Mambo Aliyopangiwa Mwanaadam Wakati Wa Kupuliziwa Roho Yanaweza Kubadilika Baadae?

 

Mambo Aliyopangiwa Mwanaadam Wakati Wa

Kupuliziwa Roho Yanaweza Kubadilika Baadae?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam aleikum,

Nimesikia kua mwnwadam kabla hajaletwa Duniani basi Allaah huandika kwenye qadar yake ya kuwa aidha huyu mtu atakua mwema ama atakua muovu. Na nimeambiwa pia kuwa kinachoandikwa kwenye qadar yake Allaah huwa hakibadiliki. Swali langu ni,je? inakuaje kwa mtu ambaye ameandikiwa kuwa yeye atakua muovu hapa duniani, ina maana kwamba mtu huyu hataweza kufanya mema na ni kweli anaweza kubadilika na kufanya mazuri na hatimaye kwenda peponi? wabillah tawfiq

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Itakuwa vyema tuinukuu Hadiyth yenyewe ili tuwe pamoja katika kufahamu maelezo.

 

 

Imepokewa kwa Abu ‘Abdir-Rahmaan ‘Abdullaah bin Mas’uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba:

 

Ametuzungumzia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye ndiye msema kweli wa kuswadikika: Hakika kila mmoja wenu katika nyinyi hukusanywa umbo lake katika tumbo la mama yake kama mchanganyiko wa mbegu ya uzazi ya mwanamme na mwanamke kwa muda wa siku arubaini; kisha kuwa kipande cha damu kwa muda kama huo; kisha kipande cha nyama kwa muda kama huo. Kisha hutumwa Malaika akampulizia roho ndani yake na akaamrishwa mambo manne: Kuandika riziki yake, ajali yake, ‘amali yake na kama ni mwema au muovu. WaLlaahi, hakuna Mola asiyekuwa Yeye, hakika mmoja wenu hufanya ‘amali ya watu wa Peponi, mpaka ikawa hapana baina yake na Pepo ila dhiraa, akatanguliwa na aliloandikiwa akafanya ‘amali ya watu wa Motoni, akaingia Motoni; na mmoja wenu hufanya ‘amali ya watu wa Motoni, mpaka ikawa hapana baina yake na Moto ila dhiraa, akatanguliwa na aliloandikiwa akafanya ‘amali ya watu wa Peponi, akaingia Peponi” [al-Bukhaariy na Muslim].

 

 

Kuandikiwa mazuri au maovu kwa mwanaadamu ni kwa ule ujuzi na elimu ya Allaah Aliyetukuka kumjua Atakavyokuwa mja wake na hali yake ya maisha. Hayo hayabadiliki kwani Allaah Aliyetukuka ni Mwenye Khabari na Mwenye elimu yote. Kwa hiyo, vitendo ni kwa lililokadiriwa na Allaah Aliyetukuka. Tatizo ni kwamba sisi hatujui lililoandikwa na Allaah Aliyetukuka, wala hali ya mtu baina yake na Mola wake, lakini twaona mwisho wake. Na ndio tunamuona mtu aliye muovu hubadilika akawa mzuri na mtu mzuri akawa muovu na ndivyo alivyotufahamisha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyotuelezea katika Hadiyth hii.

 

Tafadhali bonyeza viungo vifuatavyo upate manufaa zaidi:

 

Majaaliwa Na Makadario Ya Watu Wema Na Waovu

 

Ikiwa Ameandikiwa Ajiue Vipi Aingie Motoni?

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share