Rajab: Fadhila Za Mwezi Wa Rajab Na Yaliyozuliwa Ndani Yake
Fadhila Za Mwezi Wa Rajab Na Yaliyozuliwa Ndani Yake
Abuu 'Abdillaah
BismiLlaah Rahmaani Rahiim
Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kutupa umri wa kufika katika mwezi mtukufu wa Rajab, na Atujaalie uzima na afya tukutane tena na kipenzi chetu kitukufu Ramadhwaan. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
نَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللَّـهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّـهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ ۚ فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ ۚ وَقَاتِلُوا الْمُشْرِكِينَ كَافَّةً كَمَا يُقَاتِلُونَكُمْ كَافَّةً ۚ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ﴿٣٦﴾
Hakika idadi ya miezi mbele ya Allaah ni kumi na mbili katika hukmu ya makadirio ya Allaah, (tangu) siku Aliyoumba mbingu na ardhi. Kati ya hiyo iko minne mitukufu. Hivyo ndiyo Dini iliyo nyoofu. Basi msijidhulumu humo nafsi zenu, na piganeni vita na washirikina wote kama wao wanavyokupigeni vita nyote. Na jueni kwamba Allaah Yu Pamoja na wenye taqwa. [At-Tawbah: 36]
Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth:
عَنْ أَبِي بَكْرَةَ، أَنَّ النَّبِيَّ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ خَطَبَ فِي حَجَّة الْوداع فَقَالَ: ((إِنَّ الزَّمَانَ قَدِ اسْتَدَارَ كَهَيْئَتِهِ يَوْمَ خَلَقَ اللَّهُ السَّمَوَاتِ وَالْأَرْضَ، السَّنَةُ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا، مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ، ثَلَاثٌ مُتَوَالِيَاتٌ: ذُو الْقِعْدَةِ، وَذُو الْحِجَّةِ، وَالْمُحَرَّمُ، وَرَجَبُ مُضَرَ الَّذِي بَيْنَ جُمَادَى وَشَعْبَانَ)) رواه البخاري
Kutoka kwa Abuu Bakrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa Khutbah katika Hajj ya mwisho akasema: "Wakati umemaliza mzunguko wake kama vile siku Allaah Alipoumba mbingu na ardhi. Mwaka ni miezi kumi na mbili, ambayo ndani yake kuna minne ni mitukufu, mitatu inafuatana, Dhul-Qa’dah, Dhul-Hijjah na Muharram na Rajab upo baina ya Jumaadah na Sha'baan)) [Al-Bukhaariy]
Na Anasema pia Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تُحِلُّوا شَعَائِرَ اللَّـهِ وَلَا الشَّهْرَ الْحَرَامَ
Enyi walioamini! Msikhalifu utukufu wa ishara za Allaah, wala miezi mitukufu [Al-Maaidah: 2]
Hapana shaka kutokana na Aayah hizo kwamba miezi hii minne mitukufu hutakiwa kutukuzwa inavyopaswa, kwa kutokufanya maasi na kudhulumiana, kwani malipo ya kufanya madhambi katika miezi hii mitukufu huwa ni makubwa zaidi. Katika kuiheshimu pia ni kumcha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) zaidi kwa kila aina ya 'ibaadah. Lakini sio kwa kuchagua siku maalumu ambazo watu wametenga kwa ajili ya kusherehekea na kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kutokana na kuaminika utukufu wa siku hizo au matukio yake ya kihistoria.
Baadhi ya mambo yanayotendeka katika mwezi huu ambayo hayana uthibitisho kutoka katika Qur-aan wala Sunnah:
- Kuitukuza siku inayosemwa ni ya Mi’raaj au Israa na Mi’raaj (ambayo inadaiwa na wengi kuwa ilikuwa katika mwezi huu wa Rajab, na kudaiwa ni tarehe 27) kwa kufunga hasa siku hii pekee.
- Baadhi ya watu wameanzisha Swalaah ambayo wameiita Swalaat Ar-Raghaaib, ambayo huswaliwa mwanzoni mwa mwezi huu. Hii ni kama ile hali ya mwezi wa Sha'baan na haswa katikati yake ambayo watu wamezusha jina liitwalo Laylatul Baraa-ah (wakisema ni usiku wa ahadi na kusamehewa waliokufa au ni usiku wa kuwekwa mbali na madhambi) ambapo watu hufanya ni usiku wa 'ibaadah na kuswali sana na kufunga mchana wake.
- Watu wametunga du'aa na aina ya Istighfaar na Adhkaar mbali mbali kuwa ni maalumu zisomwe katika mwezi huu wa Rajab.
- Kuzuru makaburi.
- Watu kujumuika na kufanya mihadhara na kupeana mawaidha ya kuelezana historia ya tukio la Israa na Mi'raaj.
Hizi ni sherehe na mipangilio ya 'ibaadah ambayo hayamo katika shariy'ah katu, na wala hazijathibiti katika ushahidi sahihi sehemu yoyote katika vyanzo vya kutegemewa. Ni mambo ya uzushi ambayo baaadhi ya watu wameyazusha kwa ajili ya kuzitukuza siku hizo kutokana na kudhani kufanya hivyo kutawapatia ujira na kuwaongezea daraja yao ya Dini.
Ukifanya utafiti na kupitia katika maandiko yenye kutegemewa, utakuta hakuna uthibitisho wa kusherehekea na kufanya 'ibaadah zozote maalum katika siku hiyo na usiku huo. Pia hakuna ushahidi sahihi wa kufunga Swawm katika siku hiyo ya tarehe 27 ya mwezi wa Rajab. Kama ambavyo hakuna kitu kiitwacho Laylatul Baraa-ah ambayo baadhi ya watu wameiita hiyo siku ya katikati au tarehe 15 ya mwezi wa Sha'baan, ambao ni usiku wa masiku yenye fadhila ambao Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((Allaah Anawatazama viumbe wake katika usiku wa kumi na tano wa Sha'baan na kisha huwasamehe ila wale washirikina au wale wenye kuwa na Uadui)) [Ibn Maajah]
Hakuna ushahidi na ukweli halisi wa kuwa usiku huo wa safari tukufu ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ya Israa na Mi'iraaj, kuwa ulikuwa ni katika siku hii ya tarehe 27 ya Rajab, na hata kama ikisemwa kuwa ilikuwa ni siku hiyo na wasio na ushahidi, bado hakuna mafundisho yoyote yenye kutueleza kuwa tunapaswa kufunga katika siku hii. Bali tutakapofanya hivyo, tutakuwa tumezua jambo lililo nje ya shariy'ah. Hata hivyo, haikatazwi kwa mtu aliyezoea kufunga Jumatatu na Alkhamiys kufunga Swawm zake ikiwa zimeeangukia katika siku hii ya tarehe 27 ya Rajab, au Swawm ya masiku meupe au kulipa madeni yake n.k.
Na kama kuna masiku yenye kushukuriwa na ambayo yamepaswa kukumbukwa kwake kwa kufunga Swawm, basi ni ile siku ya tarehe kumi ya mwezi Muharram au 'Aashuraa ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliwaamrisha Maswahaba zake kuifunga kwa ajili ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kumuokoa Nabiy Muwsaa ('Alayhis-Salaam) kutoka katika balaa la Fir'awn na jeshi lake. Na lisingekuwa jambo gumu au kushindikana kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutufundisha sisi au kutuamrisha kufunga katika siku hii ya 27 ya Rajab kama angetaka, kama alivyotuamrisha kufunga Swawm ya 'Aashuraa na siku kabla yake au baada yake. Lakini hakufanya hivyo! Na maadam hakutuelekeza kufanya hivyo, na yeye hakufanya hivyo, basi hakuna maana ya sisi kuwa mahodari na mafundi wa kujipangia mambo ambayo mbora wetu hakuyaonea umuhimu kwetu kuyafanya.
Ama ya kukusanyana katika siku hiyo ya tarehe 27 Rajab, kwa ajili ya kupeana mawaidha na kuelezana historia ya tukio hilo, ni bora liepukwe na ni vizuri kuwahimiza watu kuhudhuria madarsa Misikitini na mihadhara ili waweze kuyajua hayo na mengi mengine ambayo ni muhimu zaidi katika Dini yao. Kuwepo kwa minasabaat kama hiyo ya kukusanyana kila linapotokea tukio, kunafungua milango ya uzushi na kuifanya Dini kuwa na mambo mengi na mazito hadi yale ya muhimu na yenye faida zaidi yakaachwa na kuendekezwa hayo ya mpito.
Leo hii tuna mifano mingi ya matukio sampuli hii kama vile sherehe na mikusanyiko ya Mawlid, sherehe za nusu Sha'baan, sherehe za mwaka mpya wa Kiislam n.k.
Hata kwenye baadhi ya kalenda kumewekwa siku hizo kama ni siku za sikukukuu. Na tunaona leo hii hata baadhi ya nchi zimeweka sikukuu rasmi ya Mawlid, na kuwapa Waislam mapumziko! Waislam wengi wamefurahi kuona kuwa 'wametambuliwa' na 'kuthaminiwa', ilhali mambo hayo hayana asli katika Dini.
Amiyrul-Muuminiyn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alikuwa akikataza watu kufunga mwezi huu kwa sababu ilihusiana na kushabihiana na Ujahiliya.
Inaelezwa Kwamba Kharashah bin al-Harr alisema: "Nimemuona ‘Umar akiwachapa mikono wale waliokuwa wakifunga Rajab walipokuwa wanafikia chakula chao na alikuwa akisema, huu ni mwezi walioufanya mtukufu katika Ujahiliya." [Al-Irwaa’, 957; Shaykh Al-Albaaniy kasema ni Swahiyh].
Imaam Ibn Al-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema katika kitabu chake cha Zaadul Ma'ad:
''Hakuna ushahidi ulio wazi wa kuwa ni mwezi au tarehe gani tukio hili lilitokea. Kuna taarifa nyingi kuhusiana na jambo hili (kuwa lilifanyika mwezi huu wa Rajab) lakini hakuna hata moja katika taarifa hizo yenye uamuzi kamili na sahihi. Na hakuna 'ibaadah zozote maalum zenye kufungamana nayo.''
Kwa ujumla siku zote za Muislam ni nzuri na bora kwa kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Huwa Anashuka kila usiku katika fungu la tatu la usiku kama Hadiyth inavyoeleza:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba du’aa Nimuitike? Nani Ananiomba jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Kuna masiku mengi yenye fadhila kama masiku ya mwezi wa Ramadhwaan ambao unatukaribia, masiku kumi ya mwezi wa Dhul-Hijjah ambapo 'ibaadah ya hija inaanza, na haswa zaidi siku ya 'Arafah, pia siku ya tarehe kumi ya mwezi wa Muharram ambayo tumeitaja hapo juu. Siku za Jumatatu na Alkhamiys, Ayyamul-Biydhw (masiku meupe au masiku ya usiku ung'aao - tarehe kumi na tatu, kumi na nne na kumi na tano za kila mwezi). Miezi minne mitukufu (ambayo ni Dhul-Qa'dah, Dhul-Hijjah, Muharram na Rajab). Masiku hayo hapo juu ni siku zenye kupendeza kufunga (ila sio kuihusisha siku maalum kama hiyo ya tarehe 27 kufunga katika mwezi Rajab na hali haina uthibitisho kufanya hivyo) Kufunga siku ya 'Arafah inapendezewa sana kwa yule ambaye haitekelezi 'ibaadah ya Hijjah kwa wakati huo. Masiku kumi ya Dhul-Hijjah yana fadhila zaidi kuliko masiku mengine. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyosimuliwa na Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema:
((Hakuna matendo mazuri yafanywayo katika masiku mengine yakawa bora kuliko yafanywayo katika masiku haya (ya mwanzo wa mwezi wa Dhul-Hijjah)''. Kisha baadhi ya Maswahaba wakamuuliza: ''Kuliko hata Jihaad?'' Akawajibu: Kuliko hata Jihaad, isipokuwa tendo la mtu atakayefanya kwa kujiingiza hatarini yeye na mali yake (kwa ajili ya Allaah) na harejei na chochote katika hivyo)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Masiku kumi ya mwisho ya mwezi wa Ramadhwaan ni matukufu zaidi kuliko nyusiku kumi ya mwezi wa Dhul-Hijjah na masiku kumi ya mwezi wa Dhul-Hijjah ni matukufu zaidi kuliko michana ya mwezi wa Ramadhwaan. Haya ni maoni yenye nguvu ya Maulamaa. Ama siku iliyo bora kuliko zote basi ni siku ya 'Arafah, kwani imesimuliwa kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:
((Hakuna siku iliyo na fadhila kuliko zote mbele ya Allaah kama siku ya 'Arafah))
Mifano hiyo ni kuonyesha kuwa masiku yaliyotajwa hapo juu ni bora kwa Muislam na yaliyo munasibu kwa kumwabudu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Kazipa ubora baadhi ya nyakati kuliko zingine kwa kumpa tu mtu fursa ya kufanya zaidi matendo mema kwa kadiri awezavyo, na matendo hayo ni muhimu kwa Muislam kwa maisha yake ya hapa duniani na Aakhirah.
Na ukitazama utakuta yote yamewekwa wazi na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na jinsi ya kutekeleza 'ibaadah katika masiku au nyakati hizo. Ama zile ambazo hazijatajwa na kuwekwa wazi basi ni bora na vizuri tuziache na kujiepusha na kufanya matendo ndani yake ambayo hatukufundishwa. Nako kutakuwa bora katika Dini yetu na hadhi yetu, kama alivyosema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth iliyosimuliwa na An-Nu'uman bin Bashiyr (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa):
عَنْ أَبِي عَبْدِ اللَّهِ النُّعْمَانِ بْنِ بَشِيرٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وآله وسلم يَقُولُ: (... فَمَنْ اتَّقَى الشُّبُهَاتِ فَقَدْ اسْتَبْرَأَ لِدِينِهِ وَعِرْضِهِ ... ) رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ
((...atakayekaa mbali na utata, basi atakuwa ameilinda (ameitakasa) Dini yake na heshima yake...)) [Al-Bukhaariy]
Wa Allaahu A'lam