Swalaah Ya Shuruwq Ni Sawa Na Swalaah ya Dhwuhaa?
Swalaah Ya Shuruwq Ni Sawa Na Swalaah ya Dhwuhaa?
SWALI:
Assalam alaykum
ukiwa umeamka usiku kwa ajili ya swala za usiku hukurudi kulala tena mpaka ukaswali swalul-fajri naukawa pia hukurudi tena kulala ukaendelea na adhkar za asubuhi mpaka jua likatoka baada ya dakika kumi au ishirini ukaswali rakaa mbili hizi zinakua kama uliyefa umra kwa kauli ya mtume s.a.w. swali ni hili kisha kwa baadaye unaweza kuswali tena kwa ajili swala dhuha
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza tunapenda kukumbusha ndugu yetu, kuacha kufupisha kumsalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo kuhusu makatazo yake:
Al-Lajnah Ad-Daaimah: Haijuzu Kufupisha Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Katika Maandishi
Imaam Ibn Baaz: Kufupisha Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Kwa Mfumo Wowote Haijuzu
Swalaah ya Shuruwq hakika ni kwamba hakuna katika Shariy’ah Swalaah kwa jina hilo, ila imejulikana hivyo kwa kuwa ni Swalaah ambayo huswaliwa baada ya kuchomoza jua na baada ya kukaa kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) baada ya Swalaah ya Alfajiri hadi kuchomoza jua.
Fadhila zake imetajwa katika Hadiyth ifuatayo:
عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال: ((مَنْ صَلَّى الْغَدَاةَ فِي جَمَاعَةٍ ثُمَّ قَعَدَ يَذْكُرُ اللَّهَ حَتَّى تَطْلُعَ الشَّمْسُ ، ثُمَّ صَلَّى رَكْعَتَيْنِ ، كَانَتْ لَهُ كَأَجْرِ حَجَّةٍ ، وَعُمْرَةٍ ، تَامَّةٍ ، تَامَّةٍ ، تَامَّةٍ)) رواه الترمذي (586) أخرج الترمذي صححه الألباني .
Imetoka kwa Anas kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jamaa'ah kisha akakaa anamdhukuru Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhiy na kaisahihisha Al-Albaaniy]
Tanbihi: Hadiyth hiyo wamekhitilafiana ‘Ulamaa usahihi wake, kuna waliosema ni dhaifu na wengineo wameipa daraja ya Hasan kama Imaam Al-Albaaniy
Inavyopaswa ni kukaa baada Swalaah ya Alfajiri hadi jua litoke na upite wakati wa makruwh (unaochukiza kuswali) yaani wakati pale jua linapochomoza hasa, usubiri kama takriban dakika kumi na tano hadi ishirini hivi ndio uswali rakaa mbili. Ndio maana ikaitwa Swalaatush-Shuruwq, lakini asili yake hiyo ni Swalaah ya Dhwuhaa kwani Swalaah hizi hazina tofauti baina yao katika kuswaliwa isipokuwa Swalaah ya Shuruwq inaswaliwa mapema zaidi lakini ndio hiyo hiyo Swalaah ya Dhwuhaa inayoswaliwa mwanzoni mwa wakati wake au mwishoni kabla ya Adhuhuri.
Bonyeza viungo vifuatavyo upate faida tele kuhusu Swalaah ya Dhwuhaa:
Swalaah Ya Adhw-Dhwuhaa: Idadi Ya Rakaa Zake, Wakati Wake Na Fadhila Zake
Kuna Du’aa Maalumu Ya Swalaah ya Dhwuhaa?
Vile vile kuna Hadiyth inayoonyesha kuwa a inatakiwa iswaliwe wakati jua limeshakuwa kali nayo kutokana na Hadiyth ifuatayo:
عَنْ زَيْدِ بْنِ أَرْقَمَ قَالَ خَرَجَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَلَى أَهْلِ قُبَاءَ وَهُمْ يُصَلُّونَ فَقَالَ” : صَلاةُ الأَوَّابِينَ إِذَا رَمِضَتْ الْفِصَالُ “رواه مسم
Kutoka kwa Zayd bin Arqam amesema: "Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alitoka akawaona watu wa Qubaa wanaswali akasema: “Swalaah ya Al-Awwaabiyn ni wakati ngamia wachanga wananyanyua miguu yako.” [Muslim].
Imeitwa Swalaah ya Al-Awwaabiyn kwa sababu ya umoto wa mchanga uliopigwa na jua kali..
Kwa hiyo ni bora kwa mwenye kupenda kuswali Swalaah ya Dhwuhaa aiswali wakati jua limekuwa kali wakati wowote hadi takriban nusu saa kabla ya Swalaah ya Adhuhuri. Na ikiwa amekaa mtu baada ya Swalaah ya Alfajiri hadi kuchomoza jua akimdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) ili apate fadhila za Hajj na 'Umrah, anaweza kuswali kwanza rakaa zake mbili baada ya jua kuchomoza, kisha tena aongezee rakaa mbili, au nne au sita nyingine za Swalaah hiyo ya Dhwuhaa apendavyo.
Na Allaah Anajua zaidi