Ufafanuzi Kuhusu Kusema Uongo Kwa Nabii Ibraahiym Katika Kisa Chake
Ufafanuzi Kuhusu Kusema Uongo Kwa Nabii Ibraahiym Katika Kisa Chake
SWALI:
Asalaam alaykum,
Naomba kuuliza kuhusu kisa cha nabii ibrahim katika kuongopa kwake vipi ufafanuzi juu ya uwongo wake? Alifaya kosa au la?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kisa chenyewe ni kama kifuatavyo kwani kwa kukitaja tutaweza kuufahamu uwongo huo kwa njia iliyo wazi au ni kutoelewa kwetu.
Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Nabiy Ibraahiym alihama pamoja na Sarah, wakafika katika kijiji alichokuwepo mfalme au dikteta. Mfalme aliambiwa kuwa Ibraahiym amefika hapo akiwa na mwanamke mzuri. Hivyo, mfalme alituma aletwe Ibraahiym na kumuuliza, ‘Ee Ibraahiym! Huyu mwanamke ni nani?’ Ibraahiym akajibu: Ni dadangu’. Ibraahiym alirudi kwake na kumwambia, ‘Usiende kinyume nami katika kauli kwani nimemwambia kuwa wewe ni dadangu. Naapa kwa Allaah, hakuna Waumini wa kweli katika ardhi isipokuwa mimi na wewe” [al-Bukhaariy].
Kwa hiyo katika kisa hiki ni wazi kabisa kuwa Nabii Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) hakuongopa kwa kusema Sarah ni dadake, kwani wao ndio Waumini pekee waliokuwa hapa duniani kama Hadiyth inavyoashiria. Na Hadiyth hii ni ishara ya utumiaji wa mafumbo ili kumfanya adui asiwe ni mwenyewe kuelewa hakika ya jambo au mambo.
Swahaba Abubakar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) naye alitumia njia hii alipokuwa anahama pamoja na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam). Alipokuwa anaulizwa na watu huyu unayefuatana naye ni nani, yeye alikuwa anajibu: ‘Huyu ni yule mtu aliyeniongoza njia’. Waulizaji walikuwa wanafahamu kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye mwenye kuongoza msafara ilhali Abubakar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa anamaanisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye aliyemuongoza katika Uislamu.
Na Allaah Anajua zaidi.