26-Dalili Za Kheri Katika Mambo Yamfaayo Maiti: Kutaja mazuri ya maiti na kuacha mabaya yake
Kutaja mazuri ya maiti na kuacha mabaya yake:
Ikiwa hapana budi kumzungumzia maiti ni bora wamzungumzie mazuri yake ikiwa maiti huyo ni katika jumla ya sifa aliyokuwa nayo na kuacha kuzungumzia mabaya yake ikiwa ni mtu mwenye mabaya, kwani hayo mazuri ndiyo yatakayomnufaisha yeye kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) na asisingiziwe yasiyokuwa ya kwake.
Tunajifunza katika hadithi ya Bukhari na Muslim: kuwa kuna wakati lilipita jeneza na watu wakamtaja mazuri ya yule maiti, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “Amestahiki, amestahiki, amestahiki” jeneza lingine likapita na watu wakataja mabaya ya yule maiti wa pili, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, ““Amestahiki, amestahiki, amestahiki” Umar akauliza, ‘Fidia iwe juu yako kwa baba yangu na mama yangu, ilipita jeneza watu wakamtaja kwa kheri ukasema, “Amestahiki, amestahiki, amestahiki” lilipopita jeneza la pili akatajwa vibaya ukasema, “Amestahiki, amestahiki, amestahiki” Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa Sallam) akasema, “Mtakayemtaja kwa kheri amestahiki pepo, na mtakayemtaja kwa shari amestahiki moto, nyie ni mashahidi wa Allah katika ardhi, nyie ni mashahidi wa Allah katika ardhi.”