Bid'ah – Vipengele Vyake, Madhara Na Ufumbuzi

 

Muhammad Al-Ma'awiy

 

Alhidaaya.com

 

Vipengele Vya Bid’ah:

 

Baadhi Ya Vipengele Vya Bid’ah Ni Kama Vifuatavyo:

 

1. - Kila Bid’ah ni Dhwalaalah.

Kilugha Bid’ah ni kitu chochote kipya au kitu ambacho hakijafanywa kabla, yaani, hakina mfano kabisa wa mbeleni. Katika muono wa kishariy'ah, kila Bid’ah ni Dhwalaalah na hakuna Bid’ah hasanah au sayyi’ah (Bid’ah nzuri na mbaya). Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika hadiyth, 

 

“Kullu Bid’atin dhwalaalah wa kullu dhwalaalatin fin naar (kila Bid’ah ni Dhwalaalah na kila Dhwalaalah ni motoni)” [Imepokewa na Imam Ahmad, Abu Daawuwd, at-Tirmidhy na wengineo].

 

Dhwalaalah ina maana ya kwenda kombo au kufuata njia ya upotevu na kwenda kinyume na ukweli. Tukitazama Qur-aan, tutaona vipi Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) ametumia neno hilo ‘dhwalaalah’ au ‘dhwaal’. Neno hili linatumika kwa mtu anayefanya dhambi au anafanya kosa katika mambo ya kidini lakini na pia linatumika kwa wale watu ambao wamepotea kutoka kwa njia nyoofu au wale walioigawa dini. Kwa mfano katika Suwrah Faatihah (Suwrah ya kwanza), neno lililotumika ni ‘Dhaaliin’ halikutumika kwa wafanyao madhambi pekee lakini limetumika kwa watu waliopotea kutoka kwa ile njia ya sawa, yaani Wakristo. Hivyo pale Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoielezea bid’ah, alitumia neno kali sana kwa upotevu huo, yaani dhalalah, kama alivyosema, 

 

“Kulla bid’atin dhwalaalah (kila bi’dah ni dhwalaalah)”.

Hakusema kuwa kila bid’ah ni dhambi au ni kosa lakini kwa hakika ni jambo ambalo ni kubwa kuliko hilo. Huu ni upotevu, jambo ambalo linamtoa mtu katika Swiraatul Mustaqiym (njia iliyonyooka).

 

2. - Bid’ah Inafanywa Kama Njia Ya Kumridhisha Na Kuja Karibu Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

Kwa maneno mengine, yeyote anayefanya bid’ah, anadai kwa kufanya hivyo atakuja karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hii ni tofauti kabisa na kufanya dhambi kama alivyosema Imam Ahmad Ibn Hanbal, “Mkosefu mkubwa (fasiq) katika msimamo wa Ahl-Sunnah Wal Jam’ah ni bora kabisa kuliko mchaji Allaah miongoni mwa Ahl-Bid’ah (watu wa Bid’ah)”. Mwenye kufanya dhambi (mkosefu), kwa uchache, anajua ya kwamba chochote afanyacho ni makosa na wala hadai kuwa hilo ni halali na kuwa analifanya ili kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hata hivyo, yule anayefanya bid’ah sio tu anakwenda kinyume na Qur-aan na Sunnah lakini bado anadai ya kwamba anayofanya ni sawa na anafanya hivyo ili kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na ni njia ya kumleta karibu zaidi Naye (Allaah). Na huu ni uwongo mkubwa zaidi ambao mtu anafanya kwa kusema kuwa kitendo hiki kinamridhisha Allaah na hana dalili kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa dai lake hilo.

 

Hivyo, sehemu ya wazo hili la bid’ah ni kuwa yule mwenye kufanya hudai kwamba linakubaliwa na dini pamoja na shariy'ah na ni lenye kumpendeza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Hii ndio nukta inayogawanya baina ya bid’ah na jambo lisilokuwa bid’ah.

 

3. -Bid’ah Inaweza Kuwa Kuanzisha Kitendo Kipya Na Pia Kukibadilisha Kitendo Kilichokuwepo Mwanzo.

Maana yake ni, pale mtu anapoanzisha kitendo kipya huku akidai kuwa kitendo hicho kimekubaliwa na shariy'ah bila dalili yeyote ni bid’ah. Kwa namna hiyo hiyo, pale mtu anapoacha kitu Fulani akidai kuwa kwa kuacha kitu hicho basi anamridhisha Allaah na hana dalili yeyote kutoka kwa Qur-aan au Sunnah, hiyo pia inakuwa bid’ah. Kwa mfano, wakati wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) walikuja watu watatu katika nyumba zake na kuwauliza wakeze kuhusu Ibadah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), walipoelezewa waliona ni kama kidogo sana. Hivyo wakajipangia jinsi watakavyofanya Ibadah zao, mmoja akasema yeye ataswali usiku kucha, na mwengine akasema yeye atafunga kila siku na wa tatu akasema kuwa yeye hataoa. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoambiwa habari hiyo alikwenda kwa hawa watu watatu na kuwauliza je, ndio nyinyi muliosema kadha na kadha nao wakajibu ndio. Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya haraka kuzikemea na kuzikataza bid’ah hizi ambazo zinaonekana ni nzuri (huenda sisi tukadhania na kufikiria je, kutakuwa na makosa ya mtu kumuabudu Allaah kwa wakati wote?).

 

Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaeleza hawa watu kuwa yeye anamcha Allaah zaidi kuliko wao na ana taqwa ya daraja ya juu lakini anaswali na kulala, anafunga na kula na ameoa wake (sio mke mmoja). Na akamalizia kwa kusema yeyote atakayekengeuka na Sunnah zake basi si katika mimi (yaani si pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). [Hadiyth hii imepokewa na Al-Bukhaary na Muslim] kutoka kwa Anas bin Maalik [Radhwiya Allaahu 'anhu].

 

Hapa ukitizama katika watu hawa watatu, wawili wa kwanza walikuwa tayari kuongeza Ibadah zao zaidi na zile ambazo zipo katika shariy'ah na wa tatu akataka kuacha Ibadah ya ndoa ambayo ipo katika shariy'ah na iliyokubaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Huyu wa tatu alikuwa ataka kujifananisha na makasisi wa Kikiristo au watawa wao na pia kama masufi Waislamu ambao wanadai ya kwamba wanafanya hivyo kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na huu ukawa ni uzushi na kinyume na Uislamu.

  

4. - Kila Kitu Katika Shariy'ah Kinaweza Kuwa Na Bid’ah Inayotengenezwa Au Kuhusiana Nayo.

Shariy'ah imejumlisha itikadi, ibadah na biashara au muamala na watu. Hivyo, bid’ah si mambo katika itikadi pekee au mambo ya ibadah lakini inaweza kuwa hata katika biashara na ‘uamala. Kwa mfano, ikiwa mtu atadai ya kwamba kunahitajika mashahidi wanne katika mapatano ya kibiashara na wala sio wawili kama ilivyowekwa na Uislamu hivyo atakuwa ametupa mipaka ya kishariy'ah na kuangukia katika bid’ah.

 

5. - Bid’ah Haina Dalili Katika Qur-aan, Sunnah Ya Nabiy (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Wala Haikukubaliwa na Ijmaa (kongamano) Ya Swahaba.

 

Mfano maarufu ambao unatajwa na watu wa bid’ah (Ahl-Bid’ahkatika yale matamanio yao ya kufanya aina Fulani za bid’ah ziwe halali, ni ule mfano wa ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuifanya Swalaah ya tarawehe itekelezwe kwa jamaa. Wanadai ya kwamba Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alianzisha tarawehe ya kila siku katika Ramadhwaan ambapo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitekeleza hilo kwa muda wa siku tatu pekee, na ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) akasema ya kwamba ameanzisha bid’ah nzuri, tunaweza kukubali fikra hii ya bid’ah. Hata hivyo, huku ni kufeli (kushindwa) kutofautisha baina baina ya maana ya bid’ah kilugha na maana yake ya ki-istilahi (yaani maana ya kishariy'ah).

 

Kwa mfano Allaah katika Qur-aan Anatuelezea kuhusu Sunnah Zake. Bila shaka ni kuwa yeyote anapotaja kuhusu sunnah, inarudi kwa sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na vipengele vyake vya kishariy'ah. Hivyo hivyo pale ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alipotaja hizi Swalaah za tarawehe za kila siku, alikuwa anamaanisha ile maana yake ya kilugha. Dalili ya dai hili lipo wazi kabisa. Swalaah ya Tarawehe haikuwa ni jambo geni katika dini. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alianzisha Swalaah hizi, na sababu ya pekee iliyomfanya yeye aache inaelezwa wazi katika hadithi zake ya kwamba hataki Ummah wake upate shida kwa Swalaah hiyo kufanywa faradhi. Hata hivyo, alipofariki Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), risala ya Uislamu ilikuwa imekamilishwa na Swalaah ya tarawehe itakuwa daima ni yenye kuhimizwa kwa kiasi kikubwa na wala sio faradhi. Hivyo, ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alianzisha tu kitendo ambacho tayari kilikuwa ni sunnah na wala sio kuanzisha sunnah. Na pia ile sababu ya kutoswaliwa kwa jamaa iliondoka baada ya kuaga dunia kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo hakukukuwa na aina yeyote ya uwezekano wa kuteremshwa wahyi. Na matendo ya makhalifa waongofu pia ni katika sunnah (tizama Hadithi nambari 28 ya al-Arba‘iina an-Nawawiyyah).

 

Kuhitimisha sehemu hii ya makala haya, ni lazima ieleweke ya kwamba bid’ah si jambo tu jipya ambalo limeanzishwa katika dini kwa dai la kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), lakini kwa yule mwenye kuanzisha na yule mwenye kufuata bid’ah kwa hakika anatuhumu ya kwamba dini ina upungufu. Hakika ni kuwa wao wanatuonyesha ya kwamba zipo njia za kuja karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) pamoja na kumridhisha ambako hakupatikani katika Qur-aan au Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Na kuwa wao wana njia ya kuamini au kufanya 'amali na kumuabudu Allaah ambako kunampendeza Yeye na njia mzuri zaidi kuliko zile zilizofundishwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kwamba hii dini ya Uislamu iliyokamilika ina upungufu na hiyo ndio sababu iliyowafanya wao kuongeza baadhi ya vitu au dini hii ina vitu vingi sana na hiyo ndio sababu ya wao kupunguza baadhi ya mambo. Huku (Naudhubillahi) ni nkumtusi Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kusema ya kwamba hakuweza kumkamilishia na kumfundisha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa njia bora na hivyo ilibidi watafute wao wenyewe njia nzuri. Hii ni kukana kauli ya Allaah Mwenyewe katika Qur-aan:

 

 الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah: 3]

 

Na huko ni kukana kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:

 

Hakuna kitu ambacho kitakuleta karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuliko yale niliyowaambieni kufanya na hakuna kitakacho wapeleka nyinyi mbali kuliko kufanya yale niliyowakatazeni kufanya”.

 

Hivyo, tunatakiwa kuchukia bid’ah. Hiki ndicho kiini cha mambo. Uchukivu huu ni kuonyesha mapenzi yetu kwa Allaah na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na pia kuipenda dini hii ambayo tunajua na kuwa na yakini kuwa ndio iliyo sahihi kabisa na itabaki hivyo mpaka siku ambayo Allaah Ataibadilisha ardhi hii kwa nyengine. 

 

Madhara (Hatari) Ya Bid’ah:

Kama bid’ah ingebanwa kwa yule mwenye kufanya pekee basi huenda hatungefadhaishwa au kubabaika kama tulivyo sasa, lakini hakika ni kuwa hatari za bid’ah na yale madhara na maafa yake yanasambaa kutoka kwa mtu anayefuata na kuwafikia watu wanaoishi naye na mwishowe kwa Ummah mzima. Hivyo, dini kwa ujumla inaathirika kwa ajili ya bid’ah zao na uasi wa kidini. Wanachuoni wametoa kauli mbalimbali na kuuliza maswali mbalimbali kama haya na kuyapatia ufumbuzi, “Kwa nini Uislamu umeupiga vita vikali jambo hili la bid’ah? Kwa nini Uislamu umeichukulia bid’ah kuwa ni Dhalalah? Kwa nini imemchukulia mwenye kuifanya kuwa ataingia Motoni? Kwa nini Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuonya vikali sana kuhusu jambo hilo?” Baada ya maswali haya ametoa majibu kwa nini bid’ah imepingwa vikali sana.

 

Hatari zinazotokana na bid’ah ni kama zifuatazo:

 

A.    Mzushi Anajiweka Katika Cheo Cha Kutunga Shariy'ah:

Uhakika ni kuwa Uislamu umetuonya sana na bid’ah kwa sasa mzushi anaiweka nafsi yake katika cheo cha Allaah. Na ya kuwa yeye anajua asiyojua Allaah, kama kwamba anasema: “hakika yale uliyotuletea hayatutoshi, hivyo sisi tunazidisha juu ya yale ulituteremshia”. Hivyo anajiweka katika daraja ya kutunga shariy'ah na kujipatia haki ya kuweka shariy'ah. Utungaji wa shariy'ah kwa hakika ni haki ya Allaah pekee. Qur-aan inatueleza:

 

أَمْ لَهُمْ شُرَكَاءُ شَرَعُوا لَهُم مِّنَ الدِّينِ مَا لَمْ يَأْذَن بِهِ اللَّـهُ

Je, wanao washirika waliowaamuru Dini yale ambayo Allaah Hakuyatolea idhini? [Ash-Shuwraa: 21]

 

Na kutunga yale yasiyoidhinishwa na Allaah ni hatari kubwa kwa kuwa mwanadamu ameijaalia nafsi yake kuwa sawa na Allaah Aliyetukuka. Na anaona kuwa ni haki yake kuzidisha katika dini ya Allaah, na huu ni mlango ambao huleta hatari kubwa ambayo huwapelekea watu katika shirki na hili ndilo jambo lililoharibu dini kabla.

 

Dini nyinginezo zilihalalisha nini? Zilihalalisha bid’ah kwa kuifungulia milango na wakajipatia ruhusa na haki ya kuongeza mambo katika dini ya Allaah na wakawapatia haki hiyo makasisi wao au watawa wao. Hivyo dini ikawa si dini na hili ni jambo ambalo Uislamu umelipiga vita vikali, pale Allaah Aliposema:

 

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًا ۖ لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ ۚ سُبْحَانَهُ

 

عَمَّا يُشْرِكُونَ

Wamewafanya Wanazuoni Marabai wao wa dini na Wamonaki wao kuwa ni miola badala ya Allaah, na (pia) Al-Masiyh mwana wa Maryam na hali hawakuamrishwa isipokuwa kumwabudu Ilaah Mmoja Pekee. Hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye. Utakasifu ni Wake kutokana na yale yote wanayomshirkisha nayo.   [At-Tawbah: 31]

 

'Adiy bin Haatim (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliposilimu baada ya kutoka katika Ukristo (ambao alikuwa akiufuata wakati wa Ujahiliyyah) alikuja kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye alikuwa anaisoma aayah hii: (At-Tawbah: 31). Alisema: “Hakika wao hawawaabudu”. Akasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): 

 

“Bali wanawaabudu, kwani wao huwaharamishia halali na kuwahalalishia haramu nao wakawafuata, na kufanya hivyo ni kuwaabudu” [Imepokewa na Ahmad, at-Tirmidhy na Ibn Jariir].

 

‘Adiy alifahamu Ibadah ni zile taratibu za dini (au taratibu fulani za ibadah) tu kwa mfano Swalaah, kurukuu, kusujudu na mfano wake. Na hapa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimfahamisha ya kwamba sio dharura kufanya hivyo, kwani ibadah ina maana pana zaidi. Ibadah ni twaa ya daima kwa yale wanayofanya, yale wanayoharamisha na wanayohalalisha na mengineyo katika mambo ya dini ni ibadah, kwani ni Rabb ambaye ana haki ya kuhalalisha na kuharamisha. Yeye (Allaah) ndiye mwenye haki ya kuabudiwa wala si kinyume ya hayo.

 

Mzushi hivyo anajipatia cheo cha kutunga shariy'ah na kujiweka sawa na katika upinzani na Allaah Aliyetukuka.

 

B.    Mzushi anaona kuwa dini ina upungufu, hivyo kutaka kuikamilisha:

Watu wa bid’ah wanaona upungufu katika dini nao wakawa wanafanya juhudi ya kuikamilisha katika zile kasoro. Lakini ni jambo ambalo linafahamika na kila Muislamu na hata asiyekuwa Muislamu ya kwamba dini ya Uislamu imekamilika na AllaAh Ametutimizia neema Yake kwa kutukamilishia. Anasema:

 

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu. [Al-Maaidah: 3]

 

Imam Maalik (Imam wa ardhi ya Hijrah) alisema: “Yeyote atakayezua katika Uislamu bid’ah ambayo anaiona ni nzuri amedai ya kwamba Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amefanya hiyana katika kutekeleza ujumbe, kwani Allaah Aliyetukuka anasema, ‘Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini’. Hivyo chochote ambacho hakikuwa dini wakati huo hakiwezi kuwa dini sasa”.

 

Uzushi katika dini unakuwa ni wenye kumtuhumu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa hakutekeleza jukumu aliloletewa nalo na Allaah. Na Allaah Anasema:

 

يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ بَلِّغْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ ۖ

Ee Rasuli! Balighisha yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Rabb wako [Al-Maadah: 67].

 

Dini imekamilika na hivyo haina haja ya kuzidishwa mambo kwani kilichokamilika hakikubali ziada kwa hali yeyote. Kitu chenye upungufu ndicho ambacho kinaweza kuongezwa. Hapa walisimama imara kabisa Swahaba na imamu wa Ahlus Sunnah wal Jama’ah na waliowafuata kwa wema dhidi ya bid’ah kwani huko ni kuituhumu dini kuwa imepungua na kumtuhumu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amefanya khiyana.

 

C.    Bid’ah inaifanya dini kuwa nzito na inaitoa katika maumbile yake ya wepesi na usahali:

Dini ambayo imeteremshwa na Allaah ni nyepesi na akatumwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)mwongofu na usahali, uwongofu katika itikadi na wepesi katika taklifu za amali. Allaah Anasema:

 يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu; [Al-Baqarah: 185]

 

na pia Allaah(Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema:

وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ۚ

Na Hakukufanyieni ugumu wowote ule katika Dini. Mila ya baba yenu Ibraahiym. [Al-Hajj: 78].

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakika mimi nimetumwa kufanya sahali mambo na wala sio kuleta uzito wowote” [Imepokewa na al-Bukhaariy kutoka kwa Abu Hurayrah].

 

Hivyo dini imekuja na usahali kwa watu na wale wenye kuleta bid’ah wanaitoa katika maumbile yake ya wepesi. Hivyo wanawapatia watu taabu na mashaka na wanaongeza vitu ambavyo vinakuwa ni mizigo na minyororo na taklifu kubwa kwa watu. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja kuondoa hiyo mizigo na minyororo iliyokuwa juu ya watu (kwani shariy'ah za zamani zilikuwa ngumu).

 

Allaah Anatufahamisha hayo katika Qur-aan tukufu kwa wasifu wa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyotajwa katika vitabu vya mwanzo – Taurati na Injili:

 

الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ

 

عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ

Wale wanomfuata Rasuli; Nabiy asiyejua kusoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawraat na Injiyl, anawaamrisha mema na anawakataza munkari, na anawahalalishia vizuri na anawaharamishia maovu, na anawaondoshea mizigo yao. [Al-A’raaf: 157].

 

Na Allaah Ametufundisha du'aa ambayo iko mwisho wa Suwrah Al-Baqarah ambayo inasema:

 

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۚ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَعَلَيْهَا مَا اكْتَسَبَتْ ۗ رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلْنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا بِهِ ۖ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۚ أَنتَ مَوْلَانَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ ﴿٢٨٦﴾  

Allaah Hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake. Itapata (thawabu) iliyoyachuma, na ni dhidi yake (kwa maovu) iliyojichumia. Rabb wetu Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Rabb wetu, Usitubebeshe mzigo kama Ulivyoubebesha juu ya wale waliokuwa kabla yetu. Rabb wetu, Usitutwike tusiyoyaweza, na Tusamehe, na Tughufurie na Turehemu, Wewe ni Mola Mlinzi wetu, basi Tunusuru dhidi ya watu makafiri. [Al-Baqarah: 286]

 

Hawa watu wa bid'ah wanataka kurudisha ugumu wa dini zilizotangulia katika Uislaam na wanataka kuongeza taklifu ambazo zitakuwa mzigo kwa watu na hivyo kuleta uzito siotakikana. Taklifu za dini  ni sahihi na nyepesi sana, kwa mfano: Allaah anasema:

 

إِنَّ اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa..[Al-Ahzaad: 56].

 

Na namna bora ya kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni ile aliyotufundisha mwenyewe (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): “Allaahumma Swalli ‘alaa Muhammadin wa ‘alaa Aali Muhammad…” [Imepokewa na al-Bukhaariy na Muslim] kutoka kwa Ka‘b bin ‘Ujrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  Kusema hii Swalaah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inaweza kuchukua dakika ngapi?

 

“Wanakuja watu ambao wanaongeza maneno katika Swalaah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) namna ambayo ina taklifu kubwa sana ambayo haikuteremshwa na Allaah wala Nabiy Wake. Nilikuwa nikiwaona watu wa kawaida wakisoma bila ya kufahamu chochote. Na du'aa nyingine ambazo zimeanzishwa na watu ni zile nyiradi na hizbu ambazo nilipokuwa mdogo nilikuwa nikiwaona watu katika msikiti kabla ya Alfajiri wakisoma. Nilikuwa nawaona baadhi ya watu wakihifadhi nyiradi hizo zilizokuwa zikiitwa ‘Uradi wa al-Bakari’ na hii ni du'aa inayofuata herufi za Kiarabu. du'aa inaanza na herufi ya hamzah, kisha ba mpaka mwisho. Na ulikuwa ukiwauliza kuhusu maana walikuwa hawajui kabisa! ”(As-Sunnatu wal Bid’ah, uk. 30 – 31).

 

Ee ndugu yangu katika Imani! Je, kuna du'aa iliyo nyepesi, nzuri na sahali kuliko du'aa ambazo zipo ndani ya Qur-aan au Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)? du'aa ya Qur-aan mfano wa:

رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الآخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ

Rabb wetu Tupe katika dunia mazuri na katika Aakhirah mazuri na Tukinge na adhabu ya moto. [Al-Baqarah: 201].

 

Kwa nini tunafanya mambo yawe magumu kwa watu kwa kuwahifadhisha hizo du'aa badala ya kuwahifadhisha mfano wa du'aa hii ya Qur-aan?

 

Mwandishi wa kitabu hicho cha As-Sunnatu wal Bid'ah anatoa mfano mwengine: “Mara moja nilimwuliza mtu, kwa nini huswali? Akanijibu ya kwamba: ‘Sijui kushika wudhu’. Nikamwambia: ‘Hujui kuosha uso, mikono miwili, kupaka kichwa na kuosha miguu miwili?’ Akasema: ‘Hayo ninajua, lakini sijahifadhi yale yanayosemwa mtu anapoanza kushika wudhu (kutawadha)’. Hiyo ni kusema unapoanza: ‘Alhamdulillahi alladhi ja’alal maa ….’ Unapotia maji puani, ‘Allaahumma arhamni biraihatil jannah …’ Unapoosha uso, ‘Allaahumma bayyidh wajhii…’ na kadhalika mpaka kumaliza. Kila kitu wamekiwekea du'aa na mtu wa kawaida anaona ili wudhu kuwa sawa ni lazima ulete du'aa zote hizo ili Swalaah ipate kusihi. Kwa nini yote haya?”

 

Nakumbuka nilipokuwa mtoto jinsi gani katika kisiwa cha Lamu wakati wa Ramadhwaan watu walivyokuwa wakisumbuka sana kutekeleza amri ya funga kwa kungojea mpaka saa nne au tano ili mwalimu fulani awatilishe watu nia kwa kutumia microphone. Hata mtu akiwa na usingizi namna gani ilikuwa ni lazima angoje mpaka wakati ufike na lau atalala basi saumu yake haiswihi. Na saa nyengine watu walikuwa wakimngojea shekhe fulani kwani wanapofunga kwa kunuwizwa naye basi funga inakuwa sahali. Ikiwa atakuwa mwengine basi itakuwa na taabu. Mpaka sasa katika baadhi ya vitongoji watu ambao kwao hakuna Msikiti inabidi watembee masafa ya kilomita kadha kwenda kuswali Ishaa sehemu ambayo ina Msikiti ili wapate kutilishwa nia. Kuna baadhi ya vitongoji kama vya Taita-Taveta (Kenya) na Arusha (Tanzania) au Tanga ambako mwanamke ili kujitahirisha mpaka aogeshwe na mwalimu au shekhe. Laa hawla wala quwwata illa billahi!!

 

Uislamu ulisimama imara dhidi ya bid’ah ili watu wasiingie katika mambo mazito na kuongeza vitu ambavyo vitakuwa juu sana na yale yaliyoteremshwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Natija yake ni kuwa watu watakuwa na mzigo mkubwa wa taklifu ambazo zitawapatia dhiki kubwa katika utekelezaji wa mambo ya dini.

 

D.    Bid’ah Katika Dini Zinaua (Zinaondosha) Sunnah.

Imepokewa kutoka kwa salaf saalih ya kwamba: “Hakuna watu ambao watahuisha bid’ah isipokuwa huondoka mfano wake katika Sunnah”. Hivyo ni kitu kinachoeleweka kuwa hakutaanzishwa bid’ah isipokuwa huchukua nafasi ya Sunnah. Au watu huongeza katika Sunnah mpaka Sunnah ikawa haitekelezwi katika njia yake sahihi. Ibn Abbas anasema, “Pindi bid’ah inapoanzishwa basi Sunnah hutoweka na hii huendelea mpaka bid’ah ikabakia na Sunnah ikatoweka kabisa”. Hasan Ibn Attwiyah, mmoja wa Tabii alisema: “Watu wanapoikubali bid’ah, Allaah huondosha Sunnah kutoka kwao na hairudishi mpaka Siku ya Kiyama”.

 

Na hili ni jambo la kawaida, nayo ni kanuni, kanuni ya kilimwengu, kanuni ya kijamii. Kama alivyosema msemaji ya kwamba: “sijaona israfu (ubadhirifu) ukifanywa isipokuwa kuna haki zinazokiukwa. Hivyo, mwanadamu anapotumia nguvu zake katika bid’ah, ni lazima nguvu hizi zitaiathiri Sunnah kwani mwanadamu juhudi zake zina kikomo”. Hivyo, utawaona wazushi wanashinda katika mambo ya bid’ah lakini wanapoteza Sunnah. Anaelezea Shaykh wa Misr yaliyomfika alipokuwa akisoma sekondari katika chuo cha al-Azhar (Misri) katika mji wa Twanta. Na hiki kijiji cha Twanta alikuwa akiishi As-Sayyid al-Badawi ambaye ni maarufu. Na huko kulikuwa na mashekhe ambao kila wakati (mchana na usiku) walikuwa wakikaa ubavuni mwa al-Badawi. Wakati mmoja nilijadiliana na shekhe wangu ambaye alikuwa fakihi wa Kihanafi, lakini alikuwa katika kikundi ambacho kinawatukuza mawalii. Huyu shekhe alikuwa akitufundisha mlango wa kuchinja katika Fiqhi, nami nilikuwa napenda kufunganisha Fiqhi na maisha. Nilimwambia: “Eee shekhe wetu! Watu wameisahau Sunnah hii na hivyo wenye kuchinja wamekuwa kidogo sana. Itikadi yangu ni kuwa lau mashekhe wataitilia mkazo basi watu huenda wakaihuisha sunnah hii”. Akasema shekhe: “Uwezo wa watu wa kifedha umekuwa mdogo”. Nikasema: “Lakini katika sherehe nyengine watu wanachinja na hiyo si katika sunnah”. Akasema: “Unamaanisha nini?” nikasema: “Ninamaanisha kuwa wao huchinja katika maulidi (kuzaliwa) kwa as-Sayyid. Pindi wakati huo ukifika huchinjwa mbuzi na kondoo maelfu kwa maelfu lakini katika Iidul Adh’ha (Idi ya Kuchinja) hapatikani mwenye kufanya hivyo. Lau mashekhe wangezungumzia jambo hili na kuirudisha sunnah badala ya kumchinjia Sayyid, wachinje katika Idi kubwa na hivyo watakuwa wamehuisha sunnah. Na hata kama hawatatoa sadaka kwa kitu chochote ile hali ya kumwaga damu pekee ni katika kutekeleza wito wa Uislamu kwani Allaah Amesema:

فَصَلِّ لِرَبِّكَ وَانْحَرْ

Basi swali kwa ajili ya Rabb wako na chinja kwa ajili Yake. [Al-Kawthar: 2].

 

Sikumaliza haya maneno isipokuwa nilimuona shekhe amenikasirikia na kunitoa katika darasa na akaniona mimi ni mtu wa kuleta vurugu na kuwa mimi ninawachukia mawalii na watu wema! 

 

Hii ilinikumbusha mimi ya kwamba hakuna watu wanaohuisha bid’ah na kujishughulisha nafsi zao isipokuwa wanaua sunnah mfano wake na hii ndio siri katika kupinga bid’ah. 

Hivyo, bid’ah inaleta chuki kwa Sunnah. Ahl-Bida sio tu wanakataa kuikubali Sunnah sahihi bali pia wanajikataza kwenda katika msikiti au sehemu ambazo Sunnah hutekelezwa.

 

E.    Bid’ah Zinaleta Mfarakano Katika Ummah Na Kuondoa Umoja Wao.

Nayo ni kusimama imara katika kutekeleza Sunnah inaleta umoja wa Ummah juu ya kauli moja na hili linawanya Waislamu kuwa safu moja. Lakini bid’ah haimaliziki. Haki ni moja tu lakini batili ina rangi nyingi na aina tofauti. Njia nyoofu ya Allaah ni moja lakini vinjia vya shetani ni vingi sana. Na hivyo imekuja katika hadiyth ya Ibn Mas‘ud (Radhwiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema: 

 

“Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alituchorea mstari. Kisha akasema, ‘Hii ndio njia ya Allaah’. Kisha akachora mistari kuliani na kushotoni kwake na akasema: ‘Hizi ni vijia, katika kila njia kuna shetani ambaye anawaita watu katika njia hiyo’. Hapo akasoma:

 

وَأَنَّ هَـذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ وَلاَ تَتَّبِعُواْ السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ذَلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa. [Al-An’aam: 153].

 

[Imepokewa na Imaam Ahmad, at-Twabari na al-Haakim ambaye ameisahihisha na kukubaliana naye adh-Dhahabiy].

 

Na hivyo Ummah huu uliposhikilia sunnah ilikuwa kauli yao moja na mfarakano ulipokuja ummah huu uligawanyika makundi tofauti. Watu walitoka katika mfumo wa dini, baadhi ya mambo yakiwa ya bid’ah katika itikadi ambayo yalifikia daraja ya ukafiri, mfano wa wale ambao wanakataa ya kwamba Allaah Anajua kila kitu au Allaah Alikuwa hajui mambo mengine kabla. Hawa ni wale watu ambao Ibn ‘Umar alijitenga nao na akasema: “Lau mmoja wao atakuja na 'amali mfano wa mlima Uhud haitakubaliwa na Allaah Aliyetukuka”Na kuna wengine waliomfananisha Allaah na viumbe vyake. Na kuna wale wanaokataa uwezo wa Allaah lakini hawakatai elimu ya Allaah. Na kuna wale waliowakufurisha Waislamu na wakahalalisha kuuliwa kwao mfano wa Khawaarij wakati wa Khalifa 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) na baadaye mbali na kuwa walikuwa wanafanya ibadah nyingi.

 

Swahaba wote walikuwa msitari wa mbele katika kufuata sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Walikuwa wanapendana na wakati walipokuwa na tofauti ya ijtihadi baada ya ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu 'anhu) walibaki katika mahaba baadhi yao kwa wengine. Japokuwa kulitokea vita katika baadhi ya vipindi hasa kile cha 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) lakini walibaki kupendana na kushirikiana na hata kuswali katika misikiti ya wenzi wao bila ya chuki. Hata hivyo, Makhawaarij walitoa rai zao katika Vita vya Siffin baina ya Mu‘awyiah na ‘Ali y(Radhwiya Allaahu 'anhu), Waislamu waligawanyika katika msimamo wa Ahl-us-Sunnah na hivyo kuwa watu wa kwanza wa bid’ah. Katika kikundi hiki hakukuwa na swahaba hata mmoja aliyejiunga,  na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) alimtuma Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuzungumza nao na wengi wakatoka wakatoka katika kundi hilo la Khawaarij na kurudi chini ya Uongozi wa 'Aliy (Radhwiya Allaahu 'anhu) ).

 

Ummah lau utaachiwa watu wa bid’ah basi hauwezi kuja pamoja, lakini unakuja pamoja tu wakati utasimama nyuma ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kufuata Kitabu cha Allaah na Sunnah Zake.

 

F.    Bid’ah Ni Daraja La Kuelekea Kwenye Ukafiri:

Mwanachuoni mmoja mkuu, Al-Barbahaari, mmoja wa wanafunzi wa Ahmad Ibn Hanbal, alisema:

 

“Tahadharini bid’ah, kwa sababu kila bid’ah iliyoanzishwa inaanza kama kitu kidogo na inafanana na ukweli na hivyo kuwadanganya watu. Watu wanaanza kuifuata na hivyo kuwa kubwa na watu kunaswa na kuwatoa katika Uislamu”.

 

Ibn Taymiyyah ameandika kipande kizuri sana katika vitabu vyake kwa kuonyesha kuwa:

 

“Kwa hakika, ukafiri wa Mayahudi na Manaswara ni kwa sababu ya bid’ah. Walikuwa wanaanzisha mambo mapya katika dini na mambo yaliwachukua nje kabisa ya ujumbe wa sawa wa Muwsaa na ‘Iysaa ('Alayhimaa- salam)”.

 

G.   Kwa Ummah Wa Kiislamu Kwa Jumla, Bid’ah Inarudisha Nyuma Kuenea Uislamu na Da‘wah Kwa Ajiili Ya Allaah.

Njia na rai za Ahl-ul-bid’ah zinatumiwa na maadui wa Uislamu kuuonyesha Uislamu. Vipindi vingi katika runinga vinaufananisha Uislamu na dhikri ya masufi, matendo ambayo yanakwenda kinyume na Uislamu. Wanaleta mambo kama hayo ili kuwafanya watu waukimbie Uislamu kwa sababu ya itikadi hizo za Ahl-ul-bida ambazo hazilingani na ‘fitra’ (maumbile). Ni kufuata Uislamu wa kihakika pekee ndio watu wanaweza kuvutiwa kwani watu huvutiwa na mambo ya kawaida yanaokwenda sambamba na maumbile ya mwanadamu.

 

H.    Kwa Mtu Binafsi, Bid’ah Inaharibu Akhira Yake:

Chukua mfano wa mchwa ambao unaruhusiwa kuishi katika ubao. Bid’ah ina athari hiyo hiyo ya kama mchwa ambao hula ubao, nayo bid’ah hummaliza binadamu na kumuacha kama mkakasi. Kwa wakati wa karibu au mbali mtu kama yule anaharibikiwa kwa sababu Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuonya katika hadithi zake nyingi. Bid’ah itakataliwa na Allaah na makazi ya mtu huyo yatakuwa ni motoni, kama alivyotoa wasiya huo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika hadithi iliyopokelewa na Abu Daawuwd na at-Tirmidhy. Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) ataweka kizuizi baina yake na tawba mpaka aache bid’ah yake hiyo na arudi katika mafundisho sahihi ya Uislamu. Katika ulimwengu ataona kuwa anafanya amali ya kujikaribisha na Allaah pamoja na kumridhisha Yeye, lakini akhira, atakujakuta ya kwamba hana faida yeyote kwa aliyoyafanya. Mzigo huu utakuwa mkubwa na hasa ikiwa alikuwa akiwalingania wengine wafuate yale anayoyasema au kufanya, atakuwa na mzigo mkubwa zaidi. Na wale wenye kufuata kiupofu pia watapata adhabu yao. Allaah (Subhaanahu Wa Ta'aalaa) anatuelezea hayo pale aliposema:

 

يَوْمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ يَقُولُونَ يَا لَيْتَنَا أَطَعْنَا اللَّـهَ وَأَطَعْنَا الرَّسُولَا ﴿٦٦﴾ وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءَنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا ﴿٦٧﴾ رَبَّنَا آتِهِمْ ضِعْفَيْنِ مِنَ الْعَذَابِ وَالْعَنْهُمْ لَعْنًا كَبِيرًا ﴿٦٨﴾

Siku zitakapopinduliwa nyuso zao motoni, watasema: Laiti tungelimtii Allaah, na tungelimtii Rasuli. Na watasema: Rabb wetu! Hakika sisi tumewatii mabwana zetu, na wakuu wetu, basi wametupoteza njia. Rabb wetu! Wape adhabu maradufu, na walaani laana kubwa. [Al-Ahzaab: 66-68]

 

Ufumbuzi Wa Kujitenga Na Bid’ah:

Mwanzo kabisa, watu wanaodai ya kwamba wanafuata Sunnah na kuwa katika msimamo wa Ahl-us-Sunnah Wal Jama‘ah ni lazima waelewe na wafahamu hatari za bid’ah na kuwa ni jukumu la kila mmoja kuchukia na kuipinga. Jambo lolote likifanywa kinyume na Qur-aan na Sunnah ni wajibu wa Waislamu kulikataza jambo kwa njia iliyo nzuri na kuwafahamisha watu madhara ya kwenda kinyume. Kuna mtu aliyekuja kwa Imam Maalik na kumwambia kuwa mimi nataka kuhirimia Madinah. Imam Maalik akamfahamisha kuwa kufanya hivyo ni kinyume na Sunnah kwani ihramu (nia na vazi) inavaliwa katika Miiqaat (sehemu maalumu zilizowekwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Yule mtu akasema kuna tatizo gani na kwa sababu ya umbali kutakuwa na thawabu zaidi. Imam Maalik akamsomea aya ifuatayo:

لَّا تَجْعَلُوا دُعَاءَ الرَّسُولِ بَيْنَكُمْ كَدُعَاءِ بَعْضِكُم بَعْضًا ۚ قَدْ يَعْلَمُ اللَّـهُ الَّذِينَ يَتَسَلَّلُونَ مِنكُمْ لِوَاذًا ۚ فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾

Msifanye wito wa Rasuli baina yenu kama wito wa nyinyi kwa nyinyi. Kwa yakini Allaah Anawajua miongoni mwenu wale wanaoondoka kwa kunyemelea. Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo. [An-Nuwr: 63].

 

Tuwaite watu kwa njia nzuri kwa busara na mawaidha mazuri. Allaah Anasema: 

 

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ۚ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ ۖ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ﴿١٢٥﴾

Lingania katika njia ya Rabb wako kwa hikmah na mawaidha mazuri. Na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi. Hakika Rabb wako Yeye Anamjua zaidi aliyepotea njia Yake, Naye Anawajua zaidi waliohidika. [An-Nahl: 125]

 

Hapana budi kufanya “Amru bil ma‘ruuf wa nahyun anil munkar” (kuamrisha mema na kukataza maovu). Bid’ah ni munkar mkubwa sana na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia wazi kabisa katika hadith ya kwamba ni lazima mtu aubadilishe (au aundoshe) ule munkar kwa uwezo wake wote.

 

Ni lazima tutumie fursa ya kuwaelimisha watu na kujifunga sisi wenyewe na Sunnah za kweli za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kutambua mambo ambayo ni bid’ah na yale ambayo si bid’ah. Tufanye bidii kuielewa Qur-aan na pia hadith za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Tujue imani ya kihakika na kufuata maagizo ya Allaah na Nabiy Wake. Na ikiwa tunampenda sana Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi tufuate mwendo wake na kuacha kila ambacho si katika Sunnah zake. Allaah Anatuelezea: Sema: 

 قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Aal-Imraan: 31].

 

Tunamuomba Allaah Atulinde tusiwe ni wenye kufanya bid’ah na Atuongoze katika njia nyoofu na Atusaidie katika kujenga Imani zetu. Mazuri yote yanatokana na Allaah na Nabiy Wake na maovu na mabaya yote yanatokana na Shaytwaan na marafiki zake.

 

  رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا ۚ رَبَّنَا وَلَا تُحَمِّلْنَا مَا لَا طَاقَةَ لَنَا

 

بِهِ ۖ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا ۚ أَنتَ مَوْلَانَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ

Rabb wetu Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Rabb wetu, Usitubebeshe mzigo kama Ulivyoubebesha juu ya wale waliokuwa kabla yetu. Rabb wetu, Usitutwike tusiyoyaweza, na Tusamehe, na Tughufurie na Turehemu, Wewe ni Mola Mlinzi wetu, basi Tunusuru dhidi ya watu makafiri. [Al-Baqarah: 286].

 

Share