Swalaah Za Sunnah Zilizo Sahihi Na Ambazo Si Sahihi
Swalaah Za Sunnah Zilizo Sahihi Na Ambazo Si Sahihi
SWALI:
Assalaamualaykum ndugu zangu,
Mimi siku zote naamka saa nane za usiku, yaani na amshwa naturally. Nina sali kwa mpango ufuatao:
1. Sunnatil-udhuu rakaa 2
2. Sunnati Rasulu-Allaah Swalla Allaahu alayhi wa sallam wa sallam rakaa 2
3. Sunnat tahajjud rakaa 2
4. Sunna ya usiku ule raka ....kama ilvyoandikwa
5. Sunnat hajjat rakaa 2, 2,2, mujibu wa haja zangu.
6. Sunnat tawba rakaa 2
7. Salaatul witr rakaa 3.
By the time nimewahi zote Swalah ya fajr ni tayari. na endelea kufanya dhikruAllaah baada ya swalah ya fajr mpaka time ya ishraaq na tena naendelea kuwepo kwenye msala kwa dhikru-Allaah mpaka swalah ya dhuhaa.
Je nifafanulieni wapi nimekosea na nifanye sahihi namna gani
Jazaakallahukheir
Fiamaanillah
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika ‘ibaadah ni jambo muhimu sana kwa kila Muislamu kwani katika kufanya ‘ibaadah yoyote ikiwa ya vitendo au kauli, lazima masharti mawili yapatikane ndipo ‘ibaadah hiyo ikubaliwe nayo ni:
1-Ikhlaas – Iwe kwa kutaka Radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na sio yenye Riyaa (kujionyesha) au sio yenye kutendeka kwa ajili ya maslahi ya kidunia.
2-Iwe inafanyika kutokana na mafunzo ya Qur-aan na Sunnah.
Tunakutajia hapa zilizo sahihi na zisizo sahihi kutokana na maelezo yako:
Swalaah |
Daraja yake |
Dalili/Maelezo
|
Sunnatul- Wudhuu Rakaa mbili |
Sahihi |
Bilaal (Radhwiya Allahu 'anhu) akiswali hata Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaota nyao zake ziko Jannah (Peponi) kwa kufanya hivyo
|
Sunnatul-Rasulu-Allaah |
Sio sahihi |
Hakuna dalili yoyote.
|
Tahajjud Rakaa 2 |
Sahihi |
Ni Qiyaamul-Layl (Kisimamo cha usiku) Unaweza kuswali mbili, au nne, au sita au nane ukamalizia na tatu za Witr
|
Sunnah ya usiku |
Sahih |
Nayo ni Qiyaamul-Layl. Ni Swalaah yoyote unayoswali baada ya ‘Ishaa kama ni kisimamo cha usiku.
|
Sunnah ya Haja |
Haifai |
Imepingwa na ‘Ulamaa kuwa ni Hadiyth dhaifu. Muislamu anaomba haja zake kwa kuomba du'aa kama kawaida.
|
Sunnati Tawbah |
Sahihi |
Anapofanya mja dhambi anaswali Rakaa mbili kuomba maghfirah |
Salaatul Witr |
Sahihi |
Rakaa 3 unamalizia baada ya kuswali 8 au chini yake za Qiyaamul-Layl (Kisimamo cha usiku) Hii imesisitizwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
|
Unavyomalizia kuwa inafika Alfajiri kisha unaendelea kufanya Dhikru-Allaah hadi litoke jua kisha unaswali Swalaah ya Dhwuhaa, hakika Hadiyth hiyo baadhi ya ‘Ulamaa wameona kuwa ni dhaifu na wengineo wameona kuwa ni sahihi. Nayo inatokana na Hadiyth ifuatayo:
عن أنس عن النبي صلى الله عليه وسلم ، أنه قال : من صلى الفجر في جماعة ثم قعد يذكر الله حتى تطلع الشمس ثم صلى ركعتين كانت له كأجر حجة وعمرة تامة تامة تامة أخرج الترمذي صححه الألباني
Imetoka kwa Anas kwamba Nabiy (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Atakayeswali Alfajiri katika Jamaa'ah kisha akakaa Anamdhukuru Allaah mpaka likachomoza jua kisha akaswali Raka'ah mbili, atapata ujira kama ujira wa kwenda Hajj na 'Umrah ulio kamili kamili kamili)) [Imetolewa na At-Tirmidhy na kaisahihisha Al-Albaaniy]
Kwa hiyo tekeleza ambazo ni sahihi na epukana na ambazo si sahihi au zina utata.
Na Allaah Anajua zaidi