwekesha Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa na ambao hawakutenda madhambi makubwa. Na juu ya msingi huu, inawabidi Waumini wote wajiweke sawa kwa kufuata yote aliyokuja nayo Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kutenda mema ili angalau pia waweze kupatiwa nafasi hiyo ya kufanya Shafaa’ah kwa wengineo, na kama hawatafanya hivyo, basi bila shaka mambo yatawawia magumu sana Siku ya Qiyaamah.
Tatu:
Hakitachukuliwa kikomboleo toka kwa yeyote ili aepushwe na adhabu. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anatuambia:
"وَلَا يُؤْخَذُ مِنْهَا عَدْلٌ"
“Na wala hakitochukuliwa kutoka kwake kikomboleo”. [Al-Baqarah: 48]
Siku hiyo ya Qiyaamah, kila mtu aliyetenda madhambi na makosa hapa duniani, atatamani lau kama ataweza kutoa vyote alivyokuwa anavimiliki hapa duniani kwa ajili ya kuepushwa na adhabu ya Siku hiyo. Atatamani hata watoto wake na jamaa zake awatoe ili yeye aepukane na yote yanayomsubiri. Lakini hayo yote hayatakuwa, hata kama mali yake yote itakuwa na thamani ya vyote vilivyomo duniani na mara mbili yake.
Hapa duniani mtu akiwa na mkubwa fulani, basi mambo yake yote yanakuwa sahali. Lakini huko mbele ya Allaah hayo hakuna, ni hapa duniani tu.
"يُحْشَرُ النَّاسُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حُفَاةً عُرَاةً غُرْلًا. قُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ الرِّجَالُ وَالنِّسَاءُ جَمِيعًا يَنْظُرُ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ؟ فَقَالَ: يَا عَائِشَةُ الْأَمْرُ أَشَدُّ مِنْ أَنْ يَنْظُرَ بَعْضُهُمْ إِلَى بَعْضٍ"
Bibi ‘Aaishah (Radhwiya Allaah ‘anhaa) amesema: “Nilimsikia Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: Watu watakusanywa Siku ya Qiyaamah wakiwa pekupeku, bila nguo, wakiwa hawajatahiriwa. Nikasema: Ee Rasuli wa Allaah! Wake kwa waume wote wataangaliana?! Akasema: Ee ‘Aaishah! Mambo ni mazito mno hata kuweza kuwashughulisha kuangaliana”. [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hii ni picha ndogo tu anayotupa Rasuli (Swalla Allaah ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusiana na siku hiyo ngumu kabisa ambayo inabidi kila mtu ajiandae nayo kwa amali njema. Watu wa familia moja watakimbiana. Hivyo inabidi Banu Israaiyl na Waislamu wote walikumbuke hili vyema kabisa kabla wakati haujapita.
Nne:
Waovu, madhalimu na waasi hawatapata wa kuwanusuru kama walivyokuwa wakisaidiana hapa duniani. Allaah Ta’aalaa Anatuambia:
"وَلَا هُمْ يُنصَرُونَ"
“Na wala hawatonusuriwa”. [Al-Baqarah: 48]
Ama kwa upande wa neema walizoneemeshwa Bani Israaiyl na Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa ni neema nyingi mno. Kati ya neema hizo ni:
Kwanza: Allaah Ta’aalaa Aliwaokoa kutokana na udhalimu wa Firauni. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anasema:
"وَإِذْ نَجَّيْنَاكُم مِّنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوءَ الْعَذَابِ يُذَبِّحُونَ أَبْنَاءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَاءَكُمْ ۚ وَفِي ذَٰلِكُم بَلَاءٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَظِيمٌ "
“ Na pindi Tulipokuokoeni kutoka kwa watu wa Fir’awn walipokusibuni adhabu mbaya, wakiwachinja watoto wenu wa kiume na wakiacha hai wanawake wenu, na katika hayo kwenu ulikuwa ni mtihani mkuu kutoka kwa Rabb wenu”. [Al-Baqarah: 49]
Hizi ndizo adhabu ambazo Firauni alikuwa akiwapa Bani Israaiyl. Akiwanyanyasa kwa kuwafanyisha kazi ngumu na kazi duni, akiwakalifisha kwa wasiyoyaweza, akiwachinja watoto wao wa kiume pamoja na vitendo vinginevyo vyote vibaya. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Akawaokoa toka kwenye mateso haya.
Pili: Allaah Ta’aalaa Alimwangamiza adui yao Firauni kwa kumgharakisha pamoja na askari wake. Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Anasema:
"وَإِذْ فَرَقْنَا بِكُمُ الْبَحْرَ فَأَنجَيْنَاكُمْ وَأَغْرَقْنَا آلَ فِرْعَوْنَ وَأَنتُمْ تَنظُرُونَ"
“Na pale Tulipoitenganisha bahari kwa ajili yenu, Tukakuokoeni na Tukawagharikisha watu wa Fir’awn na huku nyinyi mnatazama”. [Al-Baqarah: 50]
Katika uokozi huu, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Aliwapa Bani Israaiyl neema nyinginezo juu ya neema hii. Kwanza, Aliwafungulia njia baharini wakaweza kupita jambo ambalo hakuna wanadamu wengineo waliolishuhudia. Pili, Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Aliwazamisha Firauni na askari wake huku wao wakitizama namna maadui wao wanavyoangamia. Al-Imaam Al-Fakhru Ar Raaziy anatuambia:
“Jua kwamba tukio la kupasuka bahari, limekusanya neema nyingi kwa Banu Israaiyl. Kwanza: Ni kwamba wao walipoikurubia bahari na wakawa katika hali ngumu huku Firauni na askari wake wakiwajia kwa nyuma, hapo faraja iliwajia baada ya Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa kuwapasulia bahari iliyokuwa mbele yao. Pili: Ni kwamba Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa Amewakhusu kwa neema hii kuu na muujiza huu wa kushangaza kwa ajili ya kuwakirimu na kuwatunza. Tatu: Ni kuwa kwa kuangamia Firauni, wanakuwa wameshamalizana na mateso yaliyokuwa yakiwakabili na nyoyo zao zikajaa utulivu na ushwari. Nne: Watu wa Musa waliposhuhudia muujiza ule wa kushangaza, iliondoka kwenye nyoyo zao shaka na utata kuhusiana na ukweli wa Nabii Musa ‘Alayhis Salaam. Tano: Kwa kuyaona hayo, imani yao ilizidi, wakazidi kuthibiti juu ya haki na kuyafuata maamrisho. Sita: Walipata kujua kwamba mambo yote yako Mkononi mwa Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa, na kwamba hakuna utukufu zaidi ya aliokuwa nao Firauni hapa duniani, na hakuna udhalili uliokuwa mbaya zaidi kuliko ule waliokuwa nao Bani Israaiyl. Kisha Allaah Subhaanahu wa Ta’aalaa kufumba na kufumbua, Akamfanya mnyonge kuwa mtukufu, na mtukufu kuwa mnyonge, mwenye nguvu kuwa dhaifu na dhaifu kuwa mwenye nguvu.
Lakini pamoja na yote hayo, Banu Israaiyl baada ya kuokolewa, waliyasahau haya yote na wakaanza kumtaka Musa awafanyie sanamu walifanye kuwa mungu waliabudu! Ni ukengeukaje wa aina gani huu?!
