Amemuachisha Mke Wa Mtu Kisha Kamuoa Yeye

 

 

SWALI:

Jee ni ipi hukumu ya mtu anaemrubuni mke wa mtu na hatimae kumachisha kwenye ndoa na kumuoa yeye?



 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani kwa swali lako hilo. Hakika ikiwa jambo hilo la kumrubuni mke wa mtu limetokea kweli basi ni dalili ya kuonyesha kuwa Uislamu wetu umefifia kiasi cha unyama. Hakika hilo litaonyesha udhaifu mkubwa wa Imani zetu na hivyo kupatikana Ummah huu na mitihani pamoja na balaa moja baada ya nyingine.

Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza mtu kupeleka posa juu ya posa ya nduguye seuze kurubuni. Hii ni kuwa ikiwa binti tayari keshapelekewa posa na mume mmoja haifai kwa mwanamme mwingine kwenda kumposa binti au msichana huyo.

Huku kurubuni ni kumtoa mtu katika ndoa yake ya halali, kisha kufanya kosa kubwa na dhuluma ya wazi ya mtu huyo tena kwenda kumuoa. Tufahamu kuwa hakuna mtu mwengine anayeweza kukuachisha mke wako mpaka ima wewe utoe talaka au mkeo akushitaki kwa Qaadhiy na Qaadhiy aone kweli wewe unamdhulumu hivyo awaachishe. Ikiwa kwa njia moja au nyingine mtu yeyote amemlazimisha mtu mwengine amwache mkewe, talaka hiyo ya kutwenza nguvu huwa haikupita. Hivyo, mwanamke huyo anapoolewa na mwanamme mwengine huwa hiyo ndoa si sahihi na wanandoa hao wanazini.

Dhuluma katika Uislamu imepigwa vita vikali sana na kushutumiwa. Allaah Aluyetukuka Anasema:

 Dhalimu hatapata msaidizi” (22: 71).

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ogopeni dhuluma, kwani dhuluma ni viza Siku ya Kiyama” (Muslim).

Na Aliyetukuka katika Hadithi al-Qudsiy Anasema: Enyi waja Wangu! Mimi Nimejiharamishia dhuluma juu ya Nafsi Yangu na nikaifanya ni haramu baina yenu basi msidhulumiane (Muslim).

Dhuluma inafanya amali zote njema zianguke na mfanyaji awe ni mwenye kuingizwa motoni. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) anahadithia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliuliza: “Mnajua muflis?” Wakasema (watu): “Muflis kwetu sisi ni yule miongoni mwetu asiyekuwa na dirhamu (pesa) wala vyenye kumnufaisha yeye hapa duniani”. Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakika muflis katika Ummah wangu ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaama na Swalah, Funga na Zakaah, lakini amemtusi huyu, kumsingizia huyu mwingine kuwa amezini, amekula mali ya huyu, amemwaga damu ya mwingine na kumpiga mwengine. Thawabu zake zitapatiwa huyu na yule mpaka zimalizike. Na zinapokwisha basi madhambi ya hao (aliowadhulumu) atabandikwa nayo, hivyo kuingizwa Motoni” (Muslim).

Mbali na hiyo dhuluma aliyoifanya, kuna zinaa ambayo pia adhabu yake ni kali mno. Huenda hapa asipate lolote katika adhabu lakini adhabu kali itamgojea Siku ya Kiyama. Tufahamu kuwa pia mwanamke aliyekubali kurubuniwa ataingia katika madhambi hayo kwani bila yeye kumkubali huyo mtu hangeweza kutimiza anayotaka.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atuepushe mbali na madhambi aina hiyo na mengineyo.

Na Allaah Anajua zaidi.

Share