Watu Saba Watakaofunikwa Katika Kivuli Cha Allaah Siku Ya Qiyaamah
Watu Saba Watakaofunikwa Katika Kivuli Cha Allaah Siku Ya Qiyaamah
Hadiyth ifuatayo, Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) ametaja aina ya watu saba ambao watakuwa katika kivuli cha Allaah (عز وجل) Siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa kivuli cha Allaah:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((سَبْعَةٌ يُظِلُّهُمْ اللَّهُ فِي ظِلِّهِ يَوْمَ لا ظِلَّ إِلا ظِلُّهُ: الإِمَامُ الْعَادِلُ، وَشَابٌّ نَشَأ فِي عِبَادَةِ رَبِّهِ، وَرَجُلٌ قَلْبُهُ مُعَلَّقٌ فِي الْمَسَاجِدِ، وَرَجُلَانِ تَحَابَّا فِي اللَّهِ اجْتَمَعَا عَلَيْهِ وَتَفَرَّقَا عَلَيْهِ، وَرَجُلٌ طَلَبَتْهُ امْرَأَةٌ ذَاتُ مَنْصِبٍ وَجَمَالٍ فَقَالَ إِنِّي أَخَافُ اللَّهَ، وَرَجُلٌ تَصَدَّقَ بِصَدَقَةٍ فَأَخْفَاهَا حَتَّى لا تَعْلَمَ شِمَالُهُ مَا تُنْفِقُ يَمِينُهُ، وَرَجُلٌ ذَكَرَ اللَّهَ خَالِيًا فَفَاضَتْ عَيْنَاهُ)) متفق عليه
Amesimulia Abuu Hurayrah (رضي الله عنه): Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watu saba Allaah Atawafunika katika kivuli Chake, Siku ambayo hakutokuwa na kivuli ila kivuli Chake: (i) Imaam (kiongozi) muadilifu. (ii) Kijana ambaye amekulia katika ibaada ya Rabb wake. (iii) Mtu ambaye moyo wake umeambatana na Misikiti (iv) Watu wawili wanaopendana kwa ajili ya Allaah; wanakutana kwa ajili Yake na wanafarikiana kwa ajili Yake. (v) Mwanamme aliyetakwa na mwanamke mwenye hadhi na mrembo wa kuvutia akasema: Mimi namkhofu Allaah! (vi) Mtu aliyetoa swadaqa yake akaificha hadi kwamba mkono wake wa kushoto usijue nini ulichotoa mkono wake wa kulia. (vii) Mtu aliyemdhukuru Allaah kwa siri macho yake yakatokwa machozi.” [Al-Bukhaariy, Muslim]
Watu hao wamesifika kwa sifa na ‘amali ambazo jazaa zake ni adhimu mno, nayo ni kuweko katika kivuli cha Allaah (عزّ وجلّ) kwa sababu siku hiyo jua litakuwa karibu mno na watu watatokwa majasho hadi yawafunike mwili kama ilivyothibiti katika Hadiyth:
قال النَّبيُّ صلى الله عليه وسلم: ((إِنَّ الشَّمْسَ تَدْنُو يَوْمَ القِيَامَةِ حَتَّى يَبْلُغَ العَرَقُ نِصْفَ الأُذُنِ، فَبَيْنَمَا هُمْ كَذَلِكَ اسْتَغَاثُوا بِآدَمَ، ثُمَّ بِمُوسَى، ثُمَّ بِمُحَمَّدٍ صلى الله عليه وسلم فَيَشْفَعُ لِيُقْضَى بَيْنَ الخَلْقِ، فَيَمْشِي حَتَّى يَأْخُذَ بِحَلقَةِ البَابِ، فَيَوْمَئِذٍ يَبْعَثُهُ اللهُ مَقَامًا مَحْمُودًا، يَحْمَدُهُ أَهْلُ الجَمْعِ كُلُّهُمْ))
Amesema: “Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Hakika jua litakaribia Siku ya Qiyaamah mpaka majasho ya watu yatafikia karibu na masikio. Watakapokuwa katika hali hiyo, wataomba msaada kwa Aadam, kisha kwa Muwsaa kisha kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam). Ataomba Shafaa’ah kwa Allaah ili Ahukumu baina ya viumbe Vyake. Ataendelea mpaka atakamata kikamatio cha mlango. Siku hiyo basi Allaah Atamuinua Maqaaman Mahmuwdaa [cheo cha kusifika] na watu wote wa mkusanyiko watamsifu)). [Al-Bukhaariy]
Na katika Riwaayah:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ ـ رضى الله عنه ـ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم قَالَ " يَعْرَقُ النَّاسُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حَتَّى يَذْهَبَ عَرَقُهُمْ فِي الأَرْضِ سَبْعِينَ ذِرَاعًا، وَيُلْجِمُهُمْ حَتَّى يَبْلُغَ آذَانَهُمْ ".
Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Watu watatokwa majasho Siku ya Qiyaamah na yatadidimia ardhini kiasi cha dhiraa sabiini kisha yatapanda hadi kuwafikia midomo na masikio yao)) [Al-Bukhaariy]
Ufafanuzi wa Sifa saba hizo ni kama ifuatavyo:
1-Imaam (Kiongozi) Muadilifu
Haki katika Uislamu ni muhimu sana na ni kitu ambacho kila Kiongozi Muislamu na waongozwa lazima wafuate katika kila kitu bila ya hitilafu yoyote. Shariy'ah ni kumpa kila mtu haki anayestahiki. Waislamu au wasio waislamu, ndugu au mgeni, rafiki au adui. Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُونُوا قَوَّامِينَ لِلَّـهِ شُهَدَاءَ بِالْقِسْطِ ۖ وَلَا يَجْرِمَنَّكُمْ شَنَآنُ قَوْمٍ عَلَىٰ أَلَّا تَعْدِلُوا ۚ اعْدِلُوا هُوَ أَقْرَبُ لِلتَّقْوَىٰ ۖ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿٨﴾
Enyi walioamini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa ushahidi kwa uadilifu. Na wala chuki ya watu isikuchocheeni kutokufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu; hivyo ni karibu zaidi na taqwa. Na mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika kwa yale myatendayo. [Al-Maaidah: 8]
Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ وَإِيتَاءِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَيَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ ۚ يَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ﴿٩٠﴾
Hakika Allaah Anaamrishia uadilifu na ihsaan na kuwapa (msaada) jamaa wa karibu; na Anakataza machafu na munkari na ukandamizaji. Anakuwaidhini ili huenda mkapata kukumbuka. [An-Nahl: 90]
Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى)
فَلِذَٰلِكَ فَادْعُ ۖ وَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ ۖ وَلَا تَتَّبِعْ أَهْوَاءَهُمْ ۖ وَقُلْ آمَنتُ بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ مِن كِتَابٍ ۖ وَأُمِرْتُ لِأَعْدِلَ بَيْنَكُمُ ۖ اللَّـهُ رَبُّنَا وَرَبُّكُمْ ۖ لَنَا أَعْمَالُنَا وَلَكُمْ أَعْمَالُكُمْ ۖ لَا حُجَّةَ بَيْنَنَا وَبَيْنَكُمُ ۖ اللَّـهُ يَجْمَعُ بَيْنَنَا ۖ وَإِلَيْهِ الْمَصِيرُ﴿١٥﴾
Basi kwa hayo walinganie (ee Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم, na thibitika imara kama ulivyoamrishwa, na wala usifuate hawaa zao. Na sema: Nimeamini yale Aliyoyateremsha Allaah katika Vitabu, na nimeamrishwa niadilishe baina yenu. Allaah ni Rabb wetu na Rabb wenu; sisi tuna ‘amali zetu, nanyi mna ‘amali zenu. Hakuna kubishana baina yetu na baina yenu; Allaah Atatujumuisha baina yetu, na Kwake ndio mahali pa kuishia. [Ash-Shuwraa: 15]
Hata kama tunaikubali Shariy’ah, lakini tunasahau haraka kwenye kutekeleza. Ndio maana unaona tukizungumza kuhusu marafiki zetu na watu walio karibu nasi, tunawasifia kupita kiasi, na tukizungumza kuhusu watu kinyume na hao, hatusemi hata jema moja lao na tunayakumbuka au kuyataja mabaya yao tu. Hii imetolewa na kutupwa kabisa katika haki ambayo Allaah (سبحانه وتعالى) Anaipenda na hutoa ujira au thawabu kubwa mno kwa mtekelezaji kama ilivotajwa katika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ عَمْرٍو قَالَ، قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم " إِنَّ الْمُقْسِطِينَ عِنْدَ اللَّهِ عَلَى مَنَابِرَ مِنْ نُورٍ عَنْ يَمِينِ الرَّحْمَنِ عَزَّ وَجَلَّ وَكِلْتَا يَدَيْهِ يَمِينٌ الَّذِينَ يَعْدِلُونَ فِي حُكْمِهِمْ وَأَهْلِيهِمْ وَمَا وَلُوا " .
“Watendaji haki watakalishwa katika minbari za Nuru kwenye mkono wa kulia wa Ar-Rahmaan (عز وجل) na hakika mikono yote (ya Allaah) ipo kulia (haki) kwa wale ambao waadilifu wa Shariy'ah katika utawala wao, baina ya familia zao na kila kitu ambacho wamepewa mamlaka.” [Muslim].
Na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuagiza Abdullaah bin Mas’uwd sehemu iliowazi katika mji wa Madiynah baina ya makazi na bustani ya mitende ya Answaar na aliposema Banu ‘Abd bin Zuhrah, “Watoe hapa kwetu watoto wa Umm ‘Abd (Ibn Mas’uwd), akajibu, “Kwanini Allaah amenileta mimi. Allaah (عز وجل) Hapendi wala hawarehemu watu baina yenu ambao hawatoi haki kwa watu walio dhaifu.” [At-Tirmidhiy]
Kutekeleza shariy'ah kwa haki na uadilifu ni muhimu sana kwa mtawala yoyote, madhali yeye ndio mshika hatamu wa watu wake na yeye ndio mtoa haki wa mwisho katika sehemu husika. Kwa sababu hii, mtawala amepewa nafasi muhimu sana kama mmoja katika watu saba ambao watatunikiwa kivuli cha Allaah (عز وجل) Siku ya Qiyaamah.
2-Kijana Ambaye Amekulia Katika ‘Ibaadah Ya Rabb Wake:
Ni kheri na baraka iliyoje kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kijana ambaye ameongozwa kwenye ‘ibaadah na akawa na mwongozo mzuri katika mambo mema, kwani kama tunavojua kuwa katika ujana wa mtu ambapo hukabiliwa na vishawishi vya dunia na huwa rahisi kuteleza na kuingia katika mambo ya kipuuzi ya dunia. Hii inakuwa dhihirifu pale tunapoana kwenye jamii zetu na tunaona hadaa nyingi za kidunia, kama muziki, michezo, vilabu mbali mbali visivo vya kheri, mambo ya fasheni na kadhalika. Hivi vyote huwa vimelenga au mlengwa mkuu katika mambo hayo tuliyoyataja hapo juu ni vijana. Wapotofu huwaambai vijana: “Ujana huwa mara moja tu!” Ndio maana Waislamu wengi siku hizi wanapoteza ujana wao kufikiri kuwa wataswali, na wanawake watavaa hijaab na kwenda kuhiji na kadhalika pale watakapofikia umri wa uzee, kama vile wana uhakikisho wa kujaaliwa maisha marefu kutoka kwa Allaah (سبحانه وتعالى). Ee ndugu yangu Muislamu ni kiasi gani tunajali wasia wa Nabiy wetu Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) aliposema:
((اغتنِمْ خمسًا قبل خمسٍ : شبابَك قبل هِرَمِك، وصِحَّتَك قبل سِقَمِك، وغناك قبل فقرِك، وفراغَك قبل شُغلِك، وحياتَك قبل موتِك))
((Nufaika kwa mambo matano kabla ya matano; ujana wako kabla ya uzee wako, siha yako kabla ya maradhi yako, mali yako kabla ya ufukara wako, wakati wako wa faragha kabla ya kushughulishwa kwako, na uhai wako kabla ya mauti yako)) [Al-Haakim, Al-Bayhaqiy Ameisahihisha Al-Albaaniy katika Swahiyh Al-Jaami’ (1077), Swahiyh At-Targhiyb (3355)]
3. Mtu Ambaye Moyo Wake Umeambatana Na Misikiti:
Kuna msisitizo mkubwa katika Sunnah kwa Muislamu mwanaume kuswali Msikitini na malipo yake ni ni makubwa mno. Haimaanishi pekee kuwa inamwezesha mtu astahiki kivuli cha Allaah (سبحانه وتعالى) Siku ya Qiyaamah, bali pia kama alivyosema Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
عن أَبي هريرة رضيَ اللَّه عنهُ قال : قال رسولُ اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم : ((صَلاةُ الرَّجُلِ في جَماعةٍ تُضَعَّفُ عَلى صلاتِهِ في بَيْتِهِ وفي سُوقِهِ خمساً وَعِشْرينَ ضِعفًا، وذلكَ أَنَّهُ إِذا تَوَضَّأَ فَأَحْسَنَ الْوُضُوءَ ثُمَّ خَرَجَ إِلى المَسْجِدِ، لا يُخْرِجُه إِلاَّ الصَّلاةُ، لَمْ يَخْطُ خَطْوةً إِلاَّ رُفِعَتْ لَه بهَا دَرَجَةٌ، وَحُطَّتْ عَنْه بهَا خَطِيئَةٌ، فَإِذا صَلى لَمْ تَزَلِ المَلائِكَة تُصَلِّي عَلَيْهِ مَا دَامَ في مُصَلاَّه، مَا لَمْ يُحْدِثْ، تَقُولُ: اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَيْهِ، اللَّهُمَّ ارحَمْهُ. وَلا يَزَالُ في صَلاةٍ مَا انْتَظَرَ الصَّلاة)) متفقٌ عليه . وهذا لفظ البخاري
Kutoka kwa Abuu Huraryah (رضي الله عنه) ambaye amesema: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Swalaah ya Jamaa’ah inazidi (thawabu) na Swalaah ya mtu nyumbani kwake au dukani kwake kwa mara ishirini na tano, kwa hivyo anapotawadha akafanya vizuri wudhuu wake, kisha akatoka kwenda Msikitini, hakuna lililomtoa ila Swalaah; basi hatembei hatua moja ila hupandishwa daraja (kwa hatua hiyo), na hufutiwa dhambi kwa hiyo hatua. Atakapokuwa anaswali, Malaika wanaendelea kumswalia madamu yumo kwenye Swalaah ikiwa hatozungumza. Husema (Malaika): “Ee Allah Mswalie na Mrehemu.” Na huendelea hivyo wakati anasubiri Swalaah nyingine)) [Al-Bukhaariy na Muslim] Na hili tamshi la Al-Bukhaariy.
Bali pia, Misikiti inatakiwa iwe katika moyo wa jamii ya Kiislamu, na shughuli zao zote za kidini zitekelezwe humo kama kufunga Nikaah.
4- Watu Wawili Wanaopendana Kwa Ajili Ya Allaah; Wanakutana Kwa Ajili Yake Na Wanafarikiana Kwa Ajili Yake:
Mapenzi kwa ajili ya Allaah ni moja ya milango adhimu kuelekea kwenye mazuri ya huko Aakhirah. Kupendana kwa ajili ya Allaah inamaanisha Muislamu anatakiwa ampende Muislamu mwenzake kwa ajili ya Dini yake; mwenye kufuata Qur-aan na Sunnah ambaye hufanyia kazi maamrisho na makatazo ya Allaah (سبحانه وتعالى) na Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم). Pia ambaye mwenye taqwa, mtiifu. Kumpenda huko kuwe bila ya kujali rangi yake, hali yake mtu kama ni masikini au fakiri, na bila kujali ukabila lake au nasaba yake. Utampenda kwa ajili ya Iymaan yake. Huku ndiko kupendana kwa ajili ya Allaah. Kinyume chake ni kuchukia kwa ajili ya Allaah, na hivi ndipo mtu ataonja ladha ya Iymaan kama ilivyokuja katika Hadiyth:
عن أنسٍ رضي الله عنه، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم، قَالَ : (( ثَلاثٌ مَنْ كُنَّ فِيهِ وَجَدَ بِهِنَّ حَلاوَةَ الإيمانِ : أنْ يَكُونَ اللهُ وَرَسُولُهُ أحَبَّ إِلَيْهِ مِمَّا سَوَاهُمَا ، وَأنْ يُحِبّ المَرْءَ لاَ يُحِبُّهُ إلاَّ للهِ ، وَأَنْ يَكْرَهَ أنْ يَعُودَ في الكُفْرِ بَعْدَ أنْ أنْقَذَهُ الله مِنْهُ ، كَمَا يَكْرَهُ أنْ يُقْذَفَ في النَّارِ )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .
Imepokewa kutoka kwa Anas (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Sifa tatu yeyote mwenye kuwa nazo atapata ladha (utamu) wa Imani: Kuwa Allaah na Rasuli Wake ndiyo awapendao zaidi kuliko wasiokuwa wao; (la pili) kumpenda mtu kwa ajili ya Allaah Peke Yake, (la tatu) kuchukia kurudi katika ukafiri kama anavyochukia kutupwa motoni. [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na pia:
عن البرَاءِ بن عازب رضي الله عنهما ، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم أنَّهُ قَالَ في الأنصار : (( لاَ يُحِبُّهُمْ إلاَّ مُؤمِنٌ ، وَلاَ يُبْغِضُهُمْ إلاَّ مُنَافِقٌ ، مَنْ أحَبَّهُمْ أَحَبَّهُ الله ، وَمَنْ أبْغَضَهُمْ أبْغَضَهُ الله )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ .
Imepokewa kutoka kwa Al-Baraa'i bin 'Aazib (Radhwiyah Allaahu 'anhu) ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema yafuatayo kuhusu Ansari: "Hawapendi wao isipokuwa Muumini na hawachukii isipokuwa mnafiki. Kwa hiyo Allaah Atampenda anayewapenda na Atamchukia anayewachukia." [Al-Bukhaariy na Muslim
Fadhila nyengine za kupendana kwa ajili ya Allaah zinapatikana katika Hadiyth zifuatazo:
-Watawekwa katika Minbari Za Nuru:
عن معاذ رضي الله عنه، قَالَ : سَمِعْتُ رسول الله صلى الله عليه وسلم، يقول : (( قَالَ الله (عزّ وجلّ) : المُتَحَابُّونَ في جَلالِي ، لَهُمْ مَنَابِرُ مِنْ نُورٍ يَغْبِطُهُمُ النَّبِيُّونَ وَالشُّهَدَاءُ )) . رواه الترمذي ، وَقالَ : (( حديث حسن صحيح )) .
Imepokewa kutoka kwake Mu'aadh (Radhwiyah Allaahu 'anhu) amesema: "Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: "Amesema Allaah ('Azza wa Jall): Wanaopendana kwa ajili ya Utukufu Wangu, watakaa katika minbari za nuru huku Manabii na mashahidi wakitamani hadhi na kheri hiyo." [At-Tirmidhiy, ambaye amesema ni Hadiyth Hasan Swahiyh]
-Kupendwa Na Allaah (سبحانه وتعالى)
وعن أَبي هريرة رضي الله عنه، عن النَّبيّ صلى الله عليه وسلم: (( أنَّ رَجُلاً زَارَ أخاً لَهُ في قَرْيَةٍ أخْرَى ، فَأرصَدَ اللهُ لَهُ عَلَى مَدْرَجَتِهِ مَلَكاً … )) وذكر الحديث إِلَى قوله : (( إنَّ الله قَدْ أحبَّكَ كَمَا أحْبَبْتَهُ فِيهِ )) رواه مسلم ، وقد سبق بالباب قبله .
Na imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mtu mmoja alimzuru nduguye katika Kijiji chengine. Allaah alimwakilisha Malaika njiani...." Akataja hadiyth hadi kauli yake: "Hakika Allaah amekupenda kama ulivyompenda ndugu yako kwa ajili Yake." [Muslim].
5- Mwanamme Aliyetakwa Na Mwanamke Mwenye Hadhi Na Mrembo Wa Kuvutia Akasema: "Mimi Namkhofu Allaah!"
Tanbihi: Hadiyth hii imekusudiwa pia kuwa mwanamke naye atakayemkhofu Allaah pindi mwanamume akimtaka kuingia katika maasi ya zinaa.
Zama hizi za mwisho, zimejaa fitnah na vishawishi ya kumpelekea mtu kuingia katika zinaa, na Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuacha kuonya:
عن أَبي سعيد الخدري رضي الله عنه : أن رسول الله صلى الله عليه وسلم، قَالَ: (( إنَّ الدُّنْيَا حُلْوَةٌ خَضِرَةٌ وَإنَّ الله تَعَالَى مُسْتَخْلِفُكُمْ فِيهَا، فَيَنْظُرُ كَيْفَ تَعْمَلُونَ، فَاتَّقُوا الدُّنْيَا وَاتَّقُوا النِّسَاءَ )) رواه مسلم.
Impokewa kutoka kwa Abu Saiyd Al-Khudriy (Radhwiyah Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Hakika dunia ni tamu na kijani (imejaa utajiri) na Allaah Ta'aalaa atawafanya nyinyi kuwa makhalifa humo na atawaangalia kwa yale mnayofanya. Hivyo tahadharini na dunia na wanawake." [Muslim
Waumini wa kweli wanapaswa wajikinge na vishawishi vinayosababisha kumtelezesha mtu kuingia katika zinaa na badala yake wabakie katika kumhofu Allaah (سبحانه وتعالى). Anaonya Allaah (سبحانه وتعالى):
وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ ۖ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾
Na wala msiikaribie zinaa. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya kabisa. [Al-Israa: 32]
6- Mtu Aliyetoa Swadaqah Yake Akaificha Hadi Kwamba Mkono Wake Wa Kushoto Usijue Nini Ulichotoa Mkono Wake Wa Kulia:
Hii ni katika makatazo ya Riyaa (kujionyesha) ambayo yanamharibia mtu amali zake. Allaah (سبحانه وتعالى) Anaonya Anaposema:
وَلَقَدْ أُوحِيَ إِلَيْكَ وَإِلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكَ لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ﴿٦٥﴾
Kwa yakini umefunuliwa Wahy na kwa wale walio kabla yako kwamba: “Ukifanya shirki bila shaka zitaporomoka ‘amali zako na bila shaka utakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” [Az-Zumar: 65]
Na Anasema pia Allaah (سبحانه وتعالى)
وَلَوْ أَشْرَكُوا لَحَبِطَ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٨٨﴾
Na kama wangemshirikisha bila shaka yangeporomoka yale waliyokuwa wakitenda. [Al-An’aam: 88]
Ni hatari kwa kuwa baadhi ya watu hupenda kuonekana na kusifiwa katika kutoa kwake sadaka. Na mwenye kujionyesha amali zake atakuwa katika watu ambao watakuwa wa kwanza kuulilzwa kuhusu amali zao na wataingizwa motoni kwa riyaa zao:
عَنْ أبي هريرة رضي الله عنه قال: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهم عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يَقُولُ ((إِنَّ أَوَّلَ النَّاسِ يُقْضَى يَوْمَ الْقِيَامَةِ عَلَيْهِ رَجُلٌ اسْتُشْهِدَ فَأُتِيَ بِهِ فَعَرَّفَهُ نِعَمَهُ فَعَرَفَهَا قَالَ: فَمَا عَمِلْتَ فِيهَا؟ قَالَ: قَاتَلْتُ فِيكَ حَتَّى اسْتُشْهِدْتُ، قَالَ: كَذَبْتَ وَلَكِنَّكَ قَاتَلْتَ لِأَنْ يُقَالَ جَرِيءٌ فَقَدْ قِيلَ ثُمَّ أُمِرَ بِهِ فَسُحِبَ عَلَى وَجْهِهِ حَتَّى أُلْقِيَ فِي النَّارِ، وَرَجُلٌ تَعَلَّمَ الْعِلْمَ وَعَلَّمَهُ وَقَرَأَ الْقُرْآنَ فَأُتِيَ بِهِ فَعَرَّفَهُ نِعَمَهُ فَعَرَفَهَا قَالَ: فَمَا عَمِلْتَ فِيهَا؟ قَالَ: تَعَلَّمْتُ الْعِلْمَ وَعَلَّمْتُهُ وَقَرَأْتُ فِيكَ الْقُرْآنَ، قَالَ: كَذَبْتَ وَلَكِنَّكَ تَعَلَّمْتَ الْعِلْمَ لِيُقَالَ عَالِمٌ وَقَرَأْتَ الْقُرْآنَ لِيُقَالَ هُوَ قَارِئٌ فَقَدْ قِيلَ ثُمَّ أُمِرَ بِهِ فَسُحِبَ عَلَى وَجْهِهِ حَتَّى أُلْقِيَ فِي النَّارِ، وَرَجُلٌ وَسَّعَ اللَّهُ عَلَيْهِ وَأَعْطَاهُ مِنْ أَصْنَافِ الْمَالِ كُلِّهِ فَأُتِيَ بِهِ فَعَرَّفَهُ نِعَمَهُ فَعَرَفَهَا قَالَ: فَمَا عَمِلْتَ فِيهَا؟ قَالَ: مَا تَرَكْتُ مِنْ سَبِيلٍ تُحِبُّ أَنْ يُنْفَقَ فِيهَا إِلَّا أَنْفَقْتُ فِيهَا لَكَ قَالَ كَذَبْتَ وَلَكِنَّكَ فَعَلْتَ لِيُقَالَ هُوَ جَوَادٌ فَقَدْ قِيلَ ثُمَّ أُمِرَ بِهِ فَـسُحِبَ عَـلَى وَجْهِهِ ثُمَّ أُلْقِيَ فِي النَّارِ ))
Kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: Nilimsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi sallam) akisema: ((Wa mwanzo kuhesabiwa Siku ya Qiyaamah ni mtu aliyekufa shahidi katika vita, ataletwa na kujulishwa neema alizoneemeshwa na baada ya kuzijua ataulizwa (na Allaah): “Umezifanyia kazi gani neema hizi?” Atasema: “Nimepigana jihaad kwa ajili Yako mpaka nikafa shahidi.” Ataambiwa: “Umesema uongo, bali ulipigana ili isemwe kuwa wewe ni jasiri na imeshasemwa.” Kisha itaamrishwa abururwe kwa uso wake na kuingizwa Motoni. Na mtu (mwengine) 'Aalim aliyejifundisha Dini akaijua vizuri, akasoma na Qur-aan, ataletwa na kujulishwa neema alizoneemeshwa, kisha ataulizwa; “Umezifanyia kazi gani neema hizi?” Atasema: “Nimejifunza elimu nikafundisha na kwa ajili Yako nikasoma Qur-aan.” Ataambiwa: “Umesema uongo, bali ulijifunza elimu ili isemwe kuwa wewe ni ‘Aalim. Ukasoma Qur-aan ili isemwe kuwa wewe ni msomaji (mzuri), na imeshasemwa.” Kisha itaamrishwa abururwe kwa uso wake na kuingizwa Motoni. Na mtu (mwengine) Allaah Amempa wasaa, akampa kila aina ya mali, ataletwa na kujulishwa juu ya neema alizoneemeshwa, kisha ataulizwa: “Umezifanyia kazi gani neema hizi?” Atasema: “Sijaacha njia Unayopenda mtu atoe katika mali yake ila mimi nimetoa kwa ajili Yako.” Ataambiwa: “Umesema uongo, bali umetoa ili isemwe kuwa wewe ni mkarimu na imeshasemwa. Kisha itaamrishwa abururwe kwa uso wake na kuingizwa Motoni”. [Muslim]
Hivvo ni lazima mtu awe makini na aweke niyyah safi ya kutoa sadaka. Si kama tunavoona leo ambapo katika Misikiti yetu utakuta watu katika kipaza sauti na mabao ya matangazo yanayosema: “Fulani katoa kadhaa kumpa fulani kwa sababu kadhaa wa kadhaa!” Hii ni riyaa hakika!
7- Mtu Aliyemdhukuru Allaah Kwa Siri Macho Yake Yakatokwa Machozi:
Kulia machozi kwa ajili ya kumkhofu Allaah (سبحانه وتعالى) au kunyenyekea Kwake ni katika alama za iymaan. Na fadhila zake zimetajwa katika Qur-aan pindi Anapowasifu waja wema hao kama Anavosema Allaah (سبحانه وتعالى)
قُلْ آمِنُوا بِهِ أَوْ لَا تُؤْمِنُوا ۚ إِنَّ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ مِن قَبْلِهِ إِذَا يُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ يَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ سُجَّدًا ﴿١٠٧﴾
Sema: Iaminini au msiamini. Hakika wale waliopewa elimu kabla yake wanaposomewa (Qur-aan) wanaporomoka kifudifudi wanasujudu.
وَيَقُولُونَ سُبْحَانَ رَبِّنَا إِن كَانَ وَعْدُ رَبِّنَا لَمَفْعُولًا ﴿١٠٨﴾
Na wanasema: Utakasifu ni wa Rabb wetu; hakika ahadi ya Rabb wetu lazima itimizwe.
وَيَخِرُّونَ لِلْأَذْقَانِ يَبْكُونَ وَيَزِيدُهُمْ خُشُوعًا ۩﴿١٠٩﴾
Na wanaporomoka kifudifudi huku wanalia na inawazidishia unyenyekevu. [Al-Israa: 107-109]
Na pia katika Hadiyth:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لاَ يَلِجُ النَّارَ رَجُلٌ بَكَى مِنْ خَشْيَةِ اللَّهِ حَتَّى يَعُودَ اللَّبَنُ فِي الضَّرْعِ. ولاَ يَجْتَمِعُ غُبَارٌ فِي سَبِيلِ اللَّهِ وَدُخَانُ جَهَنَّمَ)) رواه الترمذي وقال: حديث حسن صحيح
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (رضي الله عنه) kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: ((Hatoingia motoni mtu anayelia kwa sababu ya kumkhofu Allaah mpaka maziwa yarudi katika chuchu. Wala haliwezi kujumuika vumbi katika Njia ya Allaah na moshi wa Jahannam)). [At-Tirmdihiy na amesema: Hadiyth Hasan Swahiyh]
Na pia:
“Hakuna kitu ambacho kinampendezesha na kupendwa na Allaah (سبحانه وتعالى) kama matone mawili na alama mbili: Tone la chozi lilotoka kwa ajili ya kumkhofu Allaah na tone la damu lilitoka kwa ajili ya Allaah. Na hizo alama mbili ni, alama iliyosababishwa kwa ajili ya Allaah na alama iliyosababishwa kwa kutimiza moja kati ya mambo ya fardhi yaliyoamrishwa na Allaah (سبحانه وتعالى) [At-Tirmidhiy na katika Al-Mishkaat]
Tunamuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Atujaalie sisi na vizazi vyetu kumiliki sifa hizo ili tuwe wenye kupata Fadhila hiyo ya kuwekwa katika kivuli cha Allaah Siku ambayo hakutakuwa na kivuli isipokuwa kivuli cha Allaah. Aamiyn.