11-Adabu Za Ndoa Katika Sunnah Iliyotakasika: Kukoga Pamoja Mume Na Mke
Inaruhusiwa kwa mume na mke kukoga pamoja katika sehemu moja hata kama mume ataona sehemu za siri za mke na mke ataona sehemu za siri za mumewe. Hii imethibitika katika Hadiyth Swahiyh mbali mbali, miongoni mwa hizo ni:
Kwanza:
عَنْ عَائِشَة ، قَالَتْ: كُنْتُ أَغْتَسِلُ أَنَا وَرَسُولُ اللّهِ مِنْ إِنَاءٍ. ـ بَيْنِي وَبَيْنَهُ ـ، وَاحِدٍ (تختلف أيدينا فيه). فَيُبَادِرُنِي حَتَّى أَقُولُ: دَعْ لِي، دَعْ لِي. قَالَتْ: وَهُمَا جُنُبَانِ
Imetoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah رضي الله عنها ambaye alisema: "Nilikuwa nakoga na Mtume kutoka chombo kimoja cha maji kilichowekwa baina yetu (kiasi kwamba mikono yetu ilikuwa ikipishana katika maji). Alikuwa akishindana na mimi hadi nikasema: Nibakishie (maji), nibakishie (maji)". Akaongeza: "Tulikuwa katika hali ya janaba" (yaani hali ya kutoka katika tendo la ndoa).[1]
Pili:
عن معاوية بن حدِّهِ ، قَالَ: قُلْتُ يَا نَبِيَّ الله عَوْرَاتُنَا مَا نَأْتِي مِنْهَا وَمَا نَذَرُ؟ قَالَ: ((احْفَظْ عَوْرَتَكَ إِلاَّ مِنْ زَوْجَتِكَ أَوْ مَا مَلَكَتْ يَمِينُكَ)). قُلْتُ: يَا رَسُولَ الله إذَا كَانَ الْقَوْمُ بَعْضُهُمْ في بَعْضٍ؟ قَالَ ((إِنِ اسْتَطَعْتَ أَنْ لاَ يَرَاهَا أَحَدٌ فَلاَ تُرِيَنَّهَا)) قَالَ قُلْتُ يَا نَبِيَّ الله إِذَا كَانَ أَحَدُنَا خَالِياً؟ قَالَ ((فَالله أَحَقُّ أَنْ يُسْتَحْيَى مِنْهُ مِنَ النَّاسِ))
Kutoka kwa Mu'aawiyah Ibn Haydah ambaye alisema: "Nilimwambia Ee Mjumbe Wa Allaah, sehemu gani ya tupu zetu zinaruhusiwa na zipi tujihadhari nazo?" Mtume akasema: "Chunga utupu wako isipokuwa kwa mkeo au wale iliyomiliki mikono yako ya kuume" Nikasema: "Ee Mjumbe wa Allaah, je, Vipi inapokuwa jamaa wanaishi pamoja?" Mtume akasema: "Ikiwa utahakikisha kuwa hakuna mtu atakayeona tupu zenu, basi fanya hivyo". Akasema: "Ee Mjumbe wa Allaah, je, vipi inapokuwa mmoja yuko pekee (amekaa uchi)?" Mtume akasema: "Allaah Anastahiki staha zaidi ya watu wengine”.[2]
Kwa hiyo inaruhusiwa wote mume na mke kutazamana na kugusa mwili wa mwenzake, mume au mke hata sehemu zao za siri.