Ufafanuzi Wa Ahlul Bayt (Masharifu) Na Kizazi Chake

 

Ufafanuzi Wa Ahlul Bayt (Masharifu) Na Kizazi Chake

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam aleykum warahmatullahi wabarakatu, naomba ufafanuzi kuhusu nyumba ya mtume wetu na kizazi chake cha ahlul bait kama vile kikwetu wanvyo itwa masharifu. Kulingana na ninavyo elewa masharifu wametokana na kizazi cha mtume pale mwenyezi mungu alipo sema katika kisa cha ahlul kisaa kuwa amewatahirisha mtume swaw, fatma bint muhamad, ali ibn abitalib, hassan and hussein. Shukran

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Suala hili la Ahlul Bayt (Watu wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na tafsiri yake ni mojawapo ya hitilafu kubwa baina ya Ahlus Sunnah na Shia.

 

Wakati Shia wanasema kuwa Ahlul Bayt ni ‘Aliy bin Abi Twaalib na Faatwimah bint Muhammad na wanawe (Radhwiya Allaahu ‘anhum) peke yao, Ahlus Sunnah wanaitakidi kuwa Ahlul Bayt ni wote hao waliotangulia kutajwa pamoja na wake wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na binti zake waliobakia wasiotambuliwa na Shia, na pia wajukuu zake na baadhi ya waliohusiana naye katika ukoo wake.

 

Imeandikwa katika kamusi maarufu "Lisaanul ‘Arab" kuwa; mke na jamaa za mtu ni Ahli Bayti yake. Na katika Qur-aan tukufu, Allaah Anawataja wake wa mtu kuwa ni Ahli yake.

 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

قَالُوا أَتَعْجَبِينَ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ ۖ رَحْمَتُ اللَّـهِ وَبَرَكَاتُهُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ ۚ 

(Malaika) Wakasema: Je, unastaajabia amri ya Allaah? Rahmah ya Allaah na baraka Zake ziko juu yenu enyi Ahlal-Bayt. Hakika Yeye ni Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote, [Huwd: 73].

 

'Ulamaa wote wanasema kuwa neno (Watu wa nyumba), katika Aayah hii anakusudiwa Sarah mke wa Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam).

 

Na Akasema:

إِذْ رَأَىٰ نَارًا فَقَالَ لِأَهْلِهِ امْكُثُوا إِنِّي آنَسْتُ نَارًا

Alipouona moto akawaambia ahli zake: Bakieni (hapa); kwa yakini nimeona moto,..[Twahaa: 10].

 

Inajulikana hapa pia kuwa neno (Ahli yake) anakusudiwa mke wa Nabiy Muwsaa (‘Alayhis- salaam) aliyekuwa amefuatana naye katika safari hiyo.

 

Na Allaah Aliyetukuka Akasema pia:

 

وَاسْتَبَقَا الْبَابَ وَقَدَّتْ قَمِيصَهُ مِن دُبُرٍ وَأَلْفَيَا سَيِّدَهَا لَدَى الْبَابِ ۚ قَالَتْ مَا جَزَاءُ مَنْ أَرَادَ بِأَهْلِكَ سُوءًا إِلَّا أَن يُسْجَنَ أَوْ عَذَابٌ أَلِيمٌ﴿٢٥﴾

Hakuna jazaa ya anayemtakia uovu ahli wako isipokuwa kufungwa jela au adhabu iumizayo.[Yuwsuf: 25].

 

Neno (Ahlika katika Aayah hii) na maana yake ni 'mkeo' aliyekusudiwa ni mke wa al-‘Aziyz.

 

Kwa hivyo dalili zote zinaonyesha kuwa neno Ahlul Bayt au Ahl linatumika zaidi kwa maana ya mke. Na katika Suwrah Al-Ahzaab kuanzia Aayah ya 28 hadi ya 33 Allaah Aliyetukuka Anasema:

 

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ إِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا فَتَعَالَيْنَ أُمَتِّعْكُنَّ وَأُسَرِّحْكُنَّ سَرَاحًا جَمِيلًا ﴿٢٨﴾وَإِن كُنتُنَّ تُرِدْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَالدَّارَ الْآخِرَةَ فَإِنَّ اللَّـهَ أَعَدَّ لِلْمُحْسِنَاتِ مِنكُنَّ أَجْرًا عَظِيمًا ﴿٢٩﴾يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ مَن يَأْتِ مِنكُنَّ بِفَاحِشَةٍ مُّبَيِّنَةٍ يُضَاعَفْ لَهَا الْعَذَابُ ضِعْفَيْنِ ۚ وَكَانَ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرًا ﴿٣٠﴾وَمَن يَقْنُتْ مِنكُنَّ لِلَّـهِ وَرَسُولِهِ وَتَعْمَلْ صَالِحًا نُّؤْتِهَا أَجْرَهَا مَرَّتَيْنِ وَأَعْتَدْنَا لَهَا رِزْقًا كَرِيمًا ﴿٣١﴾يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ لَسْتُنَّ كَأَحَدٍ مِّنَ النِّسَاءِ ۚ إِنِ اتَّقَيْتُنَّ فَلَا تَخْضَعْنَ بِالْقَوْلِ فَيَطْمَعَ الَّذِي فِي قَلْبِهِ مَرَضٌ وَقُلْنَ قَوْلًا مَّعْرُوفًا ﴿٣٢﴾وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ وَلَا تَبَرَّجْنَ تَبَرُّجَ الْجَاهِلِيَّةِ الْأُولَىٰ ۖ وَأَقِمْنَ الصَّلَاةَ وَآتِينَ الزَّكَاةَ وَأَطِعْنَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا ﴿٣٣﴾

Ee Nabiy!  Waambie wake zako: Ikiwa mnataka uhai wa dunia na mapambo yake; basi njooni nikupeni kitoka nyumba na nikuacheni huru, mwachano mzuri. Na ikiwa mnamtaka Allaah na Rasuli Wake na nyumba ya Aakhirah, basi hakika Allaah Amewaahidi wanawake watendao wema miongoni mwenu ujira adhimu.  Enyi wake wa Nabiy! Yeyote yule miongoni mwenu atakayeleta uchafu bayana, atazidishiwa adhabu maradufu. Na hayo kwa Allaah ni mepesi. Na yeyote miongoni mwenu atakayemtii Allaah na Rasuli Wake, na akatenda mema; Tutampa ujira wake mara mbili, na Tumemuandalia riziki ya ukarimu. Enyi wake wa Nabiy!  Nyinyi si kama yeyote yule katika wanawake; mkiwa na taqwa, basi msilegeze kauli asije akaingiwa tamaa ambaye moyoni mwake mna maradhi na semeni kauli inayokubalika. Na bakieni majumbani mwenu, na wala msionyeshe mapambo na uzuri kwa ajinabi kujishaua kama zama za ujahili. Na simamisheni Swalaah, na toeni Zakaah na mtiini Allaah na Rasuli Wake. Hakika Allaah Anataka Akuondosheeni maovu enyi ahli wa nyumba (ya Nabiy) na Akutakaseni mtakaso barabara. [Al-Ahzaab: 28-33]

 

Ahlus Sunnah wanasema kuwa; kama vile katika Aayah zote zilizotangulia, kila anapotajwa Ahli ya mtu hukusudiwa mke, na katika Aayah hizi pia Allaah Anapotaja Ahli Anawakusudia wake zake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ukizisoma kwa utulivu Aayah hizi utaona kuwa kuanzia Aayah ya 28 Allaah Anazungumza na wake wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): Allaah Aliyetukuka

Anasema:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ

"Ee Nabiy!  Waambie wake zako:.."

Akaendelea:

يَا نِسَاءَ النَّبِيِّ لَسْتُنَّ كَأَحَدٍ مِّنَ النِّسَاءِ ۚ 

"Enyi wake wa Nabiy!  Nyinyi si kama yeyote yule katika wanawake;"

Akaendelea kuwahutubia:

 

وَقَرْنَ فِي بُيُوتِكُنَّ ..... ۖ وَآتِينَ الزَّكَاةَ.... وَأَطِعْنَ اللَّـهَ 

"Kaeni majumbani mwenu" "Toeni Zakaah". "Mtiini Allaah".

Mpaka Aliposema:

إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُذْهِبَ عَنكُمُ الرِّجْسَ أَهْلَ الْبَيْتِ وَيُطَهِّرَكُمْ تَطْهِيرًا ﴿٣٣﴾

Hakika Allaah Anataka Akuondosheeni maovu enyi ahli wa nyumba (ya Nabiy) na Akutakaseni mtakaso barabara.

 

Yote haya wanaambiwa wake zake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuanzia Aayah ya 28 hadi 33. Hivi ndivyo ulivyo mfumo wote wa Aayah hizi zilizokamatana na haziwezi kutenganishwa isipokuwa kama mtu anataka kuvuka mipaka na kwenda kinyume na nassw (maandiko).

 

Mtu anaweza kuuliza: “Kwa nini basi Allaah Ametumia ‘swiyghah’ (mfumo wa maneno) ya wingi wa wanaume na wanawake kwa pamoja Aliposema: ‘Ankum’. Ikiwa Amewakusudia wake za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa nini asitumie swiyghah ya wanawake peke yao Akasema: ‘Ankunna’.

 

Kwa nini Asitumie swiyghah ya wanawake kama Alivyotumia katika Aayah nyingine zilizomo ndani ya mfumo huu?

 

Majibu ni kuwa; Aayah za mwanzo Allaah Alipozungumza juu ya hukmu za kishari’ah na makatazo na maamrisho yanayowahusu wake za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitumia Nuun ya wanawake lakini Alipozungumza juu ya wema anaotaka kuuingiza ndani ya nyumba ile pamoja na kuwasafisha watu wa nyumba ile barabara, Alimuingiza pia na mwenye nyumba ambaye ni mwanamume naye ni Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili kheri hiyo iwaenee wote. Na kawaida katika Lugha ya Kiarabu wanapotajwa wanawake na wanaume kwa pamoja hutumiwa wingi wa wanaume ‘Ankum’.

 

Nani wanaostahiki zaidi kusafishwa na kutakaswa kuliko wake zake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), watu wa nyumba yake, mama za Waislamu, na wanaostahiki pia ni jamaa zake, watu wa aila yake. Kwa sababu Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anastahiki kuwa pamoja na kila kheri na kila jema na kila kilicho bora, na anastahiki zaidi kuwa pamoja na watu wema, naye haridhiki isipokuwa awe pamoja na watu wema, kwani wema lazima siku zote uwe katika mtiririko mmoja.

 

Ikiwa tumemkubali mke wa Nabiy Muwsaa (‘Alayhis-salaam) katika Aayah tuliyotangulia kuitaja kuwa ni Ahli yake na tukamkubali mke wa Al-‘Aziyz kama ilivyokuja katika Aayah kuwa ni Ahli yake na tukamuingiza Sarah mke wa Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) kuwa ni Ahli yake, juu ya kuwa katika Aayah ile Allaah Alitumia mfumo ule ule wa wingi wa wanaume na wanawake kwa pamoja Alitumia neno (‘Alaykum). Kama Alivyotumia (‘Ankum) katika Suwrah Al-Ahzaab. Ikiwa tumewakubali wake wa Rusuli wote hao kuwa ni watu wa nyumba, tunalazimika pia kuwakubali wake wa Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni watu wa nyumba yake.

 

Kutokana na haya inafahamika zaidi tafsiri ya ile Hadiyth maarufu inayoitwa Hadiyth al-Kisaa na maana yake ni Hadiyth ya nguo au Hadiyth ya shuka, wakati Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipowaingiza ndani ya shuka ile ‘Aliy na Bibi Faatwimah na Al-Hasan na Al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhum), kwa ajili ya kuwaingiza na wao katika zile baraka zilizoteremshwa ndani ya Aayah ile ya Suwrah Al-Ahzaab. Hadiyth inasimulia kuwa baada ya kuwaingiza wote hao ndani ya shuka, akasema:

 

"Rabb wangu hawa ni watu wa nyumba yangu, waondolee uchafu na uwasafishe baarabara”. Na Ummu Salamah (Radhwiya Allaahu ‘anha) mke wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoingiza kichwa chake ndani ya shuka hiyo akasema: “Ee Rasuli wa Allaah na mimi ni katika watu wa nyumba yako”. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: “Wewe umo katika kheri wewe umo katika kheri”.

 

Na maana yake ni kuwa Ummu Salamah na wake wenzake wote wamekwishatajwa na Allaah katika Aayah hiyo na kwamba wao wamo katika kheri hiyo ya kusafishwa na kutakaswa. Ndiyo maana akaambiwa: Wewe umo katika kheri wewe umo katika kheri”.

 

Dalili nyingine inayothibitisha kuwa wake wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni katika watu wa nyumba yake imo katika [Al-Bukhaariy, Muslim, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy] na wengine kama ilivyopokelewa kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoulizwa na Swahaba:

 

"Vipi tukuswalie?” Akasema: “Semeni: Rabb wangu mswalie Muhammad na wake zake na vizazi vyake, kama ulivyomswalia Ibraahiym, na umbariki Muhammad na wake zake na vizazi vyake kama ulivyowabariki watu wa nyumba ya Ibraahiym hakika Wewe ni Mwenye kuhimidiwa uliye Mtukufu”.

 

Ikajulisha kuwa mke wa mtu na vizazi vyake ni watu wa nyumba yake.

 

Ikiwa mtu hajatoshelezwa na dalili zote tulizozinukuu kutoka katika Kitabu cha Allaah na mafundisho ya Nabiy wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), basi ipo dalili nyingine katika Swahiyh Al-Bukhaariy itakayoondoa shaka yoyote iliyobaki kwa mwenye kuutafuta ukweli bila ya chuki moyoni mwake.

 

Inajulikana kuwa mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) mke wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisingiziwa uongo katika kisa mashuhuri kinachojulikana kwa jina la Haadithatul Ifk, uongo ambao Allaah Aliyetukuka Aliteremsha Aayah katika Qur-aan tukufu kuukanusha, na wakati huo huo Aayah hizo ziliwaonya Waislamu kutorudia tena kueneza uvumi huo, na zikawatahadharisha juu ya adhabu kali itakayomfikia mwenye kurudia tena.

 

Wakati ule Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipanda juu ya mimbari yake kuhutubia, akasema:

 

"Enyi Waislamu! Nani atakayenipumzisha na mtu aliyeniudhi katika Ahli yangu (watu wa nyumba yangu), kwani WaLlaahi sijaona kwa Ahli yangu isipokuwa kheri tupu, na hakuwa akiingia kwa Ahli yangu isipokuwa akiwa pamoja nami" [Al-Bukhaariy]

 

Atakayechunguza, ataona kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amelitaja neno Ahliy (watu wa nyumba yangu) katika Khutbah hiyo fupi mara tatu, zote zikimaanisha mkewe mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa), ikituthibitishia kuwa neno Ahliy lina maana ya mke.

 

Ahlus Sunnah wanawapenda na wanawapa heshima kubwa na wanawatambua watu wote wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wale wanaokubaliwa na Shia na pia wasiokubaliwa na Shia kuwa ni katika Ahlul Bayt kama vile ‘ami zake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), watoto wa ami zake pamoja na watoto wao (Radhwiya Allaahu ‘anhum), hawa ambao Shia hawawatambui kuwa ni watu wa nyumba ya Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kama walivyotajwa katika Hadiyth iliyotangulia, nao ni kama ifuatavyo:

 

1. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

2. Wake zake

3. Binti zake wote

4. Watu wa nyumba ya Al-‘Abbaas bin Abdilmutwalib

5. Watu wa nyumba ya ‘Aqiyl bin Abi Twaalib

6. Watu wa nyumba ya ‘Aliy bin Abi Twaalib

7. Watu wa nyumba ya Ja‘afar bin Abi Twaalib

 

Hawa wote wametajwa katika Hadiyth iliyotolewa na Muslim wakati Zayd bin Al-Arqam (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipoulizwa:

 

"Wake zake si katika watu wa nyumba yake? Akasema: “Wake zake ni watu wa nyumba yake. Lakini watu wa nyumba yake (waliokusudiwa hapa) ni wale walioharimishwa kupokea sadaka. Akaulizwa: “Nani hao”. Akasema: “Hao ni watu wa nyumba ya ‘Aliy na watu wa nyumba ya ‘Aqiyl na watu wa nyumba ya Ja‘afar na watu wa nyumba ya ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhum).”

 

Kwa hiyvo watu wa nyumba hizo, juu ya kuwa wengine hawakuwemo ndani ya ile shuka (kisaa) lakini wametajwa kuwa ni watu wa nyumba yake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Wake zake bila shaka wanaingia katika watu wa nyumba yake kwa sababu ya kutajwa katika Suwrah Al-Ahzaab kama ilivyotangulia, na ndiyo maana katika kuikamilisha Aayah hiyo Allaah Akasema:

وَاذْكُرْنَ مَا يُتْلَىٰ فِي بُيُوتِكُنَّ مِنْ آيَاتِ اللَّـهِ وَالْحِكْمَةِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ لَطِيفًا خَبِيرًا ﴿٣٤﴾

Na kumbukeni yale yanayosomwa majumbani mwenu katika Ayaat za Allaah na Hikmah (Sunnah), hakika Allaah daima ni Mwenye kudabiri mambo kwa ulatifu, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika. [ Al-Ahzaab: 34].

 

Na watoto na wajukuu wa Al-Hasan bin ‘Aliy na Al-Husayn bin ‘Aliy na ‘Abdullaah bin ‘Abbaas na Muhammad bin Al-Hanafiyah (mtoto wa ‘Aliy kwa mke mwengine), na Al-‘Abbaas bin ‘Aliy na wajukuu zao na wajukuu wa wajukuu zao, wote hao pia ni katika watu wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na hii ni kwa wale waliokuwa Waislamu.

 

Abu Lahab juu ya kuwa ni ‘ami yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), lakini yeye hayumo katika Ahli yake kwa sababu hakuwa Muislamu. Nabii Nuuh (‘Alayhis-salaam) allipomuona mwanawe amekimbilia jabalini na maji yanaanza kumfikia alimuomba Allaah Aliyetukuka Amuokoe. Allaah Alimkatalia na kumuambia kuwa huyo si mwanawe, wala si katika watu wa nyumba yake kwa sababu ya kuukanusha ujumbe aliokuja nao Nabiy Nuwh (‘Alayhis salaam).

 

Shia hawakubali kuwaingiza wengine kuwa ni watu wa nyumba ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isipokuwa wale tu wanne waliotajwa katika Hadiyth ya shuka, pamoja na maimamu kumi na mbili wa Shia Ithna ‘Ashariyah kwa sababu wanaamini kuwa hao ndio viongozi wa Waislamu waliotakaswa wasiotenda makosa watakaowaongoza Waislamu baada ya kufa kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka Siku ya Qiyaamah.

 

Tafadhali bonyeza viungo vifutavyo upate maelezo zaidi:

 

Usharifu Nini Maana Yake? Je Ukoo Wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) Uko Kweli?

 

Kizazi Cha Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Bado Kinaendelea?

 

Masharifu Wasioswali Wana Maovu Na Maasi Watukuzwe? Je, Wao Bora Kuliko Mja Anayefuata Sheria?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share