Sababu Gani Zinamruhusu Mke Kuomba Talaka?
Sababu Gani Zinamruhusu Mke Kuomba Talaka?
SWALI:
Napenda kujua sababu ngapi zinakubalika katika sheria ya kiislam kwa mwanamke ikiwa atapenda kutengana na ndoa yake au hoja gani ina nguvu zaidi
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika hili ni swali ambalo limejitokeza hasa katika karne iliyopita na hii kwa yale mashambulizi ambayo yanalimbikiziwa Uislamu kuwa haujampatia haki yoyote mwanamke. Jambo la talaka ni mojawapo.
Hakika ni kuwa mke anaweza kuomba talaka kutoka kwa mumewe katika hali zifuatazo:
- Ikiwa anapata dhara kutoka kwa mumewe kama kumpiga, kutomtimizia tendo la ndoa kwa sababu yoyote ile, kughibu kwa muda bila kuwa na habari kumhusu na kadhalika. Hii inatokana na msingi wa Hadiyth ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema: "Haifai kudhuru wala kulipana madhara" (Ahmad, Ibn Maajah, ad-Daraqutwniy).
- Ikiwa mume hana istiqaamah katika Dini kama vile kuacha Swalah na kufanya maasi mengine mengi na makubwa.
- Ikiwa mume hamtimizii mkewe haja zake za msingi kama kumtizama kwa chakula, malazi, matibabu na kadhalika.
- Ikiwa mke hampendi tu mumewe, anaweza kuomba Khul'u (kujivua kwenye ndoa) na katika hali hii mke atabidi amrudishie mumewe mahari yake aliyompatia wakati wa harusi.
Hali hii ilitokea kwa Swahaabiyyah mke wa Thaabit bin Qays bin Shammaas:
عَنْ اِبْن عَبَّاس أَنَّ اِمْرَأَة ثَابِت بْن قَيْس بْن شَمَّاس أَتَتْ النَّبِيّ - صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ - فَقَالَتْ يَا رَسُول اللَّه : مَا أَعِيبُ عَلَيْهِ فِي خُلُق وَلَا دِين وَلَكِنْ أَكْرَهُ الْكُفْرَ فِي الْإِسْلَام فَقَالَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((أَتَرُدِّينَ عَلَيْهِ حَدِيقَته)) قَالَتْ : نَعَمْ قَالَ رَسُول اللَّه - صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((اِقْبَلْ الْحَدِيقَة وَطَلِّقْهَا تَطْلِيقَة)) البخاري والنسائي
Kutoka kwa Ibn 'Abbaas kwamba mke wa Thaabit bin Qays bin Shammaas alikwenda kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Ee Rasuli wa Allaah! silalamiki kwa tabia yake wala dini yake lakini nachukiwa kukufuru katika Uislamu. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamwambia: “Je utamrudishia bustani yake?” Akajibu: Ndio. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kumwambia Thaabit: “Pokea bustani na muache talaka moja” [Al-Bukhaariy na An-Nasaaiy]
Ama mwanamke kuomba talaka bila ya sababu yoyote ajue kwamba haifai na isitoshe hatopata kusikia harufu ya Pepo:
عَنْ ثَوْبَان مَوْلَى رَسُول اللَّه – صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ – عَنْ النَّبِيّ – صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ – أَنَّهُ قَالَ :((أَيّمَا اِمْرَأَة سَأَلَتْ زَوْجهَا الطَّلَاق فِي غَيْر مَا بَأْس حَرَّمَ اللَّه عَلَيْهَا رَائِحَة الْجَنَّة)) الترمذي و قال حديث حسن
Kutoka kwa Thawbaan amesema kwamba: Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwanamke yeyote anayemuomba mumewe talaka bila ya sababu yoyote, Allaah Amemharimishia harufu ya Pepo” [At-Tirmidhiy na kasema Hadiyth Hasan]
Na Allaah Anajua zaidi