Kujua Aina Ya Mtoto Aliyeko Tumboni Kwa Ultra Sound Kabla Hajazaliwa

 

SWALI:

Jee?ukiwa una mimba na doctor kakuandikia kufanya kipimo cha ultrasound kufika kule ukaingiwa na hamu yakutaka kujua ni mtoto gani utaezaa imam wa kike au wakiume jee?nidhambi au ni harram?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kutokana na teknolojia ya vyombo vya kisayansi na upana wa elimu ya madaktari, kumekuweko uwezekano wa kutambua aina ya mtoto aliye tumboni kwa mama mja mzito hata kabla hajajifungua. Japokuwa uwezekano huu upo, lakini vilevile ni mambo ambayo si yenye uhakika mia kwa mia na huenda makosa yakatokea kama kesi mbalimbali zilizotangazwa na kuandikwa. Juu ya hivyo, hawawezi kutambua hivyo hadi miezi ipite na sio mimba inapokuwa bado changa, tena lazima mama ahakikishwe anawekwa kwenye scanner katika hali ambayo yule mtoto kule tumboni awe amepanua miguu yake ili waweze kupata picha ya aina ya jinsia yake, ikishindikana mtoto kuwa katika hali hiyo, basi zoezi zima linafeli na mama ataambiwa aende mara nyingine kujaribiwa tena na tena! Hivyo si kazi rahisi na si jambo lenye uhakika sana.

 

Inapasa tutambue kwamba japokuwa madaktari wanaweza kutambua jinsia ya mtoto, lakini hawana uwezo wa kujua elimu ya kinachoumbika matumboni kama huyo mtoto ataendelea kuishi humo hadi azaliwe, au atafariki akiwa tumboni, bali ni Apendavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Kukiacha kiumbe chake kiendelee kuishi humo au kisiendelee. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

((اللّهُ يَعْلَمُ مَا تَحْمِلُ كُلُّ أُنثَى وَمَا تَغِيضُ الأَرْحَامُ وَمَا تَزْدَادُ وَكُلُّ شَيْءٍ عِندَهُ بِمِقْدَارٍ))

 

((Allaah Anajua mimba abebayo kila mwanamke, na kinachopunguka na kuzidi matumboni. Na kila kitu Kwake ni kwa kipimo)) [Ar-Ra'ad: 8]

 

Wala hawawezi kujua kama atazaliwa na kuishi muda gani, hali ya maisha yake na rizki yake, kama atakuwa mwema au muovu n.k. Haya yote ni elimu Aliyokwishaijua Muumba Mwenyewe Ambaye Humtuma Malaika Wake kuyaandika kwa kila kiumbe kinapotimia miez minne tumboni mwa mama yake:  

 

عن أبي عبد الرحمن عبد الله بن مسعود -رضي الله عنه- قال حدثنا رسول الله -صلى الله عليه وسلم- وهو الصادق المصدوق:  إن أحدكم يُجمع خلقه في بطن أمه أربعين يوماً نطفة، ثم يكون علقة مثل ذلك، ثم يكون مضغة مثل ذلك، ثم يرسل إليه الملك فينفخ فيه الروح، ويؤمر بأربع كلمات: بكتْبِ رزقه، وأجله، وعمله، وشقي أو سعيد، فوالله الذي لا إله إلا غيره إن أحدكم ليعمل بعمل أهل الجنة حتى ما يكون بينه وبينها إلا ذراع فيسبق عليه الكتاب فيعمل بعمل أهل النار فيدخلها، وإن أحدكم ليعمل بعمل أهل النار حتى ما يكون بينه وبينها إلا ذراع فيسبق عليه الكتاب فيعمل بعمل أهل الجنة فيدخلها   رواه البخاري ومسلم

 

 

 

 

 

Kutoka kwa Abu 'Abdur-Rahmaan 'Abdullaah bin Mas'uud (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba: "Ametuelezeza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye ni mkweli mwenye kuaminiwa ((Hakika kila mmoja hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arubaini zifuatazo huwa ni donge la damu, kisha arubaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah Humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho na (Malaika huyo) anaamrishwa maneno manne; Kuandika rizki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, mtu muovu au mwema. WaLlaahi naapa kwa Yule Ambaye hakuna mungu isipokuwa Yeye, hakika mmoja wenu huenda afanye vitendo vya watu wa Peponi hadi ikawa baina yake na pepo ni dhiraa na kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa motoni akaingia motoni. Na mmoja wenu hufanya vitendo vya watu wa motoni hadi ikawa baina yake na moto ni dhiraa na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti akafanya amali ya watu wa peponi akaingia peponi.)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

 

Hayo yote ni elimu ya ghayb (mambo yaliyofichikana na ambayo mwenye elimu nayo ni Allaah Pekee). Hii ni kutokana na kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) katika Qur-aan na Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama ifuatavyo:

 

Imaam Ahmad amesimulia kwamba Ibn 'Umar amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema:        

((مفاتح الغيب خمس لا يعلمها إلا الله: إِنَّ اللَّهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ))

((Funguo za ghayb ni (mambo) matano ambayo hakuna anayeyajua isipokuwa Allaah; ((Hakika kuijua Saa (Qiyaamah) kuko kwa Allaah. Na Yeye Ndiye Anayeiteremsha mvua. Na Anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi. Na haijui nafsi yoyote itachuma nini kesho. Wala nafsi yoyote haijui itafia nchi gani. Hakika Allaah Ndiye Mwenye kujua, Mwenye khabari. [Luqmaan: 34])) [Al-Bukhaariy]

Labda tuifafanue Aayah hiyo ya Surat Luqmaan vizuri kwa upande wa kilugha ili ifahamike vizuri na kwa usahihi. Anaposema Allaah:

 

 

    

   ((وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ))   

 

 

 

 

((Na Anavijua viliomo ndani ya matumbo ya uzazi))

 

Hapa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametumia neno مَا 'maa' na sio مَن 'man' hivyo ni: "maa fil-arhaam" kwa maana:  "viliomo…" na sio "man fil-arhaam" "Nani aliyomo…"Kwaniman inatumika kwa kila kiumbe chenye roho chenye akili. Kwa hiyo kusudio ni aina gani ya kiumbe hicho kitakuwa kama tulivyotaja hapo; mtu wa kheri au wa shari, ataishia Peponi au motoni n.k. Hivyo viliomo ndani ya matumbo ya uzazi sio tu kujua ni mwanamume au mwanamke bali ina maana pana zaidi ambayo hakuna ajuaye isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama Anavyosema:

 

((قُل لَّا يَعْلَمُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ الْغَيْبَ إِلَّا اللَّهُ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ))

 

 

 

 

 

((Sema: Hapana katika mbingu na ardhi ajuaye ya ghaibu isipokuwa Allaah. Wala wao hawajui lini watafufuliwa)) [An-Naml: 65]

 

 

Hitimisho ni kwamba ni vizuri kujiepusha kutaka kujua hayo bali mwachie Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na umuombe Akujaalie ujifungue kwa salama na awe mtoto wa kheri, kwani hayo ndio muhimu zaidi kuliko kutaka kujua mtoto wa kiume au kike na pengine yule unayemtaka sana awe, ageuke kuwa mtoto wa shari. Na si jambo la hekima, kwa maana kuna baadhi ya watu wanatamani watoto wa aina fulani, na pindi wanapogundua sivyo, basi hujuta na kusikitika ma kutokuwa na raha tena na kiumbe hicho hata kabla hakijazaliwa.

 

 

Pia baadhi ya hospitali za Ulaya zimekuwa zinazuia kufanya zoezi hilo kwa sababu baadhi ya jamii haswa mabaniani (Hindus) wanaua watoto pindi wanapojua kuwa ni wa kike, hayo yametokea Uingereza na kufanya baadhi ya miji kuzuia hospitali zake kufanya jambo hilo.

 

Vile vile wengine hutaka kujua mapema ni mtoto gani kwa ajili ya kujitayarisha kununua vitu vya mtoto kwa kulingana na jinsia yake. Kama wa kiume, kununua nguo za kiume na vitu vinavyomhusu mtoto wa kiume, na kama wa kike kununua nguo za kike na vitu vinavyomhusu mtoto wa kike n.k. kabla ya kuzaliwa. Jambo hili pia silo la busara kwani kama tulivyotaja juu kuwa hakuna mwenye uhakika kama huyo mtoto atazaliwa salama. Matokeo yake huwa ni khasara na huzuni ikazidi baada ya tabu na gharama zote hizo.    

 

Na Allaah Anajua zaidi 

 

 

 

    

 

   
Share