Mume Kanioa Kwa Kunidangangya Hana Mke Kisha Hataki Kunipa Talaka
SWALI:
Asalam alykum,
Swali langu ni je waweza kadai talaka endapo mume kakudanganya?Mume wangu alinidanganya kuwa hana mke hata mmoja nikakubali kuolewa nae lakini alinipeleka mji mbali kidogo na wazazi wangu kufika kule kumbe ana wake watatu (3) na mie wanne niliamua kuvumilia lakini aliamua kubadilika mara anachelewa kurudi mara nakuta ujumbe wa wanawake zake ktk simu na ilifikia wakati ananiomba kinyume na maumbile kuona inazidi nikaamua kurudi nyumbani na kuwaeleza shangazi zangu,Talaka nikadai hataki kunipa eti nikiitaka niinunue kwa garama atakayosema.Kinachonisumbua bado ananisumbua eti ananipenda ukweli simtaki tena. Je nifanyeje aniache tena kwa wema mimi sitaki ugomvi nae. Mimi ndio kwanza nini miaka 25.
Waadha asalam alykm.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu aliyeuliza swali hili kuhusu ndoa na talaka. Hakika makosa mengi hutokea na kufanyika wakati wa posa na uchaguzi baina ya wanandoa. Mara nyingi huwa hatuchukulii uzito vigezo na nasiha akizotupatia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hivyo kuja kujuta baadaye. Mazingira na malezi hucheza dauru muhimu katika ufanisi wa ndoa zetu. Hapa yaonyesha binti muuliza swali na wazazi walikosea katika uchaguzi.
Misingi aliyotupatia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haikufuatwa vilivyo mpaka imekufikisha katika janga kama hilo. Kwa hali nyingi mwanadamu anakosea na tunapokosa inafaa tujirudi na tujirekebishe ili tusiingie katika matatizo mengine. Msingi mkuu tuliopewa wa kuchagua mume au mke ni:
Dini na Maadili: Huu ni ule ufahamu wa uhakika na wa kweli wa Uislamu na utekelezaji wake. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) anatueleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Hatazami sura zenu na mali yenu lakini Anatazama mioyo yenu na amali zenu” (Muslim).
Hivyo, ikiwa msingi wa uchaguzi ni sura au mali huwa tunajiingiza katika balaa. Amesema tena Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mwanamke huolewa kwa mambo manne: Kwa mali yake, nasaba yake, uzuri wake na Dini yake. Chagua mwenye Dini usiharibikiwe” (al-Bukhaariy na Muslim).
Na mwanamme naye pia huchaguliwa au kukubaliwa kwa moja ya mambo haya manne. Ikiwa Dini haipo katika msingi wa uchaguzi basi ni hasara. Amesema tena Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Anapokujieni munayemridhia Dini na maadili yake muozeni, kwani msipofanya hivyo kutakuwa na Fitna katika ardhi na uharibifu mkubwa” (at-Tirmidhiy)
Inaonyesha vipengele vya Dini na maadili havikutazamwa wala mwenye kuposa (mume) hakuchunguzwa na familia ya mke kwani kama hilo lingefanyika basi yangebainika hayo uliyoyasema. Pindi uhakika wake ungejulikana kuwa yeye ni mtu wa aina gani uamuzi muafaka ungefanywa kwa urahisi kabisa. Inafaa kabla ya kujibu posa watu wa mume waulizie kuhusu Dini na tabia ya mke na vile vile watu wa mke. Na zipo njia nyingi za kutekeleza hilo kwa usahali.
Uongo ni tabia ambayo Muislamu hafai kabisa kuwa nayo kwa hali yoyote ile kwani kufanya hivyo ni unafiki na wanafiki watakua na adhabu kali sana. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuelezea kuwa Muislamu wa kweli hawezi kuwa muongo. Allaah Aliyetukuka Ametuhimiza kuwa na wakweli pale Aliposema: “Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kuweni pamoja na wakweli” (9: 119). Na wakweli wanaume na wanawake watakuwa na ujira mkubwa (33: 35).
Hakika ni kuwa ukweli unampeleka mtu Peponi na uongo Motoni hii ni kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na imepokewa kwa Ibn Mas‘uud (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika ukweli unamuongoza mtu katika wema na wema unampeleka mtu Peponi. Na hakika mtu huendelea kusema ukweli mpaka akaitwa mkweli mbele ya Allaah. Na hakika uwongo unampeleka mtu katika uchafu na uchafu unampeleka mtu Motoni. Na mtu huendelea kusema uongo mpaka akaandikwa kuwa ni muongo mbele ya Allaah” (al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).
Na imepokewa kwa Abu Muhammad, al-Hasan bin ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Llahu ‘anhuma), mjukuu wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na raihani wake kuwa alisema: “Nimehifadhi kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): ‘Acha lenye kukutia shaka kwa lisilokutia shaka. Hakika ukweli ni utulivu na uongo ni shaka” (Ahmad, at-Tirmidhiy na an-Nasai’iy. Isnadi yake ni Sahiih na ameisahihisha Ibn Hibbaan).
Ni adhabu kubwa na mateso hapa duniani kuwa na mume au mke ambaye ni muongo. Ushauri wetu kuhusu suala hilo ni kuwa ujaribu kuitisha kikao baina ya wawakilishi wako (kwa mfano wazazi au mzazi) na wawakilishi wake ili muzungumzie suala hilo. Mukiwa nia yenu ni suluhu basi Allaah Aliyetukuka Atafanikisha kikao hicho na kuleta suluhu. Kila mmoja katika kikao hicho ni lazima awe mkweli kwa nafsi yake na mustakbali wa ndoa yenu.
Miongoni mwa suala muhimu la kuzungumzia ni ile kauli yako uliyosema katika swali lako “ilifikia wakati ananiomba kinyume na maumbile”. Jambo hili ikiwa tumelifahamu vyema ni kuwa anataka kukulawiti (kukuingilia kimapenzi kwa njia ya nyuma badala ya mbele). Hili ni jambo ambalo ni haramu na wafanyao hivyo wana adhabu kali hapa duniani na Akhera. Ikiwa ataacha uongo wake na tabia hiyo ya kukutaka kinyume na maumbile basi fanyeni suluhu na urudi kwa mumeo. Hiyo ni bora kwako hapa duniani na Akhera na msamehe kwa uongo wake wa awali.
Ikiwa hatotaka kubadilika basi ni bora zaidi uachane naye. Inabidi uende ukashitaki ikiwa sehemu yako yupo Qaadhi au ikiwa hayupo, basi kwa Shaykh au Imaam ambaye atawaita nyote wawili. Kisheria kwa sababu makosa ni yake hufai kuinunua talaka na ikibidi kuinunua basi sheria inasema utarudisha mahari yake tu aliyokupatia sio zaidi ya hayo. Kurudisha hata kama utainunua talaka zaidi ya mahari ni dhulma na haifai kisheria.
Tunakuombea tawfiki katika amali yote hiyo.
Na Allaah Anajua zaidi