Kumsaidia Kaka Yangu Ambaye Anatuhumiwa Ni Mlevi

SWALI:

assalam aleykum.inshAllaah mungu akulipeni kheri duniani na akhera kwa msaada wenu.amma baad.mimi nipo nchi za ugenini na nina kaka yangu nyumbani africa ameniomba msaada wa kima fulani cha fedha ili ajikwamue kimaisha.lakini kwa upande mwengine jamaa zangu wengine wanahisi kwamba nismpelekee hizo pesa kwani wanamtuhumu kwamba ana tabia ya ulevi ingawa anajificha hafanyi kwa dhahiri. mie sipo huko africa na siwezi kujua uhalisi wa mambo ila  familia yangu yote wamenieleza kwamba ana tabia ya kulewa. tujaalie imenithibitikia kweli kwamba ni mlevi. Suali: je inafaa kumpelekea hizi pesa ambazo sina uhakika kwamba ana nia ya kutafutia maisha kweli au kulewa? naomba ufafanuzi na shukran kwa kutuondolea utata katika dini. waAllaahu alam

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Molai wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atupatie at-Tawfiyq ya kuweza kutekeleza ihsani kwa jamaa zetu kwa njia ambayo ni nzuri na njema. Swali lako hilo lina vipengele kadhaa ambavyo vinaonyesha utata na tatizo ulilo nalo.

Naona itakuwa muhimu tuandike zile ibara zako zako ili tuweze kukielezea kila kipengele kivyake. Ibara yako hii “tujaalie imenithibitikia kweli kwamba ni mlevi”. Ikiwa imethibitika hasa bila tatizo lolote kuwa analewa japokuwa kwa kujificha basi itakuwa hufai kumsaidia kwa mujibu wa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala): “Saidianeni katika wema na uchaji Mungu wala msisaidiane katika madhambi na uadui” (5: 2).

Lau utasaidia katika madhambi basi nawe utakuwa na sehemu yako ya madhambi mbele ya Allaah Aliyetukuka.

Ama ibara yako: “Suali: je inafaa kumpelekea hizi pesa ambazo sina uhakika kwamba ana nia ya kutafutia maisha kweli au kulewa?” Katika suala hilo nasaha ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa mtu mwenye shaka ipo wazi kabisa. Imepokewa kwa Abu Muhammad al-Hasan bin ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘Anhuma) kuwa alisema: “Nimehifadhi kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Acha lenye kukutia shaka kwa lisilokutia shaka” (at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy).

Na katika Hadiyth nyingine anasema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hawi mtu ni katika wenye kumcha Allaah mpaka aache hata lisilokuwa na ubaya kwa kuogopa kufanya lenye ubaya” (at-Tirmidhiy). Kwa hiyo, hufai kumsaidia nduguyo kwa jambo ambalo hujui hizo pesa atatumia vipi. Hata kama ataanzisha biashara faida atakayoipata atakuwa ni mwenye kutumia kunywa pombe hivyo nawe utakuwa umemsaidia katika madhambi.

Nasaha ambayo tunaweza kukupatia ni:

i)                   Swali Swalah ya Istikhaarah (kumtaka shauri Allaah Alliyetukuka). Hiyo itakusaidia kwani ishara utakayopata itakuwa inatoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala), wala usidharau hilo.

ii)                  Jaribu kuwauliza tena watu wako kuhusu hilo na nduguyo kunywa na wawe ni wenye kukueleza la haki na ukweli. Hatudhani jamaa zako ambao pia ni jamaa zake watamtakia mabaya lakini mara nyingine husuda huingia katika familia na jamaa wakawa hawataki kuona kuwa ndugu yao kafaidika na usaidizi wowote.

iii)                Pia ni wajibu wako kuzungumza na nduguyo kwa njia simu au kuwasiliana naye ikiwa ama E-Mail (barua pepe). Na katika mazungumzo ujaribu kumdadisi na kumuuliza kuhusu hilo. Mnasihi kwa kumuambia kuwa habari unazo juu ya hilo na Muislamu hafai kufanya kitendo hicho. Kwa hiyo, aachane na unywaji wa pombe, kwani hilo ni jambo lenye kumuangamiza hapa duniani na Akhera.

Tunaomba uchukue muda wako wa kuliangalia suala hilo kwa makini ili usiwe ni mwenye kumkosesha haki yake nduguyo au kumpatia asichostahiki.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akusahilishie jambo lako hilo, Amiyn.

Na Allaah Anajua zaidi

Share