Majaaliwa Na Makadario Ya Watu Wema Na Waovu

 

Majaaliwa Na Makadario Ya Watu Wema Na Waovu

 

Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Namshkuru Allah, Subhanahuu-wataala kwa kunipa fursa hii ya kuweza ku communicate Nanyi kwa mara ingine tena. Swali langu safari hii ni kuhusu maisha ya mwanadamu.

 

Inavyo semekana katika dini, yakua pindi mwanadamu anapo zaliwa, huwa ashaandikiwa Kwenye kitabu chake atakua na maisha aina kadha wa kadha (mtu mwenye uwezo, atakua Daktari, au mwalimu ), Rizki yake itatokamana na kitu fulani (biashara, ualimu, ujenzi), na ataishi kwa mda Fulani (kama miaka 20,30,60), na kifo chake kitatokea Kwa sababu Fulani ( maradhi, kuuwawa, ajali, au normal death). 

 

Swali la kwanza:

 

- Mwanadamu anaekuwa mtu wa kufuata dini, na akaja fariki ilihali yakua ni mcha Maungu,Na mwanadamu anaekua mwizi, au mzinifu, au mwenye maasi tofauti tofauti, na kifo chake Kikawa ni kwa njia ya kuuwawa, watu hawa aina mbili huwa nikuwa wameshaandikiwa Kwenye vitabu vyao, Maisha Yao,

 

Na Vifo Vyao au ni vipi? - au kuandikiwa maisha yako katika kitabu chako, huwa unaandikiwa mambo gani?

 

 

Swali la pili:

 

……..Allāh sends astray whom He wills and He guides on the Straight Path whom He wills.

 

kwa hio ni watu aina gani waliodhamiriwa hapa? Je inawezekana kuwa hata anaefanya  kosa anaweza kuwa guided kwenye straight path, ikiwa Allah  ametaka?

 

Jazaakumullahu kheir!

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Tunakushukuru kwa Maswali haya ya 'Aqiydah ambayo ni muhimu kwa kila Muislamu kufahamu kwani mara nyingi huwa yanawatatiza watu kufahamu makusudio ya majaaliwa yao. Mas-ala haya kuhusu majaaliwa yana maelezo marefu mno ili mtu apate kufahamu lakini tutajaribu kuelezeza kiasi fulani ili yaeleweke vizuri.

 

Tuanze kwanza kuelezea asili ya roho za binaadamu. Kabla ya kuumbwa sisi binaadamu, Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Alikusanya kizazi chote cha Aadam ('Alayhis-Salaam) mpaka waliokuwa hawakuzaliwa bado hadi siku ya Qiyaamah. Wakati huo zikiwa roho zao ni safi kabisa zilizo katika "Fitwrah" (maumbile ya asili ya Uislam). Kwa maana Allaah Katuumba katika hali ya kuikubali Dini Yake kwa kufuata amri zote na kuacha makatazo yake, na kutupa Iymaan ya kuamini Tawhiyd, (kuwa Yeye ni Allaah Mmoja pekee hana mshirika wala msaidizi).  Nafsi (viumbe) tukashuhudia na kuchukua ahadi kwamba tutamtii Rabb wetu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):    

وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ ۖ قَالُوا بَلَىٰ ۛ شَهِدْنَا ۛ أَن تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَـٰذَا غَافِلِينَ ﴿١٧٢﴾

Na pindi Rabb wako Alipowaleta katika wana wa Aadam kutoka migongoni mwao, kizazi chao, Akawashuhudisha juu ya nafsi zao, Je, Mimi siye Rabb wenu? Wakasema: Ndio bila shaka, tumeshuhudia! (Allaah Akawaambia): Msije kusema Siku ya Qiyaamah: hakika sisi tulikuwa tumeghafilika nayo haya. [Al-A'araaf 7:172]

 

Kisha mama anapobeba mimba na inapotimia miezi minne, huwa ni wakati wa hizo roho kupulizwa katika mwili wake kiumbe, kama inavyoelezea Hadiyth ifuatayo:

 

عَنْ أَبِي عَبْدِ الرَّحْمَنِ عَبْدِ اللَّهِ بْنِ مَسْعُودٍ رضي الله عنه قَالَ: حَدَّثَنَا رَسُولُ اللَّهِ صلى الله عليه وسلم -وَهُوَ الصَّادِقُ الْمَصْدُوقُ: ((إِنَّ أَحَدَكُمْ يُجْمَعُ خَلْقُهُ فِي بَطْنِ أُمِّهِ أَرْبَعِينَ يَوْمًا نُطْفَةً، ثُمَّ يَكُونُ عَلَقَةً مِثْلَ ذَلِكَ، ثُمَّ يَكُونُ مُضْغَةً مِثْلَ ذَلِكَ، ثُمَّ يُرْسَلُ إلَيْهِ الْمَلَكُ فَيَنْفُخُ فِيهِ الرُّوحَ، وَيُؤْمَرُ بِأَرْبَعِ كَلِمَاتٍ: بِكَتْبِ رِزْقِهِ، وَأَجَلِهِ، وَعَمَلِهِ، وَشَقِيٍّ أَمْ سَعِيدٍ؛ فَوَاَللَّهِ الَّذِي لَا إلَهَ غَيْرُهُ إنَّ أَحَدَكُمْ لَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ الْجَنَّةِ حَتَّى مَا يَكُونُ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا إلَّا ذِرَاعٌ فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الْكِتَابُ فَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ النَّارِ فَيَدْخُلُهَا. وَإِنَّ أَحَدَكُمْ لَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ النَّارِ حَتَّى مَا يَكُونُ بَيْنَهُ وَبَيْنَهَا إلَّا ذِرَاعٌ فَيَسْبِقُ عَلَيْهِ الْكِتَابُ فَيَعْمَلُ بِعَمَلِ أَهْلِ الْجَنَّةِ فَيَدْخُلُهَا)) رواه البخاري ومسلم

Amesimulia Abuu 'Abdir-Rahmaan 'Abdillaah bin Mas‘uwd (رضي الله عنه): Ametusimulia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)  ambaye ni mkweli mwenye kuaminiwa: “Hakika kila mmoja wenu hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake siku arubaini akiwa ni mkusanyiko wa mbegu (za uzazi za mama na baba), kisha arubaini zifuatazo huwa ni donge la damu, kisha arubaini zijazo huwa pande la nyama, kisha Allaah Humtuma Malaika kwake na kumpulizia roho (yake).  Na (Malaika huyo) anaamrishwa maneno manne; Kuandika rizki yake, ajali yake (umri atakaoishi duniani), amali zake, mtu muovu au mwema. Wa-Allaahi naapa kwa Yule Ambaye hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, hakika mmoja wenu huenda afanye amali za watu wa Jannah hadi ikawa baina yake na Jannah ni dhiraa na kile kilichoandikwa kikathibiti, akafanya amali ya watu wa motoni akaingia motoni. Na hakika mmoja wenu huenda afanye amali za watu wa motoni hadi ikawa baina yake na moto ni dhiraa na hapo kile kilichoandikwa kikathibiti, akafanya amali ya watu wa Jannah akaingia Jannah.” [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Majaaliwa ya uhai na rizki ni amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Ama yanayohusu maovu au mema atakayofanya binaadamu yatakuwa ni kutokana na khiari yake. Kwa sababu Muumba wetu Hakutuleta duniani ila pamoja na uongofu kamili; Vitabu Vyake na Wajumbe Wake. Na katika uongofu huu kuna mambo mawili; makatazo na amri za kutenda mema. Kisha ni khiari ya mtu kuchagua atakavyo baina ya hayo mawili. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا﴿١﴾إِنَّا خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ أَمْشَاجٍ نَّبْتَلِيهِ فَجَعَلْنَاهُ سَمِيعًا بَصِيرًا﴿٢﴾إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا﴿٣﴾

Je haikumfikia mwana-Aadam kipindi fulani katika dahari, hakuwa kitu kinachotajwa?Hakika Sisi Tumemuumba mwana-Aadam kutokana na tone la manii iliyochanganyika ili Tumjaribu; Tukamjaalia mwenye kusikia na kuona. Hakika Sisi Tumemuongoza njia; ima (awe) ni mwenye kushukuru au mwenye kukufuru. [Al-Insaan: 1 – 3]

 

Nafsi ya binaadamu imeumbwa ikiwa ina matamanio ya mema na maovu, lakini pia ni khiari yake mtu ima kuiendekeza nafsi ifanye maovu inayotamani, au kuizuia na tunaona kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ameiapia nafsi: 

 

وَنَفْسٍ وَمَا سَوَّاهَا ﴿٧﴾فَأَلْهَمَهَا فُجُورَهَا وَتَقْوَاهَا ﴿٨﴾قَدْ أَفْلَحَ مَن زَكَّاهَا ﴿٩﴾وَقَدْ خَابَ مَن دَسَّاهَا ﴿١٠﴾

Na Naapa kwa nafsi na Aliyeisawazisha. Kisha Akaitambulisha uovu wake na taqwa yake. Kwayakini amefaulu yule aliyeitakasa. Na kwa yakini amepita patupu aliyeifisidi. [Ash-Shams: 7-10]

   

Ibnu 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhu), kasema kuhusu Aayah Namba (8):

 

فَأَلْهَمَهَا فُجُورَهَا وَتَقْوَاهَا ﴿٨﴾

(Kisha Akaitambulisha uovu wake na taqwa yake)

 

kwamba Akaipambanulia baina ya kheri na shari. Wamesema hivyo pia Qataadah na Ad-Dhwahaak. [Tafsiyr Ibn Kathiyr]

 

 عَنْ أَبِي الْأَسْوَد الدَّيْلِيّ قَالَ : قَالَ لِي عِمْرَان بْن حُصَيْن أَرَأَيْت مَا يَعْمَل النَّاس فِيهِ وَيَتَكَادَحُونَ فِيهِ أَشَيْء قُضِيَ عَلَيْهِمْ وَمَضَى عَلَيْهِمْ مِنْ قَدَر قَدْ سَبَقَ أَوْ فِيمَا يَسْتَقْبِلُونَ مِمَّا أَتَاهُمْ بِهِ نَبِيّهمْ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَأُكِّدَتْ عَلَيْهِمْ الْحُجَّة ؟ قُلْت بَلْ شَيْء قُضِيَ عَلَيْهِمْ قَالَ فَهَلْ يَكُون ذَلِكَ ظُلْمًا ؟ قَالَ فَفَزِعْت مِنْهُ فَزَعًا شَدِيدًا قَالَ : قُلْت لَهُ لَيْسَ شَيْء إِلَّا وَهُوَ خَلْقُهُ وَمِلْك يَده لَا يُسْأَل عَمَّا يَفْعَل وَهُمْ يُسْأَلُونَ قَالَ سَدَّدَك اللَّه إِنَّمَا سَأَلْتُك لِأَخْبُر عَقْلَك . إِنَّ رَجُلًا مِنْ مُزَيْنَة أَوْ جُهَيْنَة أَتَى رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَقَالَ يَا رَسُول اللَّه أَرَأَيْت مَا يَعْمَل النَّاس فِيهِ وَيَتَكَادَحُونَ أَشَيْء قُضِيَ عَلَيْهِمْ وَمَضَى عَلَيْهِمْ مِنْ قَدَر قَدْ سَبَقَ أَمْ شَيْء مِمَّا يَسْتَقْبِلُونَ مِمَّا أَتَاهُمْ بِهِ نَبِيّهمْ صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَأُكِّدَتْ بِهِ عَلَيْهِمْ الْحُجَّة ؟ قَالَ   ((بَلْ شَيْء قَدْ قُضِيَ عَلَيْهِمْ)) قَالَ فَفِيمَ نَعْمَل ؟ قَالَ  ((مَنْ كَانَ اللَّه خَلَقَهُ لِإِحْدَى الْمَنْزِلَتَيْنِ يُهَيِّئهُ لَهَا وَتَصْدِيق ذَلِكَ فِي كِتَاب اللَّه تَعَالَى :   وَنَفْس وَمَا سَوَّاهَا فَأَلْهَمَهَا فُجُورهَا وَتَقْوَاهَا )) رَوَاهُ أَحْمَد وَمُسْلِم

Ibnu Jariyr amerikodi kutoka kwa Ibnul Aswad ambaye alisema: "Imraan bin Huswayn aliniambia: Unadhani kwamba watendayo watu na wanayojitahidi ni mambo yaliyokidhiwa kwao na kujaaliwa kwao? Au ni mambo ambayo wanayoandikiwa baada ya ujumbe kuwafikia kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) utakapokuweko ushahidi dhidi yao? Nikasema: Bali ni mambo yaliyokidhiwa kwao. Akasema: Basi hivyo huwa ni dhulma? Nikawa na khofu sana [kwa yale aliyoyasema] nikamwambia: Hakuna chochote ila [Allaah] Amekiumba na Amekimiliki. Haulizwi Afanyayo bali wao (viumbe Vyake) vitaulizwa. ['Imraan] akasema: Allaah Akuongoze. Nimekuuliza tu ili kukujulisha kwamba mtu mmoja kutoka kabila la Muzaynah au Juhaynah alikuja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: Ee Rasuli wa Allaah, vipi kuhusu watendayo watu na wanayojitahidi kama ni mambo yaliyokidhiwa na kujaaliwa katika Qadar, au ni mambo tu waliyoandikiwa baada ya ujumbe kuwafikia kutoka kwa Mtume wao utakapokuweko ushahidi dhidi yao? Akasema [Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam]: "Bali ni mambo yaliyokidhiwa kwao". Akasema yule mtu: Basi kuna haja gani ya sisi kutenda lolote? Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Yeyote Aliyeumbwa (Aliyejaaliwa) na Allaah kuwa katika hali mojawapo baina ya mbili; [Pepo au moto], basi Atampatia, na hilo linasadikishwa na kitabu cha Allaah: ((Na kwa nafsi na kwa Aliyeitengeneza! Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake". [Ahmad na Muslim] 

 

Vile vile:

 

عَنْ اِبْن عَبَّاس قَالَ : كَانَ رَسُول اللَّه صَلَّى اللَّه عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِذَا مَرَّ بِهَذِهِ الْآيَة  (( وَنَفْس وَمَا سَوَّاهَا فَأَلْهَمَهَا فُجُورهَا وَتَقْوَاهَا)) وَقَفَ ثُمَّ قَالَ ((اللَّهُمَّ آتِ نَفْسِي تَقْوَاهَا أَنْتَ وَلِيّهَا وَمَوْلَاهَا وَخَيْر مَنْ زَكَّاهَا ))

Ibn 'Abbaas amesema kwamba: "Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisimama anaposoma Aayah hizi:

 

وَنَفْسٍ وَمَا سَوَّاهَا ﴿٧﴾فَأَلْهَمَهَا فُجُورَهَا وَتَقْوَاهَا ﴿٨﴾

Na Naapa kwa nafsi na Aliyeisawazisha. Kisha Akaitambulisha uovu wake na taqwa yake.

 

Husema: "Ee Allaah, Ipe nafsi taqwa (ucha wa Allaah) yake. Wewe ni Mlinzi wake na Bwana wake, na Mbora zaidi wa kuitakasa". [At-Twabaraaniy 11:106]

 

Huu ni uthibitisho kwamba ni mja mwenyewe huchagua kuiharibu nafsi yake na sio majaaliwa aliyoaandikiwa, kwa maana sio Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aliyemchagulia afanye maovu, kwani ikiwa ni hivyo itakuwa ni kama kusema kuwa mja huyo kadhulumiwa wakati Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Hamdhulumu mtu kama Anavyosema katika Aayah kadha na kadhaa:

 

ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٥١﴾

Hayo ni kwa yale (maovu) yaliyotangulizwa na mikono yenu; na kwamba Allaah si Mwenye kudhulumu waja. [Al-Anfaal: 51]

 

Vile vile Anasema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَظْلِمُ النَّاسَ شَيْئًا وَلَـٰكِنَّ النَّاسَ أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ﴿٤٤﴾

Hakika Allaah Hadhulumu watu chochote, lakini watu wenyewe  ni wenye kudhulumu nafsi zao. [Yuwnus: 44]

 

Watu wanajidhulumu kwa kuiachia nafsi iwaamrishe maovu kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

إِنَّ النَّفْسَ لأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ

Hakika nafsi ni yenye kuamrisha sana maovu [Yuwsuf: 53]

 

Lakini wengine huzuia nafsi zao zisifanya zitakavyo bali huwa na khofu ya Rabb wao:

 

وَأَمَّا مَنْ خَافَ مَقَامَ رَبِّهِ وَنَهَى النَّفْسَ عَنِ الْهَوَىٰ ﴿٤٠﴾فَإِنَّ الْجَنَّةَ هِيَ الْمَأْوَىٰ ﴿٤١﴾

Ama yule aliyekhofu kisimamo mbele ya Rabb wake, na akaikataza nafsi yake na hawaa. Basi hakika Jannah ndio makaazi yake. [An-Naazi'aat: 40-41]

 

Sasa tukirudi katika kujibu Swali la kwanza ni kwamba, mambo yote atakayotenda mtu mema na maovu tayari yameshaandikwa, kwa maana kuwa yameshajulikana na Rabb Mtukufu, Mwingi wa Ujuzi na Mwingi wa elimu. Mfano Allaah Ameshajua kuwa fulani bin fulani atakuwa mtu mwema na ataendelea kufanya wema hadi kufa kwake. Au Mfano fulani atakuwa mtu mwema, lakini atakuja kupotoka baadaye awe mtu muovu aingie motoni. Au fulani atakuwa mtu mwema kisha atapotoka, kisha atarudia tena kuwa mwema n.k na vile vile kinyume chake cha mtu muovu. Na hivi ndivyo Alivyokusudia kutuumba ili iwe kama ni mtihani kwetu nani atakayefanya vitendo vyema ili Atuonyeshe Rahma Yake ya kutulipa mema na tunapokosea tukarudi Kwake Yuko tayari kutusamehe:

بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ  

تَبَارَكَ الَّذِي بِيَدِهِ الْمُلْكُ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿١﴾الَّذِي خَلَقَ الْمَوْتَ وَالْحَيَاةَ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا ۚ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْغَفُورُ﴿٢﴾

Kwa Jina la Allaah Ar-Rahmaan, Mwenye kurehemu.

Amebarikika Ambaye Mkononi Mwake umo ufalme Naye juu ya kila kitu ni Muweza. Ambaye Ameumba mauti na uhai ili Akujaribuni ni nani kati yenu mwenye ‘amali nzuri zaidi. Naye ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwingi wa kughufuria. [Al-Mulk: 1-2]

 

Jibu La Swali Pili:

 

Kauli uliyoitaja hakika haikuja kwa matamshi hayo kuunganisha 'Yudhwillu man Yashaa wa Yahdiy man Yaashaa ilaa Swiraatwil-Mustaqiym' (Humwacha akapotea Amtakaye, na Humuongoa Amtakaye katika njia iliyonyooka) bali imekuja ima 'Yudhwillu man Yashaa wa Yahdiy Man Yashaa" (Humwacha akapotea Amtakaye, na Humuongoa Amtakaye)   bila ya kutaja 'Ilaa Swiraatwil-Mustaqiym' (katika njia iliyonyooka) inapoungana kauli mbili hizo. Au imekuja kauli 'Yahdiy man Yashaa ilaa Swiraatwil-Mustaqiym' (Humuongoa Amtakaye katika njia iliyonyooka), hapa imekuja kauli ya kumuongoza mtu pekee bila ya kauli ya kumpotoa na ndio imeungwa na kumuongoza katika njia iliyonyooka. 

 

Mfano mmoja wa aina hizo za kauli ni:

 

أَفَمَن زُيِّنَ لَهُ سُوءُ عَمَلِهِ فَرَآهُ حَسَنًا ۖ فَإِنَّ اللَّـهَ يُضِلُّ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ ۖ فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ ﴿٨﴾

Je, yule aliyepambiwa uovu wa ‘amali yake akaiona ni nzuri (je, ni sawa na aliyeongoka?) Basi hakika Allaah Anampotoa Amtakaye na Anamhidi Amtakaye, basi isihiliki nafsi yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kwa ajili ya majuto. Hakika Allaah ni Mjuzi kwa yale wayatendayo. [Faatwir: 8]

 

 

Mfano wa Aayah iliyotaja kuongozwa katika Swiraatwil-Mustaqiym:

 

 

لَّقَدْ أَنزَلْنَا آيَاتٍ مُّبَيِّنَاتٍ ۚ وَاللَّـهُ يَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٤٦﴾

Kwa yakini Tumeteremsha Aayaat bayana, na Allaah Anamwongoza Amtakaye kuelekea njia iliyonyooka. [An-Nuwr: 46]

 

Ina maana kwamba kwa elimu Yake Ameshatambua kwamba fulani bin fulani atapenda kuwa mtu mwema, kwa maana ametaka nafsi yake kwa upendo wake mwenyewe,  kufuata amri za Mola Wake, hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Humfanyia njia au sababu apate kuelekea katika uongofu. Humuonyesha njia za kutafuta elimu, kusikiliza mawaidha n.k. na kila anapopata ukumbusho huzidi Iymaan yake na uchaji Allaah. Vile vile mfano mzuri ni wasiokuwa Waislamu. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatambua kuwa fulani ataukubali Uislamu. Hivyo Humfanyia kila njia imfikie habari yoyote ile kuhusu Uislamu, ikiwa ni kwa njia ya vyombo vya habari, au mtu kumtajia, au kumfikia Qur-aan, au kusikia tu kuhusu Waislamu. Popote alipo Atamfanyia njia imfikie ili afuatilie kuhusu Uislamu hadi akubali haki.

 

Hivyo ndio maana moja ya  (Humuongoa Amtakaye)

 

Na maana (Humwacha akapotea Amtakaye) kwa maana kwa elimu Yake Ameshajua kwamba fulani bin fulani ni mtu atakayependa kufanya maovu hivyo Humpa huru afanye hadi apotoke. Na ndio maana Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

..إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ ۖ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ﴿١٢٥﴾

Hakika Rabb wako Yeye Anamjua zaidi aliyepotea njia Yake, Naye Anawajua zaidi waliohidika. [An-Nahl: 125]

 

Kukamilisha jibu la muulizaji ni kama tulivyotaja juu kwamba inawezekana mtu kutenda maovu mengi kisha akaja kupata uongofu kwa kuchagua mwenyewe kutaka kutubia, kujirekebisha na kujibakisha katika Taqwa, hivyo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Humpokea na Husamehe madhambi yake kisha Akamuongoza katika Swiraatwil Mustaqiym.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share